Aug 7, 2013

Uongozaji huu wa filamu utaleta maafa makubwa


 Muigizaji wa filamu Tanzania, Maulid Mfaume, aliyevunjika miguu yote kwa kujirusha toka ghorofa ya nne wakati wa upigaji picha

UONGOZAJI wa filamu ni zaidi ya kujua “standby... action... cut!” Uongozaji wa filamu ni tatizo kubwa mno kwenye tasnia ya filamu nchini, ni tatizo kwa kuwa waongozaji wetu wa filamu hudhani kuwa kazi ya uongozaji wa filamu ni kujua “standby... action... cut!” na kusahau kuwa muongozaji wa filamu anapaswa kuwa mbunifu na kiungo muhimu kati yake na timu ya uzalishaji.

Muongozaji wa filamu anawajibika kuutafsiri muongozo wa filamu ulioandikwa kwenye karatasi na kuuhamishia katika picha halisi na sauti kwenye skrini – na anapaswa kuiona taswira halisi na kutafsiri mtindo na muundo wa filamu hiyo, na hivyo kufanya kazi zote mbili kama kiongozi wa timu na msimulizi kwa kutoa picha halisi. Pia anapaswa kuangalia mtu anayefaa kuigiza, ndiyo maana mojawapo ya majukumu ya muongozaji ni pamoja na kufanya usaili (casting).

Wakati masuala muhimu katika utayarishaji wa filamu, kama vile fedha na masoko, hubakia mikononi mwa mtayarishaji wa filamu (producer), muongozaji wa filamu anapaswa kuwa na ufahamu wa bajeti inayotumika kwenye filamu anayoiongoza na kujua ratiba. Katika baadhi ya filamu, waongozaji huhodhi majukumu mengi kama Muongozaji/Mtayarishaji au Muongozaji/Mwandishi, jambo ambalo halikatazwi kama atakuwa na uwezo wa kuyatenda kwa ufanisi.

Pia muongozaji wa filamu anapaswa kuwa na uelewa wa kina wa jinsi sinema inavyotengenezwa, kuwa na ubunifu mkubwa (creative vision), ufahamu wa namna ya kuandika script na kujitoa kwa dhati (commitment) katika kufanikisha. Yeye anahusika moja kwa moja kwenye mafanikio yoyote ya kisanii, mafanikio ya kibiashara au kushindwa kwa filamu katika soko.

Kwa maana hiyo ndiye anayepaswa kumtengeneza mhusika kwa kutegemea muongozo wa filamu (script) unasemaje. Kama muigizaji atashindwa kuuvaa uhalisia, hilo sio kosa la muigizaji mwenyewe bali ni kosa la muongozaji wa filamu kwa kushindwa kuongoza vyema na hutafsiri uwezo wa muongozaji ulipokomea.

Hivi umewahi kuona filamu (hasa za nje) ambayo mhusika mkuu katika filamu hiyo ni mtoto mdogo, ambaye huonekana amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuigiza na kuuvaa uhalisia kiasi kwamba unaweza kudhani hakuwa akiigiza bali yalikuwa ni matukio halisi? Kama uliiona sinema ya aina hii, je, umewahi kujiuliza inamaana huyu mtoto ana akili nyingi kuwazidi waigizaji watu wazima waliopo kwetu? Au hapa tofauti ni nini hasa?

Kwa vyovyote jibu ni moja tu; muongozaji wa filamu hiyo kafanikiwa kumtengeneza, kitu ambacho kinakosekana kwa waongozaji wetu wa filamu wanaodhani ukijua kusema “action... cut...” utakuwa umefuzu kuwa muongozaji wa filamu.

Ninalazimika kuyaeleza haya niliyowahi kuyaeleza hapo nyuma baada ya matukio makubwa mawili ya kusikitisha yaliyotokea katika tasnia hii yakiashilia kuvamiwa kwa nafasi ya uongozaji wa filamu na watu wasiokidhi vigezo vya uongozaji wa filamu na kusababisha madhara makubwa kwa waigizaji. Kama mwanaharakati na kiongozi wa taasisi inayosimamia masuala ya filamu nawajibika kuyasemea.

Tukio la muigizaji Maulidi Mfaume, maarufu kama Gado Balotel, aliyevunjika miguu yote miwili pamoja na kuteguka nyonga baada ya kudondoka toka ghorofa ya nne alipokuwa akiigiza filamu ya msanii mwingine aitwaye Joseph Mteme ‘Baga’ limesaababishwa na aliyekuwa muongozaji wa filamu hiyo kushindwa kumudu nafasi ya uongozaji wa filamu.

Gado Balotel alikutwa na balaa hilo akiwa Location ndani ya hotel ya Con Way, Magomeni Kagera wakati akiigiza. Kuna scene iliyomtaka mtu aigize anajirusha ghorofani, muigizaji huyu kwa maelekezo ya muongozaji wake akaruka toka ghorofa ya nne na kutua chini (ambako hakukuwa na kizuizi chochote cha kumlinda na madhara) kwa kufikia miguu ambapo alihisi moto unawaka miguuni mwake huku harufu ya damu ikimtoka puani na mdomoni na baada ya kujiangalia aliona visigino vyake vikiwa vimepasuka vyote huku tumboni kukiwa na maumivu makali sana, kumbe wakati huo nyonga ilikuwa imeachia huku miguu yake ikiwa imesogea tumboni.

Wasanii wenzake walimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Mwananyamala ambapo ilishindikana na baadaye kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Tukio jingine ni la majuzi, ambapo msanii mwingine (hadi tunakwenda mitamboni nilikuwa sijapata jina lake) alimwagiwa mafuta ya taa mwilini na kuunguzwa moto wakati wakiwa location kwa ajili ya upigaji picha ya sinema. Lengo lilikuwa eti kuonesha mtu anayeungua moto kwenye filamu hiyo.

Vitendo kama hivi si tu havipaswi kufumbiwa macho, bali vinapaswa kukemewa na kulaaniwa kwa nguvu zote, ndiyo maana nimekuwa nikipigania uwepo wa mamlaka kamili ya Shirikisho la Filamu nchini ili kuwadhibiti waongozaji wa aina hii. Chama cha Waongozaji wa Filamu nchini kimekuwa kikiendesha mafunzo mara kwa mara kwa wanachama wake kuongeza ufahamu na kujitambua kitendo kitakachopunguza matatizo kama haya, kwani kwa sasa katika filamu zetu si ajabu kumuona mwigizaji akiigiza analia lakini uso wake umebeba tabasamu la chati, au yale matukio ya utekaji nyara huku mtekwaji akionesha dalili zote za kukaa tayari kwa kutekwa!

Hii inasababishwa na waongozaji wa filamu wa aina hii waliokosa mafunzo ya msingi (nitty-gritty) ya namna ya kuongoza kazi zao katika kiwango kinachokubalika. Kukosekana kwa mafunzo na kutojielewa ni sababu kubwa ya filamu zetu kuwa ni kitu kisichozingatia au kuhitaji taaluma yoyote. Watu wamekuwa wanalipua kazi na wanafanya mambo bila kuzingatia utaalam kwa kuwa tu hawajitambui. Wanafanya mambo ili mradi wanajua watauza na kupata pesa, basi. Hali hii imekuwa ikiwakatisha tamaa hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika tasnia hii.

Pia kukosa mafunzo kumewafanya walio wengi kujawa na ubinafsi (kwa kuwa hawajiamini) ambao umekuwa ni sababu kuu ya kuufanya uwanja wa filamu wa Tanzania kuwa ni sehemu inayoongoza kwa kutokuwa na mgawanyo wa majukumu. Si ajabu kuona mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza filamu, ndiye aliyeandika skripti, ndiye muongozaji mkuu, ndiye muigizaji mkuu na kadhalika! Na mwisho wa siku hawapendi kukosolewa.

Nitaendelea kusema bila kigugumizi, tasnia yetu imebarikiwa kuwa na waigizaji wengi wazuri, wapigapicha wengi wazuri, wahariri wengi wazuri, na hata baadhi ya waandishi lakini inakosa kabisa waongozaji wazuri wa filamu. Hii haimaanishi kuwa hakuna kabisa waongozaji wazuri, wapo wengi wenye uzoefu na elimu ya kutosha katika uongozaji wa filamu, tatizo ni mfumo mbovu unaowafanya kutupwa nje ya ulingo wa soko la filamu kwa kuwa hawathaminiki, hawatumiki na wala hawapewi heshima inayostahili.

Tunasahau kuwa muongozaji wa filamu ana mchango mkubwa sana katika kufanikisha kazi nzima ya utengenezwaji wa filamu kwa kuwa ndiye mtendaji pekee anayeshiriki kwenye hatua zote za uandaaji wa filamu; kuanzia kwenye wazo hadi kwenye uhariri wa filamu.

Matatizo ya uongozaji kama haya niliyoyaeleza hapa kwetu wala hayatokei kwa kuwa eti waongozaji wa filamu nchini hawakusoma, kwangu mimi hii inaweza isiwe sababu ya msingi sana, kama waongozaji hao watajitambua na kujiendelea kwa kupata mafunzo japo ya muda mfupi wataweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Kukosa elimu ya darasani si mwisho wa kujifundisha. Hata Hollywood kuna waongozaji ambao hawakusoma kabisa katika vyuo vya filamu lakini wamepata wamekuwa waongozaji wazuri na wanaoheshimika sana duniani.

Waongozaji hao ni pamoja na Steven Soderbergh, Robert Rodriguez, Quentin Tarantino, Richard Linklater, na Spike Jonze...

Uongozaji wa filamu ni zaidi ya elimu ya darasani, unakwenda pamoja na creative vision, commitment na visualization, sifa zingine zinazoongezeka kwa muongozaji wa filamu ni uwezo wa kuandika script au kusimamia uandikwaji baada ya rasimu ya awali ya script kukamilika. Pia baada ya kupata waigizaji, muongozaji wa filamu anapaswa kusimamia masuala ya kiufundi ya sinema, ikiwa ni pamoja na kamera, sauti, taa, ubunifu na kadhalika.

Wakati wa uhariri (post-production), muongozaji wa filamu hufanya kazi kwa ukaribu na Wahariri katika mchakato wa kiufundi wa uhariri, hadi kufikia mwisho wa kazi. Katika hatua zote, muongozaji wa filamu anawajibika kuhamasisha timu yake kutayarisha kazi bora. Muongozaji wa filamu pia anapaswa kuyafahamu mahitaji na matarajio ya soko la filamu.

Mwisho, muongozaji wa filamu anapaswa kuwa na uwezo wa kufanya mawasiliano (communication skills) na watu wengine katika kufanikisha kazi iliyo mbele yake.

Alamsiki.

No comments: