Nov 19, 2010

Mwalimu Nyerere Film Festival ni Februari 2011

 Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba akitoa ufafanuzi,
pembeni yake ni Katibu Mkuu, Wilson Makubi
Katibu Mkuu wa TAFF, Wilson Makubi akifafanua jambo

Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) limetangaza rasmi tarehe ya tamasha la filamu la Mwalimu Nyerere. Kwa mujibu wa rais wa shirikisho hilo, Simon Mwakifwamba, shirikisho hilo litakuwa linaendesha tamasha la filamu za Tanzania kila mwaka, na litafanyika kwa mara ya kwanza mwezi februari mwakani, 2011.

Rais wa shirikisho alisema hayo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye ukumbi wa Baraza la sanaa la taifa (Basata) jana Alhamisi, tarehe 18 Nov, 2010 na kubainisha kuwa lengo lao ni kukuza soko la kazi za filamu nchini na kukuza mahusiano ya kisekta kati ya wasanii wa tanzania na wale wa nje ya nchi.

Wanatarajia kuwaalika wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, mmoja wa wageni toka nje aliyethibitisha kushiriki ni Rita Dominick wa Nigeria, pia bado wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya watu kutoka Marekani.

Alizidi kutanabaisha kuwa tamasha hilo litapambwa na sinema ishirini za Kitanzania zilizofanya vizuri ndani na nje ya nchi, pamoja na burudani nyingine zikiwemo ngoma za asili, vichekesho, muziki wa dansi, muziki wa taarabu, bongofleva na michezo mbalimbali.

Production Manager wa Focus Media, Mwaipopo akijitambulisha

Tamasha hilo litakuwa na tuzo ya sinema iliyopendwa na watazamaji au iliyofanya vizuri katika soko la filamu nchini, tuzo hiyo imepewa jina la People's Choice Award. Alisema kuwa jamii ndiyo itakayoamua kati ya sinema ishirini ni sinema zipi ziteuliwe kwenye nafasi tano tu ambazo baadaye zitaingia kwenye mchujo wa kugombea nafasi tatu.

Baada ya kupatikana sinema tano, jopo la watu watano litakaa kuamua na kupitisha sinema tatu tu, na hatimaye kupatikana mshindi atakayetangazwa. Jopo hilo litatumia vigezo vya kitaalamu ili kupata washindi. Pia kutatolewa tuzo nyingine zitakayoitwa TAFF Special Awards; kwa ajili ya kuwaenzi waasisi wa taifa, Mwalimu Nyerere na Mzee Rashid Kawawa kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa na tasnia ya filamu nchini.

Sinema zilizopendekezwa ni pamoja na;
  1. Mahabuba
  2. Sabrina
  3. Mtemi
  4. Kipendacho
  5. Zawadi
  6. Vita
  7. Augua
  8. Masaa 24
  9. Johari
  10. Segito
  11. Shakira
  12. Sandra
  13. Neema
  14. Babra
  15. End of the Start
  16. Life of Sandra
  17. Criminal Love
  18. Big Brother
  19. Girl Friend
  20. This is It
  21. 20%
  22. Best Wife.
Tamasha hilo litafanyika kwa siku sita kuanzia tarehe 14 Februari hadi 19, 2011 katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, na wanatarajia kuwa litafungwa na Mama Maria Nyerere.

Katika tamasha hilo, kabla ya maonesho ya siku husika kutatanguliwa na mafunzo kwa mada mbalimbali yanayohusu shughuli za filamu na maigizo kwa wakufunzi waliotayarishwa.

Kwa jitihada hizi zinazofanywa na shirikisho la filamu zitasaidia kuinua sekta hii japo bado kuna kazi ngumu sana kuweza kufikia malengo. Sekta ya utengezaji filamu haijaimarika sana humu nchini ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika. Tanzania imekuwa soko kubwa la sinema hasa za masuala ya kijamii kutoka Nigeria na India huku wasanii wa humu nchini wakiendelea kukabiliwa na changamoto chungu nzima katika fani hiyo.

Wadau mbalimbali waliohudhuria walilitaka shirikisho kujikita kwanza kwenye mipango ya muda mfupi (short term plan) ili kulijenga kwanza, hasa ikizingatiwa kuwa uongozi uliopo unatakiwa kukaa madarakani kwa mwaka mmoja tu.

No comments: