Sep 8, 2011

Ujasiriamali sekta ya filamu umedhoofishwa makusudi...

Hamisi Kibari UJASIRIAMALI ni uwezo na nia ya mtu au watu kufikiria, kubuni na kuanzisha fursa mpya za kiuchumi/uzalishaji na kuingia kwenye soko bila kuogopa ushindani au vikwazo vilivyopo au vitakavyoweza kutokea. Mjasiriamali ni mtu mwenye moyo wa kuthubutu, mbunifu, mwerevu wa kubaini na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, mpenda ufanisi na viwango bora katika kazi ya Sanaa, asiye na tabia ya kuvuruga na kuvunja taratibu za makubaliano na mikataba.

Pia mjasiriamali anasemwa kuwa ni mtu mpenda kutafuta na kupata habari mbalimbali, anayeweka malengo, mwenye kuweka mipango na kufuatilia, asiye tegemezi na anayeamini, na mwenye uwezo wa kushawishi na kuwa na mtandao.

Lakini kwa Tanzania, ujasiriamali kwenye sekta ya filamu imekuwa ni tofauti sana kwani wajasiriamali wengi waliothubutu kuingia kwenye soko la ushindani wameshindwa kudumu kutokana na vikwazo vingi wanavyokumbana navyo kiasi cha kuathiri juhudi zao.

Tasnia ya filamu nchini kwa sasa imefikia hatua kubwa mno, ambapo wastani wa filamu tatu mpya za Kitanzania hutoka kila wiki (takriban filamu 156 kwa mwaka) na hali inaonesha kwamba idadi hiyo itazidi kupanda miaka michache ijayo, hasa kama watengenezaji filamu wa Tanzania wataboresha zaidi kazi zao.

Unapozungumzia tasnia ya filamu Tanzania kwa kuwataja wanaharakati au wadau wanaoiinua na kuipigania tasni hii, ni nadra sana kuacha kuzitaja taasisi kama; Kituo cha Utamaduni cha Muungano wa Urusi na Tanzania (Russian - Tanzania Culture Center), Taasisi ya Watu wa Ujerumani (Goethe Institut), Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa (Alliance Francaise), Baraza la sanaa la Taifa (Basata), Chama cha hakimiliki na Hakishiriki (Cosota) na Shirikisho la Filamu Tanzania (Taff).

Pia kuna kampuni ambazo nikiri kuwa zimetoa mchango mkubwa wa kuifikisha tasnia hii hapa ilipo ingawa baadhi yake zinalalamikiwa kwa sasa. Kampuni hizo ni pamoja na Wananchi, Kapico, Game 1st Quality na Steps Entertainment. Pia kuna juhudi za watu mmoja mmoja ambao kwa leo sitawataja.

Lakini pamoja na juhudi mbalimbali za wadau na wanaharakati mbalimbali, mtayarishaji wa filamu na msanii wa Tanzania bado hana mafanikio!
Bado wanaishi maisha ya kuombaomba! Wengi wao kwenye tasnia ya filamu ni “wauza sura tu” kwa maana ya kupata umaarufu bila kipato kwani sekta hii imekuwa ni ya kuganga njaa!

Mzalishaji wa filamu Tanzania kila siku amekuwa anaumiza kichwa kutafuta mtaji na kuandaa bajeti ya filamu, uandaaji hadi kukamilika, lakini bado hana sauti wala nguvu sokoni! Amekuwa anafanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake bali siku zote anategemea hisani ya watu fulani!

Pindi filamu ikikamilika kinachobaki ni kuweka mikono nyuma wakati wa mazungumzo yake na msambazaji ili filamu yake isambazwe! Haijalishi atalipwa kiasi gani! Biashara ya filamu imekuwa ngumu kuliko maelezo pamoja na ukweli kwamba ukienda maeneo kama Buguruni, Kariakoo na Ubungo, filamu zimemwagwa chini, zinauzwa shilingi elfu mojamoja na watu wanazinunua kwa wingi!

Katika maongezi yetu ya kawaida na mmoja wa wajasiriamali katika tasnia ya filamu nchini, Hamisi Kibari, ambaye pia ni mhariri wa gazeti hili alinieleza kuwa filamu yake mpya ya Naomi ambayo pia imemshirikisha marehemu Tabia, na inaaminika kuwa ndiyo filamu yake ya mwisho tayari ipo madukani tangu Jumatatu wiki hii, akiwa anaisambaza mwenyewe.

Cha kusikitisha, tayari Kibari ameshakumbana na matatizo kutokana na watu walioko sokoni hasa msambazaji mkubwa aliyeamua kupanga bei ya chini ili wengine wasiweze kufanya biashara, kwa maana hiyo, anachochewa zaidi na uchoyo na ubinafsi.

Kibari anasema kuwa kila alipopeleka filamu yake kwa wauzaji wa rejareja aliambiwa kuwa kuna msambazaji mkubwa amekuwa akiuza filamu zake kwa bei ya chini sana hata kufikia 1500/-, huku akifaidika na matangazo ya biashara aliyoyaweka ndani ya filamu na hivyo kutishia uwepo wa wasambazaji wadogo kama Kibari.

Sitapenda kuizungumzia sana filamu hii ya Naomi kwa kuwa mimi pia nimehusika katika utengenezwaji wake, nachelea kufanya hivyo isije ikaonekana kuwa naizungumzia kwa kuwa inanihusu, au 'namfagilia' Kibari kwa kuwa ni mhariri wangu, lakini nitaigusia tu kama muongozo wa jambo nililokusudia kulijadili.

Binafsi naamini kuwa Kibari ni mmoja wa wajasiriamali wa kuigwa ingawa kuna wakati aliamua kujiondoa kwenye soko la ushindani kwa sababu ya kutolipwa vyema filamu yake ya mwisho aliyoitoa mwaka 2007 ya Mtoto wa RPC sehemu ya Pili, lakini anasema kwa sasa ameamua kuja na nguvu mpya, mkakati tofauti na hatorudi nyuma.

Nilipouza Mtoto wa RPC namba moja, nililipwa vyema malipo yangu lakini tatizo likaja kwenye namba mbili. Kwa kweli ilinikatisha tamaa sana hadi nikaamua nikae pembeni. Kwa kifupi nilizichukia hata filamu zenyewe,” alinidokeza Kibari katika mazungumzo yetu ambayo hata hivyo nimeamua kuyaandikia makala, japo yeye hakupenda nifanye hivyo.

Kitu kingine kilichomkatisha tamaa ni tabia ya msambazaji huyo mkubwa kufanya mambo ambayo ni kinyume na taaluma ya filamu, hivyo baada ya kukaa muda mrefu akiwa nje, ameamua kurudi na ana hakika ataliteka soko muda si mrefu baada ya kufanya utafiti na kugundua udhaifu uliopo.

Kuna udhaifu mkubwa upande wa hadithi na hapo ndipo mimi ninataka kupafanyia kazi… Zipo filamu chache nzuri nimeziona lakini nyingi kwa kweli hazinivutii kwa upande wa hadithi ingawa mambo mengine kama locations (maeneo), mavazi na hata upigaji wa picha na uhariri wanajitahidi,” anasema Kibari na kuongeza kwamba hafurahishwi na mavazi yenye ukakasi ya baadhi ya wacheza filamu wa kike ambayo yeye amejitahidi kuyaepuka katika filamu ya Naomi.

Amesema ingawa kuna mahala amelazimika kufuata soko lilivyoharibiwa, lakini kadri atakavyokubalika atabadilisha msimamo huo. Kibari amesema udhaifu mwingine ambao anauona na anataka kupambana nao hata kama itamchukua miaka kadhaa ni watu kudhani kwamba filamu nzuri lazima zitokane na majina fulani ya watu.

Inanisikitisha sana kusikia mtu ukimwambia kwamba tunaandaa filamu, anaanza kukuuliza, yumo fulani, yumo fulani… Jamani, filamu hata kama majina ya watu yanaweza kuwa muhimu lakini hayapo katika vigezo vya kuifanya filamu iwe nzuri,” anasema.

Nami sisiti kuwashauri wasomaji wa Mbiu ya Ijumaa kuinunua filamu ya Naomi ili kuanza kuona uhondo mpya unaokuja, hatua ambayo itawawezesha wajasiriamali wetu kama Kibari kuandaa vitu vikali zaidi. Pia Watanzania wanapaswa wajenge utamaduni wa kununua nakala halali ili kusaidia kukuza kipato cha wasanii na watengenezaji filamu nchini.

Mbali na filamu ya naomi na Mtoto wa RPC, Kibari pia ameshatoa filamu za Usikose Mazishi Yangu na Usiku wa Taabu.

Pia kwa upande mwingine nadhani bila serikali kuingilia kati, kutegemea soko huria kutasababisha makampuni makubwa machache kuhodhi biashara ya kuuza bidhaa zote. Kwa kawaida, masoko husababisha kuhodhi mali, wakati ambapo wazalishaji wadogo wanabanwa wanasalimu amri kwa makampuni makubwa ambayo hulenga tu kupata faida iliyo kubwa; na ndiyo maana serikali inapaswa kufuata matakwa ya walio wengi kwa kuhakikisha inapambana na uhodhi wa mali.

Je, ni kweli mfumo wa masoko huria huendeleza mchakato wa kuhodhi? Kuna sababu ndogo ama hakuna sababu nzuri ya kufikiri hivyo na kuna sababu nyingi zaidi za kutokufikiri hivyo kabisa. Masoko huria hujengwa kwenye misingi ya uhuru wa watu kuingia sokoni, kujitoa sokoni kwa uhuru, na kununua kutoka kwa ama kumuuzia yeyote wanayemtaka kama wapendavyo ingawa kwa Tanzania imekuwa ni tofauti sana.

Kama makampuni yaliyo katika biashara yenye uhuru wa kuingia wakipata faida iliyo zaidi ya wastani, zile faida huwavutia washindani kuja kushindania hizo faida ili nao waweze kuzichukua. Baadhi ya vitabu vya kiuchumi vinatoa maelezo ya mazingira ya kinadharia tete ambapo hali fulani za masoko husababisha “kodi isiyobadilikabadilika” hii ina maana kwamba pato linakuwa kubwa kutokana na chaguo bora zaidi, kinachoelezwa kama kile ambacho rasilimali hukizalisha katika matumizi mengine.

Uhuru wa kuingia sokoni na uhuru wa kuchagua ununue kwa nani hukuza matakwa ya wateja kwa kuondoa zile faida za muda ambazo huzifaidi wale wanaokuwa wa kwanza kununua bidhaa. Kinyume chake, kuipa serikali nguvu ya kupanga nani anapaswa ama hapaswi kutoa bidhaa na huduma husababisha uhodhi – halisi, hata uhodhi uliothibitika kihistoria ambao una madhara kwa watumiaji wa mwisho ambao pia unaharibu nguvu za uzalishaji za mwanadamu ulio msingi wa mafanikio ya binadamu.

Kwa nini soko la filamu lisitoe fursa sawa kwa wote ili kudumisha ushindani wa kweli kwenye tasnia hii? Iko wapi mamlaka mfano wa Ewura kwenye tasnia hii ambayo itasaidia kupanga bei?

Je, kwa mwendo huu ni kweli Tasnia hii itakuwa na kutoa ajira kwa watu wengi zaidi ama itabaki kuwa ya wachache, wateule fulani wanaokumbatia na msambazaji mkubwa?

No comments: