Nov 30, 2011

SWAHILIWOOD: Wenzetu wameweza, kwa nini tushindwe?

* MFDI-Tanzania wameanza rasmi mkakati wa mafunzo

Waziri wa Habari, Utamaduni Michezo na Vijana, 
Emmanuel John Nchimbi
 
WIKI iliyopita, kuanzia Jumanne ya tarehe 22 Novemba hadi Jumamosi ya tarehe 26 Novemba, kulikuwa na warsha ya siku tano ambayo ni ya kwanza katika mkakati maalum uliowekwa na taasisi ya Media for Development International – Tanzania (MFDI-Tanzania), kuhakikisha kuwa tasnia ya filamu nchini “Swahiliwood” kama ambavyo wanapenda ijulikane, inafikia kile ambacho tasnia zingine duniani zimeweza, kwa kuandaa warsha iliyohudhuriwa na washiriki 25, wakiwemo watayarishaji wa filamu maarufu na waandishi maarufu wa script.

Warsha hii iliyoandaliwa na MFDI-Tanzania, ambayo mimi nilikuwa mmoja kati ya washiriki waliohudhuria mafunzo maalum ya jinsi ya utafiti na uandishi wa miswada andishi.
Washiriki maarufu waliohudhuria ni pamoja na Jacob Steven (JB), Mahsen Awadhi (Cheni), Suzanne Lewis (Natasha), George Tyson, Hamisi Kibari, John Lister, Ali Yakuti (ambaye hakumaliza mafunzo), Ali Mbwana (Bashiri Mpemba), Chrissant Mhengga na wengineo.

Kwa mujibu wa waandaaji, warsha hii ni ya kwanza kati ya warsha kumi na mbili za “Mfululizo wa Warsha za Swahiliwood”. Mfululizo wa warsha hizi ulioanza wiki iliyopita umekusudiwa katika kuandaa filamu tatu ndefu za burudani lakini zenye kutoa elimu maalum kuhusu VVU na Ukimwi kwa jamii.

Warsha hii ilikuwa na lengo kuu la:

1. Kuwapa habari za kina washiriki juu ya Mradi maalum wa Swahiliwood, na malengo ya mradi huo.
2. Kuwapa mafunzo ya jinsi ya kuandika kwa kina kuhusu Mawasiliano na Mabadiliko ya Tabia (Behavior-Change Communication).
3. Kuwapa ufahamu washiriki wa malengo ya mawasiliano ya Mradi wa Swahiliwood.

Semina hii ni ya ushindani kwa washiriki kabla ya uteuzi wa pande mbili kwa ajili ya mfululizo wa warsha za uandishi wa script. Na siku ya mwisho wa warsha hii, yaani Jumamosi, kila mshiriki alipewa wiki moja ya kuandika dhana (concept paper) kwa ajili ya filamu yake. Kutokana na mitazamo (mawazo) itakayowasilishwa, stori sita zitachaguliwa na kupitishwa katika duru ya pili ambayo itakuwa ni kuziendeleza kwenye muswada andishi (script).

Mzunguko huo wa pili utashuhudia mawazo hayo yakiendelezwa katika muswada (screenplays) kamili kabla ya upigaji picha za filamu, ambapo miswada mitatu bora kati ya sita itaendelea katika kipindi chote cha warsha kumi zitakazokuwa zimebaki, ambazo zimelenga katika hatua zote muhimu za uzalishaji; kuanzia maandalizi muhimu (pre-production), uzalishaji (production), uhariri (post-production), na masoko (distribution).

MFDI-Tanzania wamefanya kile ambacho taasisi zingine zimewahi kufanya kwa kuandaa warsha kwa ajili ya kuhakikisha watayarishaji, wasanii na waandishi wa filamu nchini wanapata mafunzo yatakayowasaidia katika kuboresha kazi. Taasisi zilizowahi kuandaa mafunzo ya uandishi, sauti na utengenezaji wa filamu ni Goethe Institut (Taasisi ya Kijerumani) na Alliance Francaise (Taasisi ya Kifaransa).

Kama inavyojulikana, sekta ya filamu ni tasnia ngumu sana, hata hiyo ni moja ya tasnia muhimu, ambayo kama itaungwa mkono kwa dhati na serikali, inaweza kuchangia kwa kiwango kibwa sana pato la Taifa na kupatikana kwa ajira.

Ili kufanikisha kazi nzima ya uboreshaji wa tasnia ya filamu ili iweze kupenya katika soko la kimataifa, kila mdau hana budi kuzingatia suala la elimu na mafunzo, kwani mambo haya ni muhimu kwa ukuaji, faida, na uendelevu wa sekta ya filamu na video, na kwa mafanikio ya sekta ya Tanzania hasa kama sekta hii itafaidika kutokana na mahitaji ya burudani ambayo inapanuka sambamba na teknolojia ya digitali inayoongeza uwezekeno wa kuwa na idadi kubwa ya maduka ya kuuza filamu.

Sekta ya filamu, kwa asili yake, inaendeshwa na mambo matatu; vipaji, ubunifu na ujuzi.

Kama taifa tunapaswa kuwa na chombo maalum cha Kiserikali kitakachosaidia juhudi za taasisi hizi binafsi chenye lengo la msingi la kutoa mkakati wa kitaifa kuelekea kwenye maendeleo ya sekta ya filamu na video, katika mfumo wa ahadi za serikali za kukuza sera ya kazi kupitia Mkakati wa Stadi za Maendeleo wa Taifa na hivyo kuchangia katika kuboresha uzalishaji na ushindani wa sekta, na kukabiliana na changamoto za maendeleo ya kijamii na kutokomeza umaskini.

Ni lazima - kama tunataka tasnia ya filamu iendelee na kufikia malengo yetu – tufanye mambo yafuatayo muhimu:

Tuwe na chombo kitakachokuwa na kazi ya kutoa na kuhimiza utoaji wa nafasi kwa ajili ya watu, hasa kutoka katika jamii maskini ili washiriki katika sekta ya filamu na video.
Tusaidie kuilea na kuikuza na kisha kuitathmini sekta ya filamu na video. Na tukabiliane na tatizo la kukosekana kwa usawa wa kihistoria katika usambazaji wa filamu na rasilimali.

Mzunguko maalum kutoka kwenye wazo (concept) kupitia awamu zote za uzalishaji hadi usambazaji, na njia ambayo watazamaji watapokea na kuonesha mwitikio wao kwa bidhaa iliyokamilika (Filamu, kipindi cha Televisheni, Video nk.) ambayo hutokana na hadithi zilizoandikwa na zilizotafitiwa na kuishia kwenye miswada andishi (scripts) au maelezo ya kina ya filamu na makala (documentary).

Data za kina na za kuaminika, na utafiti unaoendelea unahitajika sana katika mahitaji yaliyopo, ambapo elimu na utoaji wa mafunzo vinahitajika pamoja na mapungufu tarajiwa. Mfumo maalum wa mafunzo katika tasnia uanzishwe pamoja na uratibu wa elimu na mafunzo kulingana na mahitaji ya tasnia.

Data za kina zitasaidia kuwepo kwa Mkakati wa Maendeleo ya Stadi wa Taifa na mifumo yake ya kutekeleza katika kufikia malengo. Kupatikana habari za fani katika sekta ya filamu pamoja na fursa zilizopo.

MFDI-Tanzania ambayo imeandaa mkakati maalum wa mafunzo ya mawasiliano na mabadiliko ya tabia kama njia muhimu ya elimu na mafunzo ya filamu kwa wadau katika kuandaa visa vitakavyosaidia kuleta filamu nzuri kwenye tasnia ya filamu nchini, ‘Swahiliwood’.

Kama kweli tunataka filamu zetu zipenye katika soko la kimataifa ni lazima serikali, kwa kushirikiana na wadau na taasisi kama MFDI-Tanzania, Goethe Institut na Alliance Francaise ianzishe mkakati wa ushirikiano na wadau hawa wa sekta ya filamu ili kutoa uratibu na ufanisi utakaosaidia kutoa taarifa za upatikanaji wa fedha kwa ajili kusaidia elimu na mafunzo ya msingi katika filamu.

Vinginevyo tukikaa tukadhani kuwa tasnia ya filamu Tanzania itakua na kuleta ufanisi bila kuwa na mikakati madhubuti ya namna tunavyoweza kutoa mafunzo ya msingi kwa watendaji waliopo kwenye tasnia ni sawa na mtu aliyeinjika sufuria tupu kwenye jiko akitarajia kunywa supu.

Alamsiki.
 

No comments: