Sep 18, 2013

Ili kuongeza ufanisi: tupiganie Bodi Huru ya Filamu

 Kama wadau wa filamu tufikirie kutumia Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kama haya ya Dar es Salaam ambayo ni njia nzuri sana katika kujitangaza kitaifa na kimataifa


INASEMWA kuwa sekta ya filamu nchini kwa sasa imerasimishwa, jambo ambalo limekuwa haliniingii akilini kwa kuwa sijaona mfumo wowote unaotuashiria kwamba sasa tuko rasmi zaidi ya huu wa kulipa kodi kupitia stika za TRA. Hivi tumerasimishwa kwa Sera ipi hasa?

Sera ni hati muhimu inayoelezea thamani na kutokosekana kwa miongozo ya lazima na visheni. Nimewahi kuandika kabla kuwa bila sera madhubuti ya filamu maendeleo katika sekta hii yatabaki kuwa ndoto hata kama viongozi wa serikali watatuahidi mambo makubwa kiasi gani. Lakini kwanini tuendelee kuongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya kupigania uwepo wa sheria?

Tarehe 9 na 10 mwezi huu tulikuwa na kongamano la kitaifa la wadau wa filamu kuhusu mapendekezo ya Sera ya Filamu itakayotuongoza katika sekta ya filamu ili tufikie mafanikio. Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) mambo mengi yalijadiliwa, lakini leo ningependa kujikita kwenye jambo moja: Bodi ya Filamu (Tanzania Film Board).

Bodi hii ya Filamu ni tofauti na Bodi ya Ukaguzi wa Filamu (Tanzania Film Censorship Board) iliyopo iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 1976, hii ninayoikusudia ni Bodi Huru ya Filamu itakayowezeshwa na serikali (an independent government supported board) ikiwa na idara kadhaa zinazoshughulikia masuala ya filamu ili kupunguza mlolongo wa taratibu ambazo zimekuwa chini ya sheria na mamlaka mbalimbali (one stop shop).

Hapa pana tofauti kubwa kati ya Bodi ya Ukaguzi wa Filamu tuliyoizoea na Bodi ya Filamu ninayoikusudia (Independent Film Board), tofauti hiyo ni katika muundo na majukumu yake. Bodi ya Ukaguzi wa Filamu iliyopo ni chombo cha Serikali na ina majukumu makubwa ya kukagua na kupanga madaraja ya filamu na michezo ya kuigiza; kukagua na kutoa vibali kwa maeneo yote yanayotumika kwa maonesho na usambazaji wa filamu au michezo ya kuigiza; kuafiki na kutoa vibali kwa shughuli za usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza; kuafiki na kutoa vibali kwa maonesho ya filamu na michezo ya kuigiza. Pia kuafiki, kuzuia au kudhibiti maonesho na usambazaji wa filamu na michezo ya kuigiza.

Bodi hii ya ukaguzi imerithi sheria zilezile za kibaguzi za mkoloni (censorship laws) zilizotumika kukagua sinema na kuondoa baadhi ya vipande visivyotakiwa kutazamwa na Waafrika. Yaani tulikuwa tunapangiwa nini cha kutazama na nini hatupaswi tutazame. Lakini kwa mazingira ya sasa, sisi wote ni Watanzania, tunaujua utamaduni wetu na tunafanya sinema za Kitanzania kwa ajili ya Watanzania, kwanini tuwe na chombo cha kutukagua, kutupangia na kutueleza kipi ni cha Kitanzania na kipi si cha Kitanzania?

Bodi Huru ya Filamu itatusaidia kuleta ufanisi hasa kwa kuangalia sekta za wenzetu waliofanikiwa. Bodi hii itaongozwa na wadau wenyewe wa filamu wenye weledi ikifanya kazi kama zifanyavyo bodi zingine za kitaaluma; mfano Bodi ya Madaktari, Bodi ya Wakandarasi, Bodi ya Wahasibu na kadhalika ambazo zimekuwa zikiendeshwa na wadau wenyewe na kusimamia masuala ya kitaaluma katika sekta husika. Ushahidi nilionao ni kwamba Bodi hizi zimeleta ufanisi mkubwa kwenye sekta hizo.

Bodi ya Filamu itakayosimamiwa na wadau wenyewe itasaidia kusimamia misingi, sheria na mazingira bora ya kufanya biashara kwa wawekezaji wa ndani na nje, itapunguza urasimu, itawadhibiti wadau/wasanii wasiofuata misingi na taratibu zitakazowekwa na kusaidia utambuzi wa bidhaa hapa nchini.

Pia itasaidia uboreshaji wa udhibiti wa mfumo wa usambazaji, italinda ubora, usalama na thamani ya kazi zetu, itarahisisha ujumuishaji wa taarifa nyingi kwa kuwezesha kuitambua sekta, mfumo wa uzalishaji, ubora, usalama na ufuatiliaji wa bidhaa na masoko (Traceability).

Bodi hii itakuwa na idara kadhaa kama vile za utoaji wa taarifa za upatikanaji wa pesa (Funding Information) na kutoa fursa kwa watengeneza sinema. Idara ya kuandaa takwimu za kina (Data Collection) na kutoa fursa ya kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine ya Afrika, na duniani na hivyo kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na kuigiza pesa za kigeni.

Idara zingine ni ile ya Uhamasishaji Biashara na Masoko, Idara ya elimu na mafunzo ya weledi (Professionalism), na Idara itakayosimamia ukusanyaji wa mapato (Revenue Collection) yatokanayo na filamu kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato (TRA). Pia Idara itakayosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia (Piracy) wa kazi za sanaa na hivyo kuwafanya watengenezaji wa kazi hizi kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato (Economic Reward) yatokanayo na kazi zao, Idara itakayopanga madaraja ya filamu (Rating of Films), Idara ya ukuzaji na utafiti (Research and Development) na Idara ya ushauri (Consultation Agency).

Katika idara hizi, acha leo niizungumzie Idara ya Uhamasishaji Biashara na Masoko ambayo itatusaidia kuwa na soko imara. Pamoja na mambo mengine ipewe jukumu la kusimamia vipaumbele vifuatavyo: kuandaa, kufuatilia na kupitia sera, sheria na programu zinazosimamia biashara ya filamu nchini; kuwezesha upatikanaji wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa kwa filamu za Tanzania; kuandaa mikakati madhubuti ya ujenzi wa miundombinu ya masoko nchini; kuwajengea uwezo wazalishaji wa filamu ili kazi zao zifikie viwango vya kimataifa; kuendeleza mfumo sahihi na madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi, usambazaji na uhifadhi wa taarifa za masoko.

Pia kuongeza uelewa wa wafanyabiashara juu ya fursa za masoko zilizopo ndani ya nchi, kikanda na kimataifa ili waweze kunufaika nazo; kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda wazalishaji dhidi ya biashara isiyo halali hususan kutoka nje; na kuendeleza na kujenga uwezo wa wajasiriamali katika kuibua na kutumia fursa za uzalishaji, biashara na masoko.

Kwa msaada wa Serikali Bodi itasaidia juhudi za wasanii katika masoko na usambazaji kwa ajili ya filamu ambazo ni kwa maslahi ya watazamaji wa Tanzania, pia itazitangaza kazi za Tanzania kwenye matamasha ya filamu ya kimataifa na masoko ya filamu na watazamaji wa ndani walio katika maeneo ambayo uwezo wa vyombo vya habari kupenya ni mdogo.

Uanzishwaji wa Bodi ya aina hii utawezesha bidhaa zinazozalishwa nchini kutambulika kitaifa na kimataifa katika uuzaji wake na kuwa na uwezo wa kuuza bidhaa hizo katika soko la kimataifa.

Katika uhamasishaji wa soko la ndani, kuwe na juhudi endelevu ya kuhamasisha Watanzania kuwa wazalendo na kununua kazi halisi (original) za Tanzania. Hiyo itasaidia kuinua soko la ndani litakalomsaidia mzalishaji wa filamu kupata kipato cha kutosha kitakachomuwezesha kuzalisha sinema zenye ubora kwa soko la nje na kuifanya Tanzania itambulike zaidi kimataifa, tofauti na ilivyo sasa.

Ieleweke kuwa masoko ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya biashara. Taarifa sahihi za masoko zikitolewa kwa wakati muafaka ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara na hivyo kuongeza mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Bodi hii iwe na kazi ya kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuleta ufanisi katika sekta ya Masoko ili kuongeza tija katika ukuaji wa uchumi sanjari na kuondoa umasikini.

Hatua hii itawawezesha Wajasiriamali kutumia Fursa za masoko zitolewazo na Marekani kupitia mpango wa AGOA (African Growth Opportunity Act). Katika eneo hili, Bodi itakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa elimu kwa wadau kuhusu fursa za soko hilo pamoja na masharti yake na kutumia fursa za masoko kupitia Vituo vya Biashara vilivyopo duniani.

Kupitia Vituo hivi fursa mbalimbali zilizopo nchini zitatangazwa. Pia itasaidia uwepo wa ushindani huru na wa haki utakaoleta ufanisi wa utendaji wa kiuchumi na kukidhi maslahi ya walaji ambao ndiyo kitovu cha kukua kwa biashara na uchumi. KupitiaTume ya Ushindani (FCC) na COSOTA, Bodi hii itaweza kuendesha misako katika maeneo zinakoingilia bidhaa kama vile bandari, Viwanja vya Ndege, Maduka na Mipakani ili kukagua uwepo wa bidhaa bandia. Aidha Bodi itatoa elimu kwa wadau kuhusu shughuli zake na athari zinazosababishwa na bidhaa bandia.

Pia tuangalie namna nzuri ya kuzitumia fursa kama za Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ambayo yamekuwa ya mafanikio makubwa na kukutanisha Wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi. Maonesho haya yamekuwa yakiratibiwa na Tantrade na yamekuwepo kwa takribani miaka arobaini sasa. Maonesho haya yatapanua fursa zaidi kwa wajasiriamali wa sekta ya filamu kubadilishana uzoefu, kupeana taarifa za masoko na kuuza bidhaa zao.

Alamsiki.

No comments: