Nov 16, 2010

Historia ya Filamu duniani

Zoöpraxiscope

FILAMU (Motion picture film), au wengine hupenda kuita picha jongefu zimekuwepo kwa zaidi ya miaka mia, historia ya filamu inaanzia mwishoni mwa karne ya 19. Filamu zimepitia hatua kwa hatua hadi kufika hapa zikianzia kwenye mawazo yaliyoonekana mapya hadi kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano na burudani, na hata kuwa mwasilisha taarifa katika karne ya 20 na ya 21. Filamu pia zina athari kubwa (substantial impact) kwenye sanaa, teknolojia, na siasa.

Machapisho mbalimbali yamekuwa yakiwataja ndugu wawili, Auguste na Louis Lumière (tamka Lumia) wa Ufaransa kama waasisi wa filamu duniani na kumsahau William Kennedy Laurie Dickson (WKL Dickson) aliyekuwa injinia mkuu katika kampuni ya Edison Laboratories ya Marekani.

William Dickson ndiye anayesadikiwa hasa kuwa “baba wa filamu duniani,” na ndiye aliyevumbua mfumo wa picha unaojulikana kitaalamu kama “Celluloid Strip”, huu ni mkanda maalum wenye picha mbalimbali za matukio yanayofuatana (sequence of images) yaliyopigwa kwa kamera maalumu ya picha jongefu (moving images) na baadaye kuzionesha kwa njia ya sinema (projecting moving images).

WKL Dickson alizaliwa katika eneo la Minihic-Sur-Rance katika nchi ya Ufaransa kutoka kwa wazazi wenye asili ya Uingereza na Uskochi (English-Scottish parents) mwaka 1860, na baadaye alihamia Marekani ambako alijiunga na kampuni ya Thomas Edison. Mwaka 1879 akiwa London, Dickson aliyekuwa kafiwa na baba yake, alisoma habari kwenye gazeti moja la London zilizomhusu Tomas Edison na maabara yake iliyojulikana kwa jina la “Menlo Park Laboratory”. Dickson alivutiwa sana na habari za maabara hiyo, miaka miwili baadaye alituma 'telegram' kwenye kampuni ya Edison akiulizia kama anaweza kupata nafasi ya kazi kwenye maabara hiyo.

Edison alimjibu Dickson kwa kifupi kwamba “hakuna kazi”. Lakini mwaka 1883, Dickson akiwa amefanikiwa kukusanya pesa za nauli aliamua kuelekea Marekani huku akiwa na ujuzi kidogo wa upigaji picha, alipofika Marekani alitafuta kijinafasi kidogo chini ya paa la kampuni ya Edison na kupafanya kuwa sehemu ya kazi zake huku akisubiri siku pengine akabahatika kupata nafasi muhimu ya kuajiriwa kwenye kampuni hiyo. Ndipo bahati yake ilipotokea, ulikuwa mwaka 1888 Dikson alipopewa kazi na Edison ya kufanya utafiti juu ya maendeleo ya mpigapicha maarufu wa enzi hizo, Eadweard Muybridge, na wavumbuzi wenzake ambao kwa wakati huo walikuwa wakirekodi picha.

Eadweard Muybridge alikuwa mpigapicha aliyefanikiwa sana enzi hizo na alikuwa amefanikiwa kutengeneza picha kadhaa za matukio mfuatano (sequential photographs) yaliyohusu mwendo wa farasi. Mwaka 1877, chini ya udhamini wa Leland Stanford, Eadweard Muybridge alifanikiwa kumpiga picha farasi aitwaye “Sallie Gardner” akiwa katika mwendo kasi kwa kutumia kamera 24 za Stereoscopic.

Majaribio hayo yalifanyika mwezi Juni 11 kwenye shamba la Palo Alto jimboni California. Sababu ya zoezi hilo ilikuwa kufanya utafiti kama farasi anapokimbia huinua miguu yote minne kwa mara moja. Kamera zilipangwa sambamba na eneo alilokuwa akikimbilia farasi, na kila kamera ilidhibitiwa kwa waya. Miaka miwili baadaye, mwaka 1879, Muybridge alifanikiwa kuvumbua kifaa kilichoitwa “zoöpraxiscope”, kifaa hicho kilikuwa kikitumika kwa ajili ya kuoneshea na kuzichangamshia (animating) picha za wanyama alizopiga.

Hivyo Dickson akaanza rasmi kazi ya kufuatilia nyendo za Muybridge akiwa na ari kubwa huku akijitahidi kupeleleza na kufuatilia kila jambo aliloona ni jipya kuhusu ugunduzi huo. Katika utafiti huo alijikuta akipata wazo la kutengeneza kamera na vifaa vingine vitakavyoweza kumsaidia kuona picha mbalimbali. Pamoja na ugumu aliokutana nao lakini Dickson hakuwa mwepesi wa kukata tamaa, alijifunza kwa bidii huku akitumia mbinu na nyendo za mtu mmoja aliyeitwa John Carbutt.

Huyu John Carbutt alikuwa mpigapicha wa Kiingereza aliyehamia Amerika kutokana na ushindani uliokuwa huko na kufanya tafiti mbalimbali juu ya mkanda maalum wa filamu wa kurekodia picha “Celluloid Photographic Film”.

Kwa kuwa Dickson alikuwa na wazo la muda mrefu la kutaka kutengeneza picha zinazotembea (sinema), aliona kuwa huo ulikuwa wakati wake wa kutimiza ndoto yake ya muda mrefu na kuamua kumweleza bosi wake Edison kuhusu majaribio yake, lakini Edison hakutilia maanani kabisa majaribio hayo (motion picture ideas) aliyoelezwa na WKL Dickson. Baada ya kuona akipuuzwa, Dickson aliamua kuachana na Thomas Edison na kujiunga na kampuni nyingine iliyokuwa ikijihusha na masuala ya aina hiyo ya George Eastman Company ili aweze kukidhi haja yake ya uvumbuzi.

Baada ya kipindi fulani, Dickson aliamua kumtafuta mchungaji Hannibal Goodwin, huyu alikuwa ni mchungaji wa kanisa la “Episcopal”, kanisa la asili la watu wa Marekani. Ilisemekana kuwa mchungaji Goodwin alikuwa amefanya tafiti mbalimbali na kufanikiwa kuvumbua na kutumia mafuta maalum mazito (photographic emulsion) yaliyokuwa yakitumika kwa ajili ya kulainishia mkanda wa picha na kuufanya uzunguke kwa urahisi. Dickson alimpata Goodwin na kumlazimisha akubali na kuidhinisha utafiti wake wa mafuta maalum utumike kwenye kampuni ya George Eastman kwa ajili ya uzalishaji.

Dickson “king’ang’anizi” hatimaye alifanikiwa kuvumbua kamera mnamo mwezi Novemba, 1890 na kuifanyia majaribio kwa kupiga picha (filming) jaribio lake la kwanza aliloliita “MONKEY SHINES” huku akimhusisha (featuring) msaidizi mwenzake, Fred Ott.

Kamera hiyo aliipa jina la “Kinetograph”, na kuionesha kwa Thomas Edison, ambaye aliamua kuunda timu maalum ambayo ilikuwa na kazi moja tu ya kuuendeleza ugunduzi wa Dickson, timu hiyo hatimaye ilifanikiwa kutengeneza kifaa kingine kilichopewa jina la “Kinetoscope”, kifaa ambacho kilikuwa na tundu (peep-hole) dogo kwa ajili ya kuonea picha ambazo walizipa jina la maajabu ndani ya sekunde tano “five second wonders.”

Uvumbuzi huo wa Dickson haukuwa na ugumu sana kwa upande wake. Ni uvumbuzi ambao mkanda wenye picha kadhaa za matukio yaliyofuatana ulikuwa ukipitishwa mbele ya lenzi yenye kutoa mwanga kwa msaada wa balbu na nyuma yake kulikuwa na gurudumu lenye kuzunguka. Gurudumu hilo lilipozunguka, muonekano wake ulimfanya mtazamaji aone jumla ya picha 46 za matukio tofauti yanayofuatana ndani ya sekunde moja tu. Mzunguko huo wa picha 46 ndani ya sekunde moja uliweza kumfanya mtu anayezitazama picha aweze kuona matendo halisi (lifelike motion).

Kutambulishwa kwa kifaa cha “Kinetograph” mwezi Oktoba, 1892 ndiyo ikawa chachu na mwanzo wa sekta ya filamu kukua na kufikia hapa ilipo kwa sasa.

Mnamo mwaka 1893, kwenye tamasha la wafanyabiashara la Chicago (Chicago World Fair), Thomas Edison alizitambulisha kwa umma vumbuzi hizo mbili zilizotokana na uvumbuzi wa William K.L. Dickson (Kinetograph na Kinetoscope). Mfumo wa kinetoscope haukuchelewa kusambaa kwa haraka sana na kwa mafanikio makubwa barani Ulaya.

Mfumo huu wa Kinescope wenye mkanda maalum wa picha zilizopigwa na Dickson kwenye studio ya Edison iliyojulikana kwa jina la “Black Maria” ulikuwa wa urefu wa futi hamsini. Picha hizo zilizokuwa katika matukio mfuatano (sequences) zilichukuliwa katika sherehe na matukio mengine mbalimbali ya kidunia, mfano “FRED OTT’S SNEEZE (1894)” na picha zingine zilichukuliwa kutoka kwenye burudani mbalimbali kama vile kwenye maonesho ya sarakasi, maonesho ya muziki hasa ya wanenguaji kwenye kumbi za starehe, na kwenye maonesho ya ngumi.

Hata hivyo Edison hakuwahi kutambuliwa kama mtu muhimu na mvumbuzi aliyekubalika kwa nchi za Atlantiki za bara Amerika, hasa kwa kuwa wao teknolojia hii ilikuwa imewafikia kupitia uvumbuzi wa awali na majaribio yaliyowafikia kabla yakitokea Uingereza na bara la Ulaya kwa ujumla.

Juhudi za Dickson zilisaidia sana katika maendeleo ya sekta ya filamu hasa kwa watengenezaji wa kamera na vifaa vingine waliofuatia, mfano mzuri ni kamera iliyotengenezwa na fundi umeme na mwanasayansi wa Kiingereza Robert William Paul na mshirika wake Birt Acres.

Paul aliyekuja na wazo la kutaka kuonesha sinema kwa hadhira (audience), aliona kuwa ni jambo zuri kuionesha sinema kwenye mkusanyiko mkubwa wa watu kuliko kuionesha kwa mtu mmoja mmoja, hivyo alivumbua mtambo maalum wa kurushia picha “film projector” na hatimaye alifanikiwa kuonesha sinema kwa mara ya kwanza mwaka 1895.

Mwaka huohuo 1895, nchini Ufaransa ndugu wawili Auguste na Louis Lumière walifanikiwa kutengeneza kifaa cha kupigia picha chenye viambatanisho vitatu ndani yake: camera, printer, na projector. Mwishoni mwa mwaka 1895 jijini Paris, Antoine Lumière ambaye ni baba wa Auguste na Louis alifanya onesho la sinema kwa malipo, huo ndiyo ukawa mwanzo wa kukua kwa sekta hii na soko la filamu (kwa mujibu wa Cook, 1990).

Itaendelea

No comments: