Feb 25, 2011

Kwaheri Tabia wa Kidedea

 
Tabia alipokuwa akiigiza katika filamu ya Usiku wa Taabu
 Tabia alipokuwa akiigiza katika filamu ya Naomi

HAMISI KIBARI
Dar es Salaam

CHRIS Magori, mwandishi wa miongozo ya filamu (script), mtunzi na muongozaji (director), aliipenda hadithi niliyowahi kuiandika katika gazeti la Nipashe miaka ya nyuma ikiitwa 'Usiku wa Taabu'. Aliipenda hadithi hiyo kwa maana ya kuifanya filamu. Wakati huo, mwaka 2004, tasnia ya filamu ilikuwa inazidi kushika kasi nchini mwetu, lakini si kwa kiwango cha sasa.

Katika hadithi hiyo niliyoiandika kutokana na kisa cha kweli, mhusika mkuu ambaye ni mke wa mchungaji, alikuwa na tabia isiyoendana kabisa na hadhi yake. Kwa lugha nyingine alikuwa mhuni ambaye alidiriki kwenda gesti na wanaume hususan mumewe anapokuwa katika safari za kichungaji.

Katika tukio moja, mke huyo wa mchungaji aliwahi kwenda gesti na mmoja wa mume wa marafiki zake, tukio ambalo mwenye mume sambamba na mdogo wa mchungaji, yaani shemeji mtu waliandaa fumanizi.

Wakafuatilia hadi gesti alikoingia mwanamke huyo na hawara yake. Katika tukio hilo, mke wa mchungaji alilazimika kukimbia nje na mashuka ya gesti baada ya chumba alimokuwa na mume wa mtu kuvamiwa na shemejie pamoja na mke wa mwanaume aliyekuwa naye ambaye pia ni rafiki yake.

Katika tukio hilo, mchungaji ambaye alikuwa akimpenda sana mkewe, licha ya kusikia kwamba alikuwa anasumbuliwa na pepo wa ngono, alirejea na kumkuta mkewe akiwa hospitali, lakini kwa mshangao wa wengi akaamua kumsamehe akionesha pia uchamungu wa hali ya juu.

Baada ya Magori kuandika script na kuanza kusaka wasanii wa kucheza sinema hiyo, kazi kubwa ilikuwa ni kumpata mhusika mkuu, yaani atakayekuwa mke wa mchungaji.

Wasanii wengi waliopatikana, licha ya kuigopa nafasi hiyo kutokana na ukubwa wake, walionekana pia kutoitaka hasa kutokana na kuhusisha fumanizi la gesti na mhusika kukimbia nje na mashuka ya gesti. Kwa lugha nyingine wasanii waliopatikana waliinyanyapaa nafasi hiyo au naweza kusema tulio nao wengi ni aina ya wasanii wanaotaka kucheza sehemu wanazoonekana vizuri mbele ya jamii, na si sehemu ambazo wanadhalilika mbele ya macho ya Watazamaji. Tulio nao ni wasanii ambao wameshindwa kujua kwamba mtu anapocheza nafasi fulani kwenye filamu ama maigizo, anachofanya ni kuwakilisha yule mhusika aliye kwenye hadithi na si yeye binafsi. 
 
Baada ya wahusika waliokuwa wamepatikana kuiogopa nafasi hiyo, ndipo likatolewa wazo kwamba msanii anayeweza kuimudu, akavaa uhusika na kuicheza bila wasiwasi ni wa kutoka Kundi la Kidedea (sijui kama bado lipo), Dalila Peter Kisinda, aliyekuwa akijulikana zaidi kwa jina la usanii la Tabia.

Naam, msanii huyo alitafutwa na alipoambiwa kushiriki nafasi hiyo aliipokea kwa mikono miwili na kuifurahia.

Ni wakati wa mazoezi ya filamu hii ambapo mimi mwandika makala haya niliigiza kama mchungaji, yaani mumewe, nilipokutana na Tabia kwa mara ya kwanza. Hakuchelewa kunizoea na tukafanya vyema katika filamu hiyo kwa mujibu wa muongozaji, Magori.

Nilichogundua muda wote wa mazoezi yetu hadi kuitengeneza picha hiyo ni kwamba Tabia alikuwa na sifa zote za msanii mzuri. Alikuwa hachagui nafasi ya kucheza na alijitahidi sana kuvaa uhusika. Lakini kubwa kuliko yote nililoligundua kwake Tabia alikuwa mcheshi sana na mkarimu. Wengine ambao hawakupata bahati ya kuwa naye karibu wanaweza kudhani kwamba ucheshi wake ulikuwa ni wa kwenye sanaa tu, la hasha. Ni mcheshi kwa asili. Hata alipoamua kutega mazoezi Tabia alitumia pia usanii na utundu ili kufanikisha hilo.

Ninakumbuka siku moja alikuwa anataka atege mazoezi na alichokifanya, kwa sababu alikuwa na simu mbili, alijipigia, akahakikisha kwamba mlio ameusikia kila mtu akiwemo mwalimu Magori aliyekuwa akisimamia mazoezi kisha akapokea akijifanya anaongea na mtu anayemjulisha kwamba kuna tatizo la haraka nyumbani na anatakiwa.

Magori, aliamini ni kweli na kumruhusu Tabia kuondoka na huku nyuma aliacha kicheko baada ya wasanii wenzake kugundua kwamba Tabia alijipigia simu ile ili kupata ruhusa na kwamba alikuwa anaongea na simu ambayo haipo!

Hivi karibuni, baada ya kukaa mbali na masuala la filamu kwa muda mrefu kutokana na kubanwa na shughuli nyingi, niliamua tena kurejea kwenye filamu baada ya kuletewa hadithi nzuri iliyoandikwa na Winfrida Thomas.

Wakati mimi na Bishop John Hiluka tunajadili watu wa kushiriki kwenye filamu hiyo iitwayo Naomi, nilitoa pendekezo kwamba Tabia naye awemo na nikaamua kumtafuta. Kwanza nilikuwa ninashangaa kutomuona katika filamu nyingi zinazotoka. Nikawa ninajiuliza maswali, kwa nini inakuwa hivyo. Je, alikuwa ameachana na masuala ya filamu baada ya kuolewa?

Lakini mimi nilikuwa bado ninakumbuka uwezo wake wa kuigiza, ucheshi na ukarimu wake. Nilimtafuta na kumpata, akaniambia alikuwa yuko tayari kushiriki.

Sijaacha fani, bali majukumu tu yamenikabili, lakini nitajitaidi kutenga muda wangu nishiriki hiyo sinema,” alinijibu.

Naam, filamu hiyo tumeshaifanya na ingekuwa imeshatoka kitambo kama si kutofautiana kuhusu malipo na wasambazaji.

Katika hali ya kushangaza, wiki ambayo tumeanza mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaitoa filamu hiyo, ili watu wapate kumuona Tabia makali yake katika fani hii katika siku za karibuni, ndipo nikapata habari kwamba msanii huyo amefariki dunia.

Mimi ni mmoja wa watu ambao nimesikitika sana na mbaya zaidi nimepata habari huku Tabia niliyemheshimu sana katika fani akiwa keshazikwa na mbaya zaidi hakuwahi kuiona filamu hiyo aliyoshiriki kuicheza na inayotarajiwa kutoka punde.

Ni masikitiko kwangu kwani, baada ya kuamua kurudi kwenye filamu na michezo ya kuigiza baada ya kukaa nje kwa kipindi kirefu kidogo, nilimtegemea Tabia kuendelea kuwa mmoja wa washiriki muhimu katika filamu zinazotokana na hadithi zangu.

Lakini ndivyo mapenzi ya Mungu yalivyo. Yeye amempenda zaidi. Ninamuomba Mwenyezi Mungu amuondolee madhambi yake na kumlaza mahala pema kwani yeye ametangulia tu.

Ina Lillahi, wa ina ilaihi Rajiuun.

No comments: