Jun 12, 2015

Sekta ya filamu inaendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake


Mmoja wa waigizaji maaruf wa sinema za Hollywood, Angelina Jolie
Ripoti moja ya utafiti wa kwanza kufanyika duniani kuhusu wahusika wa kike katika filamu, umebainisha kuwa ubaguzi wa wanawake na wasichana umeenea mno katika sekta hiyo ya filamu. Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi Septemba mwaka jana imetokana na utafiti ulioidhinishwa na taasisi ya Geena Davis kuhusu Jinsia katika vyombo vya habari, ikisaidiwa na Shirika linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women, pamoja na Wakfu wa Rockefeller.

Utafiti huo ulifanywa na Stacy L. Smith (PhD) na timu yake ya watafiti kutoka Chuo cha Mawasiliano cha Annenberg, Chuo Kikuu cha Southern California. Utafiti huo ulitathmini filamu maarufu kutoka nchi ambako sekta ya filamu imepiga hatua zaidi, zikiwemo Australia, Brazil, China, Ufaransa, Ujerumani, India, Japan, Urusi, Korea Kusini, Marekani, Uingereza, pamoja na ushirkiano unaofanywa kati ya Uingereza na Marekani.

Huku wanawake wakiwa wanawakilisha zaidi ya nusu ya idadi nzima ya watu duniani, wahusika wa kike wanaoongea katika filamu hizo ni chini ya theluthi moja. Wahusika wa kike wanaoonekana kwenye runinga ni chini ya robo ya wahusika wote, yaani asilimia 22.5.

Utafiti unaonesha pia kuwa, wanapotumiwa, wanawake hawapewi nafasi za uwezo mkubwa, na wanawakilisha chini ya asilimia 15 ya wakuu katika biashara, wanasiasa, wanasayansi na teknolojia, wahandisi na wanahisabati.


No comments: