Jun 29, 2015

“Spec Scriptwriting”, uandishi wa filamu wenye changamoto nyingi

Waandishi mahiri wa script Tanzania, Dk.Vicensia Shule na
Bishop Hiluka, katika moja ya mikutano ya Bodi ya Filamu
Ikiwa una matumaini kuwa siku moja utakuja kufanya kazi ya uandishi wa script kwa ajili ya filamu au televisheni, basi unahitaji kuwa na ufahamu wa jinsi ya kuandika “spec” script. Spec Script ni kifupi cha Speculative script, huu ni uandishi wa filamu wa kubahatisha (speculation), ambao kama mwandishi unaandika script yako ukiwa hujui nani atakuja kutumia script hiyo – hii humaanisha kuwa unaandika script bure (pasipo kulipwa au kuajiriwa na mtu). Kwa maana nyingine ni kwamba hakuna mtu aliyekuajiri au anayekulipa kuandika script hiyo. 

Unaandika ukiwa na matumaini ya kuja kuuza kwa mnunuzi yeyote atakayevutiwa na kisa chako au kuajiriwa kwa ajili ya kuandika script kwa sababu ya hiyo, lakini ili kuwa na nafasi au uwezekano, huna uchaguzi bali kuandika spec script.


Ili uwe katika upande ulio salama ‘Spec scriptwriter’ anapaswa kusimamia misingi na sheria imara za uandishi wa filamu. Mara baada ya scrpt kununuliwa, ndipo hubadilika na kufanywa kuwa shooting script, ambayo pia huitwa production script.

Production script ni toleo maalum la script iliyo tayari kwa utayalishaji wa filamu, likijumuisha pamoja maelekezo ya kiufundi (technical instructions): kama vile maelezo ya uhariri wa filamu, upigaji picha na mambo kama hayo.

Kosa kubwa ambalo Spec scriptwriter au mwandishi mchanga wa filamu anaweza kulifanya ni kuwasilisha script yake iliyojaa lugha ya kiutayarishaji (production language), ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo kamera inapaswa kuwekwa (camera angles) na maelekezo ya kiuhariri (editing transitions). Inaweza kuwa vigumu sana kutokuweka aina hii ya lugha katika script yako unapoandika kwa ajili ya filamu yako mwenyewe. Kwa kuwa, ni hadithi yako, unaandika script utakayoitumia mwenyewe na unaiona katika namna maalum sana.

Hata hivyo, ukweli utabaki kuwa ukweli tu. Kama unaandika script ambayo unataka kuiongoza mwenyewe, basi jaribu kwenda katika njia wanayotumia watengenezaji wengine wa filamu wa kujitegemea (independent filmmakers). Lakini kama nia yako ni kuandika script utakayoiuza kwenye makampuni au studio kubwa, basi ni bora usimamie katika mfumo na muundo uliokubalika wa uandishi wa filamu.

Unapoandika (spec script) kwa ajili ya televisheni mara nyingi hutegemea moja ya mambo mawili: Ni ama unaandika kutokana na sehemu ya yaliyopo (existing episode) kwenye ‘show’ husika ya televisheni au ni kazi mpya (original piece of work) ya majaribio (pilot).

Kuandika episode ya vichekesho (comedy) au drama series, njia rahisi ya kufanya ni hii: Kwanza, amua unataka kuwa mwandishi wa televisheni wa aina gani. Je, unavutiwa zaidi na comedy au drama? Ni aina gani ya show unayoifurahia ukiwa kama mtazamaji? Tengeneza orodha ya show zako uzipendazo (favorite) za televisheni. Anza kujiuliza mwenyewe, ni show ipi kati ya hizo inayoweza kuwa ‘fun’ zaidi kuiandikia. Kwa mfano, kama unapenda zaidi ‘CSI’, ‘24 HRS’ au ‘LOST’, basi hufai kuwa mwandishi wa comedy. Lakini kwa upande mwingine, kama unapenda drama zenye mchanganyiko wa vichekesho, kama ‘Desperate Housewives’ au ‘Ugly Betty’basi uchaguzi mzuri ni kuwa mwandishi wa comedy series.

Unaweza kuwa mwenye vipaji vingi (multi-talented) kuandika vyote; comedies na drama, na unaweza kupata nafasi ya kufanya hivyo. Lakini kwa ‘spec scriptwriter’ mpya, ambaye hajajitangaza akafahamika, ni muhimu sana kama utaelekeza (focus) juhudi yako kwenye jambo moja. Itakusaidia kukuondoa katika list ya waandishi wapya wenye kiburi na ujinga wanaodhani wanaweza kuandika katika kila aina ya hadithi (genre), na hivyo kujiharibia. 

Ukishafanya uamuzi kuwa wewe ni mwandishi wa comedy au drama, kinachofuata ni kuamua ni onesho (show) gani utaliandikia episode. Kwa kufanya hivyo, hebu angalia orodha ya shows zako uzipendazo. Ni show ipi maarufu zaidi? Ni ipi yenye msisimko (buzz) zaidi ndani yake?

Unachotakiwa kufanya hapa ni kuondoa shows ambazo watu wachache (tofauti na wewe) wanaziangalia au hata kuzifahamu. Fikiria zaidi kuhusu watazamaji wako ni kina nani – watayarishaji wanaotazamiwa na waandishi wengine. Hivyo, chagua show ambayo wote mtaipenda. Kuandika episode ya show itakayosisimua zaidi itafanya watu wakufahamua kwa haraka zaidi na hivyo kujiongezea nafasi nzuri ya kuaminika. 

Kisha anza kujifunza kuhusu muundo (format) wa show. Unataka kuelewa jinsi show inavyoandaliwa kwa mtazamo (perspective) wa kiuandishi. Kusema ukweli, hutataka tu kuangalia episodes nyingi uwezavyo, lakini pia utataka kufuatilia baadhi ya scripts ikiwezekana. Siku hizi zipo wavuti (websites) ambazo script mbalimbali zimehifadhiwa, ambazo unaweza kuzipakua (download) ili kuangalia.

Lakini kuwa makini usije kupakua “transcript”. Transcript ni nakala tu isiyo na cha zaidi, yenye mazungumzo yaliyosikika kwenye movie au michezo ya televisheni. Unatakiwa kupata script halisi inayohusisha mazungumzo yote, matendo, maelekeo na maelezo.

Mara upatapo scripts kadhaa, anza kufuatilia jinsi show inavyojengwa (structured). Je, ina hadithi “A” (hadithi kuu) pamoja na hadithi “B” (hadithi nyingine ambayo kwa kawaida si muhimu sana), au labda hata hadithi “C” (storyline ndogo ambayo hujifunua kwenye background ya episode husika)? Unazijua sauti za kila mhusika? Nini kinawafanya wawe wa kipekee? Je, wana maneno fulani wanayosema au wana ishara au mambo maalum wanayopenda na kuyachukia? Weka maelezo (note) ya kila unachofikiri kinaweza kuwa na manufaa kwako unapoendelea kundika episode yako uliyoichagua. 

Na unapokuwa tayari kuanza mchakato wako wa furaha (na kutisha) wa kuandika ‘spec script’ yako, elewa kuwa hakuna njia sahihi au potofu ya kuandika script. Unatakiwa kufanya chochote kitakachoonekana kufanya kazi kwako. Mimi mara nyingi hupendekeza kuanza na “Outline” ya mambo ya msingi ya hadithi na kisha polepole ongeza mambo mengine ikiwemo mazungumzo kwenye kila eneo la tukio (scene) mpaka itakapoanza kuchukua sura halisi. Outline itakusaidia kuweka hadithi yako kwenye mwelekeo na kuyaonesha mashimo yoyote yanayoweza kuwemo kabla hujarukia ndani ya mazungumzo.

Outline kwa lugha rahisi ni waraka wenye mistari kadhaa (inategemea na wingi wa scenes zako), kila mstari hulielezea eneo la tukio (scene) linalopaswa kuwemo kwenye script yako. Kwa kuwa outline mara nyingi si ndefu kama ilivyo “treatment” (kitu kingine kinachohitaji muda zaidi kukielezea), ni vizuri zaidi kuiandaa kabla hujaanza kuandika script yako. Outline hukusaidia sana kuuona mtiririko wa matukio moja baada ya jingine unayotaka kuyaandikia script.

Kwa mfano:

1. Eneo: Chumbani – Onyesha mahusiano kati ya binti mdogo (miaka 12) na mama yake
2. Eneo: Shuleni – Onyesha mazungumzo ya binti huyo na wanafunzi wenzake kuhusu malezi hafifu anayopewa mama yake
3. Eneo: Ukumbi wa Muziki – Onyesha jinsi mama huyo anavyoonyesha asivyojali malezi ya bintiye, anacheza muziki hadi usiku wa manane wakati bintiye kabaki peke yake nyumbani.

Katika spec, huhitaji kutengeneza mhusika mkuu mpya (main character) kwa ajili ya episode. Haijalishi ni namna gani atakuwa funny, kwa kuanzisha mhusika mkuu mpya, unabadilisha mwenendo wa episode. Hawa ni wahusika ambao watakwenda ‘beyond episode’ unayoandika.

Ukishaandika rasimu yako ya kwanza (first draft), unahitaji kupata maoni katika mfumo wa “maelezo” (notes). Ikiwezekana kutoka kwa watu ambao wanajua kutoa maelezo. ‘Maelezo’ hapa inamaanisha mkusanyiko wa mapendekezo muhimu ambayo yatasaidia kuboresha ubora wa jumla wa ‘spec script’ yako.

Kumbuka, kuna tofauti kubwa kati ya maelezo na maoni. Maoni ni mambo kama, “Nimeipenda”, “Inavutia sana”, “Inatisha” - na mambo mengine kama hayo. Kusema ukweli, maoni ni kazi bure. Unahitaji maelezo zaidi yanayojibainisha ambayo yatakusaidia kurekebisha palipoharibika.

Jaribu kuwapa script yako marafiki ambao ni waandishi au wapo katika sekta ya filamu – au angalau wenye uelewa wa kina kuhusu ukosoaji unaojenga (constructive criticism) ambao wewe unauhitaji. Ipitisha script yako angalau kwa watu 3-4. Hii itakupa mwanga wa kutosha kuhusiana na maoni, lakini pia utaanza kuona mambo mbalimbali yanayofanana katika ‘maelezo’ ambayo umepewa. Ukipata maelezo yanayofanana kutoka kwa watu watatu au wanne tofauti, hayo ndiyo yanayopaswa kushughulikiwa zaidi.

Kisha chukua muda wa kufanyia kazi maoni yanayostahili kuhusu mahitaji ya spec script yako. Mara upatapo maelezo yote mkononi, anza kuandika upya (rewrite) spec script yako. Shughulikia maelezo unayokubaliana nayo na yapuuze usiyokubaliana nayo. Kumbuka hii ni script yako, huhitaji kukubaliana na maelezo yote ulilopewa hata kama unadhani huyahitaji.

Kuandika upya inaweza kuchukua muda pia. Jipe muda unaohitajika. Mara nyingi Utajikuta unafanya kwa “ukamilifu”. Unavyoandika zaidi ili kuboresha script yako, ndivyo inavyokuwa bora zaidi. Kuandika ‘spec script’ inaweza kuwa mchakato wa muda mrefu na mgumu. Lakini kama utaupa muda na maandalizi, nafasi ya kuandika ‘spec script’ ambayo itafanikiwa – itakufanya sasa kuajiriwa rasmi kwa kazi hiyo!


Alamsiki.

No comments: