Jun 22, 2015

Sekta ya televisheni na mchango wa utamaduni

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel, akikata utepe kuzindua Tamthilia ya 'Doudou na Wakwe Zake' katika Viwanja vya TBC mwaka 2014
SEKTA ya Televisheni nchini kwa sasa imekuwa ni sehemu muhimu sana ambayo haiwezi kukosekana katika maisha ya kila siku ya mwananchi, iwe mwananchi huyo anamiliki seti ya televisheni au la. Kwa kutazama vipindi mbalimbali vya televisheni mtu huweza kufahamu mambo mengi makubwa yanayoendelea nchini na hata nchi za nje, na kwa kutazama televisheni unapata burudani za kila aina.

Japo sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na fursa nzuri ya maendeleo kutokana na dunia kuingia zama za dijitali lakini pia ina changamoto kubwa. Kwa upande mmoja, maendeleo ya haraka ya dijitali yameiletea sekta hiyo fursa nzuri ya kujiendeleza, na kwa upande mwingine, aina za uenezi wa habari zimekuwa nyingi, kwa mfano, televisheni kwenye mtandao wa internet, simu za mkononi zinaendelea haraka na makundi mengi ya televisheni ya nchi za nje yameingia kwenye soko la televisheni nchini, hali kama hiyo imekuwa shinikizo kubwa kwa sekta ya televisheni na filamu nchini.


Ili kuongeza nguvu za ushindani sekta ya televisheni na filamu nchini lazima iendeleze ubunifu bila kusita ndipo inapoweza kukidhi mahitaji ya watazamaji yanayoongezeka siku hadi siku, na kuwavutia wawekezaji wa matangazo ya biashara.

Pamoja na aina mbalimbali za uenezi wa habari zinavyoendelea haraka na kuwa nyingi, sekta ya televisheni nchini inakabiliwa na shinikizo kubwa la ushindani. Hivi sasa nchini tuna vituo vingi va televisheni, kikiwemo kituo cha televisheni cha taifa na vituo vingine vya kitaifa vya binafsi. Pia kuna vituo mbalimbali vya televisheni za mikoa.

Vituo vikubwa vya televisheni kama TBC1, ITV, Star TV, Channel Ten, EATV na vingine vilikuwa vinashikilia uenezi wa itikadi muhimu na utamaduni katika miaka yote tangu nchi hii iliporuhusu urushaji wa matangazo ya televisheni mwanzoni mwa miaka ya 1990, na vipindi vyake kadhaa kama ‘Taarifa ya Habari’, ‘Mazungumzo kuhusu Matatizo Yanayofuatiliwa’, ‘Tamthilia’, ‘Burudani na Michezo Mbalimbali’ nk, vilikuwa ni vipindi vinavyotazamwa na kila familia.

Vipindi vya televisheni hutiliwa maanani sana kwa kuwa taarifa zake huambatana na picha hai za matukio, hivyo katika hali ya ushindani kama huu vipindi vyote vinavyotangazwa katika vituo vya televisheni lazima viwe na mvuto mkubwa na wakati wote na vinapimwa kwa ‘idadi ya watazamaji’ ili kuhakikisha vipindi vinavyorushwa ni bora.

Ndiyo maana mara kwa mara hutokea ushindani mkubwa sana kwa vituo vya televisheni kugombea kurusha matangazo ya mashindano ya soka ya kombe la dunia au ligi za soka za ulaya, kwa kuwa matangazo haya hupata watazamaji wengi kuliko matangazo mengine.

Vipindi vya burudani ni vipindi vinavyovutia watazamaji wengi na matangazo mengi ya biashara. Kwa sasa vituo vyote vya televisheni vinajitahidi kuwa na vipindi vya michezo, drama na ucheshi (comedy) ili kuwavutia watazamaji. Lakini kutokana na athari ya vipindi vya televisheni vya nchi za nje, sekta ya televisheni nchini iliyoanza kujitafutia uhai na maendeleo, imejikuta ikiingia kwenye shinikizo la mazingira ya utandawazi wa duniani, na taratibu imeanza kumezwa na utamaduni wa kigeni.

Katika miaka ya karibuni, sekta ya televisheni nchini imekabiliwa na ushindani mkubwa zaidi, vituo vya televisheni nchini vinakabiliwa na changamoto kubwa kutoka vipindi vya televisheni vya nje. Watu sasa wametekwa kuangalia vipindi mbalimbali kutoka nje, kwa mfano, matangazo ya moja kwa moja ya mashindano ya ligi ya soka nchini Uingereza, filamu, na picha za katuni na maonesho ya mambo mbalimbali. Hivi sasa matangazo ya vituo vya nje, kutoka China, Korea, India, Ufilipino nk. yametawala nchini.

Kwenye stesheni zetu sasa hivi kumejaa tamthilia za kutoka China, Ufilipino, Mexico na Korea. Na sasa wasambazaji wakubwa wa filamu nchini wanaanza kuachana na sinema zetu na badala yake wanaanza kusambaza filamu kutoka Bollywood zenye tafsiri za Kiswahili.

Tunasahau kuwa sekta ya televisheni na sinema ni chombo muhimu sana katika kueneza utambulisho, utamaduni na fikra za nchi husika. Ndiyo maana nchi za China, Korea au India zinaingia gharama kubwa za kutafsiri filamu na tamthilia zao kwa Kiswahili kisha kuzitoa zioneshwe bure katika vituo vyetu vya televisheni.

Kwa mfano, China kupitia Idhaa ya kiswahili ya CRI, ilifanya kazi ya kutafsiri tamthilia ya ‘Doudou na Mama Wakwe zake’ na kutia sauti pamoja na kukamilisha maandalizi ya tamthiliya hii kwa zaidi ya miezi 10, kwa ajili ya watazamaji wa Tanzania na nchi za Afrika ya mashariki.

Pia kwa miaka mingi nchi kama Ufaransa, kwa mfano, imefanikiwa sana kuitumia sekta ya televisheni na filamu kutangaza utamaduni wao duniani. Ufaransa imekuwa ikitoa msaada mkubwa wa bajeti za kutengenezea filamu na vipindi vya televisheni kwa nchi zinazoongea Kifaransa (Francophone countries). Kama hiyo haitoshi, wamepanua wigo na sasa wanatoa pesa hata kwa nchi zingine kama Tanzania.

Ndiyo maana, si ajabu kwa yeyote atakayeandika script yake ya filamu au kipindi cha televisheni na kuitafsiri kwa Kifaransa, atapewa udhamini wa maelfu ya Yuro na ubalozi wa Ufaransa ili atengeneze filamu au kipindi chake cha televisheni.

Kwa sababu vipindi na tamthilia zetu hazivutii na hazina ubora unaokubalika kimataifa, vituo vya televisheni nchini vimechukulia hili kama fursa ya kuonesha vipindi vilivyotafsiriwa kutoka China, Korea na India kwa kuwa tu wanavipata bure (au kwa kulipia pesa kiduchu) lakini wanashindwa kubaini kuwa hii ni vita ya utamaduni na ya kutawalana kiakili.

Hivi tunaandaa taifa (kizazi) la kesho la aina gani? Kwa mfumo huu kizazi chetu tunakiachia urithi wa aina gani kwenye sekta ya utamaduni? Au huu ni mkakati maalum wa kujenga jamii (watoto wetu) itakayobadilisha tamaduni zake na kujifunza tamaduni za nje? Je, serikali imebariki hilo? Kwa kweli maswali haya na mengine yanahitaji majibu.

Nahisi kama tunajenga jamii ya watu waliochanganyikiwa! Ndiyo maana haishangazi sasa kuona Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, viongozi wengine na hata wasomi wetu wakiwa ni watu wa kulalamika tu pasipo kutafuta njia sahihi ya kutatua matatizo yetu. Kwa sasa inawezekana hatulioni hili ila ni uhakika lina madhara makubwa sana kwa jamii zetu na mustakabali wa nchi yetu.

Yote haya ni sababu ya Serikali kutoipa Sekta ya Utamaduni umuhimu mkubwa. Wakati Tanganyika inapata mwaka 1961, Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962. Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, na kwamba nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Kupuuzwa kwa tamaduni kumekuwa ni suala linalojitokeza katika nyanja mbalimbali hapa nchini. Kati ya mambo ambayo binadamu hana budi kuyazingatia ni uhusiano wake na mila na desturi alizotunukiwa na jamii yake. Ni katika kuzingatia hilo tu ndipo binadamu anapata uwezo wa kukua na kujichotea utajiri mkubwa unaotolewa na tamaduni za jamii yake.

Tangu mwaka 1962 shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi. Kwa sasa utamaduni pekee tuliobakiwa nao kama nchi ni lugha ya Kiswahili. Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano na hubadilika kadiri jamii inavyobadilika. Kiswahili ni lugha ambayo imejitokeza kuwa kielelezo kikuu cha ndani cha jamii yetu. Imekuwa ikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Ni sehemu ya utamaduni, ni alama ya umoja wa kitaifa na utambulisho wa jamii.

Bahati mbaya hata lugha yenyewe wengi wetu hatuijui vyema, nadhani kutokana na kutaka kuiga uzungu na mambo mengine yasiyo yetu, ndiyo maana pamoja na kujidai kuwa Tanzania ndiyo kitovu cha Kiswahili lakini walio wengi wanachanganya ‘r’ na ‘l’, ‘dha’ na ‘za’ n.k.

Wakati nikitafakari haya ninakumbuka maswali nililowahi kuulizwa na rafiki yangu mmoja: “Sisi Watanzania values (maadili) zetu ni zipi? Kama tunazo je, tunazikuza kadri muda unavyopita au bado tunaendeleza status quo (hali kama ilivyo)? Je, wakati wa mkoloni tulikuwa na values zipi na hii miaka 53 baada ya uhuru tunazo zipi?”


Tafakari.

No comments: