Nov 10, 2010

Rais Kikwete, kazi rasmi ya kuiokoa tasnia ya filamu ni sasa

Rais Jakaya M. Kikwete

KWANZA napenda kukupongeza, Rais Jakaya Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuliongoza taifa hili kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Pia nakushukuru angalau kwa kuonesha kuutambua mchango wa sekta ya filamu Tanzania. Katika hotuba yako ya kuvunja bunge la tisa uliyoitoa huko Dodoma tarehe 20 Julai 2010, chini ya kipengele cha “Michezo, Burudani na Utamaduni”, ulinukuliwa ukisema, pamoja na mambo mengine kwamba: “...Hivi sasa tumelipia mtaalamu mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam asaidie kutengeneza njia bora ya kusambaza kazi za wasanii wa muziki na filamu ili wapate malipo halali kwa jasho lao. Mafanikio ya zoezi hili yatatufundisha namna ya kuwasaidia wasanii wa fani nyingine pia...”

Ikumbukwe kuwa kwa miaka mingi sasa, wasanii na watengenezaji wa sinema miongoni mwa wadau wengine wa sanaa wameendelea kutoa sinema hapaTanzania ili kujipatia riziki kutokana na kazi yao bila mafanikio. Ingawaje sekta ya filamu ni sekta yenye thamani ya mabilioni ya  fedha, wengi wameishi na kufa maskini.

Rais, serikali yako inapaswa ibadilishe mtazamo wake kuhusu wizi wa sanaa na nakala zisizo halali (pirated copies). Mambo haya lazima iyaone kama wizi na ipinge wizi kwa nguvu zote kama inatarajia kuona taaluma hii ikinawili na kuwaajili vijana wengi na hivyo kuchangia katika kuinua uchumi wa taifa letu. Ieleweke kuwa ni kosa la jinai kuuza au kununua kazi feki, kama ilivyo kwa nchi nyingi zilizofanikiwa katika tasnia hii.

 Cover ya sinema ya Miss Bongo

Taaluma hii haiwezi kukua kama viongozi wataishia kusema tu bila kutekeleza huku kukiwa na mambo mengi yanayoirudisha nyuma. Binafsi nimetumia miaka kadhaa kujifunza na kufanya tafiti mbalimbali kuhusu historia ya filamu, matatizo makubwa katika tasnia hii, mfumo unaofaa kutumika katika tasnia ya filamu na mambo mengine mengi, kutoka na na haya, naweza kukuhakikishia kwamba sekta ya filamu Tanzania ina thamani ya bilioni 200 ya pesa za Tanzania katika biashara, kama tu serikali yako itatilia mkazo na kutoa msaada unaohitajika.

Nafahamu kuwa wewe ni mpenda michezo zikiwemo sinema za Tanzania, umelidhihirisha hilo ulipotembelea Marekani na kuongea na waigizaji nguli wa Hollywood ili kuangalia namna ya kuboresha soko letu. Sawa, ningependa kukushauri kuliangalia kwa mapana suala la uanzishwaji wa chombo kitakachosimamia utoaji wa mafunzo ya weledi kwa watengeneza filamu ambao hawakubahatika kupitia kwenye vyuo vya sanaa lakini wameonesha kuwa na kipaji.

Kama kweli umedhamiria kuiokoa tasnia hii; serikali yako inapaswa kuelekeza nguvu nyingi katika suala la utoaji wa mafunzo kwa wasanii na watengeneza filamu. Kutafuta gharama za mafunzo kwa watengeneza filamu linapaswa kuwa jambo la kwanza kabisa kwa serikali yako katika kuutambua mchango wa sekta ya filamu.

Sekta ya filamu ni sekta isiyopewa kipaumbele (political valuable) kama sekta muhimu inayoweza kuchangia pato kubwa kwa maendeleo na ukuaji wa uchumi wa taifa letu. Soko la filamu limeachwa mikononi mwa watu wachache (Watanzania wenye asili ya Kiasia) ambao wamekuwa wakilimiliki (control) watakavyo.

Endapo ningekuwa mshauri wako katika masuala yanayohusu sekta ya sanaa (filamu); ningekuomba ufikirie sana kuhusu serikali kuanzisha mpango maalum wa kutoa mikopo kwa watengeneza sinema (amateur) wasiofikiriwa na benki zetu.

Hiini kwa sababu, sekta hii inalipa na inaweza kuchangia pato kubwa la taifa iwapo sinema zinazotengenezwa zitawezeshwa na kutengenezwa kwa umakini zaidi. Ukweli ni kwamba, sinema ikiwezeshwa inadumu kwenye soko kwa muda mrefu sana (lifetime property), huku benki ikimiliki asilimia 30 ya hisa na kushikilia (hold) haki ya kumiliki (copyright) sinema hiyo hadi mkopo uliotolewa utakapolipwa.

Serikali yako inapaswa kuziagiza mamlaka husika kuandaa takwimu za kina kuhusu soko la filamu na kuzitazama fursa zilizopo kabla ya kuamua. Ipo hajakubwa kwa wewe binafsi kuifahamu nguvu ya soko la filamu (dynamics of the home-video industry) kabla ya kutoa maamuzi yoyote.

Ni muhimu sana kuufahamu msingi imara unaohitaji mipango madhubuti na ya lazima katika kuiwezesha (empower) sekta ya filamu hapa Tanzania. Pia litakuwa jambo la busara zaidi kama utawaagiza wasaidizi wako kuuchunguza mfumo unaotumiwa na Afrika Kusini kupitia chombo maalum cha kusimamia na kuwawezesha watengeneza filamuNational Film and Video Foundation (NFVF)”. Ikumbukwe kuwa sekta ya filamu inaiingizia Afrika Kusini pato lazaidi ya Rand 7.7 bilioni.

Pia Serikali yako iangalie uwezekano wa kuanzisha chombo kitakachokuwa na uwezo wa kuzitangaza filamu zetu kitakachoitwa; “Film and Video Promotions Board”; katika chombo hicho viwepo vitengo maalum vitano: Kitengo cha utoaji wa taarifa za upatikanaji wa pesa (funding information) na kutoa fursa kwa watengeneza sinema. Kitengo cha kuandaa takwimu za kina na kutoa fursa ya kuzitangaza kazi zetu katika masoko mengine ya Afrika, na duniani na hivyo kuongeza uwezekano wa kuuza kazi zetu kimataifa na kuigiza pesa za kigeni.
Kitengo kitakachowalazimisha wadau katika sekta ya filamu kupata mafunzo ya weledi (professionalism).

Kitengo kitakachosimamia mapato (revenue generation) yatokanayo na filamu. Kitengo kitakachosimamia kwa ukamilifu sheria za uharamia/wizi (piracy) wa kazi za sanaa na hivyo kuwafanya watengenezaji wa kazi hizi kutokuwa na hofu ya kupoteza mapato (economic reward) yatokanayo na kazi zao.

Utengenezaji wa filamu hapa Tanzania kwa soko la Tanzania unatafsiriwa kuwa sawa na biashara ya barafu (block of ice) inayoweza kumyeyukia aliyenayo mikononi wakati wowote, hii huwafanya watengeneza filamu wa Kitanzania wajikute wakiingia mikataba haraka ya kupata pesa japo kiduchu kabla barafu haijawayeyukia na kugeuka maji, wakati mwingine bila hata kurudisha gharama walizoingia (hili nitalieleza kwa kina zaidi siku nyingine).

Sekta ya filamu hapa Tanzania imefukarishwa kwa makusudi na watu wachache, ndiyo maana wajasiriamali wa soko la filamu wanafanya kazi kwa nguvu zote lakini hawapati kile wanachostahili. Sekta hii imefukarishwa kwa sababu ukimtazama mtayarishaji wa sinema za Tanzania (film producer) hana hadhi ya kuitwa mtayarishaji wa sinema, hasa tunapoangalia sualala mapato na ushawishi wake kisiasa (political influence).

Sijui tutaendelea hivi hadi lini na mchezo huu wa kumtafuta mchawi na kutupiana lawama (blame game)? Serikali haitusaidii, mabenki hayatukopeshi, na soko la filamu limeparaganyika… blah,blah,blah…

Rais, serikali yako inapaswa kuandaa mwongozo (roadmap) utakaotuongoza kwenye mafanikio ya soko letu. Kwa msaada wa serikali yako, tunahitaji kuwa na vyombo madhubuti katika kusimamia kazi zetu. Vyombo kama; Chama Cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kadhalika, vinahitaji kuangaliwa upya ili viweze kwenda na wakati na kusimamia kazi zetu kikamilifu.

Tunahitaji sekta hii ya filamu ichukuliwe kama sekta nyeti sana, kwanza na wewe Rais, Serikali yako kupitia kamati za mipango, na Bunge la Jamhuri. Tunahitaji Mawaziri, Wabunge, na Wakuu wa Idara ambao hawataishia tu kusifia kazi zetu kwenye hotuba zao. Kupitia mamlaka uliyonayo kisheria ya kuteua wabunge kumi, tunakuomba uteue wataalamu (professionals) utakaowapa mamlaka ya kisiasa, kuhimiza utungaji wa sheria na kuzisimamia kikamilifu, na kuhakikisha kuwa tunakuwa na nyenzo bora zitakazosaidia katika kuboresha maendeleo ya sekta hii.

Sekta ya filamu hapa Tanzania haichukuliwi kabisa kama biashara bali huchukuliwa kama burudani tu, Serikali inapaswa kuichukulia sekta hii kwa umakini zaidi kisiasa (seriously politically), kuanzisha makubaliano maalum ya kisiasa (political consensus) yatakayokuwa na ajenda kuu ya kuhakikisha kuwa sekta nzima inakua, kisiasa na kiuchumi.

Serikali inapaswa kupitia upya sheria za hakimiliki na kuziboresha, pia iishirikishe Cosota katika vituo vya forodha (bandarini na mipakani) katika uingizaji bidhaa za kazi za sanaa nchini kama vile zinavyoshirikishwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (Tanzania Food and Drug Authority) kwa bidhaa za chakula na dawa, Shirika la Viwango Tanzania (Tanzania Bureau of Standards) kwa bidhaa zenye viwango vinavyotambulika kimataifa, pamoja na Tume ya Ushindani wa Biashara (Fair Competition Commission – FCC) kwa bidhaa bandia.

Natambua kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (Tanzania Revenue Authority) imepata mafanikio makubwa katika kukusanya kodi kwa upande wa sigara na pombe kali kutokana na kuamuru matumizi ya ukanda wa lakiri (Bandroll/hologram) kwa watengenezaji/waagizaji wa bidhaa hizo, nadhani serikali yako inapaswa kuangalia kwa makini ama TRA au Cosota waanzishe utaratibu huohuo kwa kazi za sanaa. Hii itasaidia kupambanua kati ya bidhaa (CD/DVD) halisi na feki.

Pia Jeshi la Polisi lisiishie kuwakamata watengenezaji na wasambazaji wa kazi feki tu, bali pia liwakamate watumiaji (walaji) pale wanaponunua bidhaa hizo na hukumu iwe kali, ili kupunguza, kama siyo kuondoa kabisa mahitaji (market demand) ya bidhaa feki. Hii itasaidia pia kufuta tetesi kuwa watengenezaji na wasambazaji wa kazi feki za filamu wanalindwa na wana baraka kutoka kwa viongozi wa serikali.

No comments: