Jun 17, 2015

Waraka wa Bond Bin Sinnan, kwa Wasanii wa filamu Tanzania

Abdulrazaq Sinnan, maarufu kama Bond Bin Sinnan
Wasanii wa Bongo Movie wakiwasalimia wananchi waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, wakati wa kutangaza nia ya kugombea Urais kupitia CCM
Jina langu naitwa Abdulrazaq S.H. Sinnan ingawa asilimia kubwa ya Watanzania wananifahamu kwa jina la Bond Bin Sinnan kwa takribani miaka 15 sasa najishughulisha na masuala ya tasnia ya filamu nikiwa kama mtunzi, muigizaji, mzalishaji na muongozaji wa filamu. Hivyo nina upeo na uzoefu mkubwa wa tasnia ya filamu Tanzania. Naijua faida yake, matatizo yake na mengine mengi yanayoihusu tasnia hii.

Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana wasanii wenzangu wa filamu nchini kutokana na kujituma kwetu mpaka tumefanya tasnia hii kuwa ajira kubwa kwa watanzania wengi sana. Vilevile tasnia hii imekuwa ni burudani kubwa kwa wana Afrika Mashariki na Kati kwani zaidi ya watu milioni kumi wanaangalia filamu za Kitanzania.

Tasnia ya filamu imeajiri zaidi ya watanzania 500,000 ambao wanaitegemea tasnia hii ya filamu katika maisha yao ya kila siku: kuishi kwao kunategemea filamu tu na si vingine kuanzia chakula, kodi, ada za shule, usafiri na vinginevyo. Ukianza na waigizaji, waandaaji, waongozaji, watendaji wengine (camera, sounds, lights, art directors, location managers, makeup artists, editors, graphics designers, nk.) wasambazaji, video libraries, machinga, radio programs, tv programs  n.k.

Dhumuni la kuandika barua hii ni kuwakumbusha kuwa tasnia yetu inachungulia kaburi na tukumbuke kuwa tasnia hii tumeitengeneza sisi, ikifa tutataabika sisi na wa kuipa uhai iendelee kuwepo ni sisi wenyewe pia. Nasema yote haya kwa sababu hiki ni kipindi cha uchaguzi na sisi wanatasnia tuna ushawishi mkubwa sana katika mambo ya nchi yetu na ndio maana tumeweza kuona baadhi ya wasanii wenzetu kwenye majukwaa ya wanasiasa ili kuwashawishi wananchi kusogea eneo la tukio na kuwaonesha wagombea ni wa kweli kwa wayasemayo.

Tasnia ya filamu ina matatizo mengi sana na kwa asilimia 60 yanasabishwa na serikali yetu na ni kutokana na kutokuwa na sheria madhubuti za kulinda haki zetu zisipotee na hapa nazungumzia Hakishiriki na Hakimiliki, filamu imekuwa ni shamba la bibi yaani bibi yuko hoi na uzee na wanaovuna na kula ni wengine ambao hawajui hata bibi alipanda vipi shamba hilo.

Serikali ilitamka kuwa tasnia ya filamu iko rasmi na inatambulika lakini cha ajabu hakuna sera ya filamu ya Tanzania sasa huu ni urasimishaji gani? Tunajiita tuko rasmi wakati haturuhusiwi hata kupiga picha majengo ya serikali yaani hata kwa nje tu, haturuhusiwi kuvaa nguo zinazofanana na za majeshi yetu huku tunaambiwa hatuna uhalisia ndani ya filamu zetu na haohao. Haturuhusiwi hata kupiga picha kwenye mbuga zetu za wanyama ili kuzitangaza ndani na nje ya nchi wakati kila siku wizara inahangaika kutangaza utalii. Je ni kweli tuko rasmi au kiini macho?

Sheria hazijielezi waziwazi na wala hazisaidii kuleta haki hata kidogo. Ingawa tunakubali kuwa chombo cha kusimamia haki za filamu na wanafilamu wote kipo na kinaitwa COSOTA lakini kiukweli COSOTA haina msaada wowote na tasnia hii. Kwani imekuwa ikitoa vibali vya kukodisha filamu bila idhini ya wenye filamu, kuonesha Filamu kwenye vibanda bila idhini ya wenye filamu, kurusu kudurufu filamu bila idhini ya wenye filamu na kuchukua mirabaha ya filamu katika mahoteli, mabaa, mabasi vituo vya televisheni na cable network.

Ukitizama kwa uchache mianya ya utengenezaji pesa inayotumiwa na COSOTA utagundua kuwa ndio mianya mikubwa inayofanya wizi wa kazi za filamu za Kitanzania na kuwafanya waishi kimasikini na mifano hai tunayo kabisa ya waigizaji waliotangulia mbele za haki na hata walio hai maisha yao yalikuwa vipi na yako vipi mpaka sasa?

Niseme ukweli wa kutoka moyoni kuwa asilimia 95 wanaishi nyumba za kupanga na wasiopanga basi wanaishi kwa wazazi wao au nyumba za urithi. Ni asilimia 5 ndio wenye usafiri ingawa ndani ya hao pia hawajapata usafiri huo kupitia filamu bali ni njia nyingine.

Hivi wanatasnia wenzangu hatuoni matatizo yetu kweli? hatuoni serikali inatula tu na hairudishi wala kutusaidia chochote? Hatuoni kuwa hakuna sheria madhubuti kwani sheria zilizopo ni za bodi ya ukaguzi wa filamu na zimetungwa mwaka 1976. Je mwaka huo kulikuwa na filamu ngapi ukilinganisha na sasa? Kulikuwa na utandawazi kama sasa? Mbona sheria za kodi zimetungwa mpya lakini sheria za kuhusu filamu hazijabadilishwa?

Je tunatakiwa kuendelea kuwa shamba la bibi? Serikali inavuna kodi kiasi gani kupitia vifaa vyote vya utengenezaji filamu kuanzia ushuru wa uingizaji wa vifaa kutoka nje kama Camera, computer, taa, vifaa vya sauti, empty cd, cd printers, papers printers, papers, Dvd covers? Pia katika malipo ya film Board kwa ukaguzi, Cosota kwa ajili ya usajili na manispaa kwa ajili ya vibali vya kubandika matangazo n.k? Jaribu kupiga hesabu ya filamu moja serikali inaingiza shilingi ngapi na msanii au producer anaingiza shilingi ngapi utalia machozi.

Chombo ambacho wanatasnia wengi tulitegemea kuwa kinaweza kutukomboa, TAFF, lakini uongozi wake ndio umekuwa cha kwanza kutumiwa na wanasiasa, wasanii wamejiunga na Team-nani sijui na kimekuwa hakina usaidizi wa ufumbuzi wa matatizo ya tasnia ya filamu bali kuwagawa wasanii na kuwatafutia ugomvi ili pasiwe na umoja sababu aendelee kutawala.

Mpaka mwaka huu taasisi hii imetumia nguvu kubwa kuandaa Tuzo za Filamu ambazo pia inashutumiwa kuwa tuzo wamegawana viongozi wa ndani ya taasisi hiyo kupitia kazi walizozifanya. Kilio kikubwa kama cha pirates, kodi na hakimiliki wameshindwa kufanya lolote. Je hili nalo hatulioni kuwa tunahitaji mbadala wa Taff? Au tunahitaji kuibomoa Taff na kuiunda upya?

Wanatasnia wenzangu hiki ni kipindi cha sisi kuangalia yupi atakayekuwa tayari kutusikiliza na kutatua matatizo yanayotukabili. Tusihadaike na pesa ndogondogo za kusafiri na wagombea majimboni na kuwanadi, wakiingia madarakani wanafanya kilicho katika mipango ya serikali. Hebu basi kwa pamoja tuache upinzani wetu nyuma na tuungane katika kutetea haki yetu. Hivi kweli tunazidiwa ushawishi hata na madereva kwani tumeona hivi karibuni waligoma na matatizo yao yakatatuliwa.

Hatuoni kuwa tunastahili kutengenezewa sheria madhubuti za ulinzi wa kazi zetu?
Hatuoni tunahitaji misamaha (exemption) ya kodi za kuingiza vitu kama wakulima na wafanya kazi wa serikalini?

Hatuoni tunahitaji kupunguziwa makato ya kodi za ndani katika ufanyaji kazi wetu?
Hatuoni kuwa tunahitaji mirabaha ya ukodishwaji na uoneshwaji wa filamu zetu kupitia libraly, video shows, vingamuzi, mahotel, mabaa, mabasi, mashirika ya ndege, kwenye meli, mitandaoni na cable netwok?

Je, hatuoni serikali inatakiwa kuturuhusu kupiga picha majengo ya serikali hata kwa nje tu kwani kama leo inachukua kodi katika biashara zetu basi inatakiwa itambue uhitaji wetu wa matumizi ya picha za Magereza, Jeshi la polisi, Jeshi la Wananchi, Airport, Bandari, Mabenki nk?

Je, hatuoni tunahitaji kuhamishia kesi zetu katika mahakama ya biashara? Kwa sababu tunalipa kodi na makato yote wanayolipa wafanyabiashara wengine? Je, hutuoni umuhimu wa kuanzishwa kwa mahakama ya hakimiliki na hakishiriki? Je, hatuoni tunapaswa kupigana ili filamu kutoka nje nazo zikaguliwe Bodi ya filamu na pia zilipiwe stika kama ilivyo kwa biashara nyingine iwe bidhaa za ndani au nje zote hupewa stika na TRA?

Wanatasnia wenzangu kwanini tunashindwa kuungana pamoja na kuhakikisha tunatimiziwa haya kama baadhi walivyoungana na kupinga ushushwaji wa bei za filamu? Je ni kweli hatumjui adui yetu? Haya ni baadhi ya maswali tunapaswa kukaa chini na kujiuliza kabla ya kuanza kupokea vijisenti vya wanasiasa na vikatupa raha za muda mfupi huku miaka mitano ijayo tukaendelea kutaabika. Tusikubali kufunikwa na vivuli vya wasanii wachache wanaoonekana kurandaranda kwa wagombea eti wakaonekana kuwa wanaiwakilisha tasnia hii ya filamu.

Wanatasnia wenzangu kama kuna kitu tunahitaji basi tuungane na tusimame pamoja kuona tunashinda vita hii na kujikomboa katika dimbwi la mateso ya tasnia yetu na tusifanywe shamba la bibi.

Na tufahamu kuwa sanaa ina mashiko makubwa kuliko siasa na wanasiasa ni watu ambao wanaajiriwa na wananchi kwa kupiga kura lakini sisi tunawaburudisha wananchi. Mfano wangu mdogo ni kuwa nilimfahamu Michael Jackson, Arnold Schwarzenegger, Sylvester Stallone na wengine nikiwa simjui Rais wa Marekani, Nilimfahamu Bob Marley nikiwa simjui Rais wa Jamaica, pia nilimfahamu Pele nikiwa simjui Rais wa Brazil bila kusahau niliwafahamu Bruce Lee na Jacky Chain nikiwa simjui Rais wa China.

Naomba niwahakikishie hata leo kuna watoto wanawafahamu Vincent Kigosi, King Majuto, Wastara, JB na wengineo wengi lakini hawawajui hao wanasiasa wote waliochukua fomu za kugombea iwe urais au ubunge. Kama tuna akili basi tutafahamu nini cha kufanya lakini kama tunataka kuendelea kusemwa na hao wanasiasa kuwa sisi ni ombaomba kwao na kila wakituona wanatamni kujificha basi tunyamazeni kimya tena tusibiri kusemwa bungeni au tusubiri malaika ashuke na kutusaidia kama hilo linawezekana.

Asanteni kwa kusoma na nina imani kuna kitu tunaweza kujifunza kupitia niliyoyaandika hapa. Ndimi Mwanatasnia Mwenzenu.

Bond Bin Sinnan
Dar es Salaam

No comments: