Mar 23, 2011

Bodi ya Ukaguzi wa Filamu inafanya nini kuinusuru tasnia ya filamu?

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo George Mkuchika 
katika picha ya pamoja na viongozi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu mara baada ya uzinduzi. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bi. Rose Sayore.

 Msanii Hisani Muya maarufu kwa jina la Tino 
aliyecheza filamu ya Shoga iliyoleta tafrani

MAJUZI jamaa zangu ambao ni watayarishaji wa filamu za Kibongo walinikumbusha jambo la msingi sana ambalo nahisi napaswa kuliandikia makala, jambo ambalo kwa mtu asiyefahamu anaweza awashangae sana hasa pale walipoonekana kutoijua kabisa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.

Lakini si wao tu bali watayarishaji na wasanii wengi niliowahi kukutana nao hawaijui, si kwa makusudi bali ndiyo hali halisi ilivyoachwa iwe.

Maongezi ya juzi yaliyopelekea kuiongelea Bodi ya Ukaguzi wa Filamu yaliibuliwa na mdau mmoja kufuatia ucheleweshwaji wa taarifa za ukaguzi uliofanywa na bodi hiyo kuhusu filamu ya Shoga ambayo ilizuiwa kuingia madukani baada ya Bodi hiyo ya filamu kutoa tamko kuwa filamu hiyo isiingie sokoni hadi pale itakapokaguliwa ili kujiridhisha kama inafaa kuoneshwa au la.

Hakika filamu ya Shoga imekuwa gumzo kubwa sana kwa wadau wa filamu mitaani hasa kutokana na bodi hii kuizuia ili kwanza ikaguliwe, lakini binafsi sioni cha ajabu katika filamu hii kwani ni ya kawaida tu. Huwezi kuilinganisha na filamu zingine nyingi zilizopo madukani ambazo licha ya kuwa na majina mazuri lakini zina maadili mabaya mno.

Si kwamba naipigia debe filamu hii la hasha, lakini naamini kuwa kila mtu anahitaji ukweli kuhusu filamu ya Shoga, na swali hapa ni maadili yapi yanayokusudiwa katika filamu hii? Naamini hakuna kitu kibaya ambacho kimefanywa kwa filamu hii kiasi cha kuzuiwa kwa ajili ya kulinda maadili ya Watanzania ili eti jamii isije ikapotea kupitia filamu hii.

Siyo siri huku mtaani walipo wasanii na wadau wa filamu, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu si maarufu kama ilivyo Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (Cosota) ambacho wengi wanakijua, kwani Cosota pamoja na mapungufu yake imekuwa ikijitahidi kukutana na wadau na kutoa elimu kuhusu hakimiliki. Lakini chombo hiki kinachoitwa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu sijui hata kama kimewahi kuwa na mikakati ya kukutana na wadau wa filamu ili kutoa elimu.

Naamini kuwa tatizo lililopo hapa si watayarishaji wala wasanii kubeza au kutojua umuhimu wa kazi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu, tatizo lililopo hapa linasababishwa na kutokuwepo maadili ya kazi au kuzingatia weledi ndani ya bodi yenyewe kwa ajili ya mustakabali wa tasnia nzima.

Ninapatwa wasiwasi kidogo kuhusu watendaji wa chombo hiki, sidhani kama kimejumuisha wanataaluma waliobobea katika filamu na utaalamu wa aina mbalimbali katika sekta ya filamu na televisheni, au wanaokiongoza wamewekwa kisiasa.

Kwa watu wanaozingatia weledi katika bodi ya ukaguzi wa filamu wangeweza kuwakilisha vyema mbinu na mikakati sahihi kwa niaba ya serikali ili kusaidia kujenga mazingira ambayo yanaendelea na kudumisha sekta ya filamu na video, ndani ya nchi na kimataifa. Pia lazima wangejua tatizo la msingi linalowakabili wahusika, na kuangalia maslahi kwa pande zote zinazohusika na biashara ya filamu.

Nasema haya kwa kuwa mimi mwenyewe nimewahi kushiriki katika utayarishaji wa filamu kadhaa, filamu ambazo kabla ya kuingizwa sokoni huwa zinatangazwa sana kwenye magazeti na vituo vya televisheni, lakini hata siku moja sijawahi kuwaona watu wa bodi ya ukaguzi wa filamu kufuatilia filamu hizi ili kuzikagua kabla hazijatoka.

Mara kadhaa nimekuwa nikijiuliza; nini majukumu ya Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza? Je, bodi hii inafanya nini ili kuinusuru tasnia ya filamu katika kazi zetu nyingi ambazo zimeonekana kukosa kabisa maadili? Hivi huwa wanakagua filamu kweli? Je, ukaguzi wao unaishia kwenye sinema zinazopigiwa kelele tu kwa kisingizio cha 'huu si utamaduni wetu' au wanakagua hata filamu/michezo ya nje yenye maadili ya Kimagharibi inayorushwa na vituo vyetu vya televisheni?

Kwa wale wanaopenda kuangalia tamthilia za nje hasa kutoka Ufilipino watakubaliana nami kuwa tamthilia hizo huwa hazinogi bila kuwaonesha mashoga, na tamthilia hizi zinarushwa na vituo vya televisheni ambavyo hatuna uwezo wa kuwazuia watoto wetu wasiangalie. Je, hili si jukumu la Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza?

Kama bodi ingekuwa inatekeleza majukumu yake ipasavyo, naamini filamu nyingi sana zisingekuwa madukani kwa sababu ya kukosa maadili. Hili la filamu ya Shoga ambayo imeonekana kuwa ni tatizo nadhani lina ajenda fulani, maana kabla ya kuishambulia filamu hii tujiulize je, kwa filamu zilizo mtaani ambazo hazijakaguliwa kabisa Bodi ina mpango gani japo hazijatangazwa katika vyombo vya habari kuwa zinapotosha?

Kama ni maadili mabaya yanayoutangaza ushoga tunaoukataa basi hili la filamu ya Shoga ni “trela” tu, kwani picha yenyewe tayari ipo mtaani inaitwa “Mtoto wa Mama”. Hii ni Komedi ambayo inaangaliwa na watu wa rika zote; watoto kwa wakubwa, na ina mambo na maisha ya kishoga kabisa. Sijui hii haina madhara kwa jamii na maadili yake yapo sawa? Tunaomba ufafanuzi kutoka Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza.

Nimekuwa nikisia hoja kutoka kwa viongozi wanaokwepa majukumu yao kuwa wasanii na watayarishaji ndiyo kikwazo kwa bodi kutekeleza majukumu yake kwa sababu hukwepa kupeleka filamu zao katika Bodi ya filamu kwa ajili ya kukaguliwa. Lakini lazima tujiulize, jukumu la kukusanya filamu kwa ajili ya ukaguzi ni la nani? Msanii/mtayarishaji au la Bodi?

Kuna sheria/ taratibu zipi ambazo bodi imeziweka zinazomlazimisha mtayarishaji/msanii kupeleka sinema zake kwenye ukaguzi kabla hajazipeleka sokoni?

Hata baadhi ya wasanii na watayarishaji waliowahi kupeleka filamu zao wanadai kuwa hawako tayari kupeleka filamu zao tena kwa sababu bodi hii hutumia muda mrefu sana kwa ajili ya ukaguzi, ndiyo maana filamu nyingi zilizopo mtaani hazijakaguliwa ila zimesajiliwa katika Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (Cosota) ambapo hakuna ucheleweshaji wala masharti ya ajabu ajabu.

Nimewahi kuandika katika makala yangu “Tutafakari kabla ya kusema au kutenda, ili kudumisha maadili”, kuwa maadili ya sasa yanayolalamikiwa yamejengwa na jamii nzima zikiwemo taasisi kama Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza na kila mmoja anajaribu kumtupia lawama mwenzake badala ya kuwajibika.

Nadhani matatizo kama haya yangeweza kuepukwa kama Bodi ingekuwa na sheria inayomlazimisha mtayarishaji kupeleka mswada wa filamu (script) katika Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza kabla ya kuanza upigaji wa picha (shooting), lakini hali kama iliyojitokeza kwenye filamu ya Shoga inapoteza muda na kuzua mambo yasiyofaa kwa wakati usiofaa.

Viongozi wasiotaka kuwajibika wajue kuwa wanaifanya jamii yetu ambayo pamoja na kupoteza maadili yake, idhani kuwa hata zile filamu za ngono maarufu kama 'Pilau' zinazooneshwa ndani ya mabanda ya video mitaani kwetu zinastahili kuangaliwa muda wowote, tena watoto wadogo wakiwa ndiyo waangaliaji wakubwa.

Kama wajumbe wa bodi ni wanataaluma waliobobea katika filamu na utaalamu wa aina mbalimbali katika sekta ya filamu na televisheni na wakatimiza majukumu yao ipasavyo, watakuwa na nguvu ya kuwakemea wasanii kutoharibu maadili yetu kwa kigezo cha soko huria, ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo kuandaa stori kwa mujibu wa walengwa (target audience), kwa maana ya umri na kadhalika.

Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ambayo imeundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 1976. inabainishwa kuwa na majukumu yafuatayo:
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza inawajibika na kuwiana na kawaida, mila, desturi na maadili mema ya Tanzania;
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza inatoa burudani yenye mafunzo mema na safi kwa Watanzania;
-Kuhakikisha upangaji wa madaraja ya maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza unalingana na mabadiliko ya maadili mema ya jamii ya Watanzania;
-Kuhakikisha usanii na uhuru wa ubunifu wa sanaa hauzuiliwi bila sababu za msingi;
-Kuhakikisha Filamu na Michezo ya Kuigiza, nchini Tanzania, inakuwa na viwango vinavyostahili vya usanii;
-Kuafiki, kuzuia au kudhibiti maonesho na usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza;
-Kuamuru kuondolewa kutoka kwenye filamu au mchezo wa kuigiza uliowasilishwa kwenye Bodi Kuu ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza sehemu yoyote ambayo Bodi Kuu haiafiki kwa maonesho au usambazaji kwa Watanzania;
-Kuafiki, kuzuia au kudhibiti utangazaji kwa umma unaohusiana na filamu au michezo ya kuigiza;
-Kukagua na kupanga madaraja ya filamu na michezo ya kuigiza.
-Kukagua na kutoa vibali kwa maeneo yote yanayotumika kwa maonesho na usambazaji wa filamu au michezo ya kuigiza.
-Kuafiki na kutoa vibali kwa shughuli za usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza
-Kuafiki na kutoa vibali kwa maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza.

Nasisitiza kuwa hata mimi sielewi chombo hiki kina manufaa gani katika mustakabali wa tasnia ya filamu hapa nchini.

Alamsiki

No comments: