Sep 5, 2013

Maadili na uandaaji wa filamu katika nchi zinazoendelea



Elizabeth Michael maaruf kwa jina la Lulu katika pozi

IJUMAA ya wiki iliyopita nilialikwa kwenye ofisi za Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kwa ajili ya mazungumzo ya kiofisi, kuhusu mustakabali wa sekta ya filamu nchini, hasa ikizingatiwa kuwa mimi ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania, chombo cha juu cha wadau wa filamu nchini, kinachopaswa kufanya kazi kwa ukaribu na Bodi ya filamu.

Hapo kwenye ofisi za Bodi, niliongea mengi na watendaji wakuu wa ofisi hiyo, chini ya uenyekiti wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, yaliyotufikisha katika suala la maadili katika filamu zetu ambapo aliwataja baadhi ya wasanii wanaokiuka maadili na hawako tayari kujikosoa hata pale wanapoelekezwa njia sahihi.

“Kwa mfano (anamtaja jina msanii mmoja), unapomwelekeza jambo kwenye kazi zake hujifanya kukusikiliza kwa makini lakini ukweli huwa ana-pretend tu, na akitoka hapa huyafanya yaleyale. Lakini kuna wasanii wengine unaona kabisa wana nia ya dhati ya kutengeneze filamu nzuri zenye maadili na hukubali makosa pale unapowakosoa. Mfano Elizabeth Michael (Lulu), huyu ameonekana kubadilika kabisa. Tulimwita baada ya kuikagua sinema yake ya ‘Foolish Age’, jinsi alivyotoa ushirikiano mkubwa katika kuupokea ushauri wetu kwa kweli ameonekana kubadilika sana…”

Haya ni baadhi ya yale tuliyojadili ambayo yalinifanya kukumbuka mjadala mmoja niliokuwa nao na rafiki yangu mmoja raia wa nchi jirani, ambaye huwa tunakutana kwenye mtandao wa facebook, mjadala ulihusu maadili na utengenezaji wa sinema katika nchi zinazoendelea, na athari wanazozipata wale wanaoigiza na hata kwa jamii nzima.

Ukweli ni kwamba filamu ni mojawapo ya sanaa na nguzo muhimu ya Utamaduni. Filamu zimeibuka kuanzia karne ya ishirini na baadaye kuwa kishawishi kikubwa na mawasiliano ghali katika karne hii ya ishirini na moja. Hakuna aina nyingine ya sanaa ambayo imesambaa kwa ufanisi na kuonekana kuvuka mipaka ya kiutamaduni katika mataifa mengi.

Rafiki yangu huyo alizisifu sana filamu za Tanzania na akabainisha kuwa anatuonea sana wivu kwa fursa tuliyonayo, lakini akakiri kuwa kwa miaka ya karibuni filamu zetu zimeanza kukosa mwelekeo, na zinatupeleka kusikojulikana. Akaniuliza kupata maoni yangu, je, ni kwanini kila kukicha ni filamu za mapenzi tu ndizo zinazotawala kwenye soko letu? Je, kwanini hadithi zetu nyingi si za asili yetu bali tunanakili kwa wenzetu zenye vitendo na maudhui ya jamii za nje? Kwa nini hatutaki kutumia visa vyetu wenyewe hadi tuige kutoka kwa wenzetu?


Maswali hayo yakanikumbusha wakati nafanya utafiti, nilijiuliza sana maswali haya, na wakati natafuta majibu yake yakazaliwa maswali mengine: Je, filamu zetu zilivyo leo zinaweka kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo? Au kizazi chetu kinaweka kumbukumbu potofu ya filamu na sanaa zetu na utamaduni kwa vizazi vijavyo?

Kwa kweli haya ni maswali muhimu na inabidi kila mdau wa filamu ajiulize. Tusipokuwa makini tutajikuta tukipita njia potofu na kukipoteza kizazi chetu kwa kuwa njia tunayoenda nayo sasa katika filamu zetu ni ile iliyojengwa juu ya msingi wa wimbi la utandawazi inayoakisi utamaduni wa Kimagharibi.

Kwa tafsiri rahisi, filamu ni aina ya mawasiliano yanayotumiwa kutolea hadithi au kuwafundisha watu kuhusiana na fikra au mitazamo mipya katika jamii kupitia video/skrini. Wafuatiliaji wa filamu huangalia filamu ambazo zinaelezea hadithi fulani kama njia mojawapo ya kuburudika, kujifunza au kwa sababu ya upenzi tu.

Filamu ni njia bora ya kuongeza uelewa na kuteka umakini wa watu katika mada fulani au suala fulani. Hata hivyo, kabla ya kuandaa filamu, kuna masuala mengi ya kimaadili ambayo lazima yazingatiwe.

Katika karne hii teknolojia ya televisheni na maonesho mbalimbali ya wajasiriamali vimeitangaza sana tasnia ya filamu kwa watu wote; watazamaji wa mijini na vijijini katika nchi nyingi zinazoendelea. Filamu pia zimeweza kutumika kama njia muhimu ya uchumi.

Kama taifa, tumeshindwa kuipa umuhimu tasnia ya sanaa/utamaduni ndiyo sababu ya uchafu na tatizo la maadili tunalolishuhudia katika filamu zetu, kwani kumekosekana uthibiti wa kazi chafu. Wengi wamekuwa wanajiuliza kwa nini tunakosa alama ya mfano wa filamu zetu? Nini chanzo cha wasanii wetu kuigiza na kuiga filamu chafu (zisizo na maadili)?

Hapa ieleweke kuwa mapokeo ya kazi za sanaa katika jamii yoyote hufuata utaratibu wa kurithisha mfumo, mtindo, muundo, maudhui na hivyo hubaki kuelezea juhudi, matatizo au mafanikio ya jamii husika. Kama sanaa zetu haziakisi maisha yetu, tujue kuwa vizazi vyetu vitarithi mambo yasiyokuwa yetu.

Tutake tusitake, ukweli ni kwamba fani yetu ya filamu kwa sasa ipo katika hatari kubwa ya kuporomosha mfumo mzima wa maadili katika jamii zetu kwani watayarishaji na wasanii walio wengi katika tasnia hii wameshapotea njia kwa kutofuata au kutoijua miiko na maadili katika hadithi wanazoandaa, mitindo na maudhui ya hadithi yanaonekana dhahiri kupotosha kulingana na asili yetu, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Kama nilivyosema tunapaswa kuangalia masuala ya kimaadili kabla ya kuandaa filamu. Kwa kuwa wale wanaopigwa picha za sinema (waigizaji) huyafungua maisha yao kwa mtengenezaji wa filamu, mtengenezaji filamu ana wajibu wa kufikiria jinsi ya filamu itakavyowaathiri waliomo ndani yake. Ingawa suala hilo ni tata, kitabu cha ‘Introduction to Documentary’ cha Bill Nichols hutoa ufahamu: "Nini cha kufanya na watu? Weka tofauti, swali linakuwa, 'nini wajibu wa watengenezaji wa filamu na athari ya matendo yao katika maisha ya wale wanaoigiza?' Wengi wetu huufikiria wito wa kuigiza katika filamu kama fursa, nafasi ya kutoka kimaisha, au hata bahati. Lakini vipi kama wito huu si kwa ajili ya kuigiza katika filamu lakini kuyaweka maisha yako mwenyewe katika filamu? Watu wengine watakufikiria nini; watakuchukuliaje? Ni mambo gani ya maisha yako yatakuwa hadharani ambayo hukuyatarajia?...

Maswali haya yana majibu mbalimbali, kulingana na hali ilivyo, lakini yana utaratibu tofauti. Yanaweka uzito tofauti wa wajibu wa watengenezaji wa filamu ambao hupenda kuwaonesha wengine badala ya kuonesha uhusika wa uvumbuzi wao wenyewe. Masuala haya huongeza kiwango cha kuzingatia maadili kwa maandishi ambayo si maarufu sana katika utengenezaji wa filamu.”

Hivyo, watengenezaji wa filamu wana wajibu wa kuwalinda waigizaji, na wanapaswa kujitahidi kutowadhalilisha au kuwasababishia madhara. Hata hivyo, mara nyingi kuwalinda waigizaji huleta msuguano na tamaa ya watengenezaji filamu kuandaa filamu inayolazimisha.

Mbali na kuzuia madhara kwa waigizaji wa filamu, watengenezaji wa filamu lazima wajitahidi kuwa na muongozo wenye sifa za wahusika wote (character description) ili kuwafanya waigizaji wawe na ufahamu wa jinsi watakavyowakilishwa katika filamu na jinsi filamu itakavyotumika. "Maadili huwepo kuongoza mwenendo mzima sehemu ambayo mambo magumu na haraka, kanuni au sheria pekee hazitoshi.

Wakati wa kutengeneza filamu, kuna chaguzi nyingi kwa watengenezaji wa filamu. Watengenezaji wa filamu lazima waamue kipande kipi wakijumuishe, waigizaji gani, na jinsi ya kuwawasilisha washiriki katika filamu. Kwa hiyo, ni muhimu kwa watengenezaji wa filamu kutambua madhara ya maamuzi yao. Watengenezaji wa filamu wanapaswa kujitahidi kutowadhalilisha au kuwasababishia madhara wanaowapiga picha, na wanapaswa kujitahidi kuwawasilisha katika njia bora, au vinginevyo kuwajulisha jinsi watakavyowasilishwa. Aidha, ingawa watengenezaji wa filamu kawaida huandaa filamu kuwakilisha maoni yao, hawapaswi kutumia sauti moja au mtazamo mmoja tu kuiwakilisha jamii nzima.

Kinachotokea hapa kwetu ni mtayarishaji wa filamu kufanya kazi kwa shinikizo la woga wa soko! Hana uhakika wa soko lake na endapo atakuwa jeuri basi kuna hatari ya filamu yake kutosambazwa, hivyo kinachobaki kwake ni kuweka mikono nyuma awapo mbele ya msambazaji ili filamu yake isambazwe. Na hii ni hatari sana kwa mustakabali wa tasnia nzima ya filamu!

Kwa hali hii maadili yanazidi kupotea kwa kuwa mnunuzi wa mwisho bado hujikuta anafuata mkumbo wa nguvu ya soko lililoamuliwa na msambazaji bila kujali ubora wa filamu; kuanzia kwa mtunzi, muigizaji, muongozaji, mazingira na taaluma ya filamu yote! Ananunua filamu kwa mazoea ya majina na hadithi!

Ndiyo sababu filamu nyingi za Kitanzania au michezo ya kuigiza ni vitu vilivyopoteza mwelekeo kwani leo hii zinafuata mifumo na mtiririko wa kigeni zaidi. Yote hii inasababishwa na wavamizi kwenye fani waliodhani kuwa mtu akikosa kazi ya kufanya basi kimbilio lake ni kwenye sanaa hasa filamu.

Tumejikuta tukiwa na idadi kubwa ya watayarishaji filamu, waandishi, waongozaji na waigizaji bandia wasio na uelewa jambo linalosababisha kazi zetu kuwa sawa na Big G inayoisha utamu kwa muda mfupi, wakati huohuo wenye taaluma wakitupwa nje ya soko kwa kuwa sanaa siku hizi imekuwa ni biashara isiyozingatia na kufuata maadili ya Taifa.

Alamsiki.

No comments: