Jun 3, 2015

Mitandao ya kijamii inaweza kuwa darasa muhimu sana kwa wanataaluma

Baadhi ya waandishi wa Skripti wanaounda "Scriptwriters Club", 
walipokutana kujadili changamoto zinazowakabili. Mwandishi wa 
makala haya, Bishop Hiluka (nyuma ya mwenye shati nyekundu) 
ni mmoja wao
MIMI ni shabiki mkubwa wa mitandao ya kijamii, hususan Facebook, Twitter, YouTube nk. napenda kutumia mitandao hii ili kutafuta taarifa mpya na ku-share uelewa wangu (knowledge). Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu ya kutuunganisha na watu – aidha kusikia au kutaka kusikika. Natambua nguvu ya mitandao ya kijamii katika kufikisha ujumbe, na huwa nafanya kila niwezalo kuitumia ili kufikisha sauti yangu isikike na hatimaye kuleta tofauti inayokusudiwa. 

Lakini tofauti na hivi, wengi hawaitumii mitandao hii ipasavyo, ndiyo maana mimi si shabiki wa makundi (groups) yaliyopo kwenye mtandao wa WhatsApp, si shabiki kwa kuwa makundi mengi ya WhatsApp ni kama vijiwe vya porojo, hayana dira wala malengo, mara nyingi kinachofanyika ni kupiga porojo zisizo na maana.


Lakini kwa siku za karibuni nimekuwa nikihusihwa na makundi mawili, ambayo kwangu ni majukwa muhimu yanayonisaidia kukutana na wadau wengine muhimu ambao ama tulipotezana muda mrefu au sikuwahi kuonana nao kabla, pia yamekuwa na mchango mkubwa sana katika sekta ninazofanyia kazi. 

Katika makundi haya, moja linajumuisha wachoraji wengi wakongwe wa hadithi za michoro (comics) na jingine ni la waandishi wa filamu (scriptwriters). Kinachonifurahisha ni kwamba makundi yote haya mawili yana dira, na malengo yao yanafahamika, huku wanaoyaongoza (moderators) wakiwa makini kuhakikisha hakuna anayetoka nje ya (ma)lengo kusudiwa. 

Katika kundi la waandishi wa filamu, kwa mfano, mwandishi huomba waandishi wenzake wajadili maandiko yake ya filamu (script) ili kupata maoni, na hatimaye kazi yake huwa bora zaidi ya ilivyokuwa mwanzo. Au wakati mwingine mwandishi huomba waandishi wengine kufanya uchambuzi wa filamu ambayo imetokana na maandiko yake. Hii inafanywa kwa namna ya kuboresha kiwango cha uandishi ili asije akarudia makosa.

Uchambuzi wa filamu duniani ni njia nzuri ya kufanya tathmini ya filamu, iwe kwa mtu mmoja mmoja au kwa pamoja. Kwa ujumla, kazi hii ya uchambuzi wa filamu inaweza kugawanywa katika makundi mbalimbali kama vile mapitio ya filamu yanayofanywa na waandishi wa habari ambayo huonekana mara kwa mara katika magazeti, na njia nyingine maarufu, kupitia maduka ya usambazaji, au ukosoaji wa kitaaluma ambapo wasomi na wanataaluma katika filamu hutoa taarifa na nadharia ya filamu na kuchapishwa katika majarida. 

Wapitiaji wa filamu hufanya kazi kwenye magazeti, majarida, vyombo vingine vya habari, na machapisho mengine kwenye mitandao, hasa hupitia kazi mpya zilizotoka karibuni au zilizo mbioni kutoka ili kuuhabarisha umma. Kwa kuichambua filamu kitaaluma na kuweka wazi mapungufu na hata mazuri yake hasa kwa filamu ambazo zipo karibuni kutoka inaweza kuwa na ‘impact’ kubwa katika kile ambacho kama mapitio hayo yatakuwa yenye tija watu wataamua kuitafuta filamu. 

Ila kwa baadhi ya wapitiaji na wachambuzi hulenga zaidi katika kutafuta makosa tu na kushindwa hata kuyaona mazuri machache yaliyopo kwenye kazi husika jambo ambalo limekuwa linawachukiza waandaaji wa kazi hizo. 

Kwa kawaida, kama ni mpitiaji au mkosoaji wa filamu, kabla hujaanza kutoa makosa ni lazima kwanza ueleze yale mazuri (hata kama ni moja) uliyoyaona, kisha ndipo ueleze makosa uliyoyaona na kuelekeza namna nzuri ya kuyarekebisha ili mwenye kazi husika asije akayarudia tena. Hii ni aina nzuri sana ya kupeana darasa. 

Elimu inahitajika sana nchini kwa waandishi wa filamu, na hata kwa watayarishaji, waigizaji na waongozaji ili tuweze kuandaa kazi nzuri. Walio wengi wanashindwa kuelewa umuhimu wa uchambuzi au kukosoa na kukosolewa, kwani kukumbushana kwa kukosoana ndilo darasa linalohitajika. 

Lakini pia tunahitaji wachambuzi wenye taaluma ya filamu ambao watachambua kitaalamu na kuelekeza njia sahihi ya kufanya ili kuboresha, lakini nimekuwa nikishuhudia walio wengi ambao kazi yao ni kuponda tu bila kuelekeza nini cha kufanya. Uchambuzi wa filamu nchini kwa asilimia kubwa haujasaidia katika kutujengea mfumo mzuri wa kutoa kazi bora, bali umekuwa ni kichocheo cha kuangamiza tasnia hii na kujenga chuki katika ya wachambuzi na wasanii, waandaaji na wadau kwa ujumla. 

Upungufu mwingi unaojitokeza mara kwa mara katika filamu zetu wakati mwingine huzua tafrani hizi na zile ama hata wasanii husika kujikuta wakishuka thamani na kudharauliwa. Lakini hapo hapo wachambuzi wamekosa mbinu na wanashindwa kutumia njia sahihi ya kuwaelekeza wasanii hawa ili wajifunze. 

Aidha, hii imesababisha, kwa sehemu kubwa, wengi wa wachambuzi wa filamu kwenye magazeti, televisheni na redio kuonekana wanalenga katika kuzilinganisha filamu zetu na zile zinazotengenezwa katika tasnia za filamu zilizoendelea bila kujali mazingira, mifumo na bajeti, na hivyo kujenga chuki. Leo uchambuzi wa filamu kwa ujumla haushikilii nafasi ya kumwelimisha msanii bali kumbomoa. 

Wachambuzi wa filamu mara nyingi huwa ni wanataaluma waliosoma elimu ya filamu (film studies). Katika elimu hii ya filamu hufundishwa nidhamu (academic discipline) inayohusu mambo mbalimbali ya kinadharia (theoretical), kihistoria (historical), na njia bora za uhakiki makini wa sinema (critical approaches to the cinema).

Katika fani ya uchambuzi wa filamu, kuna vipengele ambavyo vinahusika sana katika filamu tu na havimo katika riwaya, tamthilia wala hadithi fupi. (angalizo: Tamthilia imo katika umbo la kitabu. Hizo wanazoziita tamthilia zinazooneshwa katika Runinga, sio tamthilia). 

Vipengele vya fani katika Filamu tu ni pamoja na sauti, milio, maleba (mavazi), matumizi ya muziki, miungurumo, matumizi ya taa hasa mwangaza; giza kwa madhumuni maalumu. 

Ni juu ya mtazamaji na mchambuzi wa filamu kujiuliza maswali iwapo Director (Mwongozaji wa Filamu) amevitumia hivi na kuvionesha vipengele hivi ipasavyo na kwamba vipengele hivi vimeongeza mvuto na uelewekaji wa maudhui ya filamu au baadhi ya vipengele hivi vimetumika vibaya na kuharibu utamu na ubora wa filamu. 

Kwa mfano: Je, Sauti za waigizaji zinasikika? Je, kuna makelele na sauti zizizohusika katika filamu? Je, mavazi (maleba) ya waigizaji yanajenga uhusika na dhamira ya filamu? Je, kuna vitendo vya aibu au vinavyohusu ngono na hivyo kwenda kinyume na maadili ya jamii yetu? Je, mavazi aliyovaa mwigizaji ni kweli yanaonesha huyo ni Hausigelo, Waziri, Mamantilie, Jambazi? n.k. 

Pia maswali mengine ni: Je, taa na mwangaza unatosheleza ama unaharibu filamu? Mandhari, Majumba na mazingira yaliyotumika katika onesho lolote yana lingana na hadithi, uhusika ama hadhi ya wahusika? Je, kuna ucheleweshaji wa tendo moja kwenda jingine; ama onesho moja kwenda onesho jingine bila sababu za maana za kanuni ya uandishi wa skripti ama ujuzi wa kutayarisha filamu? 

Ni muhimu sana kwa mchambuzi kuangalia mara tatu au hata zaidi kabla hajaandika uchambuzi/uhakiki wake wa filamu yoyote katika vipengele vyote viwili yaani kipengele cha Fani na cha Maudhui. 

Alamsiki.

1 comment:

Anonymous said...

Dah, umenipa somo kubwa sana Mwanaharakati. Hakika wewe utabaki kuwa 'Mwalimu' kwangu.