Sep 25, 2013

Fursa muhimu kwa wasanii na wadau wa filamuJengo la Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam


Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, UDSM, kimeandaa kozi ya uandishi wa filamu. Ni kozi ya siku kumi itakayoanza tarehe 1 mpaka 11 Oktoba. Kozi hii imetangazwa magazetini wiki iliyopita. Huu ni ujumbe utakaosaidia kufikisha ujumbe kuhusu fursa hii kwa wadau mbalimbali. Kozi hii itafanyika kwenye jengo la Shule Kuu ya Biashara (UDBS) ikilenga kuwezesha uandishi wa miswada ya filamu kwa kupitia ngazi zote kama vile sanaa ya uandishi wa miswada ya filamu, maandalizi kabla ya kuandika, kanuni za uandishi na usanifu wa mswada wa filamu, na muundo wa andiko la filamu.

Gharama za kozi hii ni Tsh. 300,000 (laki tatu). Gharama hizo ni kwa mafunzo, vifaa, chakula na Certificate ya UDSM.

Bodi ya Filamu: Hatuhitaji kudhibitiwa bali kupimwa

Inye, moja ya sinema zilizoonja makali ya kudhibitiwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini


MAKALA ya wiki iliyopita iliyoonesha kupinga waziwazi uwepo wa Bodi ya sasa ya Ukaguzi wa Filamu kwa kuwa imerithi sheria za kibaguzi za mkoloni (censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika, imepokelewa kwa mitazamo tofauti sana na wasomaji wangu wengi. Wapo ambao walibainisha kuwa hawajaelewa namaanisha nini hasa na wengine wameonesha kutofautiana nami kabisa katika jambo hili.

Kauli ya: “…Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?” imeonekana kutumiwa na wasomaji wangu kama reference ya kupinga vikali kuwa nataka wasanii waachiwe kufanya watakavyo bila kudhibitiwa jambo linaloweza kuzidisha mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.

Sep 18, 2013

Ili kuongeza ufanisi: tupiganie Bodi Huru ya Filamu

 Kama wadau wa filamu tufikirie kutumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kama haya ya Dar es Salaam ambayo ni njia nzuri sana katika kujitangaza kitaifa na kimataifa


INASEMWA kuwa sekta ya filamu nchini kwa sasa imerasimishwa, jambo ambalo limekuwa haliniingii akilini kwa kuwa sijaona mfumo wowote unaotuashiria kwamba sasa tuko rasmi zaidi ya huu wa kulipa kodi kupitia stika za TRA. Hivi tumerasimishwa kwa Sera ipi hasa?

Sera ni hati muhimu inayoelezea thamani na kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni. Nimewahi kuandika kabla kuwa bila sera madhubuti ya filamu maendeleo katika sekta hii yatabaki kuwa ndoto hata kama viongozi wa serikali watatuahidi mambo makubwa kiasi gani. Lakini kwanini tuendelee kuongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya kupigania uwepo wa sheria?

Sep 5, 2013

Maadili na uandaaji wa filamu katika nchi zinazoendeleaElizabeth Michael maaruf kwa jina la Lulu katika pozi

IJUMAA ya wiki iliyopita nilialikwa kwenye ofisi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya mazungumzo ya kiofisi, kuhusu mustakabali wa sekta ya filamu nchini, hasa ikizingatiwa kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, chombo cha juu cha wadau wa filamu nchini, kinachopaswa kufanya kazi kwa ukaribu na Bodi ya filamu.

Hapo kwenye ofisi za Bodi, niliongea mengi na watendaji wakuu wa ofisi hiyo, chini ya uenyekiti wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, yaliyotufikisha katika suala la maadili katika filamu zetu ambapo aliwataja baadhi ya wasanii wanaokiuka maadili na hawako tayari kujikosoa hata pale wanapoelekezwa njia sahihi.