Dec 14, 2011

Kwa hili, Tanga wamedhihirisha kuongoza jahazi la filamu nchini

Mwl. Kassim El-Siagi akizungumza na wananchi
waliohudhuria tamasha hilo muda mfupi kabla
tamasha halijaanza

Nikiwa katika picha na wadau wa filamu jijini Tanga, 
katikati ni Amri Bawji (mwenye baragashia) na kulia ni
Nassib Ndambwe, mmoja wa waandishi wa script nchini

WIKI iliyopita nilitembelea jiji la Tanga wakati wa tamasha la filamu za Kiswahili zilizotengenezwa mkoani Tanga. Tamasha hilo liliandaliwa na kampuni ya El-Siagi Movies na kudhaminiwa na StarMedia kampuni ya ving'amuzi vya StarTimes, na Nyumbani Hotels & Resorts kupitia vinywaji vyake vya Bavaria. Jiji la Tanga ndilo wanaloishi watu ninaopenda kuwaita “magwiji wa filamu nchini”, kama ambavyo nimewahi kuandika katika makala zangu kadhaa zilizopita.


Kwa nini nawaita watu hawa magwiji wa filamu? Kwa sababu ndiyo watu pekee waliothubutu kuandaa filamu za kibiashara katika miaka ya 1990 japo mazingira yalikuwa magumu sana; wakati huo hakukuwa na mahala pa kuuzia filamu, hata uoneshaji sinema kwenye majumba ya sinema ulikuwa ukisuasua kutokana na kuingia kwa vituo vya televisheni, na sinema zilizotawala nchini zilikuwa za Kihindi.


Ni filamu ya “Shamba Kubwa” (1995) iliyotungwa na kuongozwa na Mwl. Kassim El-Siagi wa Tanga ndiyo iliyofungua milango ya filamu za kibiashara nchini. Kwa walio wengi pengine watanishangaa kwa kuwa hawajahi kuiona filamu hii kwa kuwa wakati ule ilioneshwa kwenye majumba ya sinema; Majestic Cinema – Tanga, Emipre Cinema – Dar es Saalaam, Metropole Cinema – Arusha, na kadhalika.


‘Shamba Kubwa’ ndiyo filamu iliyowaibua wasanii ambao baadaye wamekuwa mahiri katika ulimwengu wa filamu, kama Hassan Master, Jimmy Master, Kaini na Amina Mwinyi, ni filamu hii iliyoteka wengi kwa wakati ule japo teknolojia ilikuwa bado ndogo sana ukilinganisha na hivi sasa.


Filamu hii na nyingine zilizofuata kama ‘Love Story Tanganyika na Unguja (1998)' ya Amri Bawji, ‘Kifo Haramu’ ya Jimmy Master, ‘Dunia Hadaa (2000)' ya Mwl. Kassim El-Siagi, na ‘Augua (2002)' ya Amri Bawji, zote zikitengenezwa na magwiji kutoka Tanga zilitengenezwa katika mfumo wa VHS (analogy), na hata uhariri wake ulitumia akili zaidi kutokana na teknolojia ya wakati huo kuwa ya kiwango kidogo, lakini zilivutia sana kutokana na maudhui na msuko mzuri wa hadithi.


Tanga pia ndiyo mkoa wa kwanza kuanzisha chama ili kukabiliana na changamoto za tasnia ya filamu. Walianzisha Chama cha Watengeneza Filamu wa Tanga (Tanga Film-Makers Association “TAFMA”), wakati huo hata ile filamu ya Girlfriend inayojulikana kwa wengi ilikuwa haijatungwa.
Chama hicho kilisajiriwa mnamo Desemba 20, 2000 na kupewa hati yenye namba BST/0785 na Baraza la Sanaa la Taifa kwa lengo la kuwaunganisha watengeneza filamu na wadau waishio Tanga ili waweze kufanikisha malengo yao na kuleta maendeleo kwenye tasnia ya filamu.


Miaka kumi baadaye ndipo wanaharakati wengine tulipoanza kufikiria kuwa na Shirikisho la Filamu katika kumkomboa mtengeneza filamu na mdau!


Nilipata heshima kubwa sana kukutana na magwiji hawa wa filamu wa jiji la Tanga baada ya kualikwa kwenye tamasha hilo la filamu za Kiswahili kwa kuwa ilionesha jinsi wanavyothamini mchango wangu katika kuikuza na kuiendeleza tasnia hii, ambapo tulipata wasaa mzuri wa kujadili mapungufu katika tasnia.


Hakika tamasha hili liliwapa wakazi wa jiji la Tanga  fursa nzuri ya kuona filamu maarufu za Kiswahili zilizoandaliwa Tanga na lilifanyika katika viwanja vya Tangamano, kuanzia Jumatatu ya tarehe 5 Desemba hadi 10 Desemba, 2011.


Tamasha hili lilikuwa na lengo kuu la kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wa Tanzania Bara (zamani Tanganyika) ambapo wadau na watengeneza filamu walipata nafasi ya kujadili mambo mbalimbali kuhusu filamu katika miaka hii hamsini tangu tuwe huru.


Kwa mujibu wa muandaaji wa tamasha hilo, Mwalimu Kassim El-Siagi, ambaye pia ni mtayarishaji maarufu wa filamu mkoani Tanga, pamoja na kuwapa fursa wakazi wa Tanga kuona filamu maarufu zilizoandaliwa Tanga, tamasha pia lilikusudia kuonesha tamaduni mbalimbali ambazo zinazaa utamaduni wa Kiswahili ambao unapatikana katika maeneo ya mwambao na zaidi ya hapo. Tamasha hilo lilikuwa likitanguliwa na maonesho ya ngoma na muziki kutoka katika vikundi mbalimbali kila siku.


Filamu zilizooneshwa ni pamoja na Fimbo ya Baba, Chukua Pipi ambazo zimetayarishwa na Shirika la Uzima Kwa Sanaa (UZIKWASA) la Pangani. Shahidi ya Amri Bawji, Augua, Ua la Matumaini, A Love Story – Tanganyika na Unguja, Shamba Kubwa, Dunia Hadaa, Habari Kubwa, ambazo zimeongozwa na El-Siagi, na filamu nyingine kibao kutoka kwa watengeneza filamu wa jijini Tanga.


Pia tamasha hilo lilikusudiwa kuwapa fursa watayarishaji na wadau wa filamu kukutana na kujadiliana changamoto ambazo wanakutanana nazo katika tasnia ya filamu; kukosekanana kwa ufadhili, matatizo ya masoko na usambazaji, na kadhalika.


Siku zote nimekuwa nikisema kuwa sekta ya burudani hapa nchini imesheheni utajiri mkubwa sana wa utamaduni na uchumi kupitia filamu, na sina shaka katika hili. Hata hivyo, hili la tanga limenidhihirishia kuwa kumbe tukiamua tunaweza, kwani nilishuhudia jinsi watu walivyo na msisimko wa ajabu kuhusu sinema zinazotokana na hadithi zetu wenyewe.


Tatizo ni kwamba hadi sasa serikali bado haijaamua kuirasimisha sekta hii ili watu kama E-lSiagi na Amri Bawji waweze kufaidi matunda ya kazi zao, na badala yake imewasababishia waandaaji hawa na wengine waendelee kuwa masikini wa kutupwa, japo serikali imekuwa inajigamba na kaulimbiu ya “Tumethubutu, Tumeweza na Tunasonga mbele!!”.


Nilidhani ile nadharia ya Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za wanyonge nchini (Mkurabita) ingesaidia kuirasimisha tasnia hii ili kuwafanya waandaaji, wasanii na wadau wafanye kazi kwenye mazingira yaliyo rasmi kwa kuwa hali ilivyo sasa inawafanya wakose fursa nyingi za kukuza kazi zao na kuongeza vipato. Mfano mzuri ni watu kama Mwalimu Kassim El-Siagi na Mzee Amri Bawji, kwa kweli hawapaswi kuwa katika hali waliyonayo sasa kwa kuwa wamethubutu na hawakati tamaa, walistahili kuwa na hadhi kubwa zaidi katika tasnia hii.


Urasimishaji wa Biashara yoyote ni jambo lisiloepukika kama tunataka kuendelea, ili wadau wa filamu waweze kuwa na maendeleo na kukua kiuchumi hawana budi kurasimishwa ikiwa ni pamoja na kazi wanazozifanya.


Hakuna 'excuse' yoyote ambapo waandaaji, wasanii na wadau wanaweza kukuza pato lao, kuondokana na umaskini na hata kushindana kimataifa kama hawataingizwa kwenye mfumo rasmi ambao utawafanya watambulike ndani na nje ya nchi ili kujenga mazingira ya wao kuweza kukopesheka, kupata fursa za kikazi na kukuza kazi wanazozifanya. Katika mataifa mengine wasanii wako rasmi na wameweza kuvuma na kupaa kiuchumi.


Nadhani sasa ni wakati muafaka Serikali ione umuhimu wa kuwashirikisha watu kama hawa katika masuala yote na nyakati zote na si kusubiri wakati wa kampeni za uchaguzi tu.


Tunahitaji kuwa na chombo kitakachozingatia kuchangia fedha kwa miradi ya maendeleo katika makundi kama; sinema ndefu na fupi, Makala (Documentaries) na Uhuishaji (Animation). Chombo mfano wa Benki ya Wasanii kitakachochangia maendeleo ya filamu kwa kuwakopesha waandaaji wa filamu na kushikiria copyright hadi pale pesa itakaporudishwa.


Misaada ya maendeleo itakayotolewa ichukuliwe kama uwekezaji na kuweka mifumo ya kufidia matumizi yote ya maendeleo na riba kwa kazi wakati mradi unaingia katika awamu ya uzalishaji (production phase). Endapo mradi utashindwa kueleweka, chombo kilichoundwa kiwe na haki ya kurejesha gharama.


Chombo hiki pia kiunge mkono juhudi za masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo zina maslahi kwa watazamaji wa Tanzania, kama nilivyojionea kwa filamu za Tanga.


Tutake tusitake uchumi wa dunia sasa unahama kuelekea zama za habari na usimamizi wa elimu na biashara; hii inathibitishwa na mkazo ulioongezeka katika utafiti na maendeleo na kuongezeka kwa teknolojia.


Tunapaswa kuwa na sera na idara ya Utafiti chini ya nguzo ya zama za habari katika kukuza utafiti sahihi na sera za kutoa taarifa ambayo itaongeza taarifa ya ndani ya usimamizi wa uwezo wa soko katika tasnia ya filamu, na kutoa taarifa zitakazofikiwa kwa urahisi na vyombo vyote binafsi na vya umma kwa anayetaka kujua zaidi kuhusu sekta hii.


Bado nasisitiza, kwa hili la Tanga, hakika wamedhihirisha kuongoza jahazi la filamu nchini.


Alamsiki.

No comments: