Mar 3, 2018

Filamu ya Watu Wote ni somo kwa Bongo Movies


JUZI nilipata nafasi ya kujadili jambo na Mpigapicha mkuu wa gazeti la HabariLeo, Fadhili Akida, ambaye alionesha nia ya kutaka kutengeneza filamu fupi, ingawa hakujua soko lake likoje.

Tulijikuta tukiwa katika mazungumzo hayo baada ya mchambuzi maarufu wa filamu nchini, ambaye pia ni mhariri wa uzalishaji wa gazeti la HabariLeo, Beda Msimbe, kuibua hoja kuhusu filamu fupi.

Wakati nikiongea na Fadhili, nilijaribu kumweleza uzoefu wangu kuhusu tasnia ya filamu na kile ninachojua kuhusu sekta hii na soko la filamu fupi. Ni mara nyingi nimekuwa nikiwashauri wasanii wetu kuligeukia soko la filamu fupi, kwani soko hili limejengwa katika misingi imara, kwani haliangalii majina ya watu bali misingi na weledi.

Soko kubwa la filamu hizi lipo kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa, ambako ukipeleka filamu yako inaweza kupata watazamaji tofauti ambao si marafiki au jama watakaoiona filamu hiyo.

Matamasha ya filamu ni sehemu nzuri zaidi kwa ajili ya kutengeneza mtandao na kumfanya mtengenezaji kujulikana kimataifa. Pia ikitokea ukabahatika kuwa mmoja wa washindi wa tuzo katika tamasha la filamu, jua itakuwa rahisi kwako kuaminiwa, na hivyo kupata udhamini wa kutengeneza kitu kikubwa zaidi.

Pia utaingia kwenye orodha ya watu wanaoaminiwa, na hapo ndiyo utakapojua kuwa upo katika mstari sahihi.

Soko la filamu fupi si la ubabaishaji kama hili tulilolizoea, kwani ukitengeneza kazi nzuri ujue itapata soko tu. Kuna matamasha zaidi ya elfu tano katika sehemu mbalimbali duniani, na idadi huongezeka kila mwaka. Matamasha haya yana taratibu zake, yapo ambayo huhitaji kutoa ada ya kiingilio na mengine hutoza malipo ya ada ya kuingia, chochote kuanzia dola 10/ na 50/.

Ni vyema kwa wasanii wa Tanzania kufikiria soko hili hasa ikizingatiwa kuwa, thamani ya filamu zetu imeshuka sana, hii inatokana na wasambazaji wa filamu waliolihodhi soko hili kutozingatia weledi wala misingi na hivyo kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizo na ubora.

Soko la filamu nchini (Bongo Movies) limejikita katika kanuni ya mwenye nguvu ndiye anayefaidi (Darwinism), kitu ambacho ni hatari, na hata muundo wa soko hili umeshusha hadhi ya utamaduni.

Umuhimu wa sinema fupi unaonekana sasa hasa kutokana na ile dhana ya filamu kusemwa kuwa hazifanyi vizuri sokoni kinyume na ukweli ulivyo, kwani tatizo ni kutokuwepo uwazi katika biashara kati ya mtayarishaji wa filamu na msambazaji.

Soko la filamu nchini ni kama yalivyo masoko mengine, hutegemea sana taarifa iliyo sahihi. Ili masoko yaweze kuwa katika ushindani mzuri, wadau wote sokoni wanapaswa kuwa wamepata taarifa sahihi kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba kutokana na matendo yao.

Ikiwa baadhi watakuwa na taarifa sahihi zaidi kuliko wengine, hizo tofauti zitasababisha kuwepo na matokeo mabaya.

Kuna matatizo mengi katika soko la filamu nchini, ugumu na makosa yanayofanya utengenezaji wa filamu kuwa wa gharama kubwa zaidi na kutumia muda mwingi kuliko inavyotakiwa, huku mtengenezaji akiwa hajui atakachopata.

Pia kadiri mtandao wa intaneti unavyoendelea kwa kasi duniani, filamu fupi za dakika kadhaa ambazo huoneshwa kwenye mtandao zimeanza kushamiri sana duniani. Kuna wakati utakuta filamu fupi baada ya kuwekwa kwenye mtandao wa intaneti, inaangaliwa na watu zaidi ya mara milioni moja. Na kila inapoangalia huingiza pesa.

Kwa vijana wengine wanaopenda kutengeneza filamu fupi imewapa fursa ya kutimiza ndoto yao, kwa kuwa gharama ya filamu za dakika chache ni ndogo ikilinganishwa na ile ya filamu za kawaida, ufundi wa utengenezaji wake ni rahisi, na kwamba filamu za aina hiyo zinazooneshwa kwenye mtandao wa intaneti, zinawafikia watu wengi zaidi.

Hivi sasa baadhi ya vijana wanataaluma nchini pia wameanza kutengeneza filamu fupi, hali ambayo pia inatia moyo sana. Tafiti zinaonesha kuwa, katika miaka mitano ijayo thamani ya soko la filamu fupi nchini itapanda mara dufu.

Nimalizie makala yangu kwa kuiangazia filamu fupi inayoitwa ‘Watu Wote’, iliyotengenezwa nchini Kenya, inayohusu shambulizi la kigaidi la Alshabaab nchini Kenya, ambapo watu 2 waliuawa ndani ya basi eneo la Mandera mwaka 2014.


Hii filamu imeteuliwa kushindania tuzo maarufu za Oscar mwaka huu. Awali filamu hii ilikuwa imeshinda Tuzo za Oscar kitengo cha wanafunzi mwaka jana na kuwa filamu ya kwanza kutoka Kenya kushinda tuzo hiyo.

Filamu hiyo ya Watu Wote imeorodheshwa kushindania kitengo cha Filamu Bora Fupi: Matukio Halisi katika Tuzo za Oscar. Kwa kweli ni hatua kubwa sana kwa waandaaji wa filamu hii.

Filamu hii inashindana na filamu nyingine nne ambazo ni Dekalb Elementary; The Eleven O'Clock; My Nephew Emmett na The Silent Child.

Hata kama haitashinda tuzo, lakini kitendo cha kutajwa kuwemo kwenye kinyang’anyiro cha kuwani tuzo tayari kimewatangaza wasanii na waandaaji wa filamu, na hivyo kujijengea jina na mtandao mkubwa kimataifa.

Filamu hii ina kisa cha kawaida, ikieleza hadithi ya Kenya, kuhusu Wakenya na imeshirikisha waigizaji wa Kenya. Filamu inasimulia shambulio hilo la mwaka 2014 kaskazini mwa Kenya, ambapo maudhui ya uadui wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu yanaangaziwa.

Ni mara ya kwanza ambapo filamu ya Kenya imeteuliwa kuwania Tuzo ya Oscars, jambo linaloisaidia nchi ya Kenya kupanda ngazi. Kufuatia mafanikio ya filamu hii fupi, Kenya sasa inaongoza katika kueleza ulimwengu hadithi za Afrika.

Katika hadithi kuhusu shambulizi hilo, Waislamu walikataa kujitenga na Wakristo walipoamriwa kufanya hivyo na magaidi wa Alshabaab kutoka Somalia.

Japo ni hadithi ya kawaida lakini kinachoipa hadithi hii upekee ni kitendo cha kuonesha undugu wa Wakenya na njia mwafaka ya kukabiliana na ugaidi kote Ulimwenguni.
Filamu ya Watu Wote imetengenezwa ikilenga kuwakumbuka mashujaa wa shambulizi hilo la kigaidi.

No comments: