Dec 21, 2011

TAFIDA: Viongozi waliochaguliwa wana kazi ngumu kupigania weledi

Mwenyekiti wa Tafida, Paul Mtendah

Makamu Mwenyekiti wa Tafida, John Lister Manyara

Viongozi wapya wa Tafida katika picha ya pamoja na
wanachama wa Chama cha Waongozaji Filamu Tanzania,
picha hii ilipigwa muda mfupi baada ya kumalizika uchaguzi

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Jumapili ya tarehe 18 Desemba, 2011 kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania (Tanzania Film Director’s Association “TAFIDA”), ambapo uongozi mpya uliochaguliwa siku hiyo uliashiria mwanzo mpya wa kuchipua tasnia ya filamu hasa kwa waongozaji wa filamu katika tasnia yetu. Nasema ni mwanzo mpya kwa kuwa nina imani na viongozi wapya waliochaguliwa ambao kwa kiasi kikubwa ninawafahamu kwa uchapakazi wao na kujituma.



Mwanzoni Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania kilipoanzishwa na kupewa usajiri wa kudumu na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata),
kilionekana kama ni chama cha watu fulani waliokosa kazi za kufanya ambao hukutana kijiweni kwa ajili ya kupiga porojo, lakini tangu chama hiki kilipofanikiwa kuandaa mafunzo kwa waongozaji wa filamu ambayo kwa kiasi fulani nilifanikisha kuyaratibu nikiwa mwenyekiti wa kamati ya uratibu, kumekuwepo msisimko mkubwa miongoni mwa waongozaji filamu nchini.



Mafunzo hayo yalifanyika chini ya mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Christian Kauzeni, yalikuwa ni mafunzo maalumu ya siku mbili yaliyowapa uwezo waongozaji wa filamu kujitambua na kujifunza misingi ya uongozaji, yalifanyika katika ukumbi wa Basata, Ilala Sharif Shamba, na yalikuwa sehemu ya mpango maalum wa kuhakikisha waongozaji wa filamu wanajitambua na kuijua misingi ya uongozaji ili kurekebisha makosa yaliyopo kwenye filamu zetu.



Natoa wito kwa viongozi wapya waliochaguliwa sasa, kutochukulia uongozi walioupata kama tunu na kulewa sifa za kuitwa viongozi, bali wanapaswa kufahamu kuwa nafasi hii ni mzigo mzito sana na wana kazi ngumu sana ya kufanya ili kuleta heshima katika tasnia na umma wa waongozaji wa filamu unawategemea.



Viongozi waliochaguliwa wakiongozwa na Mwenyekiti mpya, Paul Mtenda, Makamu Mwenyekiti John Lister na wajumbe wote, wahakikishe kuwa wanapigania sana masuala ya ueledi katika kazi ya uongozaji wa filamu na kuhakikisha kuwa wanachama wanaowaongoza (waongozaji wa filamu) wanapata mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya uongozaji filamu kwa kufuata misingi inayokubalika ili filamu zetu ziweze kufikia kiwango kinachokubalika kimataifa.



Wanapaswa wafahamu kuwa ili Chama cha Waongozaji wa Filamu Tanzania kiweze kupata ufanisi mkubwa, ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanaelekeza nguvu kubwa katika mambo makubwa mawili: kwanza kukijenga chama ili kiweze kufika hadi mikoani na kuwa na sura ya kitaifa zaidi, tofauti na ilivyo sasa ambapo kinaonekana kama ni chama cha Dar es Salaam peke yake. Pili wahakikishe kuwa wanatafuta namna yoyote katika kupata wafadhili watakaokuwa tayari kusaidia katika mafunzo ya weledi kwa waongozaji wa filamu ambao wameonekana kuyakosa, kwani kukosekana kwa weledi katika uongozaji filamu na kutojielewa kwa waongozaji wa filamu ni sababu kubwa ya filamu zetu kuwa kitu kisichozingatia taaluma.



Viongozi wanapaswa kutambua kuwa malalamiko yanayosikika kila kukicha kuhusu ulipuaji wa kazi za filamu ambapo watu wamekuwa wanajifanyia tu bila kuzingatia utaalam ili mradi kazi itoke na wao wapate pesa ni jambo ambalo limekuwa linaichafua sana taaluma ya uongozaji wa filamu nchini, na limekuwa likiwakatisha tamaa watu wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii.



Naamini sasa serikali iko mbioni kuirasimisha tasnia ya filamu ili iwe mkombozi wa vijana katika ajira, ambapo hata mapato ya nchi kupitia filamu yataweza kuongezeka. Ni wakati sasa kwa viongozi waliochaguliwa kuliona hilo na kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kuwa waongozaji wa filamu wanakuwa na hadhi sawa na waongozaji filamu wa tasnia zingine, hasa kwa kupata mafunzo na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.



Binafsi huwa napenda kuiangalia filamu katika mambo matano: Script nzuri, Waigizaji wazuri, Wapigapicha wazuri, Muongozaji mzuri na Mhariri mzuri. Na ukifuatilia kwa makini katika tasnia ya filamu nchini utagundua kuwa tuna waigizaji wengi wazuri, tuna wapigapicha wengi wazuri na tuna wahariri wengi wazuri, lakini tunakosa waandishi wazuri wa script na waongozaji wazuri wa filamu.



Si kama waongozaji wazuri wa filamu hawapo kabisa, wapo wengi tu wenye uzoefu na elimu ya kutosha, tatizo kubwa ni mfumo mbovu unaowafanya kutupwa nje ya ulingo wa soko la filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki wala hawapewi heshima inayostahili. Hivyo viongozi wapya wanapaswa kuhakikisha wanalisimamia jambo hili kwa nguvu zote ili kurudisha imani na heshima ya waongozaji wa filamu, si kama sasa ambapo kila mmoja anaweza kujiita muongozaji wa filamu hata kama haijui misingi ya uongozaji wa filamu.



Ili kufikia ubora katika kuongoza filamu muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu kwani ndiye kiungo muhimu cha timu nzima ya uzalishaji (production team). Ndiye anayewajibika katika kuitafsiri script iliyoandikwa kwenye karatasi na kuihamishia katika taswira halisi (video) – na anapaswa kuiona taswira halisi kabla ya kuanza kazi ya uongozaji na hata kutafsiri mtindo na muundo wa filamu husika, na hivyo kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa taswira halisi.



Kwa sasa hakuna heshima kwa waongozaji filamu kwa kuwa kila mmoja anadhani anaweza kuongoza, kwani tatizo kubwa lililopo ni kwa waongozaji wetu wa filamu kudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua: “standby... action... cut!...” na kusahau kuwa muongozaji ndiye mtu anayepaswa kumtengeneza muigizaji aweze kuuvaa uhusika kwa kutegemea muongozo unasemaje. Nimekuwa nikisisitiza kuwa kama muigizaji atashindwa kuuvaa uhusika, kwa vyovyote hilo siyo kosa la muigizaji huyo bali ndiyo uwezo wa muongozaji wake ulipokomeana.



Muongozaji anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mawasiliano (communication skills) na watu wengine katika kufanikisha kazi.



Hivyo, kukosa mafunzo ya weledi katika uongozaji kumewafanya waongozaji wa filamu walio wengi kuwa wabinafsi kwa kuwa hawajiamini na hiyo inasababisha wawe ni watu wasiopenda hata kukosolewa. Viongozi wapya wa Tafida wanapaswa kuliona hilo na kupigania iwepo idara itakayohamasisha waongozaji wa filamu kupata mafunzo ya weledi (professionalism).



Waongozaji wasijione wanyonge kwa sababu ya kutokwenda shule na wala wasikate tama kwani hata Hollywood kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa katika vyuo vya filamu, bali wanapaswa kuelewa kuwa elimu haina mwisho na bado wanayo nafasi ya kujiendeleza kama wanataka kuwa wazuri katika kazi, kwani sifa kubwa ya muongozaji wa filamu ni kuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa mbunifu (creative vision), na kujitoa kwa dhati (commitment) katika kufanikisha kazi nzima.



Waongozaji wa Hollywood ambao hawakwenda shule lakini wanaheshimika sana duniani kutokana na kazi zao ni pamoja na; Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater na Spike Jonze.



Alamsiki...

No comments: