Nov 28, 2011

Ili kuboresha filamu zetu tuanze kwanza na script

John Riber

Moja ya semina zilizoandaliwa na MFDI

“MWANAHARAKATI, nimekuwa nafuatili sana makala zako, kuna makala moja ilinigusa sana, hasa pale uliposisitiza kuwa uzuri wa stori yoyote unatokana na msuko mzuri wa matukio, msuko unaohitaji creativity na inspiration. Pia ukasisitiza kwamba unapotunga stori yoyote inayohitaji msuko mzuri wa matukio unahitaji sana 'meditation' na kufanya utafiti wa kina wa kile unachokiandikia...Kwa kifupi, makala yako imenifanya kuelewa kwa kiasi fulani kuhusu msuko mzuri wa matukio katika stori kwamba ndiyo utakaomfanya mtazamaji wa filamu au msomaji wa hadithi apate hamu ya kuendelea mbele zaidi ili kujua kitakachotokea.
Lakini pia nakumbuka umewahi kuandika kuwa filamu ni zao la muongozaji, na kuna mambo matano yanayoifanya filamu iwe nzuri. Sasa unadhani nini kianze kufanyika ili kuboresha filamu zetu? Pia utanisaidiaje niweze kuandaa script nzuri zaidi ili kukidhi haja ya watazamaji?”Huu ni ujumbe uliotumwa kwangu kwa njia ya barua pepe hivi karibuni kutoka kwa msomaji mmoja aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Ubaya Maulid wa Morogoro.Bahati mbaya ujumbe huu ulinifikia wakati ambao sikuwa na nafasi ya kuwasiliana na msomaji wangu ili kumuuliza mambo kadhaa ambayo yangenisaidia kujua nimsaidieje, kwa kuwa nimetingwa na pilika pilika za semina ya waandishi wa script iliyoandaliwa na taasisi ya Media for Development International – Tanzania (MFDI-Tanzania), iliyoanza Jumanne wiki hii (22 Novemba), na inayomalizika kesho Jumamosi 26 Novemba, ambapo mimi ni mmoja kati ya washiriki 15 waliopendekezwa kuhudhuria semina hiyo ya uandishi wa script.Lakini hata hivyo haijanizuia kumsaidia japo kwa namna ninayodhani itakidhi. Kama ambavyo nimekuwa nasisitiza siku zote kuwa msingi mkuu wa filamu yoyote ni muongozo/ muswada andishi (script), ambapo kama script yako itapwaya kwa vyovyote usitegemee kupata filamu nzuri. Na kama ningepewa nafasi na kiongozi wa nchi ya kuulizwa ninadhani nini serikali ikifanye ili kusaidia kuboresha filamu zetu ningesema bila kumumunya maneno kuwa, yatolewe mafunzo kwa waandishi wote wa script.Script ni nini?Script ni muongozo wa maandishi (wengine huita muswada andishi) unaoonesha kila kipengele ambacho kimekusudiwa kusikika, kuonekana, tabia, na lugha itakayotumika kuhadithia kisa kilichokusudiwa. Kwa nini hasa tunahitaji "kuonesha" yote haya? Kwa sababu filamu ndiyo chanzo muhimu kinachowashirikisha muongozaji, msanii, mhariri, na watendaji wengine, kutegemeana na mwandishi alivyoonesha, na jinsi atakavyoitafsiri hadithi yake kwa njia itakayowarahisishia wakati wakipiga picha za filamu.Kwa mwandishi yeyote, ni muhimu wakati akiandika script yake kukumbuka kwamba filamu ni zao (picha) linaloonekana. Hahitaji kuwasimulia watazamaji wake hadithi yake, bali AWAONESHE alichokikusudia. Anapaswa kujifunza jinsi ya kuandika muswada andishi (screenplay) katika namna ambayo mtu atakayeangalia atakiona kile mwandishi alichokusudia kionekane (Visually). Anapoandika, awaandikie kile WATAKACHOKIONA na WATAKACHOKISIKIA.Anaweza kuwapenda wahusika wake wakati akiandika na kujua kile wanachofikiri, lakini nidhamu kuu ya uandishi wa script ni jinsi ya kuyaonesha hayo yote kwenye video pindi watu watakapoiona kazi yake. Yanapotokea, yanaweza kufanyika tu kwa kuangalia. Hivyo mwandishi anapaswa kuandika namna picha itakavyoonekana, sauti, na mazungumzo, na mambo mengine akamwachia mtayarishaji wa filamu.Ni kitu kipi huifanya Stori kuwa nzuri?Hebu tafakari, filamu uliyoipenda zaidi na wahusika waliokuvutia, walioteka hisia zako, waliokufanya ujikute ukishiriki nao. Mara nyingi watazamaji wanapoangalia filamu si tu kwamba wanataka kuburudika na kuvutiwa na watu wanaowaona kwenye screen, wanahitaji pia kutekwa na hisia zao, wapende wasipende. Mashujaa wa kweli katika filamu wanatuvutia; Wahalifu hutufanya tujisikie kutaka kurukia ndani ya televisheni tuangaliapo!Siku zote mwandishi atambue kuwa kuna kitu fulani muhimu katika filamu nzuri. Si tu kitu ambacho mtu anakitaka, ni kitu ambacho lazima kipatikane, bila kujali hatari iliyopo, kama ilivyo katika filamu ya 'Indiana Jones' na ile ya 'Raiders of the Lost Ark'.Wakati mwingine inaweza kuwa ni jambo lisilogusika, kama uhuru wa watu katika filamu ya 'Lawrence of Arabia' au 'Gandhi'. Mambo yote haya humuongoza mhusika kutafuta ukweli/ udadisi, hata wakati mwingine kumpa shujaa nguvu na ushupavu. Inaweza kuwa jambo binafsi (mapenzi) au la manufaa kwa wote (kama kuuokoa ulimwengu na majanga) lakini linapaswa kuwa na nguvu na kukuza zaidi tamaa za watazamaji wakati hadithi ikijifunua kwao.Siku zote kunakuwa na vikwazo vinavyoleta jambo ambalo waigizaji hulipenda sana – MIGOGORO (Conflict). Migogoro ndiyo moyo wa mchezo wenyewe (heart of drama). Mtu fulani anakitaka kitu fulani na watu wengine wanajaribu kutumia njia hiyo kufikia lengo. Mara kwa mara, vikwazo vinaweza kuwa vya kawaida kwa wote; shujaa na mhalifu, na mwisho pande zote mbili zinasifiwa, kama ilivyo katika 'Jingle All The Way'. Katika filamu hii, Arnold Schwarzenegger na Sinbad wanapambana vikali kufikia lengo lilelile moja.Wote wawili wanasukumwa na ahadi walizowaahidi watoto wao, na lazima wafanikiwe na si kushindwa. Migogoro na vikwazo vinaweza kuwa vya kimwili au kihisia (physical or emotional). Lakini vinapaswa kuwemo katika hadithi yako na kama si hivyo basi elewa kuwa hapo huna hadithi.Katika hadithi nzuri zaidi, hata mhusika mkuu pia huwa na vikwazo vingine vya ndani, kama matatizo ya akili au hata ya kiroho (spiritual problem), ambayo yatatakiwa kutatuliwa kwa muda muafaka mara tu atakapojitokeza, ndiyo lengo muhimu la hadithi nzuri. Baadhi ya watu huliita pepo la ndani "mzimu," wakati wengine huita "jeraha."Mwandishi anahitaji ndoano: Uandishi unaoeleza jambo linalovuta hisia za watazamaji/ jamii. Wazo zuri linaweza kuwa rahisi tu "Ingekuwa Vipi?". Hii itaifanya script yako kuweka fumbo ambalo litahitaji muda kuteguliwa. Ndiyo maana watu wataondoka majumbani mwao na kwenda kwenye majumba za sinema, au watatumia pesa walizokusudia kununulia mahitaji muhimu kununua DVD ya filamu yako bila kujali bei yake.Watazamaji walio makini hupenda kununua aina fulani ya stori inayovutia na yenye msisimko. Hadithi zilizofanikiwa duniani zina sura mpya lakini zinazotambulika. Unaweza kuwa unakijua kinacholifanya wazo lako kuwa la kipekee, lakini je, unaweza kulielezea kwa wengine? Je, ni wazo la kutisha, la kuchekesha, la mapenzi, au tukio lisilo la kawaida/la hatari?Unachotakiwa kufanya, tafuta kisa/stori (kusanya visa vyako pamoja). Andaa mambo mbalimbali unayotaka yawemo katika mchezo unaouandaa, filamu, au kipindi cha TV. Jenga taswira/mandhali na madhumuni ya hadithi. Je, mazingira ni yepi na nini malengo ya hadithi na wahusika wakuu wanaohusishwa?Wahusika wako wataiongoza stori hatua kwa hatua kwenye filamu, kwa hiyo hakikisha unawafanya wavutie zaidi na uongeze ubunifu. Inaweza isiwe muhimu sana kwako kuwaendeleza katika mambo yote, lakini baadhi ya waandishi huhitaji kuwa na kila kitu watakachoweka kwenye stori kabla ya kuanza kazi ya uandishi. Cha msingi, tafuta njia yako utakayoona ni rahisi na uifanyie kazi.Jenga kwanza kisa chako, kabla hujaanza kuandika mazungumzo na script yenyewe, inaweza kusaidia kujenga msingi mzuri wa kile kitakachotokea katika hadithi yako na hivyo itakusaidia usisahau. Chora mpango wote na anaangalia jinsi matukio yatakavyofunguka. Hii inapaswa isimuliwe katika nafsi ya tatu.Tafuta staili yako utakayokuwa ukiitumia. Kumbuka, scripts inahusu hatua zote za matendo (action) na mazungumzo (dialogue). Hakikisha wahusika wako wanazungumza kiuhalisia, usijaribu kuchanganya mitindo ya uongeaji na msamiati migumu katika muswada wako labda tu kama unaandaa kwa ajili ya kazi fulani maalum.Hakikisha kwamba wahusika mbalimbali katika script yako wanatumia sauti 'zao' kutegemeana na mazingira yao, ambayo yataathiri uchaguzi wa maneno yao na lugha. Hali hii itawazuia wahusika wako kuchanganyana.Tengeneza tukio (scene). Usisahau kuambatanisha mambo muhimu kama vile muda, mandhali, mpangilio, na matendo ya wahusika katika tukio. Vitu hivi vina umuhimu sawa na mazungumzo yanayotokea.Jenga pia tabia ya kuhariri mwenyewe. Rekebisha mara kwa mara maandishi yako, na, kama inawezekana, muoneshe rafiki script au mtaalam ambaye ana uzoefu wa kuandika na anayeweza kukosoa na kuiboresha script kwa kadri inavyohitajika. Unaweza pia kuandika script yako katika njia mbalimbali, tambulisha watu na hata (katika mabano) muelezee msomaji nini kinatokea na kwamba msimuliaji hasomi. Kama vile; Jeff anaondoka zake au John anafunga mlango nyuma yake.Fanya kazi ya ziada ya kufanya utafiti. Kama huwezi kuchukua muda kuitafiti script yako vipi kuhusu watu unaotaka kuwapelekea, kwa nini wao wachukue muda wa kusoma maandishi yako?Alamsiki.

1 comment:

Millen Mark said...

asante sana ndugu Bishop Hiluka, mimi mi mtunzi na mwandishi wa sitory nzuri sana lakini sina uelewa mkubwa kuhusu script sijui utanisaidiaje kuweza kuandika sitory pia kuandaa script kabisa