Oct 26, 2011

Tusipodhibiti sasa kazi chafu tujue kuwa tunaandaa bomu

 Kazi za utengenezaji sinema kama hizi zinahitaji nidhamu 
na maadili ya taaluma kama ilivyo kwa taaluma nyingine.

TAKRIBANI mwezi mmoja tu kuanzia sasa, nchi yetu itasherehekea miaka hamsini tangu tujipatie uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Baada ya uhuru wa Tanganyika serikali katika kuthamini sanaa na utamaduni ilianzisha Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana iliyoundwa mwaka 1962, na rais wa Tanganyika na baadaye Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitamka wazi kuwa Utamaduni ndiyo kiini na roho ya Taifa.

Katika jitihada zake, nchi yetu ilipata kusifiwa sana kwa jitihada hizo za kushughulikia ukuzaji wa utamaduni katika duru nyingi za kimataifa. Hata hivyo, wakati tukiwa tunajiandaa kusherehekea miaka hii hamsini tangu uhuru, hali ilivyo sasa inatisha na kama hatua za dhati hazitachukuliwa, kazi iliyofanywa miaka ya nyuma, hasa mara baada ya uhuru na miaka takriban 20 iliyofuata, itapotea na tutajikuta tukiwa taifa lisilo na utamaduni wake.

Siyo hilo tu, tutajikuta pia tukiwa taifa lenye raia wasio na mwelekeo, wasiojifahamu, wasio na fahari ya utaifa wao, wasio na umoja, mshikamano au heshima mbele ya mataifa mengine. Hata hili ombwe la uongozi tunaloshuhudia sasa nchini mwetu, kukosekana kwa maadili ya taifa kunakochangia utoaji wa kazi chafu za sanaa (filamu), na kukosekana udhibiti ni matokeo ya kupotea kwa utamaduni wetu.

Katika makala hii nitajaribu kuzungumzia suala la maadili na dhana potofu inayosababisha uchafu wa kazi zetu huku nikijaribu kugusia makala iliyopita kwani kutokana na makala hiyo, “Filamu zetu na athari zake katika jamii” kuna msomaji mmoja alinitumia ujumbe ufuatao akitaka ufafanuzi wangu:

“Mwanaharakati, nimefurahi sana kwa makala yako ambayo nimeisoma na kuirudia tena na tena ili kujiridhisha. Nakubaliana kabisa na wewe katika mtazamo wako kuhusu athari zinazoachwa na filamu zetu kwenye jamii hasa kutokana na kutoipa umuhimu tasnia ya sanaa/utamaduni, ndiyo maana kila kukicha tunashuhudia filamu za mapenzi zikilitawala soko letu na hadithi zisizo zetu tunazonakili kutoka jamii za nje. Hongera sana kwa kuliona hilo…

Hata hivyo, tulipopata uhuru, jitihada kubwa zilifanywa ili kufufua na kukuza utamaduni wetu wa Kiafrika. Hili lilikuwa na kipaumbele cha juu katika nchi zetu zote mara zilipopata uhuru. Mantiki yake ilitokana na imani ile ile kuwa roho ya jamii au taifa ni utamaduni wake. Ndiyo maana nchi nyingi, Tanzania ikiwa mojawapo, ziliunda wizara maalumu za kusimamia, kufufua, kukuza na kuendeleza utamaduni wa asili.

Kwangu, utengenezaji filamu ni dhahania (subjective). Filamu ni sanaa inayohusu masimulizi (story telling). Mtu anapaswa kutengeneza filamu kama wazo la kugusa hisia za watu kwa hadithi nzuri. Anapaswa awe mwenye uwezo wa kuwafanya watazamaji wake kucheka au kulia. Awe mwenye mtazamo wa kuifanya filamu kugusa misingi yake na kumfurahisha yeye mwenyewe kwanza.

Pia naamini kuwa sekta ya filamu Tanzania ndiyo tasnia inayotoa filamu nyingi zaidi kuliko nchi yoyote katika Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (kama sipo sahihi nikosoe), lakini kinachonishangaza ni kuwa mbona filamu hizi hazionekani katika matamasha ya filamu ya kimataifa? Kwa nini? Hivi kweli watengenezaji wa filamu wa Tanzania wanajua umuhimu wa matamasha na wanajua kuwa hii ndiyo njia nzuri ya namna ya kuongeza wigo kwa watazamaji nje ya Tanzania?”

Kwa kumjibu msomaji wangu kuhusu swali alilouliza kama watengenezaji wa filamu wa Tanzania wanajua umuhimu wa matamasha ya filamu ya kimataifa, na kwa nini amekuwa hazioni filamu zetu kwenye matamasha. Nadhani jibu langu ni rahisi tu, kwamba wanafahamu umuhimu wa matamasha ila kutokana na kazi hizi kukosa ubunifu hasa zikiwa ni hadithi zisizo zetu tunazonakili kutoka jamii za nje au kuonekana zikiwa zimetawaliwa sana na mapenzi huenda ndiyo sababu inayowaogofya wengi kupeleka kazi zao.

Binafsi, nadhani kuwa haiwezekani nguvu ya kupita tu ikatusababishia mabadiliko tunayoyashuhudia sasa. Ni vyema tukaelewa kuwa aina ya kazi au uzalishaji kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu na jamii huleta athari katika uundaji wa utamaduni pia.

Ili sekta ya filamu nchini ibaki kwenye njia endelevu na hata kusaidia ukuaji wa uchumi, ni lazima wadau wote katika tasnia tuhakikishe kunakuwepo mafunzo endelevu kwa watendaji wake, wataalam na waigizaji waliopo katika sekta hii.

Sekta ya filamu ina uwezo wa kuifanya nchi iondokane na umasikini huu wa kujitakia au utegemezi kwa kupanua upeo wa macho yake kwa kuelezea hadithi nzuri na kutangaza vivutio vya Tanzania.

Tatizo nilionalo ni hii dhana ya 'biashara ni matangazo' ndiyo imesababisha hatari hii tunayoishuhudia leo, huu ni msemo hatari sana kwa uhai wa maadili katika sanaa na ni chachu ya kuchochea sanaa chafu. Hata hivyo ieleweke kuwa dhana ya biashara ni matangazo inakubalika katika biashara zingine zisizohusiana na sanaa/utamaduni ila inapotumika kuhusisha kazi za sanaa husababisha uchafu huu tunaouona.

Katika muziki kwa mfano, biashara ni matangazo imekuwa ikisababisha msanii anapotoa kazi yake mpya lazima awe na mshiko kwa ajili ya kupata Promo ili kazi yake iweze kusikika zaidi redioni na kuonekana kwenye runinga (TV), kwa hiyo hapo haijalishi kama kazi yake imekidhi mahitaji, inalinda maadili ama sanaa yake ni chafu bali kinachoangaliwa hapo ni ametoa kiasi gani cha fedha ili kazi yake isikike kwa muda gani kati ya mwezi mmoja hadi miezi sita. Kwa mantiki hiyo tunadhani maadili yetu yatalindwa vipi?

Kwa kaulimbiu hii ya biashara ni matangazo pia imekuwa ikiiathiri sanaa zingine kama inavyoathiri tasnia ya filamu, kwa kuwa, kazi zinazopata promo kubwa ni zile zinazolalamikiwa kuwa na hadithi zilizonakiliwa kutoka nje na zisizo na maadili, wakati filamu zenye maadili na hadithi nzuri zikiwa hazipewi kabisa nafasi hata ya kusikika na hivyo kusababisha mauzo yake kuwa hafifu huku zikishindwa kuwafikia watazamaji.

Je, tutaepukaje wimbi na udhibiti wa kazi hizi chafu kwa njia hii? Hivi, tunaitakia mema kweli nchi yetu ikiwa lengo letu ni kujaribu tu kukidhi matakwa binafsi au ya wale waliotoa mshiko bila kuangalia maadili ya taifa? Hali hii itaendelea mpaka lini?

Hii imesababisha hata wasanii wetu kutofanya vizuri kimataifa ukilinganisha na sifa walizonazo au kazi zao zinazotoka kwenye vyombo vyetu vya habari zinavyopapatikiwa kwa kuwa wana umaarufu wa kununua na si kwa ubora wa kazi na kiwango cha msanii.

Tukiwa tunasherehekea miaka hamsini tangu tuwe huru tunapaswa pia tujue changamoto kubwa inayotukabili katika sanaa yetu ni namna ya kuweza kudhibiti sanaa zenye mapokeo hasi na zisizoendana na maadili ya Mtanzania.

Binafsi nadhani kuwa inabidi Tanzania ipate chombo imara chenye kusimamia maadili kisicho na mlengo wa kisiasa (kama inavyoonekana sasa kwenye Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza), ili kiweze kudhibiti hali hii na kwamba kazi zote zitakazotoka kabla hazijakwenda sokoni zipate kwanza kibali/ruksa ili ziweze kuonekana. Aidha hatua zaidi ziwepo kwamba atakayekaidi maelekezo haya adhabu kali ichukuliwe dhidi yake na iwe fundisho kwa wengine.

Hali hii kwa kiasi fulani itaweza kutusaidia kulinda maadili ya sanaa na kudhibiti hizi kazi chafu, ambapo pia tutajiweka katika nafasi nzuri ya kukuza viwango vya kazi zetu za sanaa hapa nchini, na hivyo kuondoa hofu iliyopo miongoni mwa watengenezaji wetu wa filamu kukwepa kupeleka kazi zao kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa.

Pia napenda nimalizie kwa kusema kuwa kudhibiti kazi chafu liwe jukumu la kila mmoja wetu kukemea sanaa chafu, liwe ni jukumu la kila msanii kuhakikisha anatoa kazi iliyo bora, na liwe ni jukumu la serikali kupitia taasisi zake za sanaa kusimamia maadili na kuchukua hatua kali kwa atakayekiuka.

Alamsiki.


No comments: