May 27, 2015

Wasanii wanapokubali kutumika kisiasa!

Bishop Hiluka, Simon Mwakifwamba na Michael Sangu
wakati wa harakati za kupigania ukombozi wa msanii
HISTORIA huwa haina haja na wale wote wenye kushindwa, labda tu kunukuu tarehe walizokutwa na umauti wao... Sekta ya filamu Tanzania ambayo ilionekana kupiga hatua siku hadi siku, siku za karibuni imeonekana kuanza kudorora. Ipo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Ni ukweli usiopingika, sekta ya filamu ipo chumba cha wagonjwa mahututi ikisubiri kupelekwa mochwari, hasa kama hatua za makusudi hazitachukuliwa kunusuru hali hii, hali ambayo kwangu ni kama mazingaombwe.

Wasanii wanapaswa kuwa macho sana na kuacha kuendekeza njaa, pia wanapaswa kutafuta taarifa na maarifa ili kuweza kung’amua mwenendo mbaya unaowapeleka kwenye shimo la mauti – ambapo kama juhudi hazitachukuliwa – tunakwenda kuizika sekta ya filamu, na kitakachofuatia ni historia.

Hali hii inatokana na walio wengi kuchukulia sekta ya filamu kama ni sekta ya walioshindwa katika sekta zingine, waliokosa cha kufanya au ni jukwaa la kuuza sura ili uonekane na maisha yasonge. Imekuwa ni sekta ambayo ni kati ya fani zisizo na vigezo vya kupima utaalam na ubora, kwa maana nyingine haichukuliwi kama taaluma, nadhani ndiyo maana serikali imekuwa haiipi umuhimu unaostahili.

Inasikitisha sana pale maisha ya wasanii wa filamu yanapokuwa maisha ya kuigiza, wanaonekana kama ni wenye neema, kumbe wanaongoza kwa kuwa na maisha mabaya. Na hata pale inapojitokeza neema basi huwa ni kwa muda fulani tu, hasa pale wanapotumiwa na wanasiasa kwa maslahi ya wanasiasa katika kufanikisha jambo lisilowahakikishia uhakika wa soko la kazi zao, wakati ambapo mipango mingi isiyotekelezeka hujitokeza, na kwa sababu wasanii, na hata viongozi wao kupitia vyombo vyao hawajui nini wanachokihitaji na muda upi, hujikuta wakinasa kwenye chambo.

Nakumbuka mwaka 2009 kulikuwa na vuguvugu kubwa la wasanii na wanaharakati wa filamu kupigania haki yao ili soko la filamu liweze kuleta tija miongoni mwao. Katika harakati hizo ambazo mimi nilikuwa Katibu Mkuu wa harakati, hatimaye zilifanikiwa kuanzisha shirikisho la filamu (TAFF), lililoonekana kuwa mkombozi wa matatizo ya wasanii na watengeneza filamu nchini.

Wakati wa harakati hizo tulisukumwa zaidi na uzalendo wa kutaka kuiokoa sekta ya filamu na kuliokoa soko la filamu dhidi ya majangili wa kazi za filamu, ingawa hadi sasa soko la filamu (japo lilianza kuonesha matumaini) bado limeendelea kubaki kuwa kitendawili. Inasikitisha kuona mtu anatengeneza filamu lakini anaishia kulandalanda na filamu yake mkononi huku wasambazaji wakiwa hawaitaki kwa kuwa tu hakuchezesha wanaoitwa masupastaa bila kujali ubora wa filamu husika.

Uanzishwaji wa shirikisho la filamu ulitarajiwa na wengi kuwa lingekuwa muarobaini wa matatizo, lakini kitu ambacho wasanii na wadau hawakukitambua ni kuwa, chombo hiki kilianzishwa kisiasa pasipo kuangalia lengo hasa la uanzishwaji wake. Ninachokiamini katika ukombozi wa wasanii ni kuwa na Umoja wa kweli, wenye nguvu utakaohakikisha kilichokusudiwa kinafanyika huku viongozi wanaoongoza wanakijua na kunakuwepo mikakati endelevu katika ustawi na maendeleo ya sanaa. Lakini badala yake kumekuwepo chuki, majungu na ubinafsi miongoni mwa wote: viongozi wa wasanii na wasanii wenyewe!

Nikiwa mmoja wa waliokuwa wanaongoza harakati za kuipigania sekta ya filamu irasimishwe, wasanii watambulike na wawezeshwe, kwa kuamini kuwa ni vigumu kwa fani yoyote kukua kama si rasmi na wala hakuna vigezo vya upimaji wa ubora. Niliamini kuwa mchakato wa kurasimisha sekta ya filamu siyo jambo gumu, kilichokuwa kinatakiwa ni nia na uelewa wa wadau wa sanaa wakiongozwa na viongozi wa serikali ambao wamepewa jukumu la kufanikisha kile kinachoitwa maisha bora kwa kila Mtanzania.

Ukweli unabaki palepale, kazi yoyote ya sanaa inahitaji mazingira bora ili iweze kustawi, mazingira bora kwa msanii ni ulinzi wa kazi zake, kuwezeshwa ili afike anapohitaji, soko la uhakika pamoja na kuthaminiwa. Sekta ya filamu inakabiliwa na matatizo makubwa.

Pia kutokuwepo kwa vigezo vya kupima utaalam wa fani kunafanya wasanii waendelee kuwa duni, wasiothaminika na kubaki katika sekta isiyo rasmi ambayo haiwezi kuchangia maendeleo ya taifa, japo tunaaminishwa kuwa imerasimishwa. Lakini urasimishaji halisi wa sekta ya burudani utabaki kuwa ndoto ya mchana kwa wasanii kama wataendelea kukubali kutumika kisiasa, na serikali kuendelea kutafuta ufumbuzi kwa kutumia njia za kisiasa badala ya kitaaluma, huku wafanyabiashara wakiendelea kupata neema kwani hali hii inawapatia faida kubwa bila jasho.

Ni wazi hakuna taaluma isiyo na muongozo, mipaka, miiko na maadili katika utendaji. Sanaa ni moja ya taaluma ingawa si hivyo kwa Tanzania.

Hata siku moja, serikali haijawahi kuwashirikisha wasanii au kuwahusisha kwa namna yoyote katika kujadili fursa za masoko katika mikutano inayoandaliwa na mabaraza ya biashara. Na inashangaza, yale malengo tuliyokuwa nayo wakati wa kupigania uundwaji wa shirikisho yamefutika, na sasa chombo hiki kimekuwa sehemu ya wachache kuangalia namna gani wataweza kuishi, kujenga, na kuwa karibu na viongozi wa kisiasa, hasa wagombea na watangaza nia ya urais.

Kwa sasa hakuna ajenda ya ukombozi wa wasanii, bali ni jinsi gani wasanii wanavyoweza kutumika/ kutumia umaarufu wao kuhakikisha mgombea fulani anapata madaraka, kwa kigezo kuwa anajali maendeleo ya vijana. Inashangaza kuona wasanii wanaacha kupigania haki zao ikiwa ni pamoja na soko la bidhaa zao na kujiingiza kwenye masuala tofauti kama siasa.

Tumefikia hatua mbaya, wasanii wameunda timu kulingana na wagombea ili kutumika kumpigia kampeni mgombea fulani. Wasanii ni kioo cha jamii, wanao uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa jamii moja kwa moja kwa njia ya maigizo na kazi nyinginezo. Lakini, kutumika kwa mambo yasiyo na tija kwa taifa ni jambo nitakalolipinga hata kama litanigharimu.

Katika masuala ya jamii na pale wanapohitaji msaada, wasanii wanapaswa watafute njia sahihi na si kushabikia kulinda maslahi ya baadhi ya wanasiasa, eti kwa ahadi kuwa akiingia madarakani atawekeza nguvu kwa wasanii na vijana. Kufuatia mikakati na harakati walizonazo sasa – za kutumika – utatambua kuwa si wao tu hata viongozi wao wanaowaongoza pia hawajui kwanini walianzisha umoja huo? Hawajui lengo hasa lilikuwa nini? Na hawajui wanahitaji nini?

Wasanii wanapaswa kupima faida za kujipendekeza kwa wanasiasa, wanapaswa kuwa makini sana la sivyo watajikuta wanapandikiza mbegu za kujimaliza. Hivi kweli hii ni sahihi kwa wasanii kukubali kuweka kando masuala ambayo yangewasaidia kuboresha hali zao, kuweka kando harakati za kupigania mapendekezo yaliyowasilishwa serikali kwa ajili ya sera ya filamu yapitishwe na serikali, na badala yake wanajadili jinsi ya kuwaangamiza wenzao wenye kutofautiana nao, na kuegemea mlengo wa kisiasa?

Baada ya kupata shirikisho, wengi tulitegemea wasanii wangeanza juhudi za kujikomboa lakini badala yake hata wale waliojitokeza hadharani kuonesha kuwa ni wakombozi kumbe walikuwa wanatafuta jukwaa la kuuza sura ili waonwe na wanasiasa na mapedejhee, ili wapate nafasi ya kumaliza matatizo yao. Nafasi walizopata zimekuwa mwanzo wa kutengeneza makundi, fitina, chuki na hata ukiukaji wa sheria na taratibu za utendaji kazi, wakidhani wanayo hakimiliki ya kuongoza milele.

Hivi kweli hiki ndicho tulichokuwa tukikipigania? Leo hii wasanii wamekuwa watu wa kujikomba na kubembeleza ufadhili wa wanasiasa na wakati huohuo kulaumu kutothaminiwa na serikali! Vyama vya kisanii vimekuwa vikisajiliwa na kufa na kwa mwendo huu hawataweza kuifikisha sanaa mahali popote pa kuthaminiwa kwani ndani yake kumejaa unafiki na kutoambiana ukweli.

Na hata pale baadhi ya wasanii walipojitokeza kuwaambia wenzao ukweli wamechukiwa, kutukanwa na kutengwa, hali inayoashiria mgawanyiko mkubwa katika sekta ya filamu. Wasanii sasa wamebadilisha ajenda, badala ya kupigania maslahi ya sekta ya filamu sasa wanapanga kuzunguka nchi na wanasiasa kuwapigia debe!Wanapaswa kujitafakari upya kabla hawajapotea, na sekta ya filamu kuzikwa rasmi.

No comments: