Jun 10, 2015

Hadhi ya Sekta ya Filamu Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na marehemu Steven Kanumba
KUMEKUWEPO mjadala kama hali ya sasa katika soko la filamu linaweza kuitwa ‘sekta rasmi’ ambapo mitaji, mitambo na rasilimali zipo kila mahali. Hakuna maendeleo yoyote yatakayopatikana pasipo uwepo wa Sera ya Filamu. Sera ya Filamu ni hati nzuri inayoandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu na masoko.

Ni hati kuhusu hadhi na thamani ya sekta inayoonesha kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni, inayotambua kuwa Filamu ni njia ya kipekee ya mawasiliano, ni njia ya kuelimisha na kuburudisha, inayotuweka pamoja, kupashana habari na kuhamasishana.

Zaidi kuliko njia nyingine yoyote ya mawasiliano ya umma, filamu inaweza kutumika kama chombo cha kuendeleza mabadiliko chanya ya kijamii pamoja na kuimarisha na kujenga uhusiano mpya kati ya utamaduni na maendeleo ya Taifa. Filamu ni njia mtambuka ya mawasiliano ya kiutamaduni ambayo ni muhimu inayoweza kutumiwa na Tanzania kuionesha dunia rangi yake halisi.

Kwa hiyo ni dhahiri kwamba akili zinazoweka pamoja sera zinakwenda na wakati na zina maono. Hata hivyo, hali ya sasa inaonekana kutoendana na hisia zinazojionesha. Hali ya utengenezaji wa filamu inahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.

Katika suala la teknolojia ya utayarishaji wa filamu nchi kwa sasa inarudi nyuma haraka na inaoza. Utamaduni wa kuangalia filamu za kigeni uliojengwa kwa miaka mingi umekufa na kuzaliwa itamaduni wa uangaliaji wa filamu za ndani lakini zikiwa katika maudhui ambayo bado kwa kiasi kikubwa yapo katika dhana za kigeni.

Kwa vyovyote ilivyo, nchi hii inaonekana kujifunga, azimio ambalo, linahitaji jitihada za pamoja za mapinduzi ya kiutamaduni yatakayothaminiwa kwa teknolojia iliyopo na ya bei nafuu.

Inaweza isiwe muhimu sana kushiriki katika mapitio ya Sera ya Filamu au hata miundombinu isiyokuwepo au fedha za kujikimu na utaratibu wa mitaji ya fedha za uzalishaji filamu nchini kama itafanywa kuwa mada tofauti. Kwa kweli, inahitaji semina ya siku nzima kutathmini fedha na masoko ya filamu nchini. Kukosekana kwa sera kumezifanya filamu zetu kuwa kama mchezo wa soka bila refa, mkutano bila mwenyekiti, darasa bila mwalimu, au familia bila mzazi.

Sinema nyingi (zaidi ya asilimia 90) zina upungufu mkubwa katika ustaarabu wa kisanii (artistic sophistication) unaotarajiwa katika levo ya kimataifa. Lakini pia ni dhahiri kwa watazamaji wa ndani wanaonekana kutokuwa na mbadala na hivyo kulazimika kuendelea kutazama filamu hizi japo shingo upande. Ili sekta ya filamu ikue na kufika kiwango cha kimataifa ni lazima kuwe na uwekezaji mkubwa unaofanyika. Suala lililopo ni wapi fedha hizo zitatoka na nini kitaongeza ubora au hata uwezekano wa “ideology” ya filamu zinazotayarishwa. Pesa hazipatikani bure, lakini sinema zinapaswa, jambo ambalo ni ukweli kinzani (paradox) wa sekta ya filamu katika jamii ya kibepari.

Ushiriki mchache na wa mbali kati ya Benki na soko la mitaji ni ushahidi wa kutosha wa utaratibu wa kizamani wa misaada ya fedha katika dunia ya sasa. Inatosha kusema, kiwango cha ushiriki wa misaada ya fedha katika sekta yoyote ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari ya mfumo kuamua ukuaji wa uchumi, uhimili na ubora wa bidhaa unaoshindwa kuongeza uzalishaji.

Wakati huohuo, kama msingi mkuu ni dhaifu, haiwezekani kusema rasilimali watu zinapatikana kwenye sekta ya filamu (ikumbukwe kuwa sisi bado ni sekta ndogo tu) isiyo na tija. Kuna waandishi wa skripti, watayarishaji, waongozaji, na wataalamu wengine, ambao wanaweza kupambana na changamoto ya miongozo yoyote bila kujali ugumu.

Jambo moja ambalo linaonekana kwa haraka lipo kati ya rasilimali watu ni tofauti na elimu ya asili. Kwa hiyo inapaswa kuangalia kuwa elimu bora ya filamu inapatikana katika nchi. Je, kuna mwelekeo wa wazi na kiwango na ushawishi wa utamaduni katika mafunzo? Katika hati ya Sera ya Filamu, ni lazima iwepo sehemu inayohusika na mafunzo, utafiti na maendeleo.

Elimu ya filamu ni jambo muhimu sana kwetu (au taifa jingine lolote) kuhadithia hadithi zetu na kuionesha Tanzania kama inavyotakiwa kujulikana kwa mataifa mengine, bila ya kuwa na tatizo tunalolishudia la watengeneza filamu wa kigeni wanaowakilisha taifa/bara isivyo sahihi au kukosa pointi muhimu za kihistoria/masimulizi ya kisiasa (filamu za kisiasa ni kama: ‘Hotel Rwanda’, ‘Blood Diamond’, ‘Sometimes in April’ na ‘The Last King of Scotland’, zilizotengenezwa kwenye bara hili na watengenezaji filamu wa kigeni).

Tunachoweza kuzingatia kwa sasa ni jinsi ya kuifanya elimu inayopatikana katika shule za filamu (zitakazokuwepo) iweze kutumiwa kutokana na hali yetu ya sasa ambapo hakuna tena busara ya kiuchumi kwa kuwekeza katika hisa za filamu (film stock). Mitaala ya Taasisi zinazofundisha filamu lazima ijumuishe pamoja na jinsi ya kupenyeza vyote teknolojia na utamaduni wa kuzalisha kazi za viwango vya kimataifa katika masuala ya ubora wa maudhui yanayowasilishwa.

Pia tunapaswa kuipitia upya Sheria ya Filamu Na. 4 ya 1976 ambayo haifafanui wala kuweka mifumo yoyote ambayo inaweza kutoa majibu ya maswali yaliyopo. Sheria hii inazungumzia tu kuhusu uanzishwaji wa taasisi ya filamu (Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza) ambayo hata hivyo imenyimwa mamlaka kamili, kwani inafanya kazi kama taasisi ya kusimamia maadili na kupanga madaraja tu.

Filamu kama dhana nzima haiwezi kubishaniwa, kinachoweza kujadiliwa ni uwezekano zaidi wa kutatuliwa kwa dhahania (subjectivity) ya uzuri ulio katika jicho la mtazamaji.

Sababu inayoshawishi uzalishaji wa filamu nchini kama ilivyo katika nchi nyingine ni maudhui ya filamu yanayoweza kuamuliwa na sababu kubwa ya kuwa utamaduni wa watu na mbinu zao zinapelekea nchi kuwa katika hali ya utulivu. Pia kuna muingiliano (uhusiano) wa uchumi, matarajio na muingiliano wa kijamii wenye jukumu kubwa katika kuamua utamaduni wa filamu. Ni kama jamii inapata aina fulani ya wafanyakazi inaostahili, watengeneza filamu kupitia utafiti huamua nini soko linataka katika masuala ya dhamira, hata hivyo bado ‘kinachowasilishwa’ huamuliwa na mtayarishaji na muongozaji.

Bado kilicho katikati ya vikosi vya kimasoko na watu wakati mwingine ni nafasi isiyopendeza ya wakosoaji wa filamu, kwa ambaye ana wajibu wa kufanya vizuri.

Hali ya kiuchumi na kisiasa bado ni ya kiwango cha chini sana. Kuna upuuzwaji mkubwa wa sekta hii, serikali badala ya kuitazama sekta hii kibiashara na chanzo muhimu cha kichumi (new sector with economic potential) wanaichukulia kama sehemu ya burudani. Bado imekuwa haipewi kipaumbele japo imeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ajira na pato la Taifa. Kwa sababu hiyo sidhani kama tunaweza kuweka imani yetu kwa serikali iliyopo kutuunga mkono. Hii inaweza kuwa sababu ya kushindwa kwetu, na mimi sina uhakika wa uwepo wa hali hii, ambapo inaweza kuwa ya manufaa kwa baadhi ya mipango ya filamu kufanyika nchini.

Tanzania ni moja ya nchi chache zenye maeneo mazuri ya kuvutia yanayofaa kabisa kwa kutengenezea filamu, ni nchi yenye wasanii wengi wazuri wenye vipaji lakini waliokosa muongozo.

Sisemi kuwa nina ufahamu wa hali ya kiwango kikubwa zaidi, lakini nina shauku ya kujua iwapo itawezekana kuona serikali ikija na mpango madhubuti wa kuandaa na kuwapa elimu na teknolojia inayohitajika watayarishaji, waongozaji na watendaji wengine wa filamu nchini. Hii itaonekana kuwa tumekuja na mpango wenye manufaa makubwa ikiwa itawezekana.


Nawasilisha.

No comments: