Sep 21, 2011

Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania wameonesha njia sahihi

Mwenyekiti wa Tafida, Christian Kauzeni, 
katika moja ya majukumu yake kwa chama

Amanzi Ali Kisomi, akiwa jukwaani

INGAWA kimekuwa kikionekana kama ni chama cha watu waliokosa kazi ambao hukutana na kupiga porojo pasipo manufaa yoyote, lakini Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania (Tafida) kimeonesha njia sahihi kwa kuliangalia tatizo lililopo miongoni mwa wanachama wake katika tasnia hii ya filamu na kuamua kujikosoa wenyewe kabla ya kuwakosoa wengine.

Katika kujikosoa, viongozi wa chama hiki, chini ya uongozaji wa Christian Kauzeni, wameandaa mafunzo maalumu ya siku mbili yanayohusu misingi ya uongozaji yanayofanyika katika ukumbi wa Basata, Ilala Sharif Shamba, Alhamisi na kuhitimishwa Ijumaa,
kama mpango wake maalum wa kwanza kuwapatia stadi na kuhakikisha waongozaji wa filamu wanapata japo msingi mdogo wa uongozaji utakaosaidia katika kurekebisha makosa yaliyopo kwenye filamu zetu.

Chama hicho kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini, wamefanikisha mafunzo hayo yanayotolewa na wanataaluma wawili, Amanzi A. Kisomi, mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye kwa sasa anasoma shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mtaalamu mwingine wa siku nyingi, John Ndumbaro, wakiamini kuwa tatizo kubwa lililopo kwenye tasnia ya filamu ni waongozaji wa filamu nchini kukosa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kuongoza kazi zao katika kiwango kinachokubalika.

Ingawa wakati fulani niliwahi kuandika makala kuhusu uongozaji wa filamu na sifa za muongozaji wa filamu lakini nimeona niirudie mada ya uongozaji japo katika namna na mtazamo mwingine, hasa ikizingatiwa kuwa kitendo walichofanya Tafida kuanzisha mpango huu wa mafunzo ya msingi kwa wanachama wake kinapaswa kuungwa mkono na vyama vingine vya sanaa.

Inaaminika kuwa kukosekana kwa mafunzo na kutojielewa ni sababu kubwa ya filamu zetu kuwa ni kitu kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wamekuwa wanalipua kazi na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam kwa kuwa tu hawajitambui. Wanafanya mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi. Hali hii imekuwa ikiwakatisha tamaa hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii.

Pia kukosa mafunzo kumewafanya walio wengi kujawa na ubinafsi (kwa kuwa hawajiamini) ambao umekuwa ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa ni sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika! Na mwisho wa siku hawapendi kukosolewa.

Nimekuwa nikiipigia sana kelele Serikali yetu kuanzisha mpango maalum wa mafunzo kwa wasanii na watendaji wengine wakiwemo waongozaji kama ule uliopo Afrika Kusini kupitia taasisi zao za National Film and Video Foundation (NFVF) na Film and Video Promotion Board, ili kuwasaidia wajasiriamali katika tasnia ya filamu nchini kutengeneza kazi nzuri zitakazokidhi ubora wa soko letu na hata nje ya mipaka yetu.

Kwa mfano, nchini Afrika Kusini kuna idara inayowahamasisha na kuwalazimisha wasanii na watendaji wengine katika tasnia ya filamu kupata mafunzo ya weledi (professionalism) katika taasisi zao, hasa ile ya Film and Video Promotion Board.

Kwa mpango huu wa Tafida kuanzisha mafunzo kwa waongozaji wa filamu ikishirikiana na taasisi za serikali yatasaidia sana kuongeza ufahamu na kujitambua kitendo ninachoamini kitapunguza matatizo ya filamu zetu ambazo si ajabu kumuona mwigizaji akiigiza analia lakini uso wake umebeba tabasamu la chati kama ambavyo msomaji mmoja aliwahi kuniomba nitoe ufafanuzi. Au yale matukio ya utekaji nyara katika filamu huku mtekwaji akionesha dalili zote za kukaa tayari kwa kutekwa!

Mimi hupenda kuiangalia filamu yoyote na kuupima uzuri wake kwa kuangalia mambo makuu matano: Mwongozo mzuri (script), Waigizaji wazuri, Wapigapicha wazuri, Muongozaji mzuri na Mhariri mzuri.

Naamini kuwa kama ukiwa na mwongozo mzuri wa filamu, ukapata waigizaji wazuri na ukawa na wapigapicha wazuri, lakini ukakosa muongozaji mzuri hakika huwezi kupata kile unachotaka kwani muongozaji wa filamu ndiye mjenzi wa sinema yoyote tunayoiona au tuliyowahi kuiona.

Bahati nzuri tasnia yetu imebarikiwa kuwa na waigizaji wengi wazuri, wapigapicha wengi wazuri, wahariri wengi wazuri, na hata baadhi ya waandishi lakini inakosa kabisa waongozaji wazuri wa filamu. Hii haimaanishi kuwa hakuna kabisa waongozaji wazuri, wapo wengi wenye uzoefu na elimu ya kutosha katika uongozaji wa filamu, tatizo ni mfumo mbovu unaowafanya kutupwa nje ya ulingo wa soko la filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki wala hawapewi heshima inayostahili.

Kwa kawaida filamu ni zao la muongozaji na wala si la mtayarishaji, mwandishi au muigizaji kama ambavyo wengi wanadhani. Muongozaji wa filamu ana mchango mkubwa sana katika kufanikisha kazi nzima ya utengenezwaji wa filamu kwa kuwa ndiye mtendaji pekee anayeshiriki kwenye hatua zote za uandaaji wa filamu; kuanzia kwenye wazo hadi kwenye uhariri wa filamu.

Nimewahi kuandika makala kwenye gazeti hilihili kuwa ile hoja ya kwamba waongozaji wa filamu za Kibongo hawakusoma na hawataweza kuongoza vizuri filamu inaweza isiwe sababu ya msingi sana, kama waongozaji hao watajitambua na kujiendelea kwa kupata mafunzo ya muda mfupi kama haya, kwani kukosa elimu ya darasani si mwisho wa kujifundisha. Hata Hollywood kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa katika vyuo vya filamu lakini wamepata mafunzo na semina mbalimbali wakiwa kazini na wamekuwa waongozaji wazuri na wanaoheshimika sana duniani.

 Steven Soderbergh

 Spike Jonze

Waongozaji hao ni pamoja na; Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater, Spike Jonze na wengineo...

Sifa kubwa ya mtu kuwa muongozaji wa filamu ni kuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu mkubwa (creative vision), ufahamu wa namna ya kuandika script na kujitoa kwa dhati (commitment) katika kufanikisha kazi nzima. Muongozaji pia anahusika moja kwa moja kwenye mafanikio yoyote ya kisanii, mafanikio ya kibiashara au kushindwa kwa filamu katika soko.

Muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji. Muongozaji anawajibika katika kuitafsiri script iliyoandikwa kwenye karatasi na kuihamishia katika picha halisi na sauti kwenye runinga – na anapaswa kuiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa filamu hiyo, na hivyo kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi.

Kama nilivyowahi kuandika kabla, tatizo kubwa lililopo kwenye tasnia ya filamu nchini ni kwa waongozaji wetu wa filamu kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby... camera rolling... action...” na baadaye cut!”, na kusahau kuwa muongozaji ndiye anayepaswa kumtengeneza mhusika ili aonekane vile anavyopaswa kuonekana kutegemeana na muongozo (script) unasemaje. Kama muigizaji atashindwa kuvaa uhalisia, hilo halitakuwa kosa la muigizaji bali ni kosa la muongozaji na litatafsiri uwezo wa muongozaji ulipokomea.

Muongozaji anapaswa kuwa na uelewa mkubwa katika kuitafsiri script na kuihamishia katika picha halisi na hata kupendekeza sauti zitakazotumika kwenye filamu, pia anapaswa kuangalia mtu anayefaa kuigiza katika nafasi husika, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji ni pamoja na kufanya usaili (casting).

Wakati masuala muhimu katika utayarishaji wa filamu, kama vile fedha na masoko, hubakia mikononi mwa Mtayarishaji wa filamu (film producer), Muongozaji anapaswa kuwa na ufahamu wa bajeti inayotumika kwenye filamu anayoiongoza na kujua ratiba. Katika baadhi ya filamu, Waongozaji huhodhi majukumu mengi kama Muongozaji/Mtayarishaji au Muongozaji/Mwandishi, jambo ambalo halikatazwi kama atakuwa na uwezo wa kuyatenda kwa ufanisi.

Muongozaji anaweza kuandika script ya filamu au kusimamia uandikwaji wa script baada ya rasimu ya awali ya script kukamilika. Baada ya kupata waigizaji, muongozaji husimamia mazoezi (rehearsals) na upigaji picha wa filamu (shooting). Muongozaji pia anapaswa kusimamia masuala ya kiufundi ya sinema, ikiwa ni pamoja na kamera, sauti, taa, ubunifu na kadhalika.

Wakati wa uhalili (post-production), Muongozaji hufanya kazi kwa ukaribu na Wahariri katika mchakato wa kiufundi wa uhariri, hadi kufikia mwisho wa kazi. Katika hatua zote, Muongozaji anawajibika kuhamasisha timu yake kutayarisha kazi bora. Muongozaji pia anapaswa kuyafahamu mahitaji na matarajio ya soko la filamu.

Mwisho, muongozaji anapaswa kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mawasiliano (communication skills) na watu wengine katika kufanikisha kazi.

Ni matumaini yangu kuwa waongozaji waliopata bahati ya kuhudhuria mafunzo ya uongozaji ya siku mbili watakuwa wamepata msingi mzuri na kuwa mfano mzuri kwa wale ambao hawakupata nafasi hii muhimu, na wataendeleza yale mazuri waliyofundishwa na wakufunzi wao. Sitegemei kuwaona wakirudia makosa yaleyele.

Alamsiki...


No comments: