Mar 2, 2011

Tutafakari kabla ya kusema au kutenda, ili kudumisha maadili

 Anti Ezekiel na Steven Kanumba katika moja ya filamu walizoigiza

 Flora Mvungi, mmoja wa waigizaji maarufu wa kike

MAKALA yangu ya wiki iliyopita; Utamaduni wa Mtanzania ni upi...” imeibua mjadala nisioutarajia kutoka kwa wasomaji wa makala yangu, mjadala uliopelekea baadhi yao kusema kuwa makala yangu haikuwa wazi sana kuhusu suala la filamu ya shoga huku wakiwa hawajui nini msimamo wangu kuhusu filamu hiyo, na wengine wakielekeza lawama zao kwenye Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza kuwa haifanyi kazi zake ipasavyo.

Si nia ya makala hii kuendeleza malumbano na kumtupia lawama mtu au taasisi fulani, lakini nadhani nina wajibu kukemea au kuelekeza yalipo mapungufu, na ninaamini kuwa yapo mambo kadha wa kadha ambayo yanahitaji mjadala wa kina ili tupate ufumbuzi kuhusu kile kinacholalamikiwa na jamii kuhusu sanaa yetu.


Mojawapo ya mambo yaliyonisukuma kuandika makala hii ni ujumbe wa wasomaji wawili, mmoja akiandika kuwa, ule usemi wa msanii ni kioo cha jamii hivi sasa umekosa maana kwa kuwa wasanii waliopaswa kuwa mfano wa kuigwa na jamii kwa mazuri wanayopaswa kufanya hivi sasa wamepotoka.

Kwa maana nyingine, umuhimu wa wasanii ni katika suala zima la kuwaonesha wananchi njia nzuri ya kupita, hasa katika dunia ya sasa ya utandawazi, na haamini kuwa wasanii wetu wanapaswa kuendelea kuitwa kioo cha jamii, kwa kuwa wamepoteza dira.
 
Msomaji mwingine aliniandika kuwa hivi sasa kuna wimbi kubwa la vijana wanaojihusisha na mambo ya sanaa ambao hujikuta wakiwa katika matatizo ya kimaadili. Kwa mujibu wa msomaji, hii ni hali inayotia doa kabisa fani hii nzuri na vipaji walivyojaaliwa wasanii wetu na Mwenyezi Mungu. Hali hii inapelekea jamii kukosa hata thamani kubwa iliyomo katika sanaa wanazowakilisha ikiwa ni pamoja na matatizo ya kimaadili miongoni mwa wasanii kuingilia kabisa imani ya jamii si kwa wasanii tu bali kwa ulimwengu mzima wa vijana.
 
Kuna mambo kadhaa nakubaliana nayo, hasa kwenye hoja zilizo makini za msomaji wa pili niliyemnukuu, lakini sikubaliani na tafsiri iliyotolewa na msomaji wa kwanza na wengine wengi ambao sijaandika hoja zao kwa kuwa zinalenga kukivunja kioo chetu ili tusiuone ubaya wa sura zetu.

Mimi naamini kuwa wasanii bado ni kioo cha jamii, maneno yanayotokana na tafsiri ya maneno ya Kiingereza “Artists are the mirror of the society”, usemi uliozoeleka sana katika vyombo vya habari na hata baina ya wasanii wenyewe, na ninaamini kuwa msanii asiyeitafsiri jamii yake hujikuta yuko peke yake akiwa hana wapenzi wala washabiki.
 
Siku zote wasanii wataendelea kuwa kioo cha jamii na haya yote yanayoendelea katika filamu zao yanaonesha zao halisi la jamii yetu ilivyo kwa sasa. Kitendo chochote cha kuukana ukweli na kuwabeza kwa maneno haya na yale ni sawa na kukataa kutumia kioo jambo ambalo si njia ya kubadili ubaya wa sura zetu.

Naamini kuwa tatizo tulilonalo hapa si wasanii wala kazi zao, kwani wao ni sehemu tu ya jamii hii, tatizo lililopo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii nzima. Siku zote nimekuwa nikijiuliza swali hili; kwa nini tunapenda kuwa wanafiki kwa kukataa yale tunayotenda na kuhubiri tusiyotenda? Nadhani kila mmoja kabla hajataka kutoa kibanzi kwenye jicho la msanii ni bora kwanza kutazama boriti ndani ya jicho lake.

Nilishaweka bayana msimamo wangu kuwa sitaki kuwa mnafiki, na sitakuwa mnafiki katika hili hasa kwa vile hadi sasa sielewi kabisa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza inafanya nini ili kuinusuru tasnia ya filamu. Sijui huwa wanakagua nini? Hivi tunapowalaumu wasanii wetu na hadithi zao kwa kisingizio cha 'huu si utamaduni wetu' lakini wakati huohuo tunaruhusu vituo vyetu vya televisheni vioneshe filamu zenye maadili ya Kimagharibi saa 24, tunaashiria nini?
 
Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ambayo imeundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 1976. inabainishwa kuwa na majukumu yafuatayo:
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza inawajibika na kuwiana na kawaida, mila, desturi na maadili mema ya Tanzania;
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza inatoa burudani yenye mafunzo mema na safi kwa Watanzania;
-Kuhakikisha upangaji wa madaraja ya maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza unalingana na mabadiliko ya maadili mema ya jamii ya Watanzania;
-Kuhakikisha usanii na uhuru wa ubunifu wa sanaa hauzuiliwi bila sababu za msingi;
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza, nchini Tanzania, inakuwa na viwango vinavyostahili vya usanii;
-Kuafiki, kuzuia au kudhibiti maonesho na usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza;
-Kuamuru kuondolewa kutoka kwenye filamu au mchezo wa kuigiza uliowasilishwa kwenye Bodi Kuu ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza sehemu yoyote ambayo Bodi Kuu haiafiki kwa maonesho au usambazaji kwa Watanzania;
-Kuafiki, kuzuia au kudhibiti utangazaji kwa umma unaohusiana na filamu au michezo ya kuigiza;
-Kukagua na kupanga madaraja ya filamu na michezo ya kuigiza.
-Kukagua na kutoa vibali kwa maeneo yote yanayotumika kwa maonesho na usambazaji wa filamu au michezo ya kuigiza.
-Kuafiki na kutoa vibali kwa shughuli za usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza
-Kuafiki na kutoa vibali kwa maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza.

Naomba nieleweshwe, katika majukumu haya yaliyoainishwa bodi inafanya yepi hadi sasa? Je, imeshakagua, kupanga madaraja au kuzuia filamu ngapi hadi sasa? Naomba ieleweke, jambo la maadili haliwahusu wasanii tu, bali jamii yote ambayo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, kazi ya wasanii inakuwa kielelezo cha tunu bora zinazofumbatwa katika maisha yetu: kiroho na kimwili; kimaadili na utu wema. Lakini inaonekana kuwa jamii na viongozi tuliowapa dhamana kuongoza taasisi hii wanajitoa kwenye jukumu hili na kutupa lawama kwa wasanii.

Ikumbukwe kuwa mbali ya uandishi, mimi pia ni tabibu (Medical Personnel) niliyefuzu. Katika somo la Psychiatry (matatizo ya akili) ambalo nikiri kuwa nililimudu sana kiasi cha kupewa tuzo, kuna kitu kinaitwa 'mental machenism' ambacho ni aina ya mfumo wa ulinzi wa kisaikolojia au mbinu inayosaidia kupunguza msongo au mhemko ili kujifariji, kwa mfano, ukandamizaji, nk.
 
Katika mfumo huu kuna aina nyingi za mental machenism, mmojawapo ni hii inayoitwa “displacement”; kitendo cha kupenda kuhamishia lawama kwa mtu mwingine hata kama unachokilaumu kinatokana na wewe mwenyewe: Kwa mfano mwanafunzi aliyefeli mtihani hujifariji kwa kusingizia kuwa mwalimu alitunga mtihani mgumu ili kumkomoa.
 
Tunapaswa kuacha kutupiana lawama na badala yake tutambue kuwa utajiri wa maisha na vipaji vya wasanii unapaswa kuwa sehemu ya ushuhuda kwa jamii, ili kuuwezesha ujumbe wao kuwagusa na hatimaye kuleta mabadiliko kwa hadhira inayokusudiwa.

Hatupaswi kuendelea kuzihamishia lawama zetu kwa wasanii bila kuelekeza njia bora ya kufanya, bali tunapaswa, bila unafiki wowote kuendelea kukuza vipaji vyao ambavyo vinahitajika sana katika kuelimisha jamii. Lakini pia tuna jukumu la kutoa tahadhari kwa wasanii wetu, kutoishia katika usanii tu, bali kuchukua nafasi ya kwanza kabisa katika kuhakikisha kuwa kile wanachokiwakilisha katika jamii kiwe msingi na changamoto ya maisha yao katika jamii.

Nimewahi kuandika kuhusu nchi zilizoendelea kuwa na mfumo unaotengenezwa kulinda na kuendeleza maadili na kazi za ndani ya nchi husika ili jamii iishi ikiwa ina aina ya maadili ya nchi husika. Vyombo vya kurusha matangazo katika nchi hizo huwa na asilimia iliyopangwa ya matangazo “local content” ili kulinda kazi na maadili ya ndani.
 
Jambo hili huwafanya wasanii kutumia kikamilifu vipaji vyao kwa ubunifu na tija, wakiendelea kusimama kidete kulinda na kutetea maadili mema ndani ya jamii ili wasiwe chanzo cha maporomoko ya kimaadili. Kwa maana hiyo, kuendelea kutoa lawama kwa wasanii bila kutafuta suluhisho kunatufanya kuwa na changamoto kubwa ya kutafakari kabla ya kusema au kutenda.

Tunapaswa bila ushabiki kuangalia umuhimu wa kazi za sanaa katika maisha yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba kumekuwa na wimbi kubwa la vijana kujiingiza katika kazi mbalimbali za sanaa katika sehemu mbalimbali nchini.

 
Serikali imeachia utamaduni wetu uendeshwe na wafanyabiashara wachache kwa manufaa ya wachache, imeshindwa hata kuwekeza katika sekta hii ili kuweza kufufua na kukuza maadili na utamaduni wa Watanzania ambao unakoelekea kwa sasa tunauona kupitia wasanii na kazi zao (tunazozilalamikia) ambao kwa kuwazuia haitusaidii kubadili mwelekeo wa maadili ya jamii.

Kutokana na sanaa hii wasanii wamekuwa na mchango mkubwa kabisa katika kurekebisha na kukemea maovu katika jamii. Hali hii inapaswa kupongezwa na kutiwa moyo.

Kila msanii ana wajibu wa kukumbuka kuwa sanaa ni kioo cha jamii. Na kama sisi vijana ndiyo tuliokabidhiwa dhamana ya kuendeleza fani hii basi hatuna budi kuwa mstari wa mbele kuyaishi yale yote yanayojitokeza katika fani hii ya sanaa.


Kinachotakiwa sasa kwa wadau wote wa tasnia hii ni kutafakari kabla ya kutenda na tuache unafiki. Katika hali hii ya tafakari matokeo ya kila tunachokusudia kutenda yako wazi kabisa mbele yetu.

Naomba kuwasilisha

No comments: