Oct 7, 2011

Ubinafsi huu wa nini kwenye biashara ya filamu?

Kazi ya kurekodi filamu ikiendelea

Anti Ezekiel, mmoja wa wasanii wanaotingisha 
katika soko la filamu nchini

WAKATI tasnia ya filamu nchini ikiendelea kukua, imefahamika kuwa thamani ya kazi za sanaa (filamu) inaendelea kushuka siku hadi siku kutokana na sababu nitakazozieleza baadaye na kusababisha zitengenezwe filamu nyingi zisizo na ubora. Pia kumekuwa hakuna tafiti zinazofanywa kwa maana ya kuweka kumbukumbu (data) zinazowekwa kutusaidia katika kutambua thamani halisi ya tasnia na soko la filamu nchini.

Wadau wengi wa filamu wamekuwa wakiilalamikia serikali kuhusu kutoitilia maanani tasnia hii ambayo ingeweza kuwa suluhisho kubwa la ajira kwa vijana wengi, chanzo cha mapato ya nchi na ambayo ingesaidia kutangaza vivutio vya nchi na hivyo kuvutia watalii wengi na kuliingizia taifa pesa nyingi kupitia utalii.

Kinyume chake ni kwamba hadi sasa serikali imeonekana kuweka pamba masikioni isisikie kilio cha wadau japo inadai kuwa na mpango kabambe wa kupunguza umasikini nchini kwa jina la Mkukuta, na kurathimisha biashara na rasilimali za wanyonge (Mkurabita).

Siyo siri kwamba sekta ya filamu hapa nchini imesheheni utajiri mkubwa sana, tatizo ni kwamba hadi sasa pamoja na kelele za wadau lakini tasnia hii bado si rasmi kiasi cha kuwafanya wadau wake waendelee kuwa masikini wa kutupwa pamoja na kuingiza mamilioni ya pesa ambayo hata hivyo yanawafaidisha wafanyabiashara wachache huku serikali ikiwa haiambulii chochote.

Huu mpango wa Serikali wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita) hauonekani kuwasaidia wadau na wajasiriamali katika tasnia hii ili waweze kufanya kazi kwenye mazingira yaliyo rasmi kwa kuwa hali ilivyo sasa inawafanya wakose fursa nyingi za kukuza kazi zao na kuongeza vipato.

Hali hii inazifanya kazi zao za sanaa japo zinakua lakini zionekane hazina thamani kutokana na wao kutokuwa rasmi. Suala hili la Serikali ya Tanzania kutokuelewa ukubwa wa biashara hii kumesababisha tatizo kubwa sana. Katika nchi nyingine serikali huwa na mkono katika shughuli za aina hii kwani ni chanzo kikubwa sana cha pato la taifa na nafasi yenye ajira nyingi kwa wananchi.

Hata hivyo, yeyote anayeijua historia ya soko la filamu za Tanzania, hasa hizi filamu za kizazi kipya, na jinsi lilivyoanza, atakubaliana nami kuwa tunapaswa kuwashukuru sana wasambazaji (Marketers) waliojitokeza kuwekeza kwenye biashara hii ambao nadhani wanastahili kupewa sifa yao kwa kulifikisha soko la filamu hapa lilipo.

Ukweli ni kwamba soko la filamu la Tanzania limejengwa na wauzaji hawa ambao kwa kiasi fulani wamethubutu kuwekeza pesa zao katika biashara ambayo mwanzoni kabisa ilionekana kuwa ni biashara isiyo na uhakika, kwa kuwa wakati huo sinema kutoka Nigeria na kwingineko ndizo zilizoonekana kushika chati hapa nchini.

Yeyote asiyekubali kuwa wasambazaji hawa ndiyo walioleta mabadiliko na kuifikisha tasnia hii mahali fulani kwenye mstari, tena bila msaada wowote wa serikali wala taasisi zake atakuwa hana shukrani.

Bila wasambazaji hawa, tasnia ya filamu Tanzania, kama tunavyoijua leo isingekuwa chochote kwa kuwa wasanii japo wana ari ya kutengeneza filamu lakini kama wasingepata mahali ambapo wangeweza kuuza kazi zao, sidhani kama wangekuwa na ari waliyonayo.

Pamoja na kuwasifu wasambazaji wa filamu zetu, lakini bado kumekuwepo ubinafsi mkubwa kwenye biashara hii ambao ndiyo unaosababisha kushuka kwa thamani ya kazi zetu. Ubinafsi ninaouzungumzia hapa sio ule wa kusambaza kazi za wasanii walio kwenye mikataba yao tu na kuwakataa wale wasio kwenye mikataba nao, bali kitu kingine zaidi.

Kumekuwepo na tabia ya wasambazaji, hasa wakubwa, ambao wana mtandao mkubwa nchini na nje ya nchi kuuza kazi zao tu kwenye maduka yao na kukataa kuweka kazi za wasambazaji wengine wadogo, hata kama wasambazaji hao wataomba kwa makubaliano maalum. Hali hii imekuwa ikisababisha wasambazaji wengine kukosa fursa ya kazi zao kuwafikia watu wengi japo zinaweza kuwa nzuri na zinahitajika mno.

Inashangaza sana, japo biashara ya filamu ni huria kama zilivyo biashara zingine na hakuna msambazaji anayelazimishwa kuweka filamu ya mwingine kwenye duka lake, lakini bado hakumzuii msambazaji huyo kuweka kazi za mwingine kama kutakuwa na makubaliano fulani au yeye mwenyewe anadhani ni kazi nzuri inayoweza kumwingizia faida nono.

Lakini kujiwekea sheria kuwa hawako tayari kuweka filamu wasiyoitengeneza wao au na mtu wao ni haramu siyo haki hata kidogo. Kwa nini tunajenga misingi ya ubinafsi kwenye soko la filamu ambalo lina manufaa kwa pande zote? Kwa mtengenezaji na hata muuzaji. Je, ubinafsi huu unasaidia kukuza soko la filamu na tasnia kwa ujumla au unadumaza?

Kumekuwepo na dhana potofu kuwa sheria ya soko huria humaanisha mwenye nguvu ndiye anayefaidi. Wale watu ambao hawawezi kuzalisha kwa ubora wa hali ya juu kutosheleza mahitaji ya viwango vya soko huangukia njiani na kukanyagwa na wengine, au wale wasio na mtandao mkubwa walie tu.

Madai ya kanuni ya nadharia kama vile “mwenye nguvu ndiye anayefaidi” tunaposoma habari za mifumo ya viumbe hai na tunaposoma kuhusu mahusiano ya kimawasiliano miongoni mwa jamii ya wanadamu hupelekea katika upotoshaji hadi pale watakapobainisha hasa ni nani anayefaidi katika kila mfano wanaoutoa.

Kanuni hii inapotumiwa katika mabadiliko ya jamii, hata hivyo hali ya kuendelea kuishi ni tofauti sana; sio mtu binafsi tena bali ni aina ya mfumo wa mahusiano ya kimawasiliano ya jamii kama vile mila, taasisi, au kampuni, ambayo huamua kuingia katika mapambano ya kutafuta mabadiliko.

Lakini hii tabia ya wasambazaji wakubwa kukataa kuweka kazi za wengine kwenye maduka yao hata kama ni wao watakaofaidika zaidi ndiyo inayoua soko kwa kuwa si wote wenye mtandao mkubwa, na masoko ya filamu yanategemeana ili kuzifanya kazi ziwe bora.

Ili masoko yaweze kuwa katika ushindani mzuri, wadau wote sokoni wanapaswa kuwa wamepata taarifa sahihi kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba kutokana na matendo yao. Ikiwa baadhi watakuwa na taarifa sahihi zaidi kuliko wengine, hizo tofauti zitasababisha kuwepo na matokeo mabaya.

Taarifa, kama kilivyo kitu kingine chochote cha thamani tukitafutacho ni gharama kukipata, lazima tutoe kitu cha thamani ili tupate taarifa iliyo sahihi na kwa wingi zaidi. Taarifa yenyewe kama ilivyo ni bidhaa inayopitia mchakato wa ubadilishanaji kuhusu masoko; kwa mfano, tunanunua vitabu ambavyo vina taarifa kwa sababu tunathamini taarifa iliyoko kitabuni kuliko tunavyothamini kile tunachokitoa badala yake.

Hata hivyo, kule kuwepo kwa uzalishaji holela unaoathiri jamii moja kwa moja, ndiyo husababisha watu wahoji umuhimu au uhalali wa taratibu huru za masoko. Ikiwa mzalishaji anaweza akazalisha bidhaa kwa faida naye anafanya hivyo kwa sababu anawabebesha wengine gharama za uzalishaji ambao hawakuridhia kuwa sehemu ya mchakato huo wa uzalishaji.

Ikiwa tunataka kuelewa mahusiano kati ya sera na matokeo ni vizuri akilini mwetu ikaeleweka kwamba suala la mali ni dhana ya kisheria wakati ambapo utajiri ni dhana ya kiuchumi. Haya mawili huwa yana kawaida ya kuchanganywa, lakini yanapaswa kutofautishwa.

Ushindani wa Masoko yanayotawaliwa na soko huria ni tofauti na mashindano yaliyoko mwituni. Kule mwituni wanyama hushindana kwa mnyama kumla mnyama mwingine, au kwa ajili ya kuchukua nafasi ya mnyama mwingine. Katika soko, ni wajasiriamali na makampuni ndio wanaoshindana wao kwa wao kwa haki ya kushirikiana na walaji na pia wajasiriamali wengine na makampuni mengine.

Ushindani wa Masoko huria si mashindano kwa ajili ya kupata fursa ya kuishi, bali ni mashindano kwa ajili ya fursa ya kushirikiana. Hivyo sioni ni kwa nini mtu akatae kuuza kazi ya mwingine hata kama anaona itamwingizia faida kubwa, eti tu kwa sababu hataki mwenzake naye apate.

Jambo lingine linaloumiza na kuzifanya kazi za sanaa zishuke thamani ni pale unapozikuta CD za filamu zikiwa zimemwagwa barabarani zikiuzwa kwa bei ya kutupwa kabisa ya shilingi 1,000 tena kwa mtindo wa kupiga debe.

Nilikuwa najiuliza sana kila ninapokuta wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kwa jina la machinga wakiwa wamemwaga CD hizo barabarani wakiziuza kwa 1,000/-, wanathubutu vipi tena bila hata woga kuuza bidhaa hizi za sanaa kwa bei ndogo (ambayo kwa mtazamo wangu ni kwamba huwezi kupata faida labda uwe unauza nakala bandia)?

Baada ya kufuatilia nikaambiwa kuwa filamu hizo wanazitoa kwa msambazaji mwenyewe na huwa kuna mpango maalum kuwa filamu inapofikisha wiki tatu baada ya kutoka, msambazaji kwa kuona kuwa keshapata faida nzuri huamua kuwauzia wauzaji hawa kwa bei ndogo sana, nadhani ni kutokana na ubinafsi tu wa kutaka kuua masoko ya wengine.

Japo ni wazo zuri kuuza kazi kwa bei ambayo kila mtu ataweza kununua lakini si kwa bei hii kwani hali hii inaua kabisa soko la filamu kwa kuwa watu wengi watakuwa hawanunui filamu pindi inapotoka kwa kusubiri zipite wiki tatu ili wanunue filamu hiyohiyo kwa shilingi 1,000.

Narudia tena, japo hili ni soko huria lakini hii si haki kwani kwa kufanya hivyo tunaua thamani ya kazi hizi ambazo zinahitaji ubunifu mkubwa sana katika kuziandaa.

Alamsiki.
 

No comments: