Mar 15, 2018

The Theory of Everything na maisha ya Prof Hawking

Prof Stephen Hawking enzi za uhai wake

Filamu ya The Theory of Everything
NILIWAHI kusoma riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo iliyoandikwa na Profesa Euphrase Kezilahabi, inayoonesha maisha yaliyopo duniani ni sawasawa na fujo, kwani kila mtu anayekuja duniani huleta fujo zake na baadaye kutoweka.

Fujo hizo zimekuwa zikitofautiana, wapo waliofanya fujo kwa jina la amani, waliofanya fujo kwa kutumia nguvu na wengine wamefanya fujo za kimaandishi, fujo ambazo hazitafutika hadi dunia inafutika…

Nimejikuta nikiikumbuka riwaya hii baada kutafakari kuhusu maisha ya Prof Stephen Hawking, mwanafizikia maarufu duniani aliyefariki dunia jana Jumatano Machi 14, 2018 akiwa na miaka 76.
Prof Stephen Hawking ni mmojawapo wa watu waliojaliwa uwezo mkubwa wa akili, amejulikana sana si kwa sababu ya usanii au umaarufu, bali kwa sababu ya uwezo mkubwa kiakili na mchango wake katika sayansi.

Prof Hawking alifahamika sana kwa kazi yake ya kisayansi kuhusu uwepo wa eneo katika anga za juu ambapo nguvu za mvutano huwa za juu sana kiasi kwamba miali nururishi au hata mwanga hauwezi kuponyoka.

Kwa Kiingereza, eneo hilo hufahamika kama 'Black Hole' nadharia aliyoieleza mwaka 1974 ikionesha kwamba 'black hole' hutoa "Miali ya Hawking".

Alitumia hilo kujaribu kufafanua kuhusu asili ya vitu vyote duniani na angani na aliandika vitabu kadhaa maarufu vya sayansi kikiwemo A Brief History of Time (Historia Fupi kuhusu Wakati) mwaka 1988 kilichouza nakala zaidi ya milioni 10.

Prof Hawking alizaliwa Januari 8, 1942 huko Oxford, Uingereza. Alipata nafasi Chuo Kikuu cha Oxford kusomea sayansi ya mambo asilia mwaka 1959, kabla ya kusomea shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Cambridge.

Mwaka 1963, Prof Hawking alipatikana na ugonjwa ulioathiri mfumo wake wa neva na mawasiliano mwilini akiwa na miaka 21. Madaktari walimwambia hangeishi zaidi ya miaka miwili.


Ugonjwa huo ulimfanya kulemaa na kulazimika kutumia kiti cha magurudumu.
Nyakati za mwisho za maisha yake, alikuwa hawezi kuzungumza ila kwa kutumia kifaa cha kufasiri mawazo yake na kuyageuza kuwa sauti.

Kutokana na umuhimu wake, maisha yake yameigizwa kwenye filamu ya The Theory of Everything ya mwaka 2014, ambapo Eddie Redmayne aliigiza nafasi ya mwanasayansi huyo.

Filamu hii imetengenezwa kwa hadithi ya maisha yake kushangaza.
Filamu hii ya The Theory of Everything (Nadharia ya Kila kitu) iliyoandikwa na Anthony McCarten na kuongozwa na James Marsh, imejaribu kuyachora maisha ya mwanafizikia huyu mwenye kipaji cha hali ya juu na mwanafizikia wa wakati wetu.

Filamu hii imepata maoni mazuri, imesifiwa kwa muziki, upigaji picha, na uigizaji wa Felicity Jones na hasa Eddie Redmayne, kiasi cha kutajwa kwenye tuzo mbalimbali na matamasha ya filamu, pamoja na kushinda Tuzo za Oscar kama Muigizaji Bora wa Kiume.

Filamu hii pia iliteuliwa kwenye Tuzo za Oscar kwenye vipengele vya Sinema Bora, Muigizaji Bora wa Kike (Felicity Jones), Skripti Bora iliyotokana na kitabu, na Muziki Bora (Jóhannsson).

Filamu hii pia iliteuliwa kwenye maeneo kumi katika Tuzo za British Academy Film (BAFTA); na ilishinda Tuzo ya Filamu Bora ya Uingereza, Mwigizaji Bora wa Kiume (Eddie Redmayne), na Skripti Bora iliyotokana na kitabu (Anthony McCarten).

Iliteuliwa pia kuwania tuzo nne za Golden Globe, ikashinda Tuzo ya Mwigizaji Bora (Eddie Redmayne), na na Skripti Bora iliyotokana na kitabu (Anthony McCarten).

Pia iliteuliwa kuwania tuzo tatu katika Tuzo za Chama cha Waigizaji wa Televisheni; ikashinda tuzo moja ya Mwigizaji Bora wa Kiume (Eddie Redmayne).

Filamu hii imeonesha maisha ya Stephen Hawking alivyojikuta akimpenda Jane Wilde, aliyekuwa mwanafunzi wa sanaa wakati wakisoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge miaka ya 1960.

Jane Wilde alipenda sana kumwita Stephen Hawking mrithi wa Albert Einstein, na baadaye mume na baba wa watoto wao watatu.

Kwa muhtasari, filamu hii imeigizwa vizuri mno, picha zake zimepigwa vizuri na ukichanganya na muziki wa Jóhannsson, inakufanya kujikuta ukiwa sehemu ya hadithi.

No comments: