Sep 28, 2011

Tatizo la usambazaji filamu linasababishwa na makundi

 Kulwa Kikumba (Dude)

Jacqueline Wolper

 Issa Mussa (Claude)

IMEKUWA ni kawaida katika tasnia ya filamu kuwasikia wasanii au watayarishaji wa filamu nchini kuulalamikia mfumo wa soko la filamu uliopo, hasa katika hili sakata linaloendelea hivi sasa kati ya wale walio chini ya Shirikisho la Filamu na Msambazaji mmoja mwenyewe nguvu anayelalamikiwa kuhodhi soko la filamu, ingawa ni haki yake kujipangia mfumo anaodhani utamsaidia kuuza kazi zake kwani hakuna mtu anayefanya biashara kwa ajili ya mtu mwingine.

Jina la kampuni na msambazaji anayelalamikiwa vimekuwa vikitajwa sana kila mara wanapokusanyika wasanii na watayarishaji wengi wa filamu nchini ambao wamekuwa wakiwatupia lawama wasambazaji hao wa kazi zao kwa madai kuwa,
ndiyo wamevuruga mfumo wa usambazaji, jambo ambalo kwa mtazamo wangu, nadhani linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa kuliko kuongozwa na ushabiki.

Hata hivyo lawama hizi haziishii kwa msambazaji tu, bali hata Serikali imekuwa ikitupiwa lawama kwa kuonekana kutoitilia mkazo ipasavyo sekta hii ya filamu jambo ambalo limekuwa ndiyo kilio cha muda mrefu cha wasanii na wadau, ambapo viongozi waliopo katika idara zenye dhamana ya sanaa nchini hasa filamu wamekuwa mara kwa mara wakikwepa majukumu yao na wamejisahau na kusahau wajibu wao kwa wasanii.

Kuna wakati niliwahi kuishauri Serikali kuepukana na lawama hizi kwa kujaribu kuupitia kwa makini mfumo unaotumika katika nchi ya Afrika Kusini kupitia taasisi zao za National Film and Video Foundation na ile ya Film and Video Promotion Board ili tuweze kuboresha tasnia yetu iweze kufikia ubora unaotakiwa na kuleta tija kwa wasanii, watayarishaji na wadau wengine wanaohusika katika malengo waliyojiwekea.

Cha ajabu ni kwamba viongozi ambao walipaswa kuwajibika kuhamasisha hasa kwa kuzingatia kuwa dhamana ya kuongoza taasisi hizi za sanaa waliyonayo imetokana na taaluma walizonazo zinazohusiana na fani husika lakini wamekuwa wakionekana kujisahau katika hilo bila kuamka, kushituka wala kuigeukia fani hii yenye mashabiki wengi na inayoweza kuliingizia taifa pato kubwa, kuongeza ajira kwa vijana na pia kuchangia uchumi wa nchi.

Sipingani kabisa na wale wote wanaoitupia lawama Serikali yetu kuwa imeshindwa kuuona mfumo huu mbovu wa soko la filamu uliopo na usambazaji unaosababisha kundi dogo tu la watu kulihodhi soko la filamu, lakini kama nilivyotangulia kusema hapo awali; jambo hili linapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa kuliko kuongozwa na ushabiki.

Naamini kabisa kuwa kabla hatujaamua kumnyooshea kidole yeyote au kumtwisha lawama tunapaswa kwanza kuelewa kuwa yote haya yanayoendelea kwenye tasnia ya filamu yanasababishwa kwa kiasi kikubwa mno na mgawanyiko uliopo baina ya wasanii wenyewe, watayarishaji wenyewe na wadau wengine muhimu katika tasnia ya filamu.

Tukubali au tukatae, tatizo kubwa lipo kwa wasanii wenyewe na si kwa wasambazaji kama linavyoelekezwa au linavyolazimishwa na baadhi ya wasanii/ watayarishaji. Msambazaji wa filamu amejikuta akiingizwa kwenye mtafaruku huu kwa maslahi ya wasanii/ watayarishaji wachache tu wasiojiamini ambao wanadhani kuwa endapo mfumo wa usambazaji filamu utakuwa katika uwanja sawa wanaweza wasiuze kazi zao.

Mfano mdogo tu unaonesha kuwa ni wasanii wenye ubinafsi waliosababisha mamatizo haya, na hawa si wengine bali ni wale waliokuwa mstari wa mbele kupigania maslahi yao kwa kuunda umoja huku wakimpinga msambazaji wa filamu kwa nguvu zao zote, lakini walipopata nafasi ya kuingia naye mikataba ambayo inawahakikishia japo mlo wa wiki chache na kupewa magari ya mkopo wakawa wa kwanza kupinga uwepo wa umoja walioupigania na kuuanzisha huku wakiongoza kwa majungu kutaka msambazaji asichukue kazi za wengine.

Ukijiuliza sana ni kwa nini hali hii inakuzwa kiasi hiki, utapata jibu kuwa wote wanaofanya hivi wanafanya kwa kuwa hawajiamini katika kazi zao na wanadhani kuwa uwanja wa soko ukiwa sawa watanyimwa mikataba mipya.

Wanajitenga na kutengeneza makundi ambayo yanapingana yenyewe kwa yenyewe badala ya kuunganisha nguvu na kuwa na kauli ya pamoja katika kujenga misingi imara ya kuhakikisha kuwa soko la filamu linaboreka na kumfanya kila mhusika katika tasnia ya filamu kupata anachostahili kulingana na kazi yake tofauti na ilivyo sasa ambapo kila mmoja anaangalia zaidi maslahi binafsi na si maslahi kwa wote.

Jambo hili limekuwa likiiyumbisha hata serikali kwa kuwa haina takwimu sahihi za soko hili, hivyo inapotokea wasanii wakalalmika kuwa mfumo wa soko umehidhiwa na mfanyabiashara mmoja, wao hujibu kwa niaba ya anayelalamikiwa kuwa soko limekuwa na kuwafanya waweze kujipatia kipato kikubwa huku wakiwa na akiba kubwa benki.

Wakati ule wa harakati za kuanzisha shirikisho la filamu zilipopamba moto, kila mmoja aliamini kuwa huo ulikuwa ni mwanzo mzuri wa tasnia hii kukua zaidi na kuanza kuyafaidisha makundi yote katika tasnia, kumbe hawa wachache walisukumwa zaidi na njaa tu kuliko kipigania maslahi ya tasnia.

Hadi sasa imeshabainika kuwa hakuna umoja wenye nguvu ambao unaweza kutuongoza katika kuzalisha filamu zenye ubora huku tukipata maslahi kwa kila mhusika, kwa sasa hali ni mbaya kuliko hata ilivyokuwa hapo awali, kabla hata ya kuanzishwa shirikisho, maana walio wengi wanafanya kazi lakini hawana uhakika wa kuuza filamu yenyewe.

Nadhani wasomaji wangu watashangaa ninapojaribu kumuondoa msambazaji katika lawama hizi, lakini kama tukiacha ushabiki usio na maana hatutashindwa kubaini kuwa hali hii ya walio wengi kushindwa kuuza filamu zao hata kama ni filamu nzuri kwa kiwango gani haimnufaishi msambazaji wa filamu tunayemlalamikia, bali ina manufaa kwa kundi dogo tu la wasanii/ watayarishaji wenye ubinafsi ambao wanaona fahari kuitwa mastaa “wanaouza” hata kama ukweli ni kwamba filamu zao hazifanyi vizuri kulinganisha na za wengine.

Sidhani kama kuna msambazaji yeyote anayeweza kukataa kusambaza filamu ya mtu ambayo anaamini kuwa inaweza kumuingizia pesa nyingi eti tu kwa sababu aliyeitengeneza hayupo kwenye mkataba wake au si mmoja wa wale “wanaouza”, bali hali hii ya msambazaji kulalamikiwa kutochukua filamu za “wenzangu na mimi” inatokana na wapambe hawa waliomzunguka (wabinafsi) kupenyeza majungu na fitina ili waendelee kubakia sokoni.

Ndiyo maana sioni ajabu baadhi yao kujitangazia kuwa wana akaunti ya mamilioni benki hata kama ukweli unabaki palepale kuwa bado hawana uhakika na maisha yao (future) kwenye tasnia hii kwa kuwa wanaishi kwa kutegemea msambazaji huyo “acheke”, na pindi anaponuna huwa wanalia njaa!

Ingawa kuna ukweli fulani kuwa wasambazaji wana matatizo yao hasa kutokana na watayarishaji walio wengi hivi sasa kukumbana na ugumu wa kuendelea kutengeneza filamu kwa wakati kutokana na hali ya soko ilivyo, kwani hali ya usambazaji haimruhusu mtayarishaji kupanga ratiba ya kurekodi filamu, kwa kuwa wasambazaji wana sera zao ambazo haziendani na taaluma zaidi ya fikra zao.

Lakini pamoja na yote haya, bado nadhani kuwa msambazaji hana lawama zaidi kwani kukosekana kwa umoja wenye nguvu ndiyo tatizo kubwa zaidi kuliko hili tatizo lililopo kwa wasambazaji wanaolalamikiwa.

Kukosekana kwa umoja ambao ungeweza kuweka misingi mizuri ya namna ya kutengeneza filamu, namna ya kuwapata na kuwatumia wasanii wazuri kwenye filamu zetu bila kujali umaarufu wao, ndiyo sababu ya wasambazaji kuingilia kati na kuhodhi kila kitu kuanzia usahili wa wasanii (audition) hadi kwenye hadithi yenyewe jambo ambalo kwa mtazamo wangu linapoteza maudhui ya Kitanzania na kutupandikizia Umagharibi na Unigeria zaidi kwenye hadithi zetu.

Pia jambo jingine linalosababisha tuwe na mfumo huu mbovu unaotumika katika kuingiza filamu zetu sokoni, mfumo ambao umesababisha kuwepo na utoaji wa utitiri wa filamu kwa fujo na kujikuta filamu zikifurika sokoni na kuwafanya wanunuzi kushindwa kuzinunua zote kwa wakati, jambo ambalo halina tofauti kabisa na kifo cha wasanii, watayarishaji na pengine hata wadau wengine wanaohusika katika tasnia hii kwa ujumla, ni matokeo ya kukosekana kwa umoja wenye nguvu baina ya wasanii/ watayarishaji, umoja ambao ungeweza kusimamia hali hii.

Alamsiki...


No comments: