Nov 9, 2010

Uandishi ni Sanaa adimu


 Bishop J. Hiluka


Kipaji cha uandishi huanza tangu ukiwa mtoto 
hasa kama unapenda kujisomea kama 
mtoto huyu, Magdalena J. Hiluka

IMEANDIKWA kuwa; “hapo mwanzo palikuwepo na neno,” lakini unapoongelea burudani (entertainment industry) imesemwa; “hapo mwanzo palianza na wazo.” Wazo linaweza kukujia katika njia mbalimbali, linaweza kukufikia kutoka kwa mtu yeyote, mahali popote, wakati wowote. Wazo linaweza kuanzia kwa mwandishi, mtayarishaji wa sinema; linaweza kupitia kwa muongozaji wa sinema au mwigizaji. Linaweza hata kuanzia kwa msomaji wa makala, rafiki, ndugu, jamaa au jirani yako.

Wazo linaweza kumfikia yeyote hata anapokuwa akifanya kazi, akifanya mazoezi, akikimbia, akiongea au akiwa kajipumzisha nyumbani anasoma makala hii. Ni ajabu sana; eti wakia (ounce) chache katika ubongo wa mwanadamu huweza kufanya na kuleta mabadiliko au maendeleo makubwa kama tunayoyashuhudia wakati huu wa sayansi na teknolojia.



Ubongo wa mwanadamu ndiyo injini katika mwili wake kwa sababu ndiyo unao-control kazi zote na viungo vyote vya mwili. Lakini wanadamu huwa tunatumia asilimia ndogo sana ya ubongo (kama 3% tu) kwa shughuli zetu za kila siku ikiwemo kufikiri.

Watanzania (hasa kizazi chetu cha sasa) ni watu tusio na utamaduni wa kujisomea kitu kinachotunyima uwezo wa kufikiri. Kama taifa tunahitaji msukumo mkubwa katika kukabiliana na suala hili la uvivu wa kujisomea linalopelekea tuwe pia wavivu wa kufikiri.

Kujisomea vitabu au machapisho mbalimbali ndiyo njia pekee ya kutufanya tuelewe mambo mengi kwa upana wake, tofauti na hapo tutazidi kuachwa nyuma japo tunadhani kuwa tunakwenda na wakati kwa kuiga mambo.

Mara nyingi kila mtu hudhani kwamba mawazo yake ni sahihi kwa kuwa tu yamemtokea yeye na si wengine. Huwa tunadhani kwamba tuko sahihi hata pale tunapokuwa tumekosea. Mara nyingi hatutambui mwelekeo usio na mantiki ndani yetu na kwa watu wanaotuzunguka. Kama tukichunguza kwa makini kuhusu asili ya hisia zetu, mawazo na mihemko, tutakuwa na ufahamu wa haja katika kufikiri kwa kina zaidi.

Kitendo cha kukikubali kitu kuwa ni cha kweli kwa sababu tu kilitutokea au kuhukumu bila ya kuhoji vigezo ni mfano wa kutofikiri vyema. Maswali au uchunguzi tunaoushiriki tunapotafuta kuelewa, kutathmini, au kutatua hufafanuliwa kama fikra makinifu.

Mwandishi makini ana hatua nne za kufuata: Kwanza, hutafuta ushahidi ulipo. Pili, hufikiria aina na mitazamo inayowezekana na maelezo yake. Tatu, hupima madhara ya nia na upendeleo. Mwisho, hapuuzii maoni ya wengine hata kama hayana maana. Kufanya tathmini mara kwa mara ni moja ya njia nzuri ya kufikiri inayojenga uelewa.

Hapa ndipo lilipo tatizo kubwa katika tasnia ya filamu Tanzania, tatizo lipo kwenye uandishi wa miongozo (scripts). Waandishi wengi wa skripti katika tasnia hii ni wavivu wa kufikiri wasiopenda kujisomea.

Jumamosi moja nilifanya mazungumzo na waandishi kati ya 20 na 25 wa miongozo ya sinema kwenye viwanja vya Leaders Club (Kinondoni) nilipohudhuria bonanza la wadau wa filamu la kila wiki, niligundua kuwepo kwa mapungufu makubwa kwa waandishi; wengi ni wavivu, wasiopenda kujisomea na wepesi kuridhika kwa kuwa tu kazi zao zinaonekana. Nilipata waandishi wasiozidi watatu wenye uwezo wa kuandika kwa ufasaha.

Mwongozo unapaswa kuwa moja ya vipengele muhimu katika uandaaji wa filamu na michezo ya kuigiza. Ni hatua ya mwanzo, ni ramani ya kukuongoza kutoka kwenye wazo (concept) hadi kazi inapokamilika (final edit). Na mara nyingi skripti imekuwa chanzo cha mahusiano mazuri au mabaya (a love-hate relationship) kati ya mwandishi na timu ya uzalishaji, hasa muongozaji (director).

Uhusiano mbaya huja pale muongozaji wa sinema anapobadili matukio ndani ya skripti bila kumshirikisha mwandishi. Binafsi yamenikuta na pia nimeshuhudia yakitokea hata kwa waandishi na waongozaji wakubwa duniani.

Mwandishi ndiye mtu wa kwanza anayeiona sinema wakati akiandika, muongozaji huiona pale anapopitia skripti ili kuongoza upigaji picha (shooting). Tatizo linakuja pale muongozaji anapoiona kwa jicho tofauti. Omba Mungu sinema iwe nzuri lakini ikiwa mbaya basi lawama humwangukia mwandishi kama ambavyo imekuwa ikinikuta.


Ujio wa kompyuta umemfanya kila mtu ajione ni mwandishi wa miongozo. Lakini bado uandishi unabaki kuwa taaluma inayopaswa kuachwa kwa wenye utaalam huo (should be left to the professionals). Kuwa na Microsoft Word kusitufanye tudhani kuwa sisi ni waandishi wazuri.
Nilipokuwa mdogo nilikuwa napenda sana nikikua nifanye mojawapo ya kazi mbili; upelelezi au uandishi. 


Nilipenda kazi hizi ambazo pamoja na upeo wangu kuwa mdogo niliziona zikishabihiana kwa mambo mengi ikiwemo uchunguzi, utafiti na umakini katika kufuatilia taarifa. Nilisamehe chakula hata nilipokuwa na njaa endapo mtu angeanza kusimulia hadithi au kisa cha aina yoyote. Nilijenga taswira ya kitu kilichosimuliwa akilini mwangu na kukiona kama vile naangalia sinema kitu ambacho kilinifanya nianze kupenda kujisomea na kuandika visa mbalimbali tangu nikiwa mdogo.

Hadi sasa mfumo wa maisha yangu umetawaliwa na uandishi, nikilala, nikitembea, na chochote nifanyacho huwa nafikiria kuandika tu. Uandishi umekuwa sehemu ya maisha yangu.
Uandishi ni sanaa ambayo kwanza huanzia kwenye kipaji, kisha mafunzo hufuatia. Kama mwandishi, mimi ndiye mtu wa kwanza ninayeiona sinema, naliona kila tukio la sinema ndani ya akili yangu ninapoandika. Mwandishi anatakiwa kujua jinsi sinema inavyotakiwa kuonekana, na hata sauti (sound) zinazofaa kutumika kwenye sinema yake. Ujuzi wa aina hii huitwa “visualization.”

Visualization ni moja kati ya skills muhimu sana katika uandishi wa miongozo, huu ni uwezo wa kuiona picha kupitia maandishi, ni ujuzi unaochukua muda kuwa nao hasa ukishaifanya kazi ya uandishi kuwa sehemu ya maisha yako. Kuandika mazungumzo (dialogue) pia ni ujuzi wa ziada.

Kitaaluma mimi pia ni tabibu (Medical Personnel) niliyefuzu na kufanya kazi ya kutibu wagonjwa kwa miaka miwili huko Morogoro. Baadaye nikaingia kwenye mkumbo unaowakumba wasomi na wataalam wa Tanzania kukimbilia nje ya nchi kufanya kazi. Huko nje sikudumu na taaluma hiyo, niliiacha nikaingia kwenye sanaa.

Hadi sasa nimeshapata mafunzo ya fani tano tofauti na zote nazimudu. Mwanafilosofia maaruf wa Italia, Niccolò Machiavelli (3 May 1469 –21 June 1527) aliwahi kusema; “learn everything, it might help you in future”. Yaani jifunze kila kitu huenda kikakusaidia baadaye. Jifunze hata kuiba, siyo lazima uwe mwizi lakini itakusaidia kuzijua mbinu za wezi ili usiibiwe.

Nikiwa Morogoro nilipata bahati ya kukutana na gwiji la uandishi wa riyawa na mmoja wa waandishi wanaoheshimika hadi leo, marehemu Eddie Ganzel. Nilitambulishwa kwake na rafiki yangu aliyekuwa jamaa yake wa karibu.

Eddie Ganzel ndiye mwalimu wangu wa kwanza katika uandishi, alinifundisha miongozo muhimu katika uandishi. Siku tulipokutana nilijua kuwa nimepata nafasi adimu na sikutakiwa kuzembea, nikamtupia swali; “Ni ushauri gani unaweza kunipa ili niwe mwandishi mzuri?” Mzee Eddie Ganzel aliyekuwa akiandika aliinua uso huku akiivua miwani yake na kunitazama kwa muda kama vile anatafuta jibu, kisha akaniambia; “Fanya mambo matatu: Jifunze kuandika, jifunze kuandika, na jifunze kuandika.”

Kwa kweli sikumwelewa kabisa! Ilinichukua miaka mitatu kuelewa alichomaanisha, hasa baada ya kupata mafunzo ya uandishi (creative writing and journalism).

Unaweza kupata mafunzo na misingi mizuri ya uandishi lakini ili uwe mwandishi mzuri unapaswa kujenga tabia ya kupenda kuandika bila kuchoka.Waandishi wengi waliofanikiwa katika uandishi wametumia muda wao mwingi katika maisha wakiandika.

Mwandishi mzuri lazima kwanza awe na kipaji na uwezo wa kuandika. Uandishi mzuri wa miongozo ya sinema huanzia katika kuwa msikilizaji mzuri na kuwa na uwezo wa kuumba maneno ambayo yatakuwa rahisi kueleweka pindi mtu akiyasikia, siyo akiyasoma. Wengi wanachangaya mambo; kuandika kwenye gazeti ni tofauti sana na uandishi wa skripti kwa ajili ya video, ambapo watazamaji hupata muda mchache wa kusikia na kuelewa kile msemaji anachokisema.

Wakati unaandika ni muhimu sana kuzama ndani ya akili za walengwa (psyche of the target audience) ujue wanataka nini. Pia kabla hujaandika, unapaswa kuifahamu bajeti ya sinema unayoiandikia. Hii itakusaidia usiandike vitu vinavyoweza kuongeza bajeti. Mwandishi mzuri hupenda kujua bajeti – si kiasi cha pesa; bali idadi ya siku, idadi ya maeneo, idadi ya waigizaji, graphics, muziki, nk. Ndipo utakapoweza kuisuka skripti utakavyo. Kujua bajeti kutakusaidia kuangalia muundo wa filamu unayoikusudia.

Kama mwandishi, usipende kuingiza kila taarifa kwenye skripti ukasahau kuwa unaandika kwa ajili ya video na kwamba skripti inapaswa ieleweke kwa urahisi. Uzoefu ni mwalimu mzuri kwa ajili ya kujua kama skripti ni bora, hafifu, au mbaya, na huwezi kupata uzoefu kama hujengi tabia ya kuandika.

Kumbuka kuwa, video script huandikwa kwa ajili ya sikio, hivyo jisomee; ipitie kwa kuisoma kwa sauti kubwa ukijisomea mwenyewe au rafiki yako. Kwa kujisomea utagundua makosa kwa urahisi, kisha kaa chini uandike upya.

Uandishi hautaki mwandishi awe mvivu wa kufikiri. Weka akilini kwamba uandishi kwa ajili ya video si sawa na uandishi wa makala kwa ajili ya gazeti.Uandishi wa makala una wepesi tofauti na uandishi kwa ajili ya video. Kwa mfano, msomaji anaweza kurudia kuisoma sentensi kama hajaielewa, lakini akishindwa kuielewa sentensi iliyotamkwa kwenye TV maana huwa imepotea na hili ni jambo baya.

Alamsiki

No comments: