Sep 21, 2011

Basata yataka wasanii wote wajisajili

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Basata, Angelo Luhala

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limewataka wasanii pamoja na vikundi mbalimbali vya sanaa kujisajili ili kukomesha wizi wa kazi zao. Akizungumza katika Jukwaa la Sanaa siku ya Jumatatu, ambalo hufanyika kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz), Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Basata, Angelo Luhala alisema kwa mujibu wa sheria suala la kujisajili ni la lazima, hivyo akasema wasanii wote wanatakiwa kupewa vibali ili waweze kutambulika mahali popote wanapokwenda.

Luhala alisema kuwa wasanii wengi hulalamika kuibiwa kwa kazi zao, pasipo kujua aliyehusika na wizi huo, hivyo usajili ni moja ya kanuni za nchi, kwani taifa linakuwa na kumbukumbu kuhusu kazi zao na pia inamsaidia msanii mwenyewe kuwa huru na kufanya kazi yake kwa imani.

Aliongeza kuwa hapo baadaye watapita kila wilaya na kuangalia wanaofanya kazi za sanaa kama wamesajiliwa, watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu huo watachukuliwa hatua.

Alieleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ya nchi namba 23 ya mwaka 1984 Baraza limepewa mamlaka ya kusajili na kusimamia sekta ya sanaa nchini, hivyo mtu yeyote anayefanya shughuli za sanaa anapaswa kusajiliwa na kupewa kibali cha kufanya shughuli hizo.

Alieleza kuwa sanaa ni kazi kama zilivyo nyingine, hivyo kila anayefanya kazi ya sanaa hana budi kutambuliwa na Serikali na Baraza kwa niaba ya Serikali limepewa kazi hiyo.

Kwa mujibu wa Luhala, wadau wanaopaswa kujisajili Basata ni pamoja na wasanii wa fani zote, wakuzaji sanaa (mapromota), vikundi vya wasanii, kumbi zote za burudani, wafanyabiashara wa sanaa, vyama na asasi mbalimbali za sanaa.

Akizungumzia faida za kujisajili, Luhala alisema ni pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi, kutambuliwa na serikali, kupata utambulisho wa Baraza katika mahitaji mbalimbali, fursa za kushiriki maonesho, taifa kuwa na takwimu sahihi za wadau wanaojihusisha na shughuli za sanaa na faida nyingine.

Wadau mbalimbali waliohudhuria programu hiyo walionekana kuwa na shauku kubwa kwani mbali na suala la usajili, Baraza lilitoa elimu kwa wasanii juu ya kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na wasanii kutakiwa kujisajili kwenye chombo kinacholinda Hakimiliki na Shiriki cha Cosota.


No comments: