Mar 29, 2018

Nchi za SADC na mkakati wa sanaa kwa maendeleo

Ramani inayoonesha nchi za SADC



MAPEMA Machi mwaka huu kuliandaliwa Tamasha la Kusherehekea Wanawake wa SADC Katika Sanaa ya Maigizo na Dansi lililofanyika mjini Johannesburg.

Wanawake wa Zambia katika kikundi cha dansi walitumia michezo ya maigizo kwa ajili ya maendeleo kwa kuhamasisha wanakijiji kupanda zaidi ya miti 5,000 na kujenga majengo matatu ya madarasa kwa kipindi cha miaka mitatu katika Jimbo la Kusini mwa Zambia.

Tamasha hilo liliandaliwa na "Southern Africa Theatre Initiatives (SATI)" na lilikuwa na lengo la kuonesha jukumu la wanasanaa wanawake wa nchi za SADC kuungana na kuleta mabadiliko katika kanda.

“Wanasanaa wanawake wanapuuzwa pamoja na kazi kubwa wanayofanya kuunganisha na kuendeleza jumuiya. Wanachohitaji ni kutambua na kupatiwa msaada tu,” alisema Mpo Molepo, katibu wa SATI.
Mwaka 2002, kundi la sanaa la Kamoto Community lilibainisha ukataji wa miti kama tatizo kuu katika Jimbo la Kusini mwa Zambia na hali mbaya ya madarasa kama jambo linaloathiri wanafunzi katika Shule ya Msingi Chiyumu.

"Kupitia mchezo wetu tulipata fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya madarasa katika Shule ya Msingi Chiyumu ambayo baadaye tuliyakabidhi kwa serikali," alisema mkurugenzi wa kundi la sanaa la Kamoto Community, Mary Manzole Kamoto.

“Kwa suala la mabadiliko ya tabia nchi, kuna ukataji mkubwa wa miti unaoendelea na tulikuwa tukifanya maigizo kuhamasisha watu kupanda miti. Baada ya mchezo wetu, Walianza kupanda miti na hii ilibadili mwenendo wa mvua katika jimbo zima.

"Hii ilibadili mwenendo mzima wa kilimo katika jimbo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likinunua mahindi kutoka majimbo mengine na sasa linauza mahindi," alielezea Jean Shamende, mwanachama wa kikundi hicho.

Ghetto Artists, kundi jingine la wanawake vijana kutoka nchini Botswana, liliwasilisha moja ya maigizo yake, “Strength of A Woman” wakati wa tamasha hilo. Mchezo huo unaonesha maisha ya hatari na halisi ya unyanyasaji dhidi ya vijana wa kike.

“Tunaona mabadiliko chanya ya mchezo huu (nchini Botswana); wasichana walionyanyaswa wanajitokeza, baadhi wanatafuta huduma za ushauri nasaha na wazazi na wanaume wanakiri. Vijana wa kike na kiume wanarejea mashuleni kupitia mchezo huu,” alisema mkurugenzi, Saone Bokitshane.

Aliongeza: “Sanaa ina nguvu kubwa. Kupitia sanaa, unaweza kuponya watu na kupitia sanaa unaweza kuelimisha jumuiya mzima na kujenga upya nchi.

“Ni wakati muafaka serikali zetu zinafadhili wanasanaa wa kike kutengeneza michezo ya VVU/UKIMWI. Kupitia michezo ya wanawake tunaweza kukomesha kuenea kwa gonjwa hilo.”

Na kutoka Zimbabwe kulikuwa na 'Ebony and Ivory', kuhusu wanawake wawili na mabadiliko ya haraka ya moyoni na maumivu yaliyosababishwa na vita, ghasia na utesaji.

Pia ilioneshwa michezo na dansi lililoonesha maisha ya wanawake nchini Lesotho na Afrika Kusini.

Kwa kweli tamasha hilo lilitoa fursa ya kuonesha masaibu yanayoathiri wanasanaa wanawake, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika sekta ya sanaa.

Kwa mujibu wa na chama cha haki za wanasanaa kijulikanacho kama ‘Artists’ Rights Union’, ni asilimia tano tu ya watengenezaji michezo hiyo ni wanawake.

Tamasha hilo lilitokana na utafiti uliofadhiliwa na SATI nchini Afrika Kusini, Malawi, Namibia, Zimbabwe, Zambia, Mauritius, Swaziland, Shelisheli, Msumbiji, Tanzania, na Lesotho.

Prof Amandina Lihamba (Kwa hisani ya shereheyetu blog)
Utafiti wa mwigizaji na mwanazuoni wa Tanzania, Profesa Amandina Lihamba, ulitaka kujua kama sauti za wanawake zilisikika kiasi cha kutosha katika duru za sanaa na fasihi Kusini mwa Afrika.

Mbali na tamasha hili, nchi za kusini mwa Afrika zina makubaliano miongoni mwa wadau na wachunguzi wa tasnia filamu na televisheni, kwamba, utajiri uliopo wa ubunifu miongoni mwa vijana na hadithi zilizopo katika ukanda huu vitumike vyema.

Hata hivyo, wote wanakubaliana kwamba tasnia ya filamu katika nchi hizi bado iko chini sana na, katika hali halisi, inazidi kushuka.

Utafiti unaonesha kuwa tasnia ya filamu ya nchi za SADC ni ndogo na haijapiga hatua, ingawa inaonekana kutoa fursa nyingi katika kuendeleza miundombinu na hadithi zetu.

Kampuni nyingi katika sekta ya filamu na televisheni ni ndogo ndogo na zinazoonekana kuchangia katika ajira na ukuaji wa uchumi, na matatizo ya kupata fedha za kutengenezea filamu ni moja ya kikwazo kikubwa kwenye maendeleo ya sekta ya filamu na televisheni katika nchi hizi.

Katika nchi za SADC, ukiacha Afrika Kusini, haziwezi kujisema kuwa zina tasnia ya filamu, ila zina malighafi za filamu.

Afrika Kusini inaonekana kuwa nchi pekee katika nchi za SADC ambayo uwekezaji kutoka sekta binafsi (kinyume na ufadhili) kwa ajili ya uzalishaji filamu unapatikana bila matatizo.

Miundombinu maalumu katika filamu inaiwezesha nchi ya Afrika Kusini kutengeneza filamu bora za kiwango cha kimataifa. Hali hii, ukichanganya na maeneo yake mbalimbali na hali nzuri ya hewa imeifanya Afrika Kusini kuwa eneo maarufu la kutengenezea filamu.

Katika muktadha wa kidunia, hali hii inayafanya maeneo ya Afrika Kusini, Mauritius na Namibia kuwa maeneo muhimu na yenye gharama ndogo za kutengenezea filamu katika nchi za SADC.

Changamoto kubwa inazozikumba tasnia za filamu katika nchi za SADC ni ukosefu wa uwekezaji katika sekta binafsi ambazo zingeweza kutoa fedha za utengenezaji wa filamu bora kwa soko la nje.

Umiliki wa vipindi kwa vyombo vya utangazaji na tabia ya uvivu wa kufikiri katika kubuni kwenye tasnia ya filamu katika kuhakikisha maendeleo ya mipango ya kuuza nje inaendelea kuikwaza tasnia hii.

Hata hivyo, nchi za Kusini mwa Afrika zina kiwango kizuri cha miundombinu ya utengenezaji wa filamu na vipindi vya televisheni ukilinganisha na nchi zingine za Afrika nje ya ukanda huu.

Miundombinu hii ni pamoja na vitendea kazi vya uzalishaji na uhariri, vitenda kazi vya kutolea mafunzo na vifaa, ingawa filamu zinazozalishwa kutoka nchi za Afrika Magharibi mara nyingi zinachukuliwa kama filamu bora kuliko zinazozalishwa na nchi za SADC.

No comments: