Jul 18, 2013

KUPUUZWA KWA UTAMADUNI: Hii ndo fursa ya wasanii kuchangia maoni yao rasimu ya Katiba mpya


Jaji Joseph Sinde Warioba

BAADA ya uhuru mwaka 1961, iliundwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, mwaka 1962, Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alitamka wazi kuwa Utamaduni ni kiini na roho ya Taifa, nchi inayokosa utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu usiokuwa na roho na hivyo kukosa sifa ya kuitwa taifa kamili.

Sera ya utamaduni ilizinduliwa Agosti 23 mwaka 1997 mjini Dodoma ikiwa ni hatua ya pili muhimu baada ya ile ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962.


Chakushangaza, pamoja na umuhimu uliopo katika suala la utamaduni kwa maisha ya watu bado sera ya utamaduni imepewa nafasi finyu mno katika serikali yetu tangu ilipoanzishwa wizara ya kushughulikia masuala ya sanaa. Na hata rasimu ya Katiba mpya imeonesha kutokuupa nafasi kabisa utamaduni.

Pamoja na kuwepo kwa sera ya utamaduni (ingawa nayo ina mapungufu mengi), inabidi wadau wote wa sekta ya utamaduni wajiulize, je umma wa Watanzania umefikishiwa machapisho ya sera hii ya utamaduni ili waisome na kuielewa?

Je umma umeelimishwa kikamilifu juu ya sera hii ili uweze kushiriki katika utekelezaji kwa upana wake? Na je ushirikishwaji wa vyombo vya habari katika kusaidia msukumo wa wananchi kuielewa sera ya utamaduni umepewa nafasi ya kutosha?

Mipango ya Maendeleo imekuwa ikibuniwa na kutekelezwa bila kujali utamaduni wa wananchi, utamaduni haupewi dhima katika uamuzi na mipango ya maendeleo kwa sababu inaaminika kuwa maendeleo ni kuondokana na mambo ya kiasili pasipo kuchunguza misingi ya mambo hayo na faida zake.

Kwa kiasi fulani uhusiano kati ya utamaduni na maendeleo ulitambuliwa na Serikali ya Tanzania katika miaka ya 70. Kwa mfano, iliyokuwa Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana (1979) iliwateua wataalam wake kadhaa waandike kitabu kiitwacho Utamaduni Chombo cha Maendeleo. Katika dibaji ya kitabu hicho, aliyekuwa Waziri wa Wizara husika alitoa maelezo yanayojaribu kuonesha uhusiano kati ya utamaduni, uhuru na maendeleo. Nanukuu:

“Kuna sababu nyingi za kuutambua Utamaduni kuwa ni chombo ni maendeleo. Moja ni kuwa vipengele na fani mbalimbali za Utamaduni ndizo zilizoko katika kiini cha Umoja wa jamii. Utamaduni ni sehemu ya siasa ya Taifa letu lenye msingi na shabaha ya Umoja wa kweli. Uhuru wetu uliletwa na Umoja. Maendeleo hayapatikani bila ya uhuru na Umoja. Hivyo Utamaduni kama Nguzo ya Umoja, ni chombo cha maendeleo (Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, 1979, uk. vii)”.

Kama jitihada za kukuza utamaduni, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), lilianzishwa mwaka 1967, miaka sita baada ya uhuru, kwa ajili ya kukuza Kiswahili ili kiwe lugha inayoweza kutumiwa katika nyanja zote za jamii, utawala, elimu, mafunzo na biashara.

Miaka minane baadaye Serikali ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa na Baraza la Muziki la Taifa, ambayo yaliunganishwa mwaka 1984 kuwa Baraza la Sanaa la Taifa la sasa (Basata). Madhumuni ya Basata na mabaraza yaliyolitangulia, ni kufufua, kuendeleza na kukuza sanaa za asili za Watanzania.

Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzisha masomo ya sanaa tangu mwaka 1966. Mwaka 1973, mafunzo ya sanaa kwa walimu wa shule za msingi yalianzishwa katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Dar es Salaam na baadaye kuhamishiwa katika Chuo cha Ualimu Butimba Mwanza.

Chuo cha Sanaa Bagamoyo, sasa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni (TaSUBa), kilianzishwa mwaka 1981 kwa lengo la kutoa mafunzo kwa wasanii. Aidha mwaka 1985 serikali ilianzisha matamasha na mashindano ya fani mbalimbali za utamaduni kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda hadi taifa.

Tuelewe kuwa Utamaduni huipa jamii utambulisho. Sura na haiba ya jamii huweza kueleweka na kuelezeka kutokana na utamaduni wa watu wake. Utamaduni hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kupitia lugha, sanaa na imani za kiroho. Mila na desturi wanazofuata, matamasha au sherehe wanazoendesha, mavazi yao, chakula chao na taratibu nyingine za utamaduni wanazofuata huunganisha jamii.

Utamaduni ndiyo “kidhibiti mwendo” kinachoongoza mwenendo na tabia za watu katika jamii. Ndiyo msingi wa maisha ya mtu binafsi. Humuwezesha kujitambua, kuwa na mwelekeo na kujichagulia falsafa sahihi ya maisha yake. Ndiyo msingi wa maendeleo na ubunifu katika jamii. Maendeleo ya uchumi katika maana yake pana ni matokeo na sehemu ya utamaduni wa watu. Maendeleo yasiyojengwa katika misingi ya utamaduni wa jamii ni maendeleo yasiyokuwa na maana kwa jamii hiyo.

Hivi sasa nchi yetu iko kwenye mchakato wa kuwa na Katiba yake mpya, katiba iliyowashirikisha wananchi. Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tayari Mabaraza ya Katiba yameanza kukutana katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchambua rasimu ya Katiba na kutoa mapendekezo, Lakini imeonekana wazi kuwa Katiba hii imetekwa na wanasiasa na inaandaliwa kwa maslahi na utashi wa kisiasa zaidi huku ikipuuza mambo mengine ya msingi kwa jamii, hasa wasanii. Ukiisoma Rasimu ya Katiba tangu mwanzo hadi mwisho utagundua kwamba utamaduni hauna nafasi kabisa katika nchi hii kwa sasa licha ya kuambiwa kuwa ndiyo roho ya Taifa.

Kutokana na mchakato unaoendelea sasa, wasanii waitumie fursa hii kutoa maoni yao, hasa baada ya mashirikisho ya sanaa kukubaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuunda Baraza la Katiba litakalopokea maoni kutoka kwa wasanii na wadau wa sanaa na kuyachambu kisha kuyakabidhi kwenye Tume hiyo.

Wasanii waelewe kuwa hakuna mwanasiasa yeyote atakayeongelea masula ya sanaa wala utamaduni, kila mmoja anafikiria siasa tu. Kila kona unakopita utasikia majadiliano juu ya muundo wa muungano, tume ya uchaguzi na mengineyo.

Kwa kudharau utamaduni tunasahau kuwa sanaa ni zao la matokeo ya juhudi za wasanii katika kutoa ujumbe, kukidhi matumizi na mahitaji ya binadamu, na hii kama tanzu muhimu ya utamaduni wala si kitu kilichoibuka tu. Sanaa ndicho chombo ambacho jamii zisizokuwa na jadi ya kusoma na kuandika inatumia katika kuhifadhi na kuwasilisha kumbukumbu za mambo muhimu katika maisha yao.

Tutambue kuwa sanaa ni kazi ya ubunifu tena yenye ufundi na mvuto kama sumaku, kazi nzuri ya sanaa ni ile iliyo na ubunifu, uasili na inayotumia mbinu bora ya uwasilishwaji wa ujumbe kwa hadhira.

Sanaa zetu za ufundi wa asili zimesahaulika na tumepokea zile za nje na hali hii imesababisha watanzania kuwa watazamaji wa vituo vya sanaa za nje  badala ya kuweka nguvu zaidi katika kubadili fikra zetu ili bidhaa zetu za ufundi ziendane na matakwa ya dunia kwa kuziboresha sanaa zetu za asili. Jambo la msingi ni kuhakikisha tunazingatia, tunazitambua na tunazilinda sanaa zetu ili zisipoteze uasili wake pamoja na wimbi la mabadiliko ya wakati na mazingira ya sasa ya utandawazi na biashara huria.

Sanaa kama nguzo mojawapo muhimu ya Utamaduni hukua na pia hufa. Kwa kuudharau utamaduni, sanaa zetu kwa sasa zinakufa au pengine zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi, tusipochukua juhudi za ziada tutazika kabisa uasili wa sanaa zetu tulizopokezwa na wazee wetu kutoka kizazi hadi kizazi?.

Kwa kuupuuza utamaduni wetu, sanaa zetu zilivyo leo haziweki kumbukumbu nzuri itakayorithiwa na vizazi vijavyo, na kama kuna kumbukumbu basi ni kumbukumbu potofu. Kwa kudharau utamaduni kumesababisha leo hii tumekuwa tukisikiliza nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu bali zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje.

Idara ya Utamaduni ina dhina ya kuongoza, kusimamia, na kudhibiti shughuli za ukuzaji wa Sanaa za Filamu, Maonyesho, Ufundi na Muziki; kusimamia ukuzaji wa lugha ya Kiswahili, lugha za Asili na za Kigeni; na kusimamia shughuli za Mila na Desturi. Tuache kulalamika na tuchukue hatua sasa kuunusuru utamaduni na sanaa zetu.

Alamsiki.

No comments: