Dec 12, 2011

Filamu za bajeti ndogo

Unataka kuandaa filamu, lakini huna pesa ya kutosha… 

Watengeneza filamu na waandishi wakiwa kwenye semina
iliyoandaliwa na MFDI - Tanzania

TASNIA ya filamu nchini inakua kwa kasi na kuwa kimbilio la vijana wengi, lakini bado tasnia hii imekuwa ikikumbana na changamoto kubwa katika kufikia ubora unaokubalika kimataifa kwenye filamu zetu. Hata wakosoaji wa filamu wamekuwa wakijaribu kukosoa kwa kuilinganisha tasnia hii na tasnia nyingine zilizoendelea kama Hollywood, Bollywood, tasnia ya filamu ya Afrika Kusini na nyinginezo lakini wakasahau kuwa bado tuna mambo makubwa tunayotofautiana.

Katika tasnia za filamu zilizoendelea, mara nyingi huwa zimegawanyika katika mikondo mikuu miwili; mainstream film ambayo pia hujulikana kama major movies studio, na independent film au huitwa kwa kifupi Indies.

Independent film ni mkondo wa filamu zinazotengenezwa kwa bajeti ya kawaida (ndogo) kutoka kwa watengeneza filamu huru na kusambazwa na wasambazaji wadogo au wa kawaida bila msaada kutoka studio kubwa na makampuni makubwa. Mainstream ni mkondo wa filamu zinazotengenezwa kwa bajeti kubwa sana kwa msaada wa studio kubwa ambazo huwa ziko tayari kumsaidia mtengeneza filamu, mradi tu awe na wazo zuri ambalo wanadhani litauza.

Katika tasnia za filamu zilizoendelea mara nyingi waandaaji wa filamu (film producers) ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha, makampuni makubwa, au watu wanaopata msaada wa fedha za utengenezaji kutoka studio kubwa, wakati kwenye tasnia changa kama zetu waandaaji wa filamu ni watu waliochoka, waliokosa kazi/biashara nyingine ya kufanya ambao wanadhani kimbilio pekee lililobaki ni kutengeneza filamu, na wasiokuwa na mahala pa kupatia fedha kwa ajili ya kazi za utengenezaji filamu.

Hivyo, mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabilia tasnia ya filamu nchini ni ukosefu wa fedha (funds) kwa ajili ya kutengenezea filamu, jambo ambalo watengenezaji wengi wa filamu wamekuwa wakilitumia kama kisingizio hasa pale filamu zao zinapokuwa hazina ubora unaotakiwa au kukosa uhalisia.

Ni mara nyingi utasikia mtengeneza filamu akilaumu kuwa hakuwa na pesa ya kutosha kuifanya filamu yake ifikie ubora alioukusudia. Lakini ikumbukwe kuwa, si kila kitu kwenye filamu kinahitaji lazima uwe na bajeti kubwa. Hata kwa fedha kidogo ulizonazo bado unaweza kuandaa kazi nzuri tu endapo utaweka utaratibu unaofaa kabla ya kazi husika kuanza.

Filamu ni chombo muhimu sana cha mawasiliano katika jamii na ustawi wa nchi yoyote, huchangia kupatikana kwa ajira kwa vijana, huchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, husaidia kuwaambia watu wengine kuhusu hadithi zetu, huchangia maendeleo ya nchi na kadhalika.

Kama unaamini unacho kisa kizuri na unataka kutengeneza filamu, unapaswa kwanza kujifunza namna ya kuandaa kazi ya bajeti ndogo kama kweli umeamua kutengeneza filamu nzuri ya bajeti ndogo bila kutafuta visingizio.

Lakini kumbuka kuwa kuna tofauti kubwa tunapozungumzia filamu ya bajeti ndogo inayotengenezwa kwenye tasnia ya filamu kama Tanzania na filamu ya bajeti ndogo inayotengenezwa kwenye tasnia zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo. Wakati sisi tunaandaa filamu ambayo bajeti yake ni kama shilingi milioni tano na kusema kuwa ni ya bajeti ndogo, wenzetu wanatumia kipimo cha dakika moja ni sawa na dola 1000 za Marekani (sawa na zaidi ya milioni 1.6 za Tanzania).

Tasnia na serikali zao zimewekeza nguvu kubwa kwenye kusimamia usambazaji kwa sababu uwekezaji katika utengenezaji wa kazi hizi hautoshi kuhakikisha kwamba bidhaa zinalifikia soko la uhakika.

Kwa tasnia yetu changa, Serikali inapaswa kushirikiana na shirikisho la filamu lililopo katika fursa muhimu zinazopaswa kufunguliwa kama njia za usambazaji katika:
-Kuwapeleka waandaaji/wasanii kwenye matamasha na masoko ya filamu ya kimataifa kuuza bidhaa zao
-Kuanzisha mawasiliano kati ya waandaaji filamu wa Tanzania na wasambazaji wa kimataifa, na
-Kutoa fursa zaidi kwa waandaaji wa Tanzania kukutana na waandaaji wa kimataifa.

Utengenezaji wa filamu si suala la mzaha, si jambo la mtu ambaye jana usiku alilala akiwa hana kazi ya kufanya na leo asubuhi kaamka akiwa na wazo la kutengeneza filamu, bila kuwa na ujuzi, nyenzo wala mtaji wa kutosha. Utengenezaji filamu ni jambo linalohitaji gharama, ni jambo la hatari (venture) linalohitaji muda mwingi na mtengeneza wa filamu hatakiwi kuwa mvivu wa kufikiri au kupoteza muda akipiga soga na rafiki zake au kufanya mizaha.

Ikiwa unataka kutengeneza filamu lakini huna pesa za kutosha (bajeti ndogo) lakini unaamini una kisa kizuri; njia bora ni kuifanya kazi hiyo kwa uangalifu mkubwa kuliko kutumia muda mwingi ukitafuta visingizio.

Kama umepata wazo zuri ambalo unadhani kuwa linafaa kutengenezwa na kuwa sinema; wakati mwingine wala huhitaji kuwa na wazo jipya kabisa - linaweza kuwa ni muendelezo wa wazo lililokuwepo (remake) kabla. Nani anayejali? Unaweza kutumia hadithi ya kwenye kitabu kama msukumo – na kumbuka kitu chochote kilichofanywa kabla ya 1900 ni mali ya umma na unaweza kuchukua, na ukatumia.

Kama unahitaji kitu cha kushikamana nacho, jaribu kuwa na wazo kwanza. Elewa kuwa stori mbovu kamwe haiwezi kutoa filamu nzuri hata kama utakuwa na bajeti kubwa kiasi gani au wachezaji wa filamu hiyo watakuwa ni magwiji wa filamu kutoka Hollywood.

Hivyo, kama una wazo na unaamini kuwa ni wazo zuri, basi andika mwongozo. Haihitaji kuwa na ukamilifu na huna haja kufuata kwa asilimia 100. Hii itakupa tu mahali pazuri pa kuanzia. Kama unataka, unaweza kuandika tu matukio (scenes) kisha ukamtafuta mwandishi mzuri wa kukupangia msuko mzuri wa kisa chako au kuwaachia waigizaji wafanye faraguzi (improvise) kwa kutumia maneno yao.

Pia jaribu kuwa na visheni: katika kuzungumza, kuna mipaka ya mawazo, ni kikomo kwa kiasi cha uzoefu. Hivyo, visheni ya walio pembeni inahitajika ili kupanua uzoefu wako. Usipende kujifanyia kazi mwenyewe bila kushirikisha watu wengine. Fupisha matukio yasiyo na maana na kufanya mambo mengi ila ongeza mambo ya msingi.

Hata hivyo, unaweza kutumia mbinu zifuatazo kutimiza mawazo yako. Zitakusaidia kuunda mtazamo mpana juu ya kile ambacho tayari unakifikiria na kuchochea maendeleo zaidi ya mawazo yako:

Je, unaweza kuona mambo kutoka mtazamo wako? Hebu jiweke katika nafasi ya mtu mwingine na kuona kutoka mtizamo wake katika kuyaona makosa.

Ukishakuwa na mwongozo, chagua waigizaji na wape wafanye mazoezi. Hii itawafanya kuijua vizuri stori yako na kuwasaidia kuingia ndani ya stori yako kabla hawajapoteza muda, unaweza kurekodi mazoezi yao kabla ya upigaji picha za filamu. Njia hii itawasaidia kuona makosa na kuzama zaidi katika uhalisia, na kama unataka wafanye faraguzi (improvise), wakianza mazoezi mapema itawasaidia sana kupata maneno ambayo wangependa kuyatumia ambayo hayatasumbua wakati wa upigaji picha na hata kwenye uhariri.

Tafuta watendaji (crew) watakaokusaidia kwenye upigaji picha wenye ufahamu kuhusu taa, kurekodi sauti au kamera.

Baada ya hapo andaa ratiba (shooting schedule) na hata bajeti. Pangilia kwa umakini namna utakavyotumia kiasi kidogo cha fedha ulichonacho katika filamu hiyo na pangilia njia bora ya kuzitumia fedha hizo. Kumbuka, utahitaji kitu fulani kwa ajili ya kurekodi sauti, kwa ajili ya taa, na kamera.

Kitu chochote kitakachokuwa ghali zaidi ya hapo kinaweza kuleta ugumu katika kufanikisha kazi yako. Pia utahitaji kuingiza kwenye bajeti yako vitu muhimu; vitendea kazi (props), chakula kwa ajili ya waigizaji wako na watendaji wengine, usafiri kwa baadhi yao, na hata pesa za kulipia baadhi ya maeneo (locations). Kumbuka ratiba itamsaidia kila mtu katika kazi yako, kwa sababu hata hao wengine watahitaji kufahamu ni wakati gani wanahitajika kuwepo kwenye kazi yako na wewe utakuwa wapi muda huo.

hivyo weka utaratibu unaofaa. Wakati wa upigaji picha jaribu kuwa mwema kwa kila mtu na jaribu kuwaelezea nini unachokitaka wafanye bila kuwafanya wajisikie wajinga. Unapaswa kuwa na furaha, sawa?

Hivyo basi mfanye kila mmoja kwenye kazi yako ajisikie furaha pia. Kumbuka kuangalia kazi zako unazopiga (footage) mara nyingi iwezekanavyo. Bila shaka hutataka kupoteza hata pigo (shot) moja ulilopiga kwa sababu tu ilikuwa giza sana na huna uwezo wa kurudi sehemu ile kupiga tena picha kwa kuwa tu ulipewa eneo lile kwa siku moja.

Nawatakia kazi njema.

No comments: