Nov 2, 2011

BONGO MOVIE: Tasnia ya tatu Barani Afrika isiyoendana na uhalisia wake Upigaji picha wa filamu ya Mzimu wa Maisara

 Filamu ya Fasta Fasta

IMEKUWA ikisemwa na wadau mbalimbali kuwa Tasnia ya Filamu nchini imekua na kupiga hatua, lakini kwa bahati mbaya kati ya wote wanaosema hivyo hakuna hata mmoja ambaye anaweza kuelezea kwa vitendo zaidi ya kusema tu siku hizi filamu zinatoka kwa wingi, jambo ambalo bado si mwafaka kwa tathmini inayoweza kutumiwa kumshawishi mtu makini aliye nje sekta hii kuingia na kuwa Mwekezaji.

Na imekuwa ikiaminika kuwa sekta ya filamu imeanza kuwa biashara rasmi baada ya mwaka 2002 ambapo ni baada ya filamu ya “Girlfriend” kuingia kwa kishindo na kuwaaminisha Watanzania kuwa kuna Watanzania wanaoweza kupigana vita na filamu kutoka nje ya nchi ambazo kwa kiwango kikubwa zilikuwa zimeshika chati,
hata hivyo kwa wakati huo filamu za Tanzania zilikuwa ni zile zilizoandaliwa na Tanzania Film Company (TFC) ambazo hazikuwahi kuuzwa madukani zaidi ya kuonekana kwenye matamasha ya filamu tu.

Pamoja na kuonekana kuwa filamu ya Girlfriend ndiyo filamu ya kwanza ya kibiashara nchini lakini nimekuwa nikisisitiza kuwa ni mkoa wa Tanga ndiyo uliotoa waasisi wa filamu za zama hizi, waliotia chachu na kusababisha hata watengenezaji wa filamu ya Girlfriend kuthubutu, kwani Tanga ndiko wanatoka magwiji waliothubutu kuandaa filamu miaka ya tisini japo mazingira yalikuwa magumu na hawakujua wangeuza wapi kazi zao.

Filamu kama 'Shamba Kubwa' (1995) iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim Al Siagi ilifungua milango ya filamu hizi za kibiashara hapa nchini. Baadaye zilifuatia sinema za ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Kassim Al Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji. Zote zikiandaliwa na watu wanatokea Tanga.

Baada ya msisimko wa soko la filamu uliosababishwa na filamu ya Girlfriend, watengenezaji wengine walijitokeza na kufanya vizuri ambapo filamu kama Nsyuka, Fungu la Kukosa, Masaa 24, Johari na nyinginezo ziliibuka na kuleta upinzani, zikifanya vizuri wakati huo kwa kuwa tu zilitolewa kwa mpangilio na kuruhusu wateja na wapenzi wa filamu kukusanya fedha kwa ajili ya kununua filamu hizo kwa kuchanga fedha kwa muda muafaka.

Hivi sasa soko la filamu limekuwa shaghalabaghala kwani hakuna tena mpangilio wa utokaji wa filamu zetu. Hata hivyo, watafiti wa masuala ya filamu Barani Afrika na duniani wanasema kwamba tasnia ya filamu nchini kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika Bara la Afrika kwa kutoa filamu nyingi na ambazo zimekuwa zikitamba Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Mfano ni filamu za Tanzania zinazotamba katika ukanda huu wa Maziwa Makuu, Afrika ya Kati na Kusini mwa Afrika. Tasnia hii inazifuatia tasnia za filamu za Nigeria inayoongoza Barani Afrika na tasnia ya filamu ya Ghana inayoshika nafasi ya pili. Hizi tasnia mbili (Nigeria na Ghana) ndizo zinazounda Nollywood.

Hata hivyo, wakati sekta ya filamu ya Nigeria ikisemwa kuwa na thamani ya Naira 52.2 bilioni (sawa na Dola za marekani 450 milioni), na imekuwa ikiingiza pato la wastani wa dola za marekani milioni 250 kwa mwaka, tasnia ya filamu nchini haina takwimu zozote na imekuwa ikiingiza pato dogo sana katika taifa, ingawa kiuhalisia imekuwa ikiingiza pesa nyingi sana zinazoishia mikononi mwa wajanja wachache, na wala serikali haioneshi kustushwa na hili.

Kwa umri wa tasnia hii toka kuwepo kwake, Mtayarishaji wa filamu ambaye amekuwa anategemea mauzo ya filamu ili kuweza kumlipa, bado anakabiliwa na changamoto kubwa kwa kuwa wakati sekta hii ilipokuwa ikiibuka (miaka ya mwanzoni mwa 2000) kazi zilikuwa na thamani kubwa; kwa mfano bei ya VHS ilikuwa Tshs. 5, 000/= kwa kaseti moja na DVD iliuzwa kwa Tshs. 7, 000/ = hadi 8, 000/= lakini leo hii DVD inauzwa hadi 1,000/= tena kwa bei ya kupiga debe!

Jambo la kujiuliza, wakati maisha yakiendelea kupanda na bei za filamu nazo zinashuka kila kukicha, ni kweli soko la filamu limekua au limeshuka? Hapa naomba ieleweke kuwa, kukua kwa soko la filamu si kuwa na picha nzuri tu, wala wasanii kuvaa vizuri, kuendesha magari ya thamani, bali uwiano sawa kwa zile filamu zenye ubora fulani, filamu kuleta tija na kuongeza mapato kwa watayarishaji na wasanii kuliko ilivyo sasa zinapokosa mustakbali katika soko la hili.

Najua wapo ambao wamekuwa wakipingana na mtazamo wangu kwani wanajaribu kupima ukuaji wa tasnia ya filamu kwa kuangalia wingi wa filamu zinazotoka bila kuangalia zinachangia pato kiasi gani kwa watayarishaji, wasanii na taifa kwa ujumla kama si sekta ya kuganga njaa tu, jambo ambalo mimi naliona kama soko kuendelea kushuka kwani hadi sasa mtengenezaji anaogopa kuwekeza fedha nyingi katika filamu kwa kuwa hana uhakika na soko lenyewe. Kutokana na hali hii hatma ya filamu za Tanzania ni finyu kuendelea kupanuka kama wengi wanavyoamini.

Ni kweli kuwa sanaa ya maigizo inashika kasi na ni wazi kuwa imetoa ajira za kutosha tu kwa vijana wengi wa Kitanzania, huku pia ikiwa sehemu ya mambo yenye kuchangia katika pato la taifa. Na ni wazi kuwa kwa kasi hii kama serikali itaamua kuirasimisha na kuwawezesha watayarishaji wa filamu tutafikia mahali ambapo sekta hii itakuwa moja ya sekta zenye kutoa asilimia kubwa ya ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuchangia asilimia kubwa katika pato la taifa.

Tukiangalia kwa undani zaidi, si kwamba soko la filamu halijakua bali hata hilo neno lenyewe la Tasnia ya filamu hatustahili kulitumia kwani hatuna, hali hii imekuwa ikisababisha kuwe na fujo na kila mtu kujifanyia atakavyo.
Hata hivyo, mafanikio kidogo yanayopatikana katika tasnia hii yamekuwa yakiwasambaratisha wasanii na kuwaweka katika makundi ambayo naamini kuwa hayawajengi bali yanawabomoa na kuibomoa tasnia yenyewe, kwani naamini hawana hata muda wa kubadilishana mawazo na kunyooshana pale mmoja anapopinda bali wanaishia kujengeana chuki kati ya msanii na msanii, kati ya kundi na kundi, hali hii inatishia kudumaa kwa tasnia ya filamu.

Kwa takwimu za tasnia hii kuwa ya tatu Barani Afrika kwa kutoa filamu nyingi, bado hakuna maana kama hatutavunja roho hii ya utengano miongoni mwetu, na tunatakiwa tuache ubaguzi na hulka ya kila mmoja kujiona yeye ana thamani zaidi ya mwingine, ndipo tutakapofanikiwa. Naweza kusema kwamba hali hii ya makundi inasababishwa na woga na kutojiamini.

Hata hivyo, kwa kadiri ambavyo siku zinazidi kwenda, ndivyo ambavyo kumezidi kuwa na dalili za wazi za sanaa hii ya maigizo na filamu kuonesha kuwa huenda isiwe na manufaa makubwa kwa jamii ya Kitanzania, kutokana na ukweli kuwa, tasnia imeingiliwa na wavamizi wasioelewa kanuni na misingi ya uigizaji.

Uvaaji wa ovyo (au unaweza kuuita wa nusu uchi), limekuwa ni jambo la kawaida katika filamu nyingi zinazotoka sasa, mtindo huu ukiwa umeasisiwa na watu wa fani ya urembo na ulimbwende walioamua kujiingiza katika fani hii, hili si jambo la kujivunia kwenye tasnia.

Hatupaswi kuufumbia macho ujinga huu, upotoshwaji wa maadili na uvaaji nusu uchi eti kwa kisingizio cha maendeleo! Ni ujinga kuukubali ujinga kwa kisingizio cha maendeleo.

Jambo la kutia moyo ni pale Bodi ya ukaguzi wa filamu ilipoonekana kuanza kuzinduka kutoka usingizini, kwani tarehe 14 Oktoba, 2011, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, alizindua rasmi kanuni mpya za sheria ya filamu na michezo ya kuigiza ya mwaka 2011. Dk Bilal alifanya uzinduzi huo mjini Musoma kabla ya kesho yake kushiriki kuongoza sherehe za kuzindua mbio za Mwenge kijijini Butiama.

Kuzinduliwa kwa kanuni hizo kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, kutawezesha kuwabana wanaotengeneza filamu zisizo na ubunifu na zenye kukiuka maadili. Tasnia hii inatajwa kuwa kutokana na kukosekana kanuni, imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukiukwaji wa maadili, filamu kukosa weledi kiasi cha kutouzika na nyingine kuiga kwa kiwango kikubwa mambo ya nchi za Magharibi ikiwemo uvaaji wa nguo fupi.

Naomba kutoa hoja.


No comments: