Nov 3, 2010

Tasnia ya Filamu: Tunamuenzi vipi Mzee Kawawa?

Mzee Rashid Mfaume Kawawa

NAKUBALIANA na maneno kwamba; wasanii ni watu wenye akili nyingi sana. Msanii (wa aina yoyote) ni mtu mbunifu, mwenye uwezo wa kuumba jambo likakubalika kwenye jamii, na ni mtu anayefanya tafiti za kina katika fani yake. Wasanii wanaweza kuwa viongozi wazuri wakiingia kwenye siasa; mojawapo ya waigizaji maaruf walioingia kwenye siasa na kuongoza ni pamoja na Ronald Reagan, Rais wa Marekani (1980-1988), na Arnold Schwarzenegger, gavana wa jimbo tajiri la California.

Tanzania tulikuwa na kiongozi mahili aliyeanzia kwenye uigizaji wa filamu, huyu ni Simba wa Vita, shujaa wa kupigania uhuru wa Tanganyika, Mzee Rashidi Kawawa. Alizaliwa Februari 27, 1926 katika Kijiji cha Matepwende, Tarafa ya Ligera, Songea Vijijini mkoani Ruvuma.

Alianza shule ya msingi mwaka 1935 huko Tunduru akiwa na umri wa miaka tisa, aliandikishwa shule kwa jina la Baraka ambalo lilikuwa jina lake la utoto.

Maendeleo yake katika masomo yalikuwa mazuri lakini kama ilivyokuwa kawaida wakati ule, watumishi wa serikali ya kikoloni walikuwa hawaishi kuhamishwa.

Mnamo Agosti 1940, ilihamia Shule ya Kilwa Kivinje kumfuata baba yake aliyehamishwa Liwale. Mwishoni mwa mwaka huo alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu waliofaulu mtihani na kuingia darasa la nne.

Mwaka 1941, Kawawa alisikia habari zilizomfurahisha. kutoka kwa Mkuu wa Elimu Jimbo la Kusini kuwa kungepelekwa mtihani wa kushindania kuingia darasa la tano mjini Dar es Salaam. Wakati huo Dar es Salaam kulikuwa na shule iliyoitwa Dar es Salaam African Central School ambayo hivi sasa inaitwa Shule ya Uhuru. Hii ilichukua watoto waliofuzu darasa la nne kutoka kwenye shule za Kanda ya Kusini.

Katika mtihani huo walifaulu watoto wawili tu ambao ni Rashidi Kawawa na Anthony Kiliani na kuanza shule darasa la tano mwaka 1942. Baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule hiyo alijiunga na shule ya sekondari ya Tabora na kumaliza darasa la 12 Novemba 1949.

Kawawa alianza vita ya kuikomboa Tanganyika alipokuwa kiongozi wa vyama vya wafanyakazi kama vile TAGSA na NUTA. Mwalimu Julius Nyerere alivutiwa na ushupavu wake na kumteua kuwa Waziri Mkuu wake wa kwanza baada ya nchi kuwa Jamhuri mwaka 1962.

Mwaka 1951, akiwa mfanyakazi Idara ya Maendeleo ya Jamii, wakuu wake wa kazi walimuuliza kama angependa kuwa mchezaji/mwigizaji katika sinema. Hii ilitokana na kwamba tangu akiwa mtoto shuleni, Mzee Kawawa alipenda sana michezo ya kuigiza inayofurahisha watu na kutoa mafunzo fulani.

Alikubali na kupewa script ya mchezo wa “Muhogo Mchungu”. Alisaidia kuboresha Kiswahili kilichotumika katika maandishi ya mchezo huo na sehemu mbalimbali zilizohusu utamaduni wa Waafrika.

Alisaidia pia kuchagua wachezaji wa mchezo huo, mwenyewe akiwa kama muongozaji (director) na mchezaji kiongozi (leading character).

Mchezo wa “Muhogo Mchungu” uliwalenga vijana wa vijijini wanaovutwa na maisha ya mjini, kuwatahadharisha juu ya matatizo ya ugumu wa maisha ya mjini. Mchezo mwingine alioutunga yeye mwenyewe ni “Meli Inakwenda”. Lengo lilikuwa kuwaasa wasichana wanaovutwa na maisha ya mjini ambayo yana matatizo ya namna nyingi. Katika mchezo huo, yeye alikuwa mchezaji kiongozi, akishiriki kama kijana aliyemlaghai msichana wa kijijini (Halima) aliyetoroka kwao kwenda Mombasa. Alipofika huko, “Halima” alikutana na taabu za kila aina na kuamua kurudi nyumbani kijijini, na kumkuta mchumba wake ameoa msichana mwingine.

Halima” alijaribu kumuua mchumba huyo ila hila zake ziligunduliwa na askari polisi, waliomkamata na kumfikisha mahakamani. Sina hakika kama nakala ya filamu hizi zipo Maktaba kama inavyodaiwa.

Mzee Kawawa alicheza kama mchezaji kiongozi katika michezo ifuatayo:
Muhogo Mchungu”, uliopigwa Dar es Salaam, “Dawa ya Mapenzi”, uliopigwa Dar es Salaam, “Meli Inakwenda”, uliopigwa Bukoba mjini na vijijini, “Wageni Wema” uliopigwa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro Vijijini.

Pamoja na hayo alikuwa ni mhamasishaji wa elimu na kisomo na ilikuwa katika hili ndiyo akawa mwigizaji wa filamu za kutoa elimu kwa wananchi, na akawa mtu mweusi wa kwanza kupewa nafasi ya mwigizaji mkuu.

Hadithi za mitaani zilisema kuwa mzee Kawawa hakuifahamu lugha ya Kiingereza, lakini mzee Kawawa aliijua lugha hiyo vizuri sana. Wengi wanashindwa kujua kuwa utani mwingi juu ya mzee Kawawa ulitokana na kuwa mcheza filamu. Ni kama alivyo Arnold Schwarzenegger, Gavana wa California. Wapo watu wanaofanya utani mwingi kumhusu Arnold! Tatizo ni kuwa sisi tumeamini hadithi za filamu! Kawawa alikuwa mtu mwenye uwezo wa kiuongozi.

Sijui wadau wa filamu wana mpango gani katika kumuenzi mzee huyu?

1 comment:

Anonymous said...

Unatuzengua tu. Sidhani kama hata wewe umesomea filamu so stop talking kitu usichokijua. unajifanya unajua but Bro! you know nothing trust me.