Nov 14, 2011

Kwa nini hatutafuti watunzi wazuri wa stori katika filamu? KULIKONI, NOV 11, 2011

 Hamisi Kibari

 Hussein Tuwa

 Adam Shafi

MAJUZI nilikutana na mdau mmoja wa filamu ambaye tumefahamiana kupitia mtandao wa jamii wa facebook. Katika mazungumzo yetu yaliyochukua takriban saa mbili mdau huyo aliniambia kuwa anapenda sana kusoma makala zangu kwa kuwa anaamini kama zingekuwa zikifanyiwa kazi basi tasnia hii ingefika mbali.

Katika mazungumzo hayo, kikubwa zaidi alitaka kujua kwa nini filamu zetu nyingi zinatumia sana hadithi za kuiga kutoka Nigeria na kwingineko. Aliniambia kuwa kwa uelewa wake anadhani tatizo kubwa lililopo kwenye filamu (nyingi) za Kitanzania ni uwezo mdogo wa uandishi wa hadithi na miongozo ya filamu, kitu ambacho kinasababisha filamu zetu kuonekana hazina muelekeo.

Yeye anaamini kuwa waigizaji wa Kitanzania wengi ni wazuri sana katika uigizaji lakini si wazuri katika kuandaa miongozo ya filamu, na kwa kuwa lengo ni kuzifanya filamu za Kitanzania kuwa na ubora, hajui ni kwa nini waandaaji wa filamu wasitafute hadithi nzuri ambazo anaamini zipo nyingi mno kutoka kwa waandishi wakongwe wa vitabu na riwaya.

Mdau huyo aliniambia kuwa ana amini kuwa tatizo ni uandishi kwa kuwa wengi wa wanaojiita waandishi wa miongozo ya filamu anawafahamu na anaamini kuwa hawana kabisa uwezo wa kuandika visa vizuri zaidi ya kukopi vile vya Nigeria na kwingineko, na uandishi wao umeegemea katika kunakiri hadithi zingine na mara nyingi inavyoonekana ni waongozaji ndiyo wanaofanya kazi kubwa kuziboresha hadithi hizo ili angalau zionekane nzuri.

Katika mazungumzo yetu tuliongea mambo mengi lakini nimeona nilizungumzie hili la uandishi wa stori na miongozo kwa kuwa tumeendelea kuonekana kuwa wabinafsi hata katika kuboresha kazi zetu wenyewe kwa kutowatumia watunzi wazuri, na kama hatutaamua kuwatumia basi tusitegemee kuona filamu zetu zikiwa na msisimko mzuri kama za wenzetu, hata kama tunauza.

Bahati mbaya watunzi wazuri wanazidi kuondoka huku tukiwa hatuwatumii kabisa, miaka ya nyuma nchi yetu ilisifika kwa kuwa na watunzi mahiri ambao ni hazina bora kwa taifa hili ambao naamini nchi hii haiwezi kupata mfano wao lakini wanatuacha bila kuwatumia au kujifunza kwao. Baadhi ya magwiji katika utunzi waliotangulia ni pamoja na Shaaban Robert, Eddie Ganzel, Ben R. Mtobwa, Aristablus Elvis Musiba, Agolo Anduru, Kassim Chande, Rajabu Mbega, Hammie Rajabu na John Rutayisingwa.

Jambo lililo wazi katika filamu zetu ambalo kwangu naliona kama ni tatizo la kitaifa ni kuwa na stori mbovu ambazo nyingi zinafanana. Ieleweke kuwa, stori mbovu kamwe haiwezi kutoa filamu mzuri hata kama wachezaji wa filamu hiyo watakuwa ni magwiji wa filamu kutoka Hollywood.

Kosa kubwa tunalofanya ni kudhani kuwa kila mtu anaweza kuwa mtunzi mzuri au mwandishi mzuri, tukakasahau kuwa tuna hazina kubwa ya watunzi wazuri ambayo hatuitumii kabisa, tunasubiri waage dunia tuishie kuwasifia.

Nimewahi kuandika katika makala moja kuwa kuna siku nilikuwa nikiongea na mtunzi mwingine mahiri hapa nchini, mzee Faraji H.H. Katalambula, aliyelalamikia kuwa watayarishaji wa filamu nchini hawataki kumtumia ingawa ana hadithi nzuri ambazo zingeweza kuchezwa kwenye filamu zetu.

Nilimwambia kuwa kwa tasnia hii hapa nchini, unaweza kufa na njaa kama utasubiri watayarishaji wa filamu zetu waje kununua stori yako, kwani kila mmoja anadhani yeye ni mtunzi mzuri.

Tasnia yoyote ya filamu katika nchi zilizoendelea hupenda kuwatumia watunzi wazuri ambao hapa kwetu tunawakwepa kwa kisingizio cha bajeti kutoruhusu, lakini tukasahau kuwa hata wao ni binadamu wanaoelewa hali halisi ya soko letu. Pia kitendo cha kuwashirikisha watunzi mahiri peke yake kitaonesha namna tunavyowathamini.

Mi' nadhani bado hatujachelewa, kwani bado tunayo hazina ya hadithi nyingi walizotuachia watunzi hawa, pia tuna watunzi wengine ambao bado wapo hai tunaoweza kuwatumia ili kuboresha stori za filamu zetu. Watunzi kama Beka Mfaume, Hussein Tuwa, Hamisi Kibari, Faraji Katalambula, Juma Mkabarah, Adam Shafi, Jackson Kalindimya, Amri Bawji na wengineo.

Naamini kuwa utunzi wa stori unahitaji kipaji zaidi kuliko vinginevyo. Ni rahisi kumfundisha mtu kuwa mwigizaji na akawa mwigizaji mzuri sana lakini ni vigumu kumfundisha mtu kuwa mtunzi na akawa mtunzi mzuri.

Kwa kawaida uigizaji unahitaji Ubunifu na Kipaji lakini utunzi wa stori unahitaji Kipaji, Lugha, Ubunifu na Msuko. Mwalimu wangu wa kwanza katika uandishi, marehemu Eddie Ganzel, aliwahi kuniambia kuwa kwa asili watu wote ni watunzi, lakini ili uwe mtunzi mzuri unahitaji kuwa na kipaji, kuijua vizuri lugha, kuwa mbunifu na kuwa na inspiration.

Katika filamu, stori ni ramani kama ilivyo ramani ya nyumba, na script ni msingi kama ulivyo msingi wa nyumba. Ili kuwa mwandishi mzuri wa stori/script unapaswa kuwa na sifa kuu tisa:
-Analytical ability: Lazima uwe na uwezo wa kuchambua habari, kuyagusa mahitaji halisi ya walengwa na uwezo wa kutofautisha mambo muhimu na yasiyo muhimu.
-Interest in diverse topics: Mwandishi mzuri anahitaji kufanya utafiti wa kina na makini katika kile anachokiandikia.
-Organizational skill: Lazima uwe na uwezo wa kukusanya taarifa, kuandaa taarifa zenye mantiki kuhusiana na kisa.
-Empathy for your audience: Lazima uwe na uelewa kuhusu watazamaji wako, lazima uzame ndani ya mitazamo yao, vitu wanavyovipenda, mitindo yao, na matamanio yao.
-Writing skill: Lazima uwe na uwezo wa kuandika kwa uwazi na kwa ufupi, na lazima uwe na uwezo mzuri katika matumizi ya sarufi.
-Ability to think visually: Lazima uwe na uwezo wa kuwasilisha taarifa/ mawazo yako sambamba na picha, na si maneno tu.
-Creativity: Lazima uwe mbunifu katika kufikiri unachokihitaji kwa ajili ya kuandika stori nzuri.
-Presentation and selling skills: Lazima uwe na uwezo wa kuwasilisha mawazo yako kwa ufanisi kwa wateja wako na uwezo wa kuuza kazi yako.
-Ability to work on a team: Kiutendaji utajikuta ukifanya kazi na watu kadhaa wenye kazi tofauti, hivyo uwe na uwezo wa kufanya kazi katika kundi.

Uzuri wa stori yoyote ile unatokana na msuko mzuri wa matukio. Msuko wa matukio unahitaji sana creativity na inspiration. Unapotunga stori yoyote inayohitaji msuko mzuri wa matukio unahitaji sana 'meditation' na kufanya utafiti wa kina wa kile unachokiandikia. Katika utunzi, inafika wakati mtu unakwama na kujikuta ukiwa huna kitu cha kuandika.

Mtunzi mzuri akishaona hana kitu cha kuandika ataacha kuandika kwa muda na kuzama katika tafakuri (meditation) ili apate kitu bora cha kuendelezea stori yake badala ya kukurupuka tu mradi amalize. Watunzi wetu wengi katika tasnia ya filamu wanakosa uvumilivu na hawana muda wa kutafakari kwa kina au kufanya utafiti na matokeo yake huishia kukopi stori za wengine na kubadilisha kidogo tu, hivyo kukosa msuko mzuri wa matukio.

Msuko mzuri wa matukio katika stori yako ndiyo utakaomfanya mtazamaji wa filamu au msomaji wa hadithi apate hamu ya kuendelea mbele zaidi ili kujua kitakachotokea.

Stori iliyopwaya inaleta filamu mbovu hata kama waigizaji ni wazuri. Stori iliyosukwa vizuri inazalisha filamu itakayovutia kutazamwa, hata watu wasiojua lugha iliyotumika kwenye filamu husika. Ndiyo maana nasisitiza umuhimu wa kuwatumia watunzi wazuri wa stori.

Watengenezaji wa filamu wa Tanzania wasiwe wabinafsi kama wanataka kuboresha kazi zao na wanapaswa watafute watu wenye uwezo mzuri wa kutunga stori watakaoisuka stori vizuri kuliko kulazimisha kufanya kazi hiyo wao wenyewe kwani endapo yatakosekana niliyoyainisha lazima filamu itapwaya, na ndo haya tunayoyashuhudia kila siku kwenye filamu zetu.

Alamsiki


No comments: