May 13, 2015

Kuna nini Sekta ya Utamaduni?

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, 
Dk. Fenella Mukangara
MUUNDO wa uendeshaji wa sekta au shughuli yoyote hutokana na azma ya kushughulikia matatizo yaliyopo. Muundo huo huwa ni nyenzo ya awali kabisa ya kutatua matatizo hayo. Kwa hiyo idara na sehemu zinazoundwa katika asasi na aina ya wataalamu wanaoajiriwa huzingatia majukumu na kazi za asasi ile katika muhula husika.

Ingawa Sekta ya Utamaduni imekuwa katika mfumo wa serikali tangu 1962, nafasi yake katika maendeleo ya taifa bado haijatambuliwa kikamilifu. Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Katika kipindi chote tangu mwaka 1962, shughuli za sanaa zilipewa nafasi katika mfumo wa kiserikali lakini zimekuwa hazithaminiwi. Haiyumkiniki muundo wa Idara ya Utamaduni leo kuwa ileile ya mwaka 1962!

Muundo wa sasa wa Serikali wa kusimamia Sekta ya Utamaduni si muundo muafaka. Lipo tatizo la kusambaa kwa sekta. Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 na kuundwa kwa Serikali kulikofuata, Sekta ya Utamaduni iliwekwa katika Wizara nne tofauti. Sekta ndogo za Sanaa na lugha zilikuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, Sekta ndogo ya Nyaraka ilikuwa Ofisi ya Rais (Utumishi), Sekta ndogo ya Michezo ilikuwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo na Mambo ya Kale, ilikuwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Serikali ikaunda Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, huku Idara ya Utamaduni ikisahaulika kutajwa wakati wa kutangaza Baraza la Mawaziri, ingawa baadaye tulipewa taarifa kuwa jambo hilo lilitokea kwa bahati mbaya, na hivyo wizara hiyo kubadilika na kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kwa hiyo, Sekta ndogo za sanaa, lugha na michezo zikawekwa pamoja wakati nyaraka, mambo ya kale na makumbusho zikabaki zilikokuwa kabla ya uchaguzi.

Ukiangalia kwa makini, mfumo huu unaweza kufaa zaidi kwa utendaji wa Serikali Kuu, lakini unaweza usiwe muafaka kwa utendaji wa tawala za mikoa, serikali za mitaa na wadau wengine nje ya serikali, kwa kuwa mambo ya utamaduni yanaingiliana.

Kwa kuelewa mapenzi aliyonayo Rais Jakaya Kikwete kwa sanaa, nilitegemea uongozi wake wa Awamu ya Nne ungetuanzishia wizara inayojitegemea ya Vijana, Utamaduni na Michezo na kuifanya Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kuwa na sehemu za miundombinu ya utamaduni/sanaa, utafiti na ukuzaji wa masoko ya bidhaa na kazi za utamaduni/sanaa, utawala na uendeshaji wa shughuli za utamaduni, na ajira ya wasanii.

Pamoja na kwamba zipo Wizara ambazo zingeweza kushughulikia maeneo haya, lakini hawafanyi hivyo. Wizara ya Miundombinu haijishughulishi na miundombinu ya utamaduni, Wizara ya Viwanda na Biashara haitafuti masoko au kutangaza kazi za utamaduni, hata Bodi yake ya Biashara ya Nje. Idara ya Utumishi wa Umma haihusiki kabisa na kuhakiki au kushauri juu ya miundo ya utawala na uendeshaji ya asasi na vikundi vya utamaduni vilivyo nje ya mfumo wa serikali, wala Wizara ya Kazi haijihusishi kwa dhati na taratibu au wingi wa ajira za wasanii!

Nyaraka na Mambo ya Kale ni fani za uhifadhi wa urithi wa utamaduni. Urithi usioshikika,na hata baadhi ya unaoshikika kama sanaa za kuchonga, kuchora, sanaa zinazohifahidhiwa katika kanda za sauti na video na fasihi, unazalishwa katika Wizara nyingine. Utendaji pia unaingiliana. Lipo tatizo la kuondolewa kwa Ofisi ya Utamaduni katika Sekretariati za Mikoa. Nani anamshauri Mkuu wa Mkoa kuhusu Utamaduni?

Nani anasaidia kufuatilia na hata kusimamia shughuli za utamaduni kwenye ngazi ya mkoa kama vile mashindano au matamasha ya michezo na sanaa? Hapa inavyoonekana ni kwamba Serikali imeamua kujitoa kabisa katika kushughulikia utamaduni katika ngazi hii! Hata waliopewa dhamana kwenye Kamati za Michezo, Sanaa, Lugha, Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Jukwaani ngazi ya mkoa, bado hawana fungu la kutosha kushughulikia hayo.

Tatizo la halmashauri ni kuwepo kwa watumishi wachache katika halmashauri. Karibu halmashauri zote zenye maafisa utamaduni zina mtu mmoja tu. Lakini pia zipo baadhi ya halmashauri ambazo hazina mtumishi hata mmoja, na hakuna anayeshtuka kabisa! Si TAMISEMI, Mkurugenzi Mtendaji wala Baraza la Madiwani! Tatizo hapa siyo la uwezo mdogo wa bajeti tu, bali pia uelewa mdogo wa dhana na dhima ya utamaduni katika mkondo mzima wa serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Kama zilivyo shughuli zote, kila shughuli ina mahitaji ya miundombinu mahsusi, vivyo hivyo kwa shughuli za utamaduni. Sanaa za maonesho, kwa mfano, zinahitaji majengo maalumu yenye majukwaa upande mmoja, na sehemu ya kukaa watazamaji inayoinuka kuelekea nyuma. Pia zinahitajika taa maalumu kwenye majengo hayo, na kunahitajika vipaza sauti kama ukumbi ni mkubwa. Kama hiyo haitoshi, kunahitajika kuwepo vyoo na mabafu ya wasanii na watazamaji, kunahitajika mapazia.

Nchi yetu haina kwa sasa kumbi zinazokidhi mahitaji haya. Kulikuwa na kumbi za sinema karibu katika kila mji mkuu wa Mkoa na kwenye Wilaya. Baada ya biashara ya sinema kudorora na waendeshaji kuzitelekeza, ilidhaniwa kuwa kumbi hizo zingefanyiwa marekebisho kidogo tu na zikaweza kufaa kwa sanaa za maonesho. Haikuwa hivyo! Kumbi hizo zimegeuzwa kuwa vitu vingine kabisa.
Baadhi zimegeuzwa kuwa maghala, baadhi zimekuwa sehemu za biashara za ulevi, baadhi maduka. Na yale majumba ya Starehe (Community Centres) yaliyojengwa katika Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya, sasa hivi mengi ni vitu tofauti kabisa na ilivyodhamiriwa. Matokeo haya ni ishara kuwa mahitaji ya utamaduni hayashughulikiwi tena!

Sekta ya Utamaduni kwa sasa ina changamoto kubwa, ni kama imetelekezwa na wadau – walio ndani ya serikali na asasi zake na wale ambao tupo nje ya serikali. Badala ya kuunganisha nguvu zetu ili kuiokoa, tunalumbana! Tumeshindwa kuunganisha ujuzi wetu na elimu yetu ili jitihada zetu ziwe na mafanikio kwa maslahi yetu na vizazi vyetu vijavyo.

Kwa miaka mingi, kwa kutumia mtindo wa sanaa kwa maendeleo, wasanii wamekuwa wakitumiwa na sekta nyingine kutetea mambo ya sekta hizo na kushawishi watu kukubaliana na hoja na misimamo ya sekta hizo. Huu sasa ni wakati wa wasanii kutumia mtindo huo, na mingine, kutoa hamasa kwa sekta yao ya utamaduni!

Serikali inapaswa kuiokoa sekta hii kwa kuelekeza nguvu katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wasanii. Serikali zinazothamini utamaduni wa nchi zao hutafuta gharama za mafunzo kwa wasanii wao, hivyo, kutafuta gharama za mafunzo kwa wasanii wa nchi hii lilipaswa kuwa jambo la kwanza kabisa kwa serikali katika kuutambua mchango wa sekta ya utamaduni.

Mafunzo ni kitu muhimu kwa mtu yeyote yule katika kumuongezea stadi zake za utendaji. Kwa jumla kuna upungufu mkubwa wa mafunzo ya fani mbalimbali za utamaduni, ikiwemo sanaa. Wasanii wengi wanajifunza kwa kuiga wenzao. Ingawa hii ni moja ya njia za kujifunza, tatizo lake ni kuwa huchukua muda mrefu na haina uhakika kama kinachoigwa ni sahihi au la.

Matokeo yake ni wasanii wengi kufanya kazi bila kupitia mafunzo maalumu na kwa hiyo ufanisi wao kuwa chini. Kuna tatizo pia la mafunzo yatolewayo kutokidhi kikamilifu mahitaji ya wasanii kutokana na upungufu wa walimu waliobobea, vifaa vya mafunzo na vitabu. Kwa hiyo eneo hili la mafunzo linahitaji msukumo siyo tu wa kuongeza nafasi bali pia ubora wake.Naomba kuwasilisha.

No comments: