Apr 22, 2015

Tunahitaji mapinduzi ya kweli ya sekta ya filamu Tanzania

Simon Mwakifwamba, Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania
Dilesh Solanki, Mkurugenzi wa Kampuni ya Steps Entertainment
HALI ya tasnia ya filamu nchini kwa sasa inakatisha tamaa, wasanii na viongozi wao wengi wamefikia ukomo wa kufikiri, wanaonekana kuridhika na hali ilivyo au pengine wamekata tamaa, ingawa bado wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi. Vyombo vya kuwasimamia, likiwemo Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), vimekosa dira.

Ni wasanii wenyewe kupitia chombo chao, ndiyo wamesababisha sekta hii ishuke kutokana na tabia zao, hii inawagusa wasanii wote, wanawake na wanaume. Wamechukulia kada hii kama sehemu ya kujitangaza zaidi kuliko kazi, viongozi wao wanachukulia nafasi zao kama fursa ya kuwakutanisha na wakubwa au matajiri ili wapige vibomu, ilimradi siku ziende.

Wanalilia kuthaminiwa wakati wamesahau kuwa mambo yote haya ni lazima yaanze ndani yao wao kisha yaende kwenye jamii. Wengi wamekosa kujipa thamani na kujipenda, na hivyo imekuwa vigumu kutoa kwa wengine. Wengine wengi wanahisi hawana stahili ya mambo yote hayo. Wanajitazama wenyewe kama dhaifu kuliko wengine ama bora kuliko wengine.

Kwa hali ilivyo wanapaswa wajue kwamba watu wanaoshabikia ujinga ni wachache sana; na watu wa maana wanaoelewa nini wanafanya ni wengi zaidi na hawana muda na upumbavu. hivyo imefika mahali watu wanaendelea na mambo yao ya maana, na kuupa kisogo kabisa upande wa filamu, sekta inayoongoza kwa umbumbumbu, majungu na mambo yanayotia kichefuchefu katika jamii.

Viongozi wa wasanii waliopewa dhamana, wameshindwa kuifanya sekta hii kuthaminiwa, imefikia hatua mtu mwenye busara hawezi kushughulika kabisa na filamu zetu maana vituko vyao vinawafanya kuonekana hawako ‘serious’ bali wapo kuuza sura na kujinadi uongo mtupu wa maisha yao kwamba wana mafanikio wakati hamna lolote la maana. Tunahitaji mapinduzi ya kweli kama tunataka sekta hii iheshimike, kwani jamii ya watu wenye busara ni asilimia kubwa.

Tatizo liko pande zote, kuanzia kwenye soko la filamu ambalo linadhibitiwa na wafanyabiashara wachache, wasiozingatia taaluma na wasioongozwa na weledi, wasanii wenyewe hadi kwenye vyama na shirikisho. Soko la filamu hata halieleweki kwa sasa. Hali hii imesababisha watu kushindwa kutofautisha iwapo wanachokiona ni filamu, maigizo au mkanda wa harusi wenye “taito” za majina ya wasanii na wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia!

Nchi hii imebarikiwa kuwa na wacheza filamu wengi wazuri, waliokwenda shule na hata ambao hawakwenda shule, ingawa ulipwaji wao haueleweki unawaweka katika fungu gani la mshahara, mfanyabiashara mmoja tu anaamua kuhusu malipo yao, na kuna mambo ya chinichini yasiyoeleweka kwa uwazi.

Soko kwa sasa limebakia kwa mwenye pesa ambaye ndiye anayeamua hadithi iweje, wengine waliobaki wanaitiwa kazi, na hawapaswi kuuliza mara mbili bali kukubaliana na soko linavyotaka, ndiyo maana binafsi nimekuwa nalilia sana uwepo wa sera ya filamu, ili kuwasaidia wasanii, watengeneza filamu na wadau kufanya kazi zake kwa ufanisi, badala ya hali hii ya sasa ya mwenye nguvu ndiyo anakula.

Nimekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) kwa miaka miwili, hadi hivi majuzi nilipoamua kukaa kando, sababu kubwa, japo nilipigania mfumo mna dira lakini nilijikuta nikiwa peke yangu, wengi wakitumia nafasi zao kama fursa ya kuula. Shirikisho halina dira, mfumo uliopo ni mbovu na haufai kabisa. Taasisi hii imeundwa kisiasa lakini si kupigania ustawi wa wasanii na wadau wa filamu.

Tasnia ya filamu nchini kwa sasa inasikitisha. Wasanii wetu wanafanya filamu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani tu (home videos) na wakiingia kwenye maonesho ya bendi wakarushwa, wanaridhika! Hata viongozi waliopewa dhamana wameridhika! Au hapa ndipo walipotaka wafike? Kwanini hawana mipango ya kupasua mawimbi waende mbali zaidi nje ya mipaka? Kama wameamua kuridhika hapo walipofika basi wasubiri kushuka, kwa sababu kiukweli hawawezi kukaa juu milele! Hebu tujiulize, kwanini wameridhika hivi? Nini tatizo?

Kila siku mazingira ya kufanya filamu Tanzania yanakatisha tamaa, wizi wa kazi pia umezidi na wasambazaji wengi wa filamu wamekimbia, ingawa tasnia ya filamu inashika nafasi ya pili kwa kukubalika zaidi baada ya muziki. Idadi ya watazamaji na wafuatiliaji inathibitisha hilo!

Bahati mbaya tasnia hii inaelekea kufa kibudu. Ndiyo, Tasnia ya Filamu nchini inakufa kibudu kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa. Kama hatutapata viongozi wenye maono (dira). Hali ni mbaya sana, licha ya kuwa ndiyo fani inayoongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi nchini. Tukubaliane hapo kwanza!

Makosa kwenye filamu zetu yapo mengi. Mbaya zaidi yote si makosa yanayohitaji kuonwa na wataalam pekee. Hata asiye na utaalam wa sauti atajua kwamba sauti kwenye filamu zetu ni tatizo, asiyefahamu mambo ya script akitazama tu atajua, asiyejua umuhimu wa muendelezo (continuity) naye hali kadhalika, achilia mbali yule asiyejua Kiingereza kwa ufasaha, inamuhitaji elimu ya kujua cha kuombea maji kung'amua kwamba ‘subtitle’ zetu ni majanga. Mtiririko wa hadithi na uhalisia ni tatizo sugu. Inasikitisha sana! Leo sitaki kugusia hata moja katika hayo!

Ngoja nizungumzie upande wa mapinduzi ya ujumla. Kwanini tasnia hii inaporomoka badala ya kukua zaidi? Kwanini hakuna mabadiliko chanya? Kwanini filamu nchini zimebaki kuwa na mabaka mabaka ya ulalahoi? Kwanini hatuvuki mipaka? Kwanini hatufanyi kweli? Kwanini muziki unapaa zaidi kuliko filamu? Nini tatizo?

Jibu la yote haya ni moja, wasanii kupitia vyombo vyao waanze kwanza kutengeneza 'Image' nzuri kwenye jamii. Maana kwa sasa imeshachafuka. Tasnia ya filamu ina taswira ya uhuni kupitiliza. Na hii ni kutokana na wasanii wakubwa kukumbwa na kashfa chafu. Kucha kutwa magazetini kuandikwa upuuzi, pengine wapo wanaolipwa kwa kuuza gazeti, lakini sidhani kama wanacholipwa kina thamani kubwa kupita kazi wanazofanya.

Baada ya hapo uanzishwe mkakati madhubuti. Itengenezwe mipango madhubuti na mikakati itakayowaongoza kufanya kazi kwa umakini, na kuacha kutumika kisiasa. Inawezekana ipo mipango ilishajaribiwa huko nyuma, lakini kwa kuwa hakuna dira imekuwa ngumu. Kunapokuwepo dira kila kitu kinawezekana.

Watanzania na wapenzi wa filamu zetu ni wengi sana. Hatuna tu utaratibu wa kufanya utafiti ili kuwa na data kamili, lakini kwa kuangalia tu ni dhahiri filamu zetu zinaweza kufanya vizuri kuliko ilivyo sasa. Ni basi tu viongozi wa wasanii wanachosha. Sijui dira yao ni nini hasa! Ni ajabu mtu kuua ajira yako kwa mikono yako mwenyewe!

Tunasahau wapenzi wa hizi filamu (japo hawazitazami) ni watu wenye uwezo mkubwa pengine hata wa kuwekeza. Achana na “Mapedejhee” wanaohonga kwa lengo la kufurahisha nafsi zao, kuonekana, au malengo yao binafsi yasiyo na tija (japo wakitumiwa vizuri inaweza kusaidia). Hapa nazungumzia Matajiri, wafanyabiashara wakubwa, wanasiasa, hata mawakala wa biashara, wakitumika vizuri, watafanya kitu.

Kinachohitajika ni ushawishi tu kutoka kwa chombo cha wasanii. Kihakikishe kina mipango na uwezo wa kushawishi watu/mashirika/makampuni kuwekeza. Serikali pengine imeshindwa hili! Na ushawishi huja pale penye tija. Mtu aone umuhimu wa kufanya hivyo, na si kuchoma pesa zake bure. Tujiulize, inakuwaje michezo mingi inadhaminiwa? Soka, Ngumi, Riadha, Urembo n.k? Kwanini isiwe kwenye sekta ya filamu? Tujikague upya kabla hatujachelewa.

Pia kuna hiki kilio cha wasanii wengi kushindwa kufanya filamu zenye ubora kwa sababu ya kukosa mitaji. Wanalalamika hawana fedha za kutosha kutengeneza baadhi ya stori. Ni kweli kabisa. Na hii pengine ndiyo sababu kubwa hata thamani ya kazi zao kwa wasambazaji inashuka siku hadi siku. Hii ni kutokana na bidhaa kuwa ni low quality.

Ni wajibu wa chombo chao kuweka mikakati ni vipi watapata mitaji. Kisha watafute soko zuri la kuuza kazi zao kwa bei itakayowanufaisha, si kama sasa wanavyopangiwa na “Wahindi”. Kupitia viongozi wanaotambua majukumu yao, wasanii wapiganie access kubwa kutoka serikalini ili waweze kutambulika rasmi na kuaminiwa. Haya yote yanawezekana endapo viongozi wa shirikisho la filamu nchini watakuwa na dira na sauti ya nguvu, na waache kutumika kisiasa.

Mfumo mzuri na dira ndivyo vitakavyowafanya waandaaji wa filamu na wasanii waanze kushirikisha wataalam kwenye kazi zao. Hii ni faida kwani 'uhalisia' wa filamu utakuwa maradufu! Ushirikishwaji uanzie kwenye masuala ya stori, uzalishaji mpaka kwenye suala zima la masoko. Uwanja huu ni mpana sana, ila penye dira mwanga unaweza kuonekana!

Ieleweke, filamu hazitengenezwi kama chombo cha kutoa mafunzo na ujumbe tu bali kama ala ya kuchochea watazamaji kutafakari na kuzua majadiliano. Watengenezaji wa filamu walio makini huonesha imani yao katika jamii kutambua, kuchunguza na kutatua masuala yao wenyewe waliyoyapa kipaumbele, kupitia njia yao wenyewe.


Alamsiki.

No comments: