Aug 1, 2013

Utamaduni wa Mtanzania: Ni nani wenye dhamana ya kutoa tafsiri sahihi?


  • Walioaminiwa wanatupoteza, sasa hatuna mwelekeo

Huu ndiyo utamaduni wa Kiafrika unaopingana na tafsiri ya wakubwa


“UTAMADUNI wa Mtanzania, are we sure?” nilijikuta nikitupiwa swali na jamaa yangu mmoja kwa utani baada ya kusoma makala yangu moja iliyokuwa na kichwa cha habari: “Kupuuzwa kwa Utamaduni: Hii ndo fursa ya wasanii kuchangia maoni yao kwenye rasimu ya Katiba mpya”.

Nilimtazama kwa mshangao nikiwa sielewi alichokuwa akimaanisha. Alitabasamu na kuketi kando yangu akiwa kashika gazeti, nikalitupia jicho na kuuona ukurasa aliuokuwa akiusoma.

“Naona umewataka wasanii wachangie maoni kuhusu utamaduni wetu, vipi kuhusu mambo kama mikataba, ufisadi na mengineyo? Hivi umeshapata kusikia kauli ya wizi wa pesa ya umma ni kinyume cha Utamaduni wa Mtanzania au kusaini mikataba mibovu ni kinyume cha utamaduni wa Mtanzania? Na huo utamaduni wetu kama kweli tunao ni upi?”

Wakati nikiwa bado natafakari maswali yake aliuliza maswali mengine; “Je, sisi Watanzania values (maadili) zetu ni zipi? Kama tunazo je, tunazikuza kadri muda unavyopita au bado tunaendeleza status quo (hali kama ilivyo)? Je, wakati wa mkoloni tulikuwa na values zipi na hii miaka 52 baada ya uhuru tunazo zipi?”

Hakusubiri nimjibu, alicheka na kuinuka, akaondoka zake. Lakini hakujua kuwa alikuwa ameniachia mtihani mkubwa wa kutafakari, ingawa aliuliza katika hali ya utani lakini kwangu yalikuwa ni maswali yenye mantiki. Nilijiapiza kuwa ni lazima nipate majibu yake. Kama kuna nisichokipenda maishani mwangu basi ni kukosa majibu ya swali/jambo lolote lile ili mradi liwe na mantiki, na mara nyingi huwa naumiza sana kichwa hadi pale nitakapopata jibu ninaloamini ni muafaka ndipo huwa natulia.

Wakati nikiyatafakari maswali ya jamaa yangu nilijikuta nikipata maswali mengine kichwani mwangu ambayo ilinilazimu kuyatafutia majibu ili niweze kupata majibu ya maswali yake: “Hivi huu unaoitwa utamaduni wa Mtanzania ni upi hasa? Na umekuwa ‘documented’ wapi? Ni nani mwenye jukumu la kutoa tafsiri ya kipi ni utamaduni wetu na kipi si utamaduni wetu?”

Tunaposema utamaduni wa Mtanzania tunamaanisha utamaduni upi, hasa kwa Tanzania yenye makabila 123 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake? Tusipokuwa makini tutakuwa tukiimba wimbo tusioujua maana yake, na hii haitusaidii kufikia malengo tunayoyapigania.

Muda mrefu nimekuwa nikishuhudia kauli za "sinema hii ni kinyume cha maadili ya Mtanzania", au mavazi haya "si utamaduni wa Mtanzania". Hii ni kauli inayosisitizwa sana na viongozi waliopewa dhamana ya kulinda maadili na utamaduni wetu, lakini wao wenyewe wakionekana kutojua hasa utamaduni wa Mtanzania wanaoukazania ni upi?

Imeonekana kuwa hata waliokabidhiwa dhamana wamekuwa hawajui chochote kuhusu upi utamaduni na upi si utamaduni. Ndiyo maana huwa sioni ajabu ninaposikia kiongozi fulani aliyepewa dhamana ya kukagua, kulinda na kudumisha tamaduni zetu anapotoa tafsiri anayoijua yeye kuhusu utamaduni ili kuzuia filamu fulani isitoke, jambo ambalo halitusaidii kama Taifa.

Mfano kwenye suala la mavazi, sote tunajua kuwa jamii zetu nyingi kabla ya kuja haya mavazi ya kisasa walivaa ngozi au mavazi yaliyotengenezwa kwa nyasi na magome ya miti. Mavazi haya yalifunika sehemu za siri tu huku yakiacha sehemu kubwa ya mwili wazi. Hadi leo bado zipo jamii hapa Tanzania ambao wanavaa mavazi ya aina hii, huku mabinti wakiacha matiti nje.

Sasa inapotokea unaamua kutengeneza sinema inayoakisi jamii hiyo, anatokea mtu mmoja anayeamua kutoa tafsiri kuwa huo siyo utamaduni wetu! Ni kama tunavyoambiwa leo hii kuvaa nguo fupi siyo utamaduni wetu!

Wizara inayohusika na mambo ya Utamaduni ni vyema ikatoa mwongozo sahihi kuhusu tamaduni za Watanzania katika nyanja mbalimbali ili kuondoa mkanganyiko huu. Tamaduni zitakazoakisi jamii za Watanzania.

Kusema kweli, kama Taifa tumepotea na tumechanganyikiwa. Tumekumbatia baadhi ya tamaduni za Kiarabu na kuzigeuza kuwa tamaduni za Watanzania bila kujali kama zinaakisi jamii husika.

Katika kutafakari hayo, nilijikuta nimepata majibu ya maswali yaliyoulizwa na jamaa yangu. Nijuavyo, kuanzia nchi ilipozaliwa hatujawa na utamaduni mmoja kama Taifa ila tuna tamaduni tofauti katika jamii mbalimbali ndani ya taifa moja.

Hakuna heshima kubwa kama mtu kutambulika kuwa ni sehemu ya utamaduni fulani, utamaduni unaoweza kutupatia urithi usiofutika. Yale tunayoyaonesha katika maisha yetu ya kawaida, hayaishii hapo tu bali yanaathiri hata maisha yetu ya kiimani.

Kuhusu ‘Utamaduni’ wa kutia mikataba mibovu yenye hasara kwa taifa si kitu kigeni kwetu, ni kitu tulichorithi toka kwa mababu zetu. Wao ndiyo walianzisha kutia mikataba iliyotufanya tuwe watumwa, ingawa waandishi wa historia wameiita mikataba hiyo ni ya kilaghai, kama jitihada za kuwatupia lawama wageni walionufaika na mikataba hiyo huku ‘machief’ wetu waliokumbatia mikataba hiyo wakifanywa kuwa watakatifu. Eti historia inawalaani walionunua watumwa huku ‘ikiwabeba’ machief waliouza watumwa! Ni mambo ya ajabu kabisa!

Tangu wakati huo, Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Hata sanaa zetu zimekuwa hazilindwi, hazitambuliki na wala hazipewi umuhimu unaostahili. Jambo muhimu na la msingi ni kuzingatia, kuzitambua na kuzilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria. Ieleweke wazi kwamba sanaa ni kazi ya ubunifu tena yenye ufundi na mvuto kama sumaku, kazi nzuri ya sanaa ni ile iliyo na ubunifu, uasili na inayotumia mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.

Sanaa kama kielelezo cha utamaduni wa mtu husaidia katika kukamilisha utu wake ambapo mtu hujiona huru na pia hujithamini lakini cha kusikitisha hali hiyo ilianza kupotea katika kipindi cha ujio wa wageni hapa nchini.

Ukweli ni kwamba sanaa ni mali ya jamii kwa hiyo ni zao la mazingira, mahali na wakati pamoja na Tanzania kuwa na makabila 123, tunaziona sanaa zetu licha ya kutofautiana lakini hali ya kufanana kwa kiasi fulani tumeiona kitaifa.

Watanzania wote kwa ujumla wetu tunajukumu la kuhakikisha tunalinda tamaduni zetu na kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo ili nao wawe na kitu cha kujivunia kutoka kwenye jamii yao ya asili.

Nimeeleza mambo mengi, pengine wasomaji wengine wanajiuliza, hivi hili neno utamaduni maana yake ni nini hasa?

Utamaduni ni neno lenye asili ya Kilatini “Cultura” ambalo lina usuli wake katika neno colere, linalomaanisha “kulima”. Neno hili lina fafanuzi nyingi. Kwa mfano, mwaka 1952, Alfred Kroeber na Clyde Kluckhohn walikusanya orodha ya vielelezo 164 vya neno “utamaduni” katika kazi yao: Culture: a Critical Review of Concepts and Definitions.

Hata hivyo, neno “utamaduni” linatumika kimsingi katika njia tatu zifuatazo:
-Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vilevile hujulikana kama utamaduni wa juu
-Mkusanyiko wa maarifa ya kibinadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kiishara
-Ni jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi fulani.

Mjadala nauacha wazi…

No comments: