Dec 28, 2011

ILI KUDUMISHA MAADILI: Kanuni za sheria ya filamu sawa, lakini ada zinatia shaka! KULIKONI DESEMBA 30, 2011

Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu
na Michezo ya Kuigiza, Rose Sayore

Katibu Mtendaji wa Bodi, Joyce Fisso

MIAKA ya karibuni tasnia ya filamu imekuwa ndiyo kimbilio kubwa, chanzo cha ajira na njia ya kujikwamua kiuchumi kwa wasiojiweza au walioshindwa katika fani zingine. Jambo hili limesababisha kuwa na watendaji wasio na uwezo wala taaluma na hatimaye kuzalishwa filamu mbovu zisizokidhi viwango.

Kama mdau na mwanaharakati wa sanaa, mara nyingi nimekuwa nikishauri kuwa tuboreshe kazi zetu na kubadili mtazamo/ dhana iliyojengeka miongoni mwetu kuwa sanaa ya filamu ni kimbilio la wasiojiweza kiuchumi. Na kutambua kuwa sanaa hii ni kazi kama kazi nyingine ambayo inahitaji ubunifu, akili, maarifa na
ni muhimu katika kuinua pato la mtu husika na taifa kwa ujumla kwani inatoa fursa mbalimbali: ajira na kuendeleza biashara ndani na nje ya nchi na kukuza pato la taifa kwa ujumla.

Katika kukabiliana na wimbi la watendaji wasio na uwezo wala taaluma, Serikali kupitia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ilizindua kanuni mpya za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza mjini Musoma mkoani Mara, zilizozinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal. Kanuni hizo zimeainisha adhabu mbalimbali ikiwemo kulipa faini ya papo kwa hapo isiyopungua Shilingi milioni mbili kwa watengenezaji, waoneshaji na wasambazaji wa filamu watakaozikiuka.

Kuzinduliwa kwa kanuni kuliambatana na kauli ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi, kuwataka wote kufuata sheria na kusajiri kazi zao kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao. Waziri Nchimbi alisema Serikali imechoshwa na uwepo wa filamu zisizo na maadili.

Kanuni hizi zinaelekeza kuwa anayetaka kutengeneza filamu lazima aombe kwanza kibali. Miongoni mwa mambo yanayohitaji kibali ni pamoja na kutumia vifaa na mavazi rasmi yanayotumiwa na majeshi ya ulinzi na usalama, madaktari, viongozi wa dini, manesi na sare za wanafunzi. Kibali hakitatolewa kwa picha ambazo uchezaji, miondoko ya mwili wa mshiriki au msanii unalenga ama lengo pekee ni kushawishi, kuwashawishi watazamaji kupata, kujenga taswira na hisia za ngono au kujamiiana.

Nakubaliana kabisa na hatua za serikali katika kuunda kanuni hizi ambazo naamini zitasaidia kurudisha heshima na maadili katika tasnia ya filamu, lakini kuna mambo kadhaa ambayo kwa mtazamo wangu yananitia shaka na ninahisi yanahitaji kupatiwa majibu, vinginevyo hii itakuwa ndo sababu ya kuiua kabisa tasnia hii.

Shaka yangu imejikita katika gharama (ada na tozo kwa filamu na michezo ya kuigiza) zilizowekwa na sina uhakika kama Bodi ya Filamu walifanya utafiti ikiwa ni pamoja na kuongea na wadau ili kuijua hali halisi katika tasnia kabla hawajapitisha ada hizi. Kwani walipaswa kwanza kuifahamu nguvu ya soko la filamu (dynamics of the home video industry) kabla hawajapanga viwango vya ada badala ya kutumia hisia. Pia walipaswa kuufahamu msingi imara unaohitaji mipango madhubuti na ya lazima katika kuiwezesha sekta ya filamu hapa Tanzania.

Nina shaka kwa kuwa nilimsikia mtendaji wa Bodi akijaribu kutetea ada hizi kwa hoja dhaifu zinazokinzana na ukweli huku akionesha dhahiri kuwa, nia ya Bodi ni kukusanya pesa tu, na si kuangalia nguvu ya soko wala kujishughulisha katika kujua waandaaji wa filamu wanapata nini!

Pia naamini kabisa kuwa hakuna data za kuaminika juu ya sekta ya filamu nchini na hakuna utafiti kamili ambao unaeleza ongezeko la uzalishaji wa filamu katika taifa. Wala hakuna mwongozo unaofaa ambao wanaweza kutuambia kuwa wameutumia kutathmini filamu na gharama walizoweka.

Hii inanitia wasiwasi mkubwa; kuwa pamoja ya nia nzuri ya kusimamia weledi kupitia kanuni hizi isije kuwa kuna nguvu fulani inayochochea haya ili kuwaondoa wazalishaji na wasambazaji wa filamu wadogo wadogo katika soko ili wabakie watu fulani, kwani mambo haya yamekuwa yakifanyika na tumeyashuhudia na nimewahi kuyakemea katika makala zangu na hata nilipoitwa kwenye vituo vya televisheni kuzungumzia hali ya soko la filamu. Wamekuwa wakifanya haya kwa kuzihusisha taasisi za serikali.

Tasnia ya filamu duniani imegawanyika katika mikondo mikuu miwili; ‘mainstream’ au ‘major movies studio’, na ‘independent film’ au kwa kifupi ‘Indies’. Wakati kuna filamu zinatengenezwa kwa bajeti kubwa kwa kupata pesa kutoka kwenye mifuko, mabenki au makampuni makubwa (mainstream), kuna filamu nzuri, bora na zenye maadili zinazotengenezwa kwa bajeti ndogo sana kutoka kwa watengeneza wadogowadogo na kusambazwa na wasambazaji wadogo bila msaada wa makampuni makubwa (Indies).

Kuna maswali ambayo Bodi walipaswa kujiuliza na kutafuta majibu kabla hawajapanga kiwango hiki ambacho kwa vyovyote kina nia ya kuwakomoa walio wengi ili kuwabakisha wachache:

• Je, tasnia ya filamu nchini ina thamani kiasi gani kwa sasa?
• Je, gharama kiasi gani inapaswa kutumika kuzalisha filamu?
• Je, waandaaji wa filamu nchini wanatumia gharama kiasi gani kuzalisha kazi zao?
• Je, soko la filamu nchini likoje?
• Je, nini wastani wa mauzo ya kila mwaka ya uzalishaji wa filamu?
• Je, makampuni ya filamu katika sekta ya filamu yana dhamana gani kwa ajili ya kupata mikopo?

Baada ya kujiridhisha kwa majibu yao, ndipo wangepanga viwango kulingana na mikondo iliyopo. Sijui kama Bodi wanalifahamu hili kwani walipaswa kuweka viwango kulingana na mikondo na si kuangalia uraia wa mtu tu, badala ya sasa wanapoamua kuweka kiwango kikubwa bila kujali uwezo wa soko! Kwa vyovyote huwezi kuweka viwango sawa kwa mtu anayetengeneza makala (documentary) iliyowezeshwa na anayetengeneza filamu ya kibiashara kwa kutegemea soko lisilo na uhakika linalodhibitiwa na wafanyabiashara wachache wa Kiasia ambao ndiyo chanzo cha mkanganyiko uliopo.

Hivi hiki kiwango cha sh 500,000 hadi 1,000,000/- kwa kila ombi la kibali cha kutengeneza filamu kitasaidia kukuza maadili au ni mradi fulani? Gharama hizi kwa kibali tu kwa soko lipi la filamu? Kwa nini tunapenda kuvuna pasipo kupanda?

Pia hii gharama ya ukaguzi wa filamu ambapo kwa kila saa ni sh 60,000 hadi 100,000/ na ukaguzi wa mchezo wa kuigiza sh 30,000 hadi 50,000/ ni ya nini? Hivi kwa nini nilipe gharama hii? Kwani kazi ya Bodi ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza ni ipi kama si ukaguzi ambao wanataka tena walipwe? Wameajiriwa kwa ajili ya kukagua filamu na michezo ya kuigiza, na wanalipwa mshahara kwa kazi hiyo, sasa hii ada ya nini tena?

Hali ya uzalishaji wa filamu nchini umekuwa ukiongezeka lakini bado soko limeendelea kuwa duni likichangiwa na ukosefu wa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha, kukosa sera zinazosimama katika misingi ya utendaji, kukosa elimu, ubinafsi na kutokuwa na malengo. Haya ni mambo ambayo Bodi walipaswa kuyasimamia kwanza kabla hawajafikiria kukusanya pesa.

Ukosefu wa fursa za kupata mikopo kwenye asasi za kifedha ni tatizo kubwa mno, walipaswa kulisaidia shirikisho la filamu (ambalo sikuona ajabu lilipoonekana kutotambuliwa kwenye kanuni zao) ili kuinua ubora wa kazi za sanaa na kufikia malengo katika suala la masoko na usambazaji maana ndipo lilipo tatizo. Wazalishaji wa filamu na wasambazaji wa ndani wangepewa nafasi ya kuomba ufadhili kutoka kwenye taasisi ya serikali kama misaada au mikopo kwa ajili ya soko na kutangaza bidhaa.

Kumekuwa hakuna mfumo rasmi wa usambazaji wa filamu nchini. Muundo uliopo katika sekta za filamu zilizoendelea ambapo biashara ya filamu huanzia kwenye box office (mfumo maalum wa sinema unaoanzia kwenye uoneshaji sinema ndani ya majumba ya sinema), kurushwa kwenye vituo vya televisheni za kulipia, kisha katika televisheni za umma, na hatimaye kutolewa kama bidhaa rasmi (DVDs, VCDs, VHS) kwa matumizi ya nyumbani, haupo nchini mwetu.

Utengenezaji filamu nchini unatafsiriwa kama biashara ya barafu inayoweza kumyeyukia aliyenayo mikononi wakati wowote, jambo linalowafanya watengeneza filamu wajikute wakiingia mikataba haraka ya kupata pesa kiduchu kabla barafu haijawayeyukia na kugeuka maji, wakati mwingine bila hata kurudisha gharama walizoingia.

Suala la kusaidia katika masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo ni kwa maslahi kwa Watazamaji wa Tanzania lingekuwa kipaumbele kabla ya kufikiria kujitengenezea miradi. Pia kungewekwa utaratibu kwa watakaotuma maombi na kuwezeshwa kusaidiwa kuzitangaza kazi za Tanzania kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa na masoko ya filamu na watazamaji wa ndani walio katika maeneo ambayo uwezo wa vyombo vya habari kupenya ni mdogo.

Pia uhamasishaji wa soko la ndani ungetiliwa maanani na kuwe na juhudi endelevu ya kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na kununua kazi halisi (original) za Tanzania. Hiyo ingesaidia kuinua soko la ndani linalomsaidia mzalishaji wa kazi za sanaa kupata kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazomsaidia kuwa na uwezo wa kuuza hata katika soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike kwa uzalishaji wa bidhaa bora kimataifa.

Hata ng’ombe wa maziwa hutunzwa kwanza na kulishwa vizuri ndipo ukamue maziwa na si kufikiria kukamua tu bila kumlisha! Kwa mpango huu, kwa nini Bodi wanataka kuvuna pasipo kupanda? Suala hili waliangalie kwa umakini mkubwa vinginevyo litaleta mtafaruku katika tasnia.

No comments: