Sep 16, 2011

Tasnia ya filamu nchini ni kama shamba la bibi

 Mwanaharakati wa sanaa nchini, John Kitime

HUWA napata wakati mzuri sana pale ninapopata nafasi ya kukutana na kuwa katika mazungumzo na wadau muhimu wa sanaa hapa nchini na tasnia ya burudani kwa ujumla, na mmoja wao ni mwanaharakati wa sanaa na mtu aliyebobea katika masuala ya hakimiliki nchini, John Kitime, ambaye pia amekuwa akijitolea muda wake mwingi kujaribu kuelimisha wadau wengine kuhusu haki zao na mambo mbalimbali yanayoendelea katika tasnia ya sanaa, jambo ambalo ni nadra sana kufanywa na wengine.

Namheshimu sana Kitime kwa mchango wake na heshima yangu si ile ya kinafiki kama ilivyo kawaida ya Watanzania wengi kutothamini mchango wa mtu anapokuwa angali hai, na husubiri pale anapoaga dunia ndipo hujidai wanamfahamu sana na kumwagia sifa kemkem japo ni haohao waliokuwa wakimponda wakati wa uhai wake.

Kwangu mimi Kitime ni mtu muhimu na mwalimu bora kutokana na mchango wake katika tasnia ya burudani ya nchi hii japo si rahisi kwa walio wengi kuelewa umuhimu wake, binafsi kuna mengi sana nimekuwa nikijifunza kupitia mwanaharakati huyu muhimu wa sanaa hasa katika suala zima linalowasumbua wasanii na wadau wengi la uelewa kuhusu sheria za hakimiliki na hakishiriki.

Katika mazungumzo mbalimbali ambayo yamewahi kunikutanisha na mwanaharakati huyu hasa yanayoihusu tasnia ya burudani; kwa maana ya filamu na muziki, Kitime mara nyingi amekuwa akijenga hoja zake kwa kutumia mifano na visa mbalimbali ambavyo humfanya anayemsikiliza kuelewa kwa undani kile kinachoendelea kupitia hoja hizo.

Mfano ni kisa hiki ambacho Kitime anaanza kwa kusema:

Hebu jaribu kupata picha, umelima shamba lako na kupanda mahindi ambayo umeyatunza vizuri na yako tayari kuvunwa… unaamka siku moja na kukuta kuna mtu kayavuna na ameanzisha biashara anapata fedha nzuri wakati wewe huna hata fedha ya kula.

Au umenunua suti nzuri akaja mtu akaivaa harusini, kesho yake anakuja kukutaarifu jinsi walivyomsifia harusini kwa kupendeza na suti yako. Hiyo ndio picha ilivyo katika shughuli za sanaa Tanzania. Na haswa katika mambo ya muziki na filamu...

Katika mifano hii moja kwa moja unapata picha halisi ya kile kinachoendelea kwenye tasnia ya burudani hapa nchini, ambayo ukiitazama kwa undani zaidi unaweza kuiita kuwa ni shamba la bibi, kila anayejisikia anaingia, anavuna tani yake na kufaidi mazao pasipo kulima wala kukemewa.

Kitime anasema kuwa mara nyingi wasanii wa nchi hii hufanya kazi ngumu ya kutunga na kufanya mazoezi kisha kurekodi kazi zao, lakini kabla hawajafaidi matunda ya kazi zao hukuta shamba lao likiwa linavunwa kwa njia mbalimbali. Wengine kwa kurudufu kazi zao, wengine huzitumia kutangaza biashara zao. Wengine huzitumia kuhamasisha mikutano yao, wengine huziuza kwa kuwarekodia watu katika simu, katika yote haya mwenye shamba anabaki masikini na haoni mafao yoyote.

Kwa hali hii ndiyo maana mwanaharakati huyu amekuwa akijaribu kutoa elimu ya hakimiliki na hakishiriki kila anapopata nafasi ama anapokutana na wadau wa sanaa, hasa kutokana na mambo kadhaa yanayosababisha ugumu wa kudhibiti kazi hizi ambapo sheria zinazoitwa za Hakimiliki hutumika katika kulinda maslahi ya mtunzi kwa upande mmoja na mtumiaji kwa upande mwingine.

Wakati nilipokuwa nikifanya utafiti wangu kipindi fulani nilipata somo zuri sana baada ya kukutana na Kitime ambapo mwanaharakati huyu alinidokeza kuwa ulinzi wa hakimiliki umekuwa mgumu sana hapa nchini kwetu hasa kutokana na kuwepo kwa utamaduni wa Watanzania kutokuheshimu ubunifu wa mtu wala sheria zinazolinda haki za ubunifu.

Akifafanua kuhusu kutokuheshimu ubunifu wa mtu alitoa mfano kuwa ukianzisha kibanda cha chips chenye mapambo tofauti na vingine, muda mfupi baadaye mtaa mzima utajaa vibanda vinavyofanana na chako jambo linaloashiria kuwa Watanzania hawaoni shida wala ubaya kunakili ubunifu wa mtu mwingine.

Kukosekana kwa ubunifu kumekuwa kunafanya biashara zetu nyingi tunazofanya zifanane, si jambo la kushangaza kukuta mtaa mzima ukiwa na grosari zilizojipanga kuanzia mwanzo wa mtaa hadi mwisho, eti tu kwa sababu mtu mmoja alianzisha biashara hiyo mtaa huo na alipata mafanikio makubwa!

Au si ajabu kukuta mtaa mzima una vibanda vya kuuza nguo za kike au za watoto, kisa tu muuzaji wa kwanza mtaani hapo alifanikiwa sana katika biashara hiyo, hivyo imeonekana kuwa mtaa huo unafaa zaidi kwa biashara ya nguo za kike!

Jambo hili la kukosa ubunifu na kuishia kunakili ubunifu wa watu wengine nimewahi kuliongelea hata wakati nilipoleta mada kuhusu vipindi vyetu vya ucheshi vinavyorushwa na vituo vyetu vya televisheni hapa nchini, hasa pale vituo vya televisheni karibu vyote vilipoamua kuifanya siku ya Alhamisi kuwa ndiyo siku ya vichekesho ambavyo kwa sasa vinaonesha kuchukua nafasi kwa kuteka watazamaji, tena katika muda unaokaribiana sana utadhani siku zingine za juma zilizobaki watu huwa hawaangalii televisheni!

Yote hii ni kutokana na kituo kimoja cha televisheni kufanikiwa na kukonga nyonyo za watazamaji kwa kurusha vichekesho vyake siku hiyo! Hali hii ya Watanzania kuwa ni watu wa kusubiri kwanza ajitokeze mtu mmoja wa kuanzisha jambo na apate mafanikio ndipo tujitose kuiga imekuwa ni sababu ya kutufanya kuendelea kuwa nyuma siku zote, tukizidiwa na jirani zetu Kenya, Uganda na hata nchi kama Rwanda.

Inasemwa kuwa hata watetezi wa haki mbalimbali za wananchi wa Tanzania, watatetea kila haki lakini wakati wa kampeni zao watatumia kazi za wasanii na kuwa wagumu kulipia matumizi hayo. Wanasiasa wakiwa katika kampeni za kuwaeleza wananchi ni jinsi gani wakipata madaraka watatetea haki zao hutumia kazi nyingi za sanaa bila kuzilipia na wala hawaoni kuwa tayari kuna wananchi wanawanyanyasa kwa kutumia kazi zao bila kulipia.

Katika yote yanayoendelea kwenye tasnia ya burudani hapa nchini Serikali haiwezi kukwepa lawama kwa kuwa ndiyo yenye mchango mkubwa wa kuhakikisha marekebisho ya sheria za hakimiliki na hakishiriki kwa wasanii wa Tanzania ya mwaka 1992 ambayo imekosa meno ya kuwanasa wezi wa sanaa inapitiwa upya na kuboreshwa, kisha watendaji waliopewa dhamana wanaisimamia ipasavyo na adhabu kali inatolewa kwa watakaokiuka.

Hali ya kutokuwepo marekebisho haya ya sheria ndiyo iliyoisukuma taasisi ya Rulu Arts kuguswa na mabadiliko hayo ili wasanii waweze kufanikisha maendeleo yao, ambapo taasisi hii imejaribu kuisukuma serikali ili iharakishe mabadiliko ya sheria za hakimiliki kwa sababu kila kukicha wasanii wamekuwa wakipiga kelele bila kupata msaada kutoka vyombo vya serikali kutokana na upungufu wa sheria zake.

Haiwezekani siku zote sisi tu tuwe nyuma katika kila nyanja zinazoihusu sekta ya michezo na burudani, kama tumeshindwa kwenye kandanda, tumeshindwa kurudisha enzi za kina Filbert bayi, Juma Ikangaa na wengineo katika riadha na tumeshindwa kutamba katika michezo mingine, iweje tuwe nyuma hata kwenye sanaa wakati tuna rasilimali za kutosha na vijana wenye vipaji lukuki?

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa yote hii ni kutokana na kukosa sheria kali zitakazowadhibiti wanyonyaji wa jasho la wasanii. Ni wakati sasa tukaanza kusaka maendeleo ya sanaa, jambo litakalotuweka pia katika mfumo bora wa soko la pamoja la Afrika Mashariki badala ya sasa tunapoonekana kulala usingizi wa ‘pono’ pasipo kujipanga vilivyo kwa maendeleo yanayopigiwa kelele na wengine. Hii ni aibu kwa taifa!

Naomba kuwasilisha...


No comments: