Feb 23, 2011

Utamaduni wa Mtanzania ni upi, na unahusishwaje na filamu zetu?

 Filamu iliyozua utata ya Shoga

 Filamu ya Off Side

KWA kweli suala la mila na utamaduni wa Mtanzania linatatiza sana. Tunaposema utamaduni na mila za Watanzania hasa tunamaanisha nini kwa Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake? Huu utamaduni na mila za Watanzania ni upi hasa?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo kila mtetezi wa mila na utamaduni ndani ya jamii za Kitanzania anapaswa kuyajibu. Vinginevyo tutakuwa tukiimba wimbo tusioujua maana yake, na hii haitatusaidia kufikia malengo tunayoyapigania.


Siku za hivi karibuni kulifanyika uzinduzi wa filamu ya Shoga ambayo kabla haijaingia sokoni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilibidi iingilie kati kwa kuiagiza Kampuni ya kutengeneza filamu ya Al-Riyamy Production Company kuiwasilisha filamu hiyo kwa Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi.
 
Tukio hilo limefuatia baada ya watu wengi wakiwemo baadhi ya waandishi wa habari kuilalamikia filamu hiyo hata kabla hawajaiona wakidai kuwa inapotosha maadili na haiakisi utamaduni wa Watanzania. Naomba niweke wazi, makala yangu haikusudii kuendeleza mjadala kuhusu filamu hiyo bali ieleweke kuwa sakata hilo ndilo lililonifanya kuibua mada kuhusu utamaduni wa Watanzania.

Utamaduni ni neno lenye asili ya Kilatini “Cultura” ambalo lina usuli wake katika neno colere, linalomaanisha “kulima”. Neno hili lina fafanuzi nyingi. Kwa mfano, mwaka 1952, Alfred Kroeber na Clyde Kluckhohn walikusanya orodha ya vielelezo 164 vya neno “utamaduni” katika kazi yao: Culture: a Critical Review of Concepts and Definitions.

Hata hivyo, neno “utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:
-Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vilevile hujulikana kama utamaduni wa juu
-Mkusanyiko wa maarifa ya kibinadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kiishara
-Ni jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi fulani.

Dhana hii ilipoibuka kwanza katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa barani Ulaya, ilimaanisha mchakato wa kulima au kuboresha kilimo au kilimo cha mboga. Katika karne ya kumi na tisa dhana hii ilimaanisha kuboreshwa kwa mja kupitia elimu na hali kadhalika ilimaanisha kutekelezwa kwa maazimio ya kitaifa au maadili.

Katikati mwa karne ya kumi na tisa, wanasayansi wengine walitumia dhana ya utamaduni kurejelea uwezo wa kiubia wa binadamu.

Katika karne ya ishirini, “utamaduni” ilijitokeza kama dhana ya kimsingi katika somo la Anthropolojia. “Utamaduni” ulihusisha mambo yote yaliyomhusu binadamu ambayo hayakufungamana na matokeo ya kimaumbile. Dhana ya utamaduni katika Anthropolojia ya Kimarekani ilikuwa na maana mbili: (1) Uwezo wa kibinadamu wa kuainisha na kuwasilisha tajiriba za kibinadamu kiishara na kutenda mambo kiubunifu; na (2) Namna mbalimbali watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni huainisha na kuwasilisha tajiriba zao za maisha na kutenda mambo kiubunifu.

Kufuatia vita vya pili vya dunia, dhana hii ilipata umaarufu ingawa na fafanuzi tofauti tofauti katika taaluma kama vile sosholojia, Mafunzo ya utamaduni, saikolojia ya mipangilio na mafunzo ya usimamizi.

Leo hii tukiwa tunaelekea miaka 50 ya Uhuru wetu hapo Disemba 9, jamii ya Kitanzania inaonekana kupoteza mila na tamaduni zake kila kukicha.

Utata unaojitokeza kuhusu neno utamaduni wa Mtanzania, binafsi nadhani kuwa utamaduni tunaoweza kuuita wa Watanzania unamaanisha lugha ya Kiswahili, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi, ujenzi wa nyumba na tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika).

Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo kikuu cha ndani cha jamii yetu. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.

Ikumbukwe kuwa mara baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962. Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.


Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.

Pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwenye jamii yetu lakini bado sera ya utamaduni hapa nchini imekuwa haipewi nafasi katika serikali hii tangu ilipoanzishwa wizara inayoshughulikia masuala ya sanaa. Tangu mwaka 1962 shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi.

Ingawa mimi si mtu wa imani ya kiroho lakini naamini kuwa hali ya mtu kujitenga na tamaduni asilia kunaweza kuwa tishio katika kupokea hata imani ya kidini. Hii inatokana na ukweli kwamba imani ambayo mtu aipokeayo kama zawadi toka kwa Mungu ina msingi wake katika mila na desturi tuziishizo. Hakuna uwezekano wa kuwa na imani ya kidini iwapo mtu hakujengeka katika utamaduni wa kweli. Ni katika tamaduni zetu ndipo tunapata maana ya utu, upendo na kadhalika.

Hatari kubwa ya kupotea kwa tamaduni asilia inatukumba sana vijana ambao bila kujua huwa tunajikuta katika utamaduni hasi unaotusukuma kudharau tamaduni zetu na kujiingiza katika mienendo ambayo kwa kiasi kikubwa si tamaduni ila vurugu zinazotokana na kukosekana kwa tamaduni.


Hii inajionesha hasa katika sanaa zetu na hasa filamu tunazoziandaa ambazo nyingi zinajengwa katika misingi isiyo na maana katika jamii. Uigaji usio na uchambuzi umetupelekea kukosa kabisa vipaumbele katika maisha yetu, na kubaki kuwa bendera kufuata upepo.

Filamu zisizo na maadili si zile zenye majina yanayoashiria mmomonyoko wa maadili tu kama ilivyo kwa filamu ya Shoga, ambayo mbali na jina lake kama utabahatika kuitazama kwa kweli utakubaliana nami kuwa mambo yanayolalamikia na watu wala hayajaoneshwa kabisa, iko tofauti kabisa na filamu zenye majina mazuri yasiyoashiria mmomonyoko wa maadili lakini maudhui yake hukosa kabisa maadili.

Katika hili watu wameingia katika mkumbo wa wengi kuhukumu jina la kitabu zaidi ya vilivyoko ndani. Sijui hapa tunalalamikia jina au maudhui yaliyomo ndani ya sinema? Na kama ni maudhui, je hizi zenye majina mazuri lakini hadithi zake zinakosa maadili zinaziongeleaje? Mbona Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo haijawahi kuagiza zipelekwe Bodi ya Taifa ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya ukaguzi?
 
Ninachoamini ni kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, jambo hili linaonesha umuhimu wa utamaduni si kitu kilichoibuka tu.

Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.


Sanaa yetu ya filamu imesahaulika kabisa, na tumepokea ile ya nje tena kwa fujo, hali hii imesababisha Watanzania kuwa wafuatiliaji na waigaji wa filamu za nje badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili filamu zetu ziende na matakwa ya dunia kwa kuziboresha.

Sasa ni wakati muafaka wa kujaribu kufikiria na kuchambua kila tunapoiga mambo ya kigeni iwapo yana mchango wowote katika makuzi ya tamaduni zetu au yanakuwa chanzo cha kuziangamiza. Hatuna budi kuelewa kwamba kuanguka kwa tamaduni ni anguko letu pia.


Tunapaswa kuiga hekima na busara za wenzetu waliondelea na kuacha yale yasiyofaa ambayo yanatupotosha. Ni wakati sasa wa kuyatenda yale tunayoyahubiri na kuacha propaganda zisizotusaidia kuboresha kazi zetu.

Alamsiki

No comments: