Mar 12, 2018

Mapokeo ya kazi za sanaa yanavyotuathiri



INGAWA Tanzania kuna zaidi ya makabila 120 na lugha 128 zinazotumika, Watanzania tumeweza kubaki kama tulivyo, Watanzania. Popote pale Mtanzania atakapokwenda atajiita  Mtanzania, akiulizwa zaidi ya hapo, anaweza akataja kabila yake. Ila, Watanzania hupenda zaidi kuwa Watanzania. Ndiyo utamaduni wetu.

Kinachoonekana sasa ni Watanzania kutaka kugawanyika kwa misingi ya kidini, hasa kati ya Wakristo na Waislamu, japo wameishi pamoja vizuri tangu uhuru.

Pamoja na hayo, Sera ya Ujamaa na lugha ya Kiswahili zimechangia sana kutufanya kuwa wamoja. Rangi, ladha, urafiki na uchangamfu ndiyo viungo muhimu vya utamaduni wa Tanzania.


Japo yapo mambo mengi yanaweza kutofautiana kutoka kabila moja hadi jingine, lakini lugha ya Kiswahili, muziki wa asili (ngoma), sanaa, mwenendo mzima wa maisha katika vyakula, mavazi, ujenzi wa nyumba na tunavyofanya sherehe mbalimbali (harusi, jando, misiba na kadhalika), ni mambo yanayoshabihiana sana.

Hata hivyo, lengo la makala yangu ni kuibua mjadala zaidi kwa hoja mbalimbali ambazo zimekuwa zikiibuka juu ya suala la maadili katika kazi za sanaa na namna au changamoto zinazotukabili sote juu ya namna ya kukuza na hata kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya KiTanzania.

Swali la kujiuliza: Je, njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatusaidia kujenga juu ya msingi sahihi wa waliotutangulia au tunapotea na wimbi la utandawazi?

Ukweli tatizo la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu limekuwa gumzo, ingawa kwenye upande wa filamu mamlaka yenye dhamana imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti tatizo hili.

Kwenye muziki, bado wengi wanajiuliza kwa nini tunakosa alama ya mfano muziki wetu? Ni nini chanzo cha wanamuziki wetu kuimba nyimbo zisizo na maadili?

Utafiti na wachambuzi wengi wa masuala ya sanaa huelezea kuwa fani ya muziki nchini ipo katika hatari kubwa ya kuporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika uteuzi wa maneno katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa na waliotutangulia.

Hivyo haya yote yanaashiria hatari ya kuporomoka kwa fani hii. Je, kama ni kweli hatua zipi zichukuliwe ili kunusuru au kudhibiti tatizo hili?

Unaweza kujuliza, tunawezaje kuwa na utamaduni wa muziki mmoja wakati Tanzania kila kabila lina muziki wa asili yake, wenye sauti tofauti?

Kitu kikubwa ni kwamba ngoma ni kitu cha kipekee utakachokikuta kwenye muziki wa asili wa karibia makabila yote. Hivyo, muziki wa kiTanzania kwa ujumla unaongozwa na ngoma. 

Kwa miaka dahari tumekuwa na utamaduni fulani, iwe kwenye furaha au huzuni, nyimbo, kucheza na muziki kwa ujumla imekuwa njia ya Watanzania kujieleza na kujiburudisha kwa namna moja au nyingine.

Changamoto inayotukabili katika muziki wetu ni namna ya kuweza kudhibiti muziki wenye mapokeo hasi na usioendana na maadili yetu.

Hali hii imesababisha hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuzifungia nyimbo kadhaa zisizokuwa na maadili baada ya kupokea orodha kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Nyimbo hizo zimefungiwa kutokana na kuwa na maudhui ambayo ni kinyume na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005, ingawa hatua ya kuzifungia nyimbo hizi imezua maswali mengi sana kuliko majibu.

Ni kweli tumekuwa na idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi, ambao hufanya kazi zao kuisha kwa muda mfupi.

Si hivyo, tutazidi kuwa wasindikizaji wa kupokea mitindo ya muziki toka nje na baadaye kulalama kudai ni chetu huku tukiendelea kutengeneza kazi kwa kunakili, kama hatutakuwa makini katika kuchagua kilicho bora kwetu.

Sina tatizo na mamlaka zilizofungia nyimbo zisizokuwa na maadili, lakini tunahitaji kuangalia zaidi ya hapo, kwa kutafuta njia sahihi zaidi ya kuwasaidia wasanii badala ya kusubiri wakosee ili tukimbilie kuwafungia.

Kwa nini zisitungwe kanuni (kama si sheria) zitakazofanya kazi zote zitakazotoka kabla hazijakwenda sokoni zipate ithibati au kwa lugha nyepesi kibali ili ziweze kusikika na kuonekana.

Pengine kwa kiasi fulani kama si sana tutaweza kulinda maadili ya sanaa na kudhibiti kazi chafu, pia kukuza viwango vya kazi zetu za sanaa hapa nchini. Aidha hatua zaidi ziwepo kwamba atakayekaidi maelekezo haya adhabu kali ichukuliwe dhidi ya msanii yeyote nchini bila kujali umaarufu wake.

Na hali hii isiangalie muziki na unenguaji tu, pia fani nyinginezo za sanaa. Baraza la Sanaa la Taifa lisiangalie muziki tu wakasahau ngoma za asili. Yako wapi mashindano ya taifa ya muziki wa asili nchini? Ziko wapi tuzo za muziki wa asili Tanzania? Baraza la Sanaa lina mpango gani kuhusu muziki wa asili?

Nilidhani ili kuendeleza muziki utakaofuata maadili ingekuwa vyema kuwekeza katika muziki wa asili ili wasanii wa muziki wa kizazi kipya waache tabia ya kukana nyimbo zao za asili na kuiga muziki wa nchi nyingine ambao hutokana na nyimbo za asili za nchi zao.

Kuiga huko ndiyo kunaelezwa kusababisha kupoteza ladha na uhalisia wa muziki wa Tanzania, na hatimaye mamlaka kuzifungia nyimbo na kuwafungia wasanii ambao tulipaswa kuwalea kimaadili.


Pia Baraza la Sanaa la Taifa liwekeze nguvu katika fani za uchoraji na uchongaji ambazo kwa kiasi kikubwa bado zinalinda maadili yake ya mapokeo ya utandawazi na bado tunajivunia Watanzania katika michoro ya Tingatinga na michoro mingine ya kina mzee Lilanga na mingi inayoelekeza maisha halisi ya Mtanzania na Mwafrika kwa ujumla.

Wakati sanaa ya kucheza au kuigiza ikiwa inakua nchini, sanaa ya uchoraji na uchongaji vinyago imeenea. Uchoraji wa Tingatinga na vinyago vya Wamakonde vinapendwa sana na watalii na wenyeji pia.

Uchongaji ni fani isiyoteteleka kabisa, ona vinyago vya Wamakonde (lipiku, mashetani) moja ya vinyago maarufu na bora kabisa duniani, ni fani ambayo haijaingiliwa na sanaa chafu. Hata hivyo, ubunifu zaidi unahitajika katika fani hizi za kazi za mikono ili ziweze kushindana kitaifa na kimataifa.

No comments: