Nov 23, 2010

HISTORIA YA FILAMU 2: Kuibuka kwa ukoo wa LumiereNdugu wawili, Auguste na Louis Lumière

Mwaka1895, nchini Ufaransa ndugu wawili Auguste na Louis Lumière (tamka lumia) walifanikiwa kutengeneza kifaa cha kupigia picha chenye viambatanisho vitatu ndani yake: camera, printer, na projector.

Mwishoni mwa mwaka 1895 jijini Paris, Antoine Lumière ambaye ni baba wa Auguste na Louis alifanya onesho la sinema kwa malipo, huo ndiyo ukawa mwanzo wa kukua kwa sekta hii na soko la filamu (kwa mujibu wa Cook, 1990).Baba huyo wa wavumbuzi hao wawili, Antoine Lumière alizaliwa tarehe 13 Machi 1840 katika eneo la Haunte-Saone, Ormoy, nchini Ufaransa. Alipokuwa na umri wa miaka kumi na nne alifiwa na wazazi wake na kubaki yatima. Aliamua kujifunza useremala na baadaye alikuwa akijisomea vitabu vya sayansi kabla ya kupata nafasi ya kwenda kujifunza sayansi chini ya mwalimu Auguste Constantin. Baadaye alilitumikia jeshi la nchi hiyo na baada ya hapo alijifundisha upigaji picha.

Alioa mke mwaka 1861 akiwa na miaka 21 na kuanzisha studio ndogo ya kupiga picha katika eneo la Besancon, eneo ambalo ndipo wanaye Auguste na Louis walipozaliwa.

Baadaye alihamia Lyon ambako alimzaa mtoto wake wa tatu, Edward na mabinti wengine watatu. Kutokana na juhudi zao, ukoo wa Lumière walijikuta wakiwa ndiyo wazalishaji (producers) wakubwa wa filamu barani Ulaya. Baadhi ya kazi zao ni kama “WORKERS LEAVING THE LUMIÈRE” na “THE SPRINKLER SPRINKLED” (zote za mwaka 1895).

Kutokana na mikakati mizito na changamoto iliyotolewa na ukoo wa Lumière kuliifanya kampuni ya Edison kufanya kazi ya ziada ili kuukabili ushindani, kwa kumtumia Dickson kampuni hiyo ilijikita kwenye kutafuta mbinu mpya ili kukabiliana na ukoo wa Lumière na hatimaye walifanikiwa kuvumbua matumizi ya kifaa kijulikanacho kama ‘Vitascope’ ndani ya miezi sita tu.

Baada ya Dickson kuhangaika sana akifanya tafiti na gunduzi mbalimbali hatimaye mfumo wa mwisho wa ‘Vitascope’ ulioneshwa mwaka huo 1895, ilikuwa ni kamera kubwa yenye uwezo mkubwa na mtambo wa kurusha picha na hivyo kuleta mapinduzi halisi ya sinema.

Bahati mbaya mapinduzi hayo yaliipindua pia tamaa ya Edison. Wakajikuta Edison na Dickson wakishindwa kufikia makubaliano kuhusu malengo yao ya baadaye (future) juu ya uvumbuzi huo mpya wa vitascope. Wakatengana kila mmoja akaamua kufanya kazi kivyake.

Dickson alianzisha kampuni aliyoiita American Mutoscope Company, na kuuendeleza uvumbuzi wake wa Mutoscope kwa nguvu zote, hatimaye akafanikiwa kutengeneza ‘Mutograph’, kifaa kilichokuja kutoa ushindani mkubwa kwa kampuni ya Edison ndani ya mwaka wa kwanza tu wa historia ya soko la sinema.

Dickson akatoa sinema yake ya kwanza akiwa na kampuni yake ya American Mutoscope iliyoitwa “EMPIRE STATE EXPRESS (1896)” na hatimaye kuifanya studio yake kuwa moja ya studio kubwa na tishio, na huo ukawa mwanzo wake wa kuibua vipaji vya watu kama Edwin S. Porter, D.W. Griffith, Billy Bitzer, Mary Pickford, Lilian Gish, na Mack–Sennett.

Dickson hakuishia hapo, aliamua kutengeneza kamera na mtambo maalum wa kurushia picha (projector system) aliouita jina la “Biograph”, mtambo huo ulikuwa na uwezo mkubwa kuliko wa Vitascope, lakini bahati mbaya hakuwa na mauzo mazuri ya kazi katika kampuni yake ya kumwezesha kutoa ushindani wa nguvu kwa kampuni ya Edison.

Dickson akaamua kuuza sehemu ya hisa zake zinazohusu uvumbuzi wa ‘Biograph’ na kuamua kurudi nchi ya mama yake, England, mwaka 1897.
Miaka miwili baadaye, Dickson aliweza kutambuliwa na kupewa heshima na wanahistoria kama ndiye “Baba halisi wa sinema” na ndiye aliyechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo na uvumbuzi wa sinema.

Dickson alifariki kwa kansa tarehe 28 Septemba, 1935 katika eneo la Twickenham, Middlesex, England. Katika kipindi cha uhai wake, Dickson alioa mara mbili na alipokufa aliacha mtoto mmoja wa kiume (adopted son) aliyemuasili.

Mwanzo wa maonesho ya Sinema:

Inasadikiwa kuwa onesho kubwa la sinema la kwanza kwa watu lililofanyika barani Ulaya lilikuwa ni onesho lililofanyiwa na ndugu wawili, Max na Emil Skladanowsky wa Berlin, Ujerumani, ambao walitumia kifaa cha kuoneshea sinema kilichojulikana kama ‘Bioscop’ na lilianza tarehe 1 hadi 31 Novemba, 1895.

Lakini kwa Marekani, maonesho ya kwanza ya sinema kwa hadhira yaliyofana zaidi ni yale ya Jean Aimè (Acme) Le Roy, mpigapicha wa Kifaransa. Hiyo ilikuwa tarehe 5 Februari, 1894, wakati akitimiza miaka arobaini ya kuzaliwa kwake aliamua kutambulisha kazi yake “MARVALLOUS CINEMATOGRAPH” kwa watu, akitumia maonesho takribani ishirini ya wafanyabiashara jijini New York.

Pia Lauste, alifanikiwa kuonesha sinema mnamo mwezi Mei, 1895 nchini Marekani kwa kutumia kifaa cha “Eidoloscope” ambacho baadaye alikuja kukimilikisha kwa familia ya Latham.

Zama za Sinema Bubu (Silent Era):

Sekta ya filamu duniani imepitia vipindi tofauti hadi kufika hapa ilipo sasa, kipindi cha kwanza kilijulikana kama kipindi cha sinema bubu (the Silent Era), katika kipindi hiki sinema zilizotengenezwa hazikuwa na sauti za mazungumzo na pia hazikuwa zikiwekwa nakshi ya muziki au sauti nyingine maalum (sound effects) zinazoambatana na matukio muhimu.

Katika kipindi hiki, wavumbuzi na waandaaji (producers) walijaribu sana tangu mwanzoni kabisa mwa zama za sinema hizi kutaka kuchanganya picha za matukio na sauti za muziki ili kuleta burudani zaidi, lakini hakuna uvumbuzi wowote uliopatikana hadi ilipofikia mwishoni mwa mwaka 1920.

Katika kipindi cha miaka thelathini ya mwanzo ya historia ya watengeneza sinema, sinema zilizokuwa zikizalishwa zilikuwa bubu (silent) ingawa wakati mwingine ziliambatanishwa na muziki hai (live musicians) kutoka kwa wanamuziki waliotumbuiza moja kwa moja, na wakati mwingine muziki huo ndio uliotumika kama sauti maalum (sound effects) huku mazungumzo (dialogue) ya wahusika yakiwakilishwa kwa njia ya maandishi kwenye skrini ‘intertitles’.

Kilele cha mafanikio ya sinema katika zama za sinema bubu kilikuwa ni sinema ya “SAFETY LAST (1923)” iliyoandaliwa na Harold Lloyd, na CharlieChaplin katika sinema ya “THE GOLD RUSH (1925)”.

Lakini, mafanikio ya soko la sinema za Hollywood hayakuanza au kupata nguvu ghafla, sinema zao zilikuwa zikisambaa taratibu na kuonekana duniani kote huku zikiwavutia wengi taratibu.

Mwaka 1915, baada ya tangazo lililotolewa kupiga marufuku kusitishwa nchini Ufaransa ndiyo ukawa mwanzo wa sinema za Hollywood kupenya na kusambaa na hivyo kuleta mwanzo mpya (cinematic avant-garde) wa sekta ya filamu duniani.

Makundi ya watengeneza sinema yakaanza majaribio yao muhimu ya uhariri katika picha na kutengeneza mwongozo maalum. Mwongozo huo wa uhariri ulikuja kujulikana kama “Frech Impressionist Cinema”.

Pia kuzaliwa kwa sekta ya filamu kwa nchi za Kisovieti ilikuwa ni chachu na mwanzo muhimu zaidi wa sekta hii. Kwa hiyo, ujuzi wa uhariri (cinema editing) ukakua kwa haraka na kufikia upeo wa juu zaidi kuweza kuinogesha hadithi yenyewe.

Sergei Eisenstein alianzisha utaratibu na muongozo kamilifu uliojulikana kama “dialectical/ intellectual montage”, ambao ulisimamia katika utengenezaji wa sinema zisizotegemea mstari mmoja (non-linear) na zenye kusababishwa na nguvu kubwa (violently clashing), picha ambazo zilionesha matendo ya haraka na ya nguvu kwa watazamaji.

Sergei  Eisenstein alizaliwa 23Januari 1898 na kufariki 11 Februari 1948, alikuwa mwongozaji namtayarishaji wa filamu katika Umoja wa Kisovieti. Alikuwa ni kati ya waongozaji filamu wa kwanza walioandika juu ya nadharia ya filamu na hivyo kuweka msingi kwa sanaa changa ya filamu. Mtindo alioanzisha na kuendeleza ulikuwa kukata vipande vya filamu na kuviunganisha baada ya kupiga picha.

Katika kipindi hicho cha mwongozo uliobuniwa na Eisenstein, sekta ya filamu ilianza kukua kwa kasi sana ikizileta sinema hizi (silent film) kwenye kongamano la kilele (aesthetic summit) cha mafanikio. Uwezekano wa kupata picha nzuri ulikuwa ukiongezeka kila kukicha hasa baada ya kugunduliwa kwa kamera zinazoweza kusogea (mobile) wakati tendo la upigaji picha likiendelea (shukrani kwa waliogundua ‘booms’ na ‘dollies’ ), na mikanda ya kuchukulia picha (film) yenye ubora.

Kuigiza kwenye skrini ikawa ni zaidi ya sanaa, huwezi kuandaa kazi bila kuyatia chumvi au kuyakuza matukio (theatrical exaggeration) na kuyatengeneza kwa kiwango cha juu matukio ili kuiteka akili ya mtazamaji ikubaliane na wewe. Ushawishi mkubwa (visual eloquence) uliongezeka, imani juu ya mbinu za kizamani za ‘intertitles’ ikapungua kabisa.

Sinema za kimatukio (occasional films) kama ile ya F.W. Murnau wa Ujerumani “THE LAST LAUGH (1926) zikaepukwa kabisa. Ukweli hasa ni kwamba, ni katika kipindi hicho ambapo sinema bubu (silent cinema) zilikoma rasmi na ndiyo ukawa mwanzo wa sinema mpya.

No comments: