Mar 24, 2018

Tuwe macho, hii ni vita ya utamaduni



MIAKA kadhaa iliyopita niliwasiliana na kampuni ya Sony Pictures yenye makao yake Los Angeles (Culver City) nchini Marekani. Hii ni kampuni kubwa Hollywood ya burudani iliyoanzishwa Agosti 7, 1991 baada ya kujitenga kutoka kampuni ya Columbia Pictures Entertainment.

Kampuni hii inafahamika kwa filamu za The Karate Kid, Ghostbusters, Spider-Man, Men in Black, Underworld, Robert Langdon, The Smurfs, Sniper na nyingine nyingi. Niliwasiliana na Sony Pictures nikiwaomba watafute njia ya kudhibiti filamu za Hollywood zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika Mashariki.

Walichonijibu Sony Pictures ni kwamba, hawajali kuona filamu zao zikisambaa, maana walikwishapata faida maradufu kupitia box office, na kusambaa kwake kunasaidia kuwatangaza zaidi!

Hapo ndiyo shaka yangu ilipoanzia, maana pia nilikuwa na sababu ya msingi kutaka kunusuru soko la filamu zetu kwa kuwa filamu za nje hazilipi kodi huku wasanii wetu wasio na mitaji wala dhamana katika benki wakibanwa kulipa kodi bila uhakika wa soko lao.



Ukiangalia kwenye stesheni zetu za televisheni kumejaa tamthilia kutoka China, Ufilipino, Mexico, India na Korea, ambazo zinaruka karibu kila kituo na tunashuhudia hata matangazo yakinakshiwa na miziki kutoka nje.

Hivi sasa vipindi kutoka nje, filamu, picha za katuni na maonesho ya mambo mbalimbali vimetawala nchini na watu wametekwa kuangalia vipindi hivyo.



Na katika mkumbo huo, wasambazaji wakubwa wa filamu nchini wameachana na sinema zetu na badala yake wanasambaza filamu kutoka Bollywood zenye tafsiri za Kiswahili.
Kuna wakati niliongea na watu wa kituo cha utamaduni cha Ufaransa (Alliance Française) wakasema kuwa filamu ndiyo chombo kikuu kilichoisaidia Ufaransa kutangaza utamaduni wao duniani.

Pia kwa miaka mingi Ufaransa imefanikiwa sana kuitumia sekta ya televisheni na filamu kutangaza utamaduni wao duniani.

Ufaransa imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa bajeti za kutengenezea filamu na vipindi vya televisheni kwa nchi zinazoongea Kifaransa. Kama hiyo haitoshi, wamepanua wigo na sasa wanatoa pesa hata kwa nchi zingine kama Tanzania.

Ndiyo maana, yeyote atakayeandika script yake ya filamu au kipindi cha televisheni na kuitafsiri kwa Kifaransa, atapewa udhamini wa maelfu ya Euro na ubalozi wa Ufaransa ili atengeneze.

Unaweza ukashangaa, kwa nini wanatoa udhamini kwa watengeneza filamu katika nchi zetu? Nadhani unaanza kupata picha kuwa sasa dunia imeingia kwenye vita ya utamaduni, ya kutawalana kiakili.

Utamaduni ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake. Hiyo inajumlisha ujuzi, imani, sanaa, maadili, sheria, desturi n.k. ambavyo mtu anajipatia kama mwanajamii.

Kama sifa maalumu ya binadamu, inayomtofautisha na wanyama, utamaduni ni suala la msingi, ukihusisha yale yote yanayopokezwa katika jamii fulani, kama vile lugha. 

Tunasahau kuwa sekta ya televisheni na sinema ni chombo muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika.

Ndiyo maana nchi za China, Korea au India zinaingia gharama kubwa za kutafsiri filamu na tamthilia zao kwa Kiswahili kisha kuzitoa zioneshwe bure katika vituo vyetu vya televisheni.

Kwa mfano, China kupitia Idhaa ya kiswahili ya CRI, ilifanya kazi ya kutafsiri tamthilia ya ‘Doudou na Mama Wakwe zake’ na kutia sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthilia hii kwa zaidi ya miezi 10, kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na Afrika ya mashariki.

Watazamaji wanavutiwa na vipindi vya nje kwa sababu vipindi vyetu havivutii na havina ubora unaokubalika kimataifa, vituo vya televisheni nchini vimechukulia hili kama fursa ya kuonesha vipindi vilivyotafsiriwa kutoka China, Korea na India kwa kuwa wanavipata bure (au kulipia pesa kiduchu).

Hivi hatujiulizi: kwa nini nchi za China na Korea wanaingia gharama kubwa za kutafsiri tamthilia zao kwa Kiswahili na kuzitoa zioneshwe bure kwenye televisheni zetu?

Kwa nini Sony Pictures au nchi ya Marekani hawataki kudhibiti filamu za Hollywood zinazorudufiwa kiharamia na kusambaa kila kona ya Afrika?

Au hatujiulizi kwa nini India nao wameruhusu filamu zao zitafsiriwe Kiswahili na kuuzwa kwenye nchi zetu? Ni kwa sababu hii ni vita ya utamaduni, ya kutawalana kiakili.

Hivi tunaandaa taifa (kizazi) la aina gani? Kwa mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani wa utamaduni? Tuamke, huu ni mkakati maalumu wa kujenga jamii itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje, na hivyo kutawaliwa kiakili.
Nadhani tunajenga jamii ya watu waliochanganyikiwa. Hatulioni sasa ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu.

Tunaona vichupi vya vijana wetu kwenye video za miziki zinazooneshwa kwenye vituo vyetu vya televisheni, utazuiaje hizo wakati vituo hivyo vinarusha video za nje zenye vichupi?

Ukiangalia kwa makini, hata mfumo wa utangazaji katika baadhi ya vituo vya Redio na Televisheni umeigwa kutoka Magharibi, kitu kinachotoa taswira ya kuua suala la ubunifu na kubaki watupu tusio na kitu chochote.

Bahati mbaya sana katika dunia hii ya vita ya utamaduni, ukitaka kupata fedha nyingi kwa urahisi basi fanya jambo linalodhalilisha utamaduni wako au taifa lako au fanya jambo linalotukuza utamaduni wa mataifa ya Magharibi.

Kwa sasa, katika tasnia ya muziki na filamu, Watanzania tumebakiwa na kitu kimoja tu tunachoweza kujivunia kwamba ni chetu: lugha ya Kiswahili.

Lakini bahati mbaya ni kwamba lugha hii hata hivyo wasanii wetu hawaijui vyema, ndiyo maana si ajabu kukuta wakichanganya R na L, DHA na ZA n.k.

No comments: