Nov 16, 2011

Hadhi ya Tasnia ya Filamu nchini

 Upigaji picha za filamu Hollywood

Filamu ya Harusi ya Mariam iliyotengenezwa nchini

KUMEKUWEPO mjadala mkubwa kuhusu ukuaji wa soko la filamu hapa nchini na nini kifanyike ili tuweze kutoa filamu nzuri zaidi zenye ubora. Mimi nimekuwa nikitamani kwanza sekta hii ya filamu iwe rasmi kabla ya mambo yote kwa kuwa naamini mitaji, vifaa na rasilimali zipo kila mahali, ila bila kuwa rasmi yote haya tunayoyatarijia hayatawezekana.

Leo nimeamua kuandika mada hii hasa kufuatia mada niliyoandika wiki mbili zilizopita ambapo nilieleza jinsi tasnia yetu ya filamu ilivyopiga hatua katika uzalishaji wa filamu na kuwa ya tatu Barani Afrika (kwa kutoa filamu nyingi bila kujali ubora), ikizifuatia Nigeria inayoongoza na Ghana. Lakini bahati mbaya tuliyonayo ni kwamba mafanikio haya ya kuwa wa tatu katika Afrika hayaendani kabisa na uhalisia wake.

Mada ya leo inatokana na baadhi ya maoni kutoka kwa wadau na wasomaji wa makala zangu waliotaka kujua kuwa, kama sisi ni wa tatu na hatuendani na uhalisia wake kwa maana ya kuitwa tasnia ya tatu kwa kuzalisha filamu nyingi katika Bara la Afrika, je, nini kifanyike?

Kuna msomaji mmoja aliuliza, kwa kuwa soko la filamu limekuwa shaghalabaghala na hakuna tena mpangilio wa utokaji wa filamu zetu, je, kuna mpango gani wa kurekebisha hali hii?

Kwa historia ya filamu ya nchi hii (hasa hizi za kibiashara) inayoanzia miaka ya 2000, ambapo ndipo tulipopata hamasa kubwa ya kutengeneza filamu hizi, tunapaswa kwanza kabla ya jambo jingine lolote kufikiria namna ya kuunda jopo maalum la wataalam litakaloangalia sera na kanuni zilizopo na mapungufu yake kwa lengo la kuoanisha na kuhuisha kiini cha sera ya filamu.

Sera ya filamu katika tasnia yoyote ya filamu bahati nzuri ni hati nzuri ambayo haielezi tu kwa ufasaha uwezekano mbalimbali lakini pia inaonesha majaribio katika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji wa filamu na masoko yake.

Hali kadhalika, hati kuhusu thamani yake inapaswa iambatane na miongozo ya lazima na visheni (vision), kwa mfano kunapswa kuwepo na dibaji inayotambua kuwa filamu ni njia kuu ya mawasiliano, ni njia ya elimu na burudani, jamii, habari na kuhamasisha zaidi. njia yoyote ya mawasiliano ya umma filamu inaweza kutumika kama chombo cha kuendeleza mabadiliko chanya ya kijamii kama vile kuimarisha na kujenga uhusiano mpya kati ya utamaduni na maendeleo ya taifa.

Kwa hali hii ni dhahiri kwamba akili zinazoweka pamoja sera zinakwenda na wakati na zina visheni. Hata hivyo, hali ya sasa ya tasnia hii inaonekana kutoendana kabisa na hisia zinazojionesha. Hali ya utengenezaji wa filamu na matumizi yake vinahitaji kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Katika suala la teknolojia ya uzalishaji wa filamu nchini kwa sasa inarudi nyuma haraka na inaoza. Utamaduni wa kuangalia filamu za kigeni uliojengwa kwa miaka mingi umekufa na kuzaliwa kwa utamaduni wa uangaliaji wa filamu za ndani lakini zikiwa katika maudhui ambayo bado kwa kiasi kikubwa yapo katika dhana ileile za kigeni.

Kwa vyovyote ilivyo uangaliaji filamu /uzalishaji umeandaliwa, nchi hii inaonekana kujifunga, azimio ambalo, linahitaji jitihada za pamoja za mapinduzi ya kiutamaduni yatakayothaminiwa kwa teknolojia iliyopo na ya bei nafuu.

Inaweza isiwe muhimu sana kushiriki katika mapitio ya sera ya filamu au hata miundombinu isiyokuwepo au fedha za kujikimu na utaratibu wa mitaji ya fedha za uzalishaji filamu nchini kama itafanywa kuwa mada tofauti. Kwa kweli, inahitaji semina nzima kutathmini fedha na masoko ya filamu nchini kabla hatujajikita kwenye mambo mengine.

Huwa naamini kuwa kama msingi mkuu ni dhaifu, basi haiwezekani kusema kuwa rasilimali watu zinapatikana kwenye tasnia ya filamu isiyo na tija. Kuna waigizaji, waandishi wa script, wazalishaji, mafundi wa mitambo na waongozaji wengi nchini ambao wanaweza kupambana na changamoto ya miongozo yoyote bila kujali kama ni ngumu au la.

Jambo moja ambalo linaonekana kwa haraka liko kati ya rasilimali watu ni tofauti zetu na elimu ya asili. Zamani, shule ya filamu iliyoanzishwa na Uingereza ilikuwa ndiye msambazaji mkuu wa filamu nchini kabla ya kuingia kwa filamu za Wamarekani-Weusi na waongozaji wengine kutoka tasnia ya filamu ya Marekani.

Kwa hiyo inafaa kuangalia pia ubora wa elimu ya filamu inayopatikana au tunayoitaka katika nchi hii. Je, kuna mwelekeo wa wazi na ushawishi wa kiwango gani na utamaduni katika mafunzo? Kwa kuwa sijui sera yetu ya filamu inasemaje (kama ipo) lakini naamini tunapaswa kuwa na sera ya filamu inayohusika na utafiti, mafunzo na maendeleo.

Sidhani kama bado tuna haja tena ya kuendelea kulaumiana kutokana na mfumo mzima wa tasnia ya filamu kuparaganyika, kuchunguza uhalali au kuwasakama watengenezaji wa filamu kuwa hawajaenda shule katika kipindi hiki.

Tunachoweza kuzingatia ni kuangalia jinsi ya kuwasaidia kupata elimu kwa kuanzisha shule/ taasisi za mafunzo ya filamu au warsha ambazo zinaweza kutumiwa kwa hali yetu ya sasa ambapo kiuchumi, pamoja na kujiandaa kusherehekea miaka hamsini ya uhuru lakini bado tuko ovyo na hakuna anayethubutu kutaka kuwekeza katika filamu.

Sababu ya kuwa na ushawishi kwenye uzalishaji wa filamu na matumizi yake: Katika Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine maudhui ya filamu yanaweza kuamuliwa na sera zitakazowekwa, ili kulinda utamaduni wetu. Sababu kubwa ni kuwa na utamaduni wa watu na mbinu zao. Hii pia ni kazi ya ziada ya mapato na bidhaa za kutosha tayari kwa ajili ya matumizi wakati wowote. Kwa uchumi huu unaoyumba, matarajio yetu yaendane na jukumu kubwa katika kuamua utamaduni wa filamu.

Tukutane wiki ijayo.

No comments: