May 6, 2015

SEKTA YA FILAMU: Kenya inapiga hatua wakati sisi tunasinzia

Gavana wa Kaunti ya Machakosi, Alfred Mutua
SEKTA ya Filamu nchini Kenya imetajwa kama sekta muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa nchi hiyo, hasa katika kuvutia watalii na kutoa nafasi za ajira kwa vijana wa Kenya. Lakini sekta hiyo kwa muda mrefu imekosa wafadhili wa kuiwezesha kufikia kiwango hicho na kuendelea kubaki nyuma huku sekta zingine kama utalii zikinawiri.

Sasa sekta hii imeanza kupiga hatua kubwa baada ya kupigwa jeki na hazina ya vijana nchini humo, ambayo ilitenga kiasi cha shilingi milioni 300, ili zitumiwe na vijana kwa njia ya mikopo katika kuijenga sekta hiyo na kuiimarisha nchini kote. Kwa miaka sasa sekta hii ya filamu nchini Kenya imekuwa iking'ang'ana kujikita, lakini isiwezekane.

Wadau katika sekta ya filamu wanabainisha kuwa sekta ya filamu nchini humo ilikosa kupiga hatua kutokana na ukosefu wa wafadhili ambao mara nyingi huwa wanaogopa kuwekeza fedha zao kwa kuwa hawana imani kama sekta hii inaweza kuwalipa. Kutengwa kwa fedha hizo kulikuja miezi michache baada ya rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta, kutangaza kujitolea kuimarisha sekta hiyo.

Tofauti na jinsi tunavyoichukulia sekta hii nchini Tanzania, sekta ya filamu nchini Kenya imetambuliwa rasmi kama sekta ambayo inaweza kuleta mwamko mpya wa kiuchumi, kupitia kuunda fursa za ajira kwa vijana, kuvutia utalii na pia uwekezaji. Mambo mengine ambayo Wakenya wamegundua kuwa wanaweza kufaidika nayo kutoka kwa sekta hii ni pamoja na kuongeza pato la taifa na la mtu mmoja mmoja.

Katika kuhakikisha sekta hii inakua na kufikia kiwango bora zaidi, Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imeweka masharti kwa vyombo vya habari kuwa na asilimia 60 ya vipindi vya ndani kwa vyombo vya habari vya Kenya. Mpango huu mpya unalenga kuwapa Wakenya soko la wazi la filamu, ili kuonesha jinsi walivyo na utamaduni ulio mpana. Sekta ya filamu ya Kenya kwa sasa inaingiza zaidi ya shilingi bilioni sita (zaidi ya trilioni 1 za Tanzania) kila mwaka.

Tume ya filamu nchini Kenya inasema kuwa inaendelea na harakati za kuweka mikakati muhimu ya kuboresha sekta hiyo ili iweze kuzifikia sekta zingine thabiti, kama vile kilimo na utalii. Aidha tume hiyo inataka kuongezwa kwa ushuru unaotozwa kwenye filamu zinazotoka nje ya nchi, ili kusaidia kujikita kwa sekta hiyo nchini humo.

Hali hii ni tofauti kabisa na ilivyo nchini Tanzania, ambapo filamu za nje zimezagaa mitaani (filamu ambazo zinatokana na uharamia) na hakuna juhudi zinazofanywa kuhakikisha serikali inaongeza ushuru kwa kazi hizi ili kulinda kazi za ndani.

Lupita Nyong'o

Pia Wakenya wameuchukulia ushindi wa Lupita Nyong'o, katika tuzo za Oscar wa muigizaji bora msaidizi katika filamu ya “Twelve Years a Slave” kama hamasa, ambapo watengenezaji wengi wa filamu nchini Kenya wamekuwa na matumaini ya kufanya vizuri zaidi, kwamba kupitia vipawa vyao wanaweza kutambulika kimataifa kama Lupita.

Katika Kaunti ya Machakos nchini humo, Gavana wa Kaunti hiyo, Alfred Mutua, ameanzisha kituo maalum cha kutengeneza filamu, kukuza vipaji vya watengenezaji filamu pamoja na burudani, maarufu kwa jina la Machawood, kituo kitakachokuwa cha aina yake barani Afrika.

Nimewahi kuwa na mazungumzo na maafisa wa Machawood, ambao walikuwa wakiangalia fursa zilizopo nchini na namna wanavyoweza kuanzisha ushirikiano kati ya kituo hiki na wasanii waliopo Tanzania, ushirikiano kama uliopo baina ya wasanii wa Nigeria na Ghana, uliotengeneza Nollywood.

Afisa Mkuu ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa mradi huu wa Machawood, Peter Kimeu, aliwahi kusema kuwa mpango huo wa Machawood umeanzishwa ili kumaliza changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta hiyo na kuleta tumaini katika sekta ya filamu nchini Kenya na pia katika bara la Afrika.

Kwa mujibu wa afisa mkuu huyo, sekta ya filamu ya Kenya imekuwa ikikua taratibu kwa miaka mitatu, kwa sasa Kenya kupitia mradi huu inataka kufanya filamu ziwe katika kiwango cha juu sana barani Afrika, hivyo, wanaangazia mbele sana, zaidi ya Machakos na zaidi ya Kenya. Wanataka kuanzisha shule na kutoa mafunzo ya hali ya juu ya filamu kwa sababu hapa barani Afrika hakuna shule ya aina hiyo.

Na kwa mujibu wa Tume ya Filamu ya Kenya, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sekta ya filamu iliajiri zaidi ya watu 4,000. Aidha taasisi hiyo inasema sekta hiyo kwa mwaka uliopita iliipatia Kenya pato la zaidi ya shilingi zaidi ya shilingi bilioni sita, na mikakati inaendelea kuwekwa ili kuona pato hilo likiongezeka.

Hata hivyo, mradi wa Machawood pekee ukikamilika, unalengwa kuwa na uwezo wa kuajiri zaidi ya watu elfu kumi, na kuwa na uwezo wa kutoa pato la mabilioni ya shilingi kwa mwaka. Huu ni mradi utakaoipa Kenya fursa ya kuendelea kutoa wanafilamu wa kimataifa, na kuongeza kwa asilimia kubwa pato la taifa. Utafiti unaonesha kuwa sekta ya filamu inaweza kubadili kabisa uchumi wa taifa, na kuifanya Kenya kuwa taifa kubwa kiuchumi Afrika, nyuma ya Nigeria na Afrika Kusini.

Utafiti unaonesha kuwa sekta ya filamu ya Kenya inaweza kuajiri watu laki mbili na nusu na kuingiza pato la zaidi ya shilingi bilioni 40 (bilioni 800 za Tanzania), pato ambalo ni zaidi ya sekta ya kilimo. Sekta ya elimu ni moja wapo ya sekta ambazo huchangia ukuaji wa sekta zingine katika kila taifa popote pale duniani.

Wadau wa filamu nchini humo wanahisi kwamba mradi wa Machawood utakuwa Baraka kubwa kwao, wakibainisha kuwa katika muda wa miaka kadhaa ijayo maisha ya wasanii na wadau kwa ujumla yatabadilika sana.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, kupitia Halmashauri ya Mawasiliano nchini Kenya imevisisitiza vyombo vya habari nchini humo kuwasilisha asilimia 40 ya maudhui ya ndani (local contents) kwenye vipindi, filamu na nyimbo katika televisheni na radio kuanzia mwaka huu ili kuhakikisha sekta ya burudani inapiga hatua kubwa. Katika hatua nyingine, Wizara ya Habari na Mawasiliano ya Kenya ilishatangaza kushirikiana na vyombo vya habari vya China kutokana na ufanisi wao mkubwa waliopata kwa kuwekeza mfumo wa dijitali.

Kufikia mwaka 2018 televisheni na radio zote za Kenya zitatakiwa kuwasilisha vipindi, filamu na nyimbo zilizo na asilimia 60 ya maudhui ya ndani. Hatua hii inalenga kutoa fursa ya ubunifu, ukuzaji wa vipaji pamoja na kutoa fursa za ajira.

Kufuatia ushirikiano huu China imepewa nafasi ya kuwasilisha vipindi na filamu za Kichina zinazotafsiriwa kwa Kiswahili na kuoneshwa kwenye televisheni za Kenya. Vipindi hivi vinavyohusu mambo ya kimila na kitamaduni vimeorodheshwa miongoni mwa asilimia 40 ya maudhui ya ndani ya nchi kama inavyosema sheria mpya ya matangazo ya maudhui ndani ya Kenya.

Katika mpango huu, ulifanikisha televisheni ya taifa ya Kenya ya KBC, ilianza kuonesha kwa mara ya kwanza katika historia tamthilia ya China iliyotiwa sauti za Kiswahili na Wakenya na Watanzania miaka miwili iliyopita. Tamthilia hiyo maarufu hata hapa Tanzania na inaitwa Dodo na mama wakwe zake. Tamthilia hii imewahi kuoneshwa nchini kupitia TBC1.


Alamsiki.

No comments: