Oct 12, 2011

Filamu yaweza kukufanya uishi hata baada ya kifo!

 Susan Lewis (Natasha)

 Marehemu Dalillah Kisinda (Tabia)

 Wakati wa upigaji picha ya Naomi

FILAMU (Movie au Motion pictures) maana yake ni mfululizo wa picha zinazoonesha mwendo wa watu au vitu na kuonekana mbele ya watazamaji kupitia kioo cha seti ya televisheni (screen). Ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kwa ajili ya kuhadithia/ kusimulia au kuwaelezea watu kuhusiana na kujifunza fikra au mitazamo mipya katika jamii.

Watu tofauti katika kila pembe ya dunia huwa wanaangalia filamu ambazo zinasimulia hadithi fulani ikiwa kama kiburudisho, mafunzo au njia mojawapo ya upenzi.

Katika tasnia ya filamu nchini, wapo wasanii wengi ambao wamejitokeza kuigiza kwenye filamu mbalimbali kwa malengo tofauti, wachache kati yao wamejitokeza kuigiza kwa kuwa wanaamini kuwa wana vipaji na wanazingatia nidhamu ya uigizaji huku wakiwa wamejiwekea malengo maalum katika kazi zao kwa kuamini kuwa sanaa hii ni sawa na taaluma nyingine yoyote hivyo lazima iwe na miiko yake.

Jambo hili huwafanya wasanii hawa kutumia kikamilifu vipaji vyao kwa ubunifu na tija, wakiendelea kusimama kidete kulinda na kutetea maadili mema ndani ya jamii ili wasiwe chanzo cha maporomoko ya kimaadili.

Kutokana na sanaa hii wasanii wa aina hii wenye kuzingatia maadili na kutumia vipaji vyao na ubunifu wamekuwa na mchango mkubwa kabisa katika kurekebisha na kukemea maovu katika jamii kupitia kazi wanazoigiza. Hali hii inapaswa kupongezwa na kutiwa moyo na ninaamini wataendelea kuishi miaka mingi kupitia kazi zao hata baada ya vifo vyao.

Lakini wasanii walio wengi ama wamevutiwa kuigiza kwa kuwa tu wanataka kuwa watu maarufu kama fulani, wakiamini kuwa umaarufu una raha yake kwenye jamii.

Kwa hali hiyo, wasanii wa aina hii wengi wamejikuta wakiingia kwenye uigizaji bila kujua miiko ya uigizaji kwa kuwa tu wanataka kuwa maarufu, watokee kwenye vyombo vya habari kama magazeti bila kujali athari zinazoweza kutokea baadaye, hasa kwa kuwa msanii ni kioo cha jamii. Ndiyo maana nimekuwa nikijiuliza kama kweli wasanii (walio wengi) wanaijua thamani yao!

Kila msanii anapaswa bila ushabiki kuangalia umuhimu wa kazi anazoigiza katika maisha yetu. Hii inatokana na ukweli kwamba kumekuwa na wimbi kubwa la vijana kujiingiza katika kazi mbalimbali za sanaa katika sehemu mbalimbali nchini kwa lengo moja tu, la kutaka kupata umaarufu, basi!

Hali hii ya kuusaka umaarufu bila kujua kuwa kila msanii ana wajibu wa kukumbuka kuwa sanaa ni kioo cha jamii ndiyo inayofanya kazi zetu nyingi zisiishi. Na kama sisi vijana ndiyo tuliokabidhiwa dhamana ya kuendeleza fani hii basi hatuna budi kuwa mstari wa mbele kuyaishi yale yote yanayojitokeza katika fani hii ya sanaa huku tukifikiria zaidi athari tutakazoziacha baada ya vifo vyetu.

Ukweli unabaki pale pale kuwa (kama msanii) ukifanya kazi nzuri ujue kazi yako itadumu milele na hivyo utaendelea kuishi hata baada ya kifo chako, na itakupatia heshima kubwa kwa miaka mingi baada ya kifo. Mfano halisi ni sinema za Bruce Lee ambaye amekufa tangu mwaka 1973, lakini hadi leo sinema zake zimekuwa zikimfanya aendelee kuishi kwenye fikra za watazamaji na amejizolea umaarufu mkubwa kuliko hata wakati alipokuwa hai.

Nimeamua kuandika haya kwa kuwa nimeguswa na mfano halisi ulio hai kuhusu mmoja wa waigizaji wa filamu ya Kitanzania iitwayo Naomi iliyotoka siku za hivi karibuni.

Siku chache tu baada ya filamu hiyo kuanza kuuzwa madukani nchini kote, baadhi ya watu waliokuwa hawajui kama Dalillah Peter Kisinda, maarufu kwa jina la Tabia (wa Kidedea) keshafariki dunia walikuwa wakihaha kuthibitisha habari hizo wasiamini kama kulikuwa na ukweli wowote juu ya kifo chake hata baada ya kuthibitishiwa.

Mtayarishaji wa filamu hiyo ya Naomi, Hamisi Kibari, amenibainishia kuwa amekuwa akipata simu nyingi kutoka kwa watu wanaojitambulisha kwake kama mashabiki wa Tabia wakitaka awathibitishe kama kuna ukweli wowote kuwa muigizaji huyo aliyejizolea umaarufu mkubwa akiwa na kundi la maigizo la Kidedea hayupo tena duniani.

Simu hizo zimekuwa zikimiminika kwa kuwa tu Kibari aliamua kutoa tangazo la Tanzia kwa ajili ya kumbukumbu ya Tabia lililoandikwa mwisho wa sehemu ya pili ya filamu hiyo, Tabia ambaye alifariki kabla ya kuanza upigaji picha wa sehemu hiyo ya pili (part II) ya sinema ya Naomi. Kupokea simu nyingi za mashabiki kunadhihirisha kuwa msanii huyo alikuwa akipendwa kutokana na kazi zake nzuri, na hivyo bado anaishi kwenye fikra za mashabiki.

Ndiyo maana nimekuwa nikitoa ushauri kwa wasanii kuzingatia miiko na maadili ya taaluma ya uigizaji na ubunifu ili waweze kuishi miaka mingi hata baada ya kifo.

Filamu ya Naomi inayoaminika kuwa ndiyo filamu ya mwisho kuigizwa na marehemu Tabia, filamu hiyo mbali ya kumshirikisha marehemu Tabia pamoja na wasanii wasio na majina makubwa ambao wamefanya vitu vya kutisha katika filamu hiyo, sinema ya Naomi pia imewashirikisha wasanii maarufu kama Bakari Makuka (Beka) na Suzane Lewis (Natasha).

Alamsiki.


No comments: