Sep 25, 2013

Bodi ya Filamu: Hatuhitaji kudhibitiwa bali kupimwa

Inye, moja ya sinema zilizoonja makali ya kudhibitiwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini


MAKALA ya wiki iliyopita iliyoonesha kupinga waziwazi uwepo wa Bodi ya sasa ya Ukaguzi wa Filamu kwa kuwa imerithi sheria za kibaguzi za mkoloni (censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika, imepokelewa kwa mitazamo tofauti sana na wasomaji wangu wengi. Wapo ambao walibainisha kuwa hawajaelewa namaanisha nini hasa na wengine wameonesha kutofautiana nami kabisa katika jambo hili.

Kauli ya: “…Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?” imeonekana kutumiwa na wasomaji wangu kama reference ya kupinga vikali kuwa nataka wasanii waachiwe kufanya watakavyo bila kudhibitiwa jambo linaloweza kuzidisha mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.

Lakini pia wapo wengi walionipongeza kwa kuliona hili, hasa katika kile nilichoandika kuwa tunahitaji bodi huru ya filamu chini ya wadau wenyewe kama ilivyo kwa Bodi ya Madaktari, Bodi ya Wakandarasi, Bodi ya Wahasibu na kadhalika ambazo zipo chini ya wadau wenyewe na kusimamia masuala yao ya kitaaluma.

Msomaji mmoja amenitumia ujumbe kunipongeza akisema kuwa hata yeye amekuwa haelewi mantiki ya kuwa na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu ambayo ni kitengo kidogo kwa ajili ya ukaguzi na udhibiti tu wa filamu ndani ya Idara ya Utamaduni, badala ya kuwa na Bodi ya Filamu yenye ‘mandate’ kamili katika kusimamia mambo yote ya filamu nchini.

Pia ameshangaa kuwa kama kweli hatuna sera ya filamu tumekuwa tukiendesha vipi shughuli za filamu nchini, kwa sheria zipi, kwani pasipo sera humaanisha hata sheria pia hakuna.

Nawashukuru walioliona hilo na kuelewa nilichomaanisha, lakini pia nawaeleza waliopingana nami kuwa nilichoandika wiki iliyopita ndicho nilichomaanisha. Na leo nauendeleza mjadala kwa ufafanuzi zaidi. Sitaki kuuma maneno;  hatuhitaji sheria za kutudhibiti katika filamu zetu bali kutupima. We don’t need to be censored, we need to be rated.

Udhibiti unapaswa ufanywe kwa vipindi vya TV, hii ni kwa sababu watoto wasikumbane na baadhi ya mambo yaliyopaswa kuoneshwa kwa watu wazima tu: mambo kama unyama wa wazi uliokithiri, vurugu, ngono, na mambo mengine yenye ukakasi (profanity) ambayo yanapaswa kuzuiwa (kudhibitiwa) yasioneshwe kwenye televisheni hasa wakati ambapo watoto huangalia TV.

Lakini kwenye filamu ni suala tofauti kabisa. Kwenye filamu hakuna ‘censorship per se’. Filamu zinahitaji kupimwa na kupangiwa daraja kulingana na maudhui, kwa kuwa mzazi ana ‘option’ ya kuamua kama atainunua kwa ajili ya familia yake au la. Suala la kwamba watoto wanaangalia filamu zenye ukakasi kwenye mabanda ya kuoneshea video si suala la mtayarishaji wa filamu, ni suala la waliopewa dhamana kushindwa kufanya kazi zao sawaswa.

Mfumo wa upimaji filamu umewekwa maalum kuainisha aina za filamu zinazofaa kuoneshwa kwa makundi tofauti ya watazamaji. Upimaji huo unaweza kuitwa Uainishaji, Tathmini au Upangaji Madaraja. Upimaji na upangaji madaraja ya sinema huwapa wazazi taarifa muhimu kuhusu maudhui ya sinema husika, na hatimaye ni juu yao kuamua kama sinema hiyo inafaa kwa familia zao.

Ieleweke kuwa ubongo wa mtoto mdogo ni kama kaseti tupu inayosubiri kurekodi matukio, hivyo, sinema huumba ulimwengu mpya kwa watoto kuchunguza na kujifunza, na unaweza kuwasaidia kwa kuhakikisha safari yao ina mtazamo chanya. Wasaidie watoto wako kuchagua sinema za kuangalia na jadiliana nao kuhusu maudhui. Imarisha na jenga maadili mazuri kupitia sinema kwa kukaa chini na watoto wako baada ya kuangalia na mjadili kile walichokiona. Wakati mwingine tumia sinema kama misaada ya kielimu na kubadilishana mawazo mapya.

Sinema zinaweza kuwafumbua macho watoto wetu kwa maeneo mapya, utamaduni na mawazo, na wazazi wana jukumu muhimu katika kuhakikisha kwamba wanajifunza mambo chanya yatakayowasaidia watoto wao. Hivyo wazazi wanahitaji kuamua iwapo sinema ni nzuri kwa watoto wao kuiangalia. Kutokana na kuelewa jinsi madaraja yanavyowekwa husaidia wazazi kutafuta sinema sahihi kwa watoto wao.

Mfumo wa kupanga madaraja kwa ajili ya makundi tofauti ya watazamaji ulianza kutumika Marekani mwaka 1968, kama mbadala wa Kanuni za Uzalishaji Filamu za Hays (William Harrison Hays, Sr. aliyekuwa mkuu wa Chama cha Watayarishaji Filamu Marekani “MPPDA”, 1922 hadi 1945). Kanuni za Uzalishaji Filamu za Hays zilitumika tu kutoa kibali cha ama kuikubali au kuikataa filamu, bila hata kupima maudhui ya filamu.

Kuwasilishwa kwa rufaa mara kwa mara za filamu zenye ukakasi kulikifanya Chama cha Picha Jongevu Marekani (MPAA), kwa kushirikiana na Chama cha Taifa cha Wamiliki wa Kumbi za Kuoneshea Sinema (NATO) na Waagizaji na Wasambazaji wa Kimataifa wa Filamu Marekani (IFIDA), kubuni mfumo mpya wa kuzipima na kuzipa madaraja ili kuwasaidia wazazi kuwalinda watoto wao. Mfumo huu ulihusisha madaraja manne ingawa sasa yapo matano.

Bodi ya Filamu ina wajumbe wa kudumu wanane hadi 13 na ni sehemu ya Uainishaji madaraja (Classification) na Upimaji (Rating). Hii ni Bodi Huru inayosimamiwa na wadau wenyewe (si ya serikali), ambapo Rais wa MPAA huteua mwenyekiti wa Bodi ingawa baadaya ya kuteua hana mamlaka yoyote juu ya maamuzi yatakayotolewa na bodi. Wajumbe wa Bodi hutoka katika maeneo mbalimbali, lakini wenye uzoefu katika mambo ya malezi ya watoto ili waweze kuziangalia sinema kwa mtazamo wa mzazi/mlezi. Wajumbe wa Bodi huangalia kila filamu iliyowasilishwa kwao kwa umakini, huitathmini kwa usahihi kila mmoja kwa nafasi yake (individually), kisha hujadiliana na kupiga kura juu ya daraja gani filamu inapaswa kupewa.

Kisha Bodi humpa mtayarishaji wa filamu hiyo majibu ya uamuzi wao pamoja na maelezo, endapo atayahitaji. Kama mtayarishaji hatafurahishwa na daraja iliyopata filamu yake, anaweza kuihariri upya na kuiwasilisha tena kwenye Bodi, au anaweza kukata rufaa juu ya uamuzi wa bodi. Katika kesi hii, Bodi ya Rufaa, ambayo ina wataalam 14 hadi 18 wa sekta ya filamu, watasikiliza hoja za pande zote na kupiga kura kama wanaweza kubadili uamuzi wa Bodi. Maamuzi yanaweza tu kubadilishwa kwa theluthi mbili ya kura.

Mchakato wa upimaji filamu kwa kiasi kikubwa ni wa upande mmoja (subjective). Bodi hupima na kutoa madaraja yenye alama za G, PG, PG-13, R na NC-17 kama ilivyoainishwa:

G - "General Audience” – Imekubalika kwa watu wote: daraja hili hutumika pale sinema inapokuwa haina matukio yoyote ya unyama wa wazi uliokithiri, utupu, ngono au mambo mengine yenye ukakasi. Au kama matukio ya vurugu ni machache na maudhui yanafaa kwa watoto wadogo. Lakini daraja G halimaanishi kuwa ni filamu ya watoto.

PG - "Parental Guidance” – Mwongozo wa Wazazi: Ni daraja linaloelezea kuwa baadhi ya picha zinaweza zisifae kwa Watoto wadogo: Bodi hutumia daraja hili wakiamini kuwa filamu ina maudhui ambayo pengine wazazi watapima wenyewe kama yanafaa kwa watoto wadogo. filamu inaweza kuwa na baadhi ya vipande vyenye lugha chafu, vurugu na kadhalika, lakini katika kiwango kidogo mno.

PG-13 "Parents Strongly Cautioned” – Onyo kwa Wazazi kuwa baadhi ya matukio kwenye sinema si Muafaka Kwa Watoto Chini ya Miaka 13. Daraja hili limeongezwa na MPAA mwaka 1984 kuashiria kuwa filamu ina matukio ya vurugu, lugha chafu au maudhui yasiyofaa kwa watoto chini ya umri huu, ambapo wazazi wengi wasingependa kuyaonesha kwa watoto wao wadogo, lakini si yenye ukakasi mkubwa kiasi cha kupewa daraja R.

R - " Restricted” – Bodi hutumia daraja hili ambalo wajumbe wake wanaamini sinema ina matumizi makubwa mno ya maudhui yenye ukakasi. Katika baadhi ya majimbo ya Marekani, umri wa chini ya kuangalia sinema yenye daraja R ni miaka 18.

NC-17: "No One 17 and Under Admitted": daraja hili asili yake ni daraja X, hutumika kwa filamu ambazo si muafaka kabisa kwa watoto. Huonesha kuwa maudhui yake ni ya ukakasi zaidi kuliko katika daraja R. haipaswi kuoneshwa kwa watu chini ya miaka 18.

Sasa utaona kuwa filamu bado inatoa ‘option’ kwa wazazi na watazamaji, Bodi tuliyonayo imekuwa ikikagua na kuzuia maonesho ya filamu za Kitanzania tu kwa kisingizio cha utamaduni wetu lakini imekosa ‘meno’ kwenye filamu na tamthilia za nje zinazorushwa kwenye vituo vya televisheni jambo ambalo ni hatari zaidi kwa watoto wadogo.

Alamsiki.

No comments: