Jun 6, 2015

Makundi mapya ya sanaa za maigizo yajirekebishe

Wasanii wa Kundi la Sanaa la ABY, Malapa Buguruni
Jacob Steven maaruf kwa jina la JB
Ni wazi kwamba huwezi kuzungumzia maendeleo yaliyopatikana kwenye tasnia ya filamu nchini bila kutaja Nyota Academia, Kaole Sanaa Group, Kidedea, Kidedea Original, Mambo Hayo na makundi mengine ya sanaa za maigizo.

Kimsingi makundi haya ndiyo yaliwaibua wasanii wakubwa nchini kama marehemu Steven Kanumba, Vicent Kigosi (Ray), Jacob Stephen (JB), Yvonne Cherry (Monalisa), Blandina Chagula (Johari), Jengua na wengine wengi ambao wanaendelea kuipeperusha vyema bendera ya filamu za Bongo ndani na nje ya Tanzania.


Makundi ya sanaa za maigizo bado yapo, tena siku hizi yamekuwa mengi zaidi. Takriban makundi matatu hadi matano kwa kila kata hasa jijini Dar es Salaam huku mengine yakiwa hayana hata usajili kutoka Basata.

Hata hivyo, licha ya makundi haya kuwa mengi na kuashiria kwamba Tanzania tuna vipaji vingi lakini bado naona utofauti mkubwa wa ubora kati ya makundi ya sasa na yale zamani.

Haya ya siku hizi yameacha kutoa wasanii kama Kemi wa Kaole, Tabia wa Kidedea (kwa sasa ni marehemu), Richie Richie wa Nyota Academia na wengine wa mfano huo.

Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa siyo sekta ya kuzalisha waigizaji bora bali ni sehemu ya kupotezea muda kwa wale wasiokuwa na kazi. Mengi yamesheheni watu wanaopenda kujionyesha lukuki kuliko kuwa na shauku ya kutimiza ndoto zao za kimaisha kupitia sanaa ya maigizo.

Hali hiyo imesababisha wachache wenye nia ya dhati ama kuvunjika au kuvunjwa moyo na wengi waliojiunga na makundi haya wakidhani kwamba baada ya wiki mbili wataonekana kwenye runinga na kuwa maarufu kama wasanii waliotangulia.

Makundi mengi ya siku hizi yamesheheni walimu wasio na sifa wasioifahamu kwa kina sanaa pana ya maigizo. Wengi ni wenzangu na mimi ambao wamejipachika taji la ualimu mara tu baada ya kuigiza kwenye filamu mbili tatu ambazo hazijauza hata kopi mia moja.

Nao tayari wamejiona wamekwiva kuwafunza wengine na matokeo yake ni kujazana ujinga kwa kusifiana wenyewe kwa wenyewe kila wanapokutana kwenye mazoezi. Wanasahau kwamba sanaa ya uigizaji ni kazi kama ilivyo uhasibu na ukandarasi. Sanaa hii imewahi kubadilisha maisha ya baadhi ya watu duniani, kutoka walalahoi kuwa mabilionea hivyo ni tasnia inayotakiwa kuheshimiwa tena siyo kidogo.

Makundi mengi ya siku hizi yamesheni michango kila kukicha tena mingi ni ile iliyokosa kichwa wala mkia. Pia hiyo inasababishwa na makundi haya kugubikwa viongozi wenye njaa, wasio na kazi wala kibarua hivyo kuamua kuwageuza wasanii kuwa kitega uchumi.

Makundi mengi ya siku hizi yamekuwa kichaka cha wapenda ngono zembe. Ngono ya kuchanganyana wenyewe kwa wenyewe. Pia, mara nyingi uchafu huo hufanywa na watu wenye vyeo ndani ya makundi haya. Usishangae mwalimu, mwenyekiti au hata katibu wa kundi akawa na uhusiano na wasichana zaidi ya watatu katika kundi hilo hilo moja.

Mchezo huu mchafu umekuwa moja ya magonjwa sugu yanayosababisha kufa kwa makundi haya kwa sababu pindi wasichana husika wanapogundua kuwa wanachanganywa huzua tafrani na kutoelewana na husababisha kundi kuyumba na hata kuvunjika kabisa.

Makundi mengi ya siku hizi yametawaliwa na wasanii wasiokuwa na uvumilivu, wengi hutaka mafanikio ya haraka. Hawataki shida wala tabu ya kutangatanga ili kutafuata nafasi zaidi za kuonyesha uwezo ama kipawa walichojaaliwa na Mungu.

Wamekaa wakisubiri fursa ziwafuate kwenye makundi yao. Pengine walitakiwa kupata nafasi ya kukaa na watu ambao wamefanikiwa kutoka na wawaeleze jinsi mlima wa kukubalika ulivyo mgumu kuupanda. Mtu asiye mvumilivu ni lazima ataishia kati tu. Msanii ni lazima ajitoe mwenyewe, kuhangaika huku na kule ili kutafuta chochoro ya kuibukia kileleni kwani siku nzote hakuna ‘shortcut’ ya mafanikio.

Makundi mengi ya siku hizi siyo ya muda mrefu, mengi huanzishwa na kudumu kwa miezi michache kabla ya wanakikundi kusambaratishwa na sababu hizo nilizotangulia kuzisema.

Hata hivyo, bado nina matumaini na makundi ya sanaa za maigizo, naamini kama wanavikundi wataamua kufanya kazi kweli, basi wale wauza sura wataogopa hata kusogeza pua zao karibu na makundi haya. Wasanii wa kweli pekee ndiyo watakaosalia na kazi itafanyika.

Wale walimu wasio na sifa nao watatafuta shule za sanaa na kusoma ili watakaporudi kwenye makundi yetu wawe walimu wa uhakika na watuivishe vilivyo. Viongozi wanaojifanya viwembe kwa kuwachanganya madada zetu nao watakoma na hata ile michango yao ya ovyoovyo itapungua kama siyo kufa kabisa na tasnia yetu itasonga.


Source: http://mobile.mwananchi.co.tz/

No comments: